Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 1/22 kur. 13-17
  • Everglades ya Florida—Kilio cha Dharura Kutoka Porini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Everglades ya Florida—Kilio cha Dharura Kutoka Porini
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kilio cha Dharura cha Kutaka Msaada
  • Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
    Amkeni!—1998
  • Mabwawa ya Ulimwengu—
    Amkeni!—1994
  • Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru
    Amkeni!—2003
  • Sehemu Zenye Shida Zaidi
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 1/22 kur. 13-17

Everglades ya Florida—Kilio cha Dharura Kutoka Porini

WAGENI milioni moja hivi humiminikia paradiso hii ya kitropiki kila mwaka ili kuona maajabu makubwa ya kazi ya Muumba Mtukufu. Hapa, hakuna mabonde yenye vina vyenye kufika kilometa moja wala magenge yenye vimo vya juu sana ya kustaajabisha, hakuna maporomoko ya maji ya kupiga picha, hakuna kongoni-miti wenye kutangatanga au dubu-grizli wenye kwenda dalji na ambao hutazamwa kwa umbali salama. Badala ya hivyo, Hifadhi ya Kitaifa ya Everglades ndiyo hifadhi ya kitaifa ya kwanza duniani iliyoanzishwa kwa sababu ya wingi wa viumbe badala ya kutokana na mandhari yenye kuvutia.

Sehemu zayo nyingine zikiwa nyasi, na sehemu nyingine zikiwa bwawa la kitropiki, hiyo imeitwa “mto wa nyasi.” Maisha ya wakazi wayo huendelea kama ambavyo yamekuwa kwa karne nyingi. Aligeta wenye urefu wa meta 3.3 huota jua kwenye joto lenye mvuke, wakiwa chonjo kuona chakula chao kitakachofuata. Usiku bwawa hilo hujaa ngurumo zao na ardhi hutetemeka wanapofanya desturi zao za kujamiiana. Kasa wanaotoshana na beseni kubwa la kuogea hupita katikati ya nyasi kutafuta chakula. Fisi-maji wa mto walio wepesi na wenye michezo mingi huishi hapo pia. Nyayo za karibuni sana za puma wa Florida wakitembea zaweza kuonekana katika matope. Dia wenye mkia mweupe wahitaji kuwa macho sikuzote, kwani puma hao watawala kila wakati wapatapo fursa. Rakuni, mara nyingi wakionyeshwa wakiosha chakula chao katika vijito vilivyo karibu, wamestarehe katika Everglades, kwa kuwa kuna chakula tele hapo.

Kuna viumbe vingi pia ambavyo karibu havionwi na wageni wanaozuru Everglades. Vyura wa aina nyingi huketi wakiwa wamejificha kwenye matawi yaliyo juu ya ardhi, kwenye matawi makubwa ya yungiyungi, na kwenye kwekwe maridadi ya maji katika mifereji iliyotengenezwa na watu. Na atambaaye kwa mwendo wa polepole sana katikati ya mimea ya maji ni konokono-tofaa—ambao ni moluska wakubwa kama mipira ya gofu, na wenye mashavu kama samaki na pafu sahili, ambazo huwawezesha kupumua ndani ya maji na nje ya maji. Hayo maji machache yamejaa kamba-mto, kaa, na samaki wa aina nyingi. Kuna nyoka na wadudu na watambazi wengi sana—wote wakingoja kula au kuliwa.

Kati ya ndege wanaoonekana hapa ni domokijiko-roseati walio warembo, kwarara-mweupe, yangeyange weupe pe ambao huzunguka-zunguka juu wakati wenzi wao wanapoatamia mayai yatakayotoa makinda. Kuwaona kulasitara-wakubwa-buluu wenye kuvutia kule angani, na wenye kuruka kwa kasi hivi kwamba hawawezi kuhesabiwa, hakuwezi kusahaulika. Shakwe, mwari, na shaunge-zambarau pia huruka pamoja na furukombe wenye adhama, ambaye ni ishara ya kitaifa ya Marekani.

Kisha kuna mnandi mwenye shingo ndefu na yule mbizi, au ndege-nyoka, akiitwa hivyo kwa sababu yeye huonekana zaidi kama mnyama-mtambazi kuliko ndege anapokuwa ametoa shingo yake ndefu yenye umbo la S juu ya maji. Aina hizo mbili za ndege, ambao kiasili ni walaji sana, hutafuta chakula katika hayo maji machache ya Everglades. Wakilowa maji, wote huanika mabawa yao na kupanua manyoya ya mikia yao, wakitokeza wonyesho maridadi kana kwamba wametulia wapigwe picha. Ni wakati tu mabawa yao yakaukapo kabisa ndipo wawezapo kuruka.

Ili asipuuzwe, limpkini afananaye na taji hushtua kila mtu kwa vilio vyake vikubwa. Ndege huyu mkubwa mwenye madoa-madoa ya hudhurungi na meupe ameitwa ndege-mliaji kwa sababu yeye hulia kama mwanadamu mwenye huzuni apigaye mayowe kwa kukata tamaa. Ndege nadra na aliye hatarini mwa kutoweka ni kipanga wa Everglades, ambaye ni ndege mwindaji atoshanaye na kunguru-mdogo—ambaye kusalimika kwake kwategemea kupatikana kwa konokono-tofaa—ni mwono wa kukumbukwa kwa watazamaji wa ndege. Wakitazama juu, wageni watastaajabia kusanyiko kubwa la ndege wakipumzika katika miti mikubwa ya oki ambayo imejaa majani ya kijani-kibichi chenye kumetameta na kuviringwa-viringwa kwa mosi ya Kihispania. Yenye kulandana vizuri na rangi za ndege ni maua mekundu na ya kijani-kibichi yakining’inia kutoka kwa mimea yenye kutambaa iliyo dhaifu na ambayo imezingira miti. Hapa, wageni wanaweza kusahau wapo katika nchi gani na katika kontinenti gani. Huu ni ulimwengu wa kipekee, unaokaribia kufanana na paradiso, wa asili na maridadi.

Hatimaye, kuna yale maji machache na nyasi ya rangi ya dhahabu—ambayo ndiyo ishara kubwa ya Everglades. Na kufikia upeo wa macho mtu aona tu mto huu wa nyasi ulio kimya na kumeta-meta, ukiwa tambarare kama juu ya meza, na kuinama kidogo sana kuelekea kusini kwa mwinuko wa sentimeta nne kwa kila kilometa. Maji hayo yakiwa kimya, bila hata mkondo uonekanao, huenda polepole kuelekea baharini. Maji hayo ndiyo uhai wa Everglades; bila hayo, Everglades inakwisha.

Mapema katika karne hii, kabla ya Everglades kuharibiwa mno na mwanadamu, bahari hii ya nyasi ilifikia kilometa 80 toka mashariki hadi magharibi na kuenea kilometa 500 toka Mto Kissimmee hadi Ghuba ya Florida. Mtu mwenye kimo cha kawaida anaweza kuvuka umbali huo bila maji kufikia mabega yake. Boti za hewa hupita juu ya maji hayo machache katikati ya nyasi ndefu za rangi ya dhahabu kwa mwendo wa kasi sana, zikiwapa watalii wenye kupigwa na upepo msisimko ambao hawatasahau maishani. Wavuvi huja kuvua samaki aina ya besi na wengineo wa maji matamu na wa maji ya chumvi, kama ambavyo wamefanya kwa vizazi vingi.

Kilio cha Dharura cha Kutaka Msaada

Mwanzoni mwa karne hii, wanasiasa wa Florida na wafanyabiashara walifikiria Everglades kuwa bwawa la matope lenye viumbe visivyotakikana ambavyo vilipaswa kuondolewa ili nafasi ipatikane kwa ujenzi, upanuzi wa mji, na maendeleo ya kilimo. “Zuieni maji, iondoeni maji kwa kufanyiza kipito, ondoeni maji yote, geuzeni mkondo wayo” zikawa ndizo shime zao. Katika 1905, kabla ya kuchaguliwa kuwa gavana wa Florida, N. B. Broward aliazimia kukausha kabisa maji ya “bwawa hilo lenye kujaa magonjwa.”

Hizo hazikuwa ahadi za bure. Mashine kubwa-kubwa zenye kubomoa ardhi na vifaa vya kuzoa matope vililetwa. Chini ya mwelekezo na usimamizi wa Kikosi cha Uhandisi cha Jeshi la Marekani, mifereji ya kilometa 90 ilichimbwa ikiwa na vina vya meta 9, ikiharibu zaidi ya meta milioni moja za mraba za mabwawa. Vizuizi vikubwa, kuta, na vituo vya pampu vilijengwa, na mifereji mingi na barabara zilipitana-pitana katika Everglades. Maji yenye thamani ya kuendeleza maisha yalielekezwa kwingine kutoka kwenye ardhi hiyo yenye viumbe vingi ili yadumishe mashamba makubwa yaliyotoka kuanzishwa. Majiji ya pwani yalipanuka kuelekea magharibi, yakizidi kumeza sehemu za Everglades kwa ajili ya mitaa mikubwa, barabara, maduka, na nyanja za kuchezea gofu.

Ingawa sehemu ya Everglades ilitangazwa kuwa hifadhi ya kitaifa katika 1947, uondoaji wa maji na kugeuzwa kwa maji yaelekee kwingine uliendelea kwa njia ya kudhuru sana. Wanamazingira wanakubali kwamba kuondolewa kwa maji ya Everglades—na kutumia mamilioni ya dola katika kufanya hivyo—kulikuwa kosa kubwa sana. Ni wachache walioelewa kwamba kukatizwa kwa mtiririko wa maji kungeharibu kabisa maisha katika Everglades. Ilichukua miongo mingi kabla ya madhara hayo kuonekana.

Hata hivyo, kufikia miaka ya katikati ya 1980 wanamazingira na wanabiolojia walikuwa wakitangaza hali ya hatari kwamba Everglades ilikuwa inakwisha. Ilionekana kana kwamba kila kiumbe kilikuwa kinateta, kikipaza kilio cha kutaka msaada. Mashimo ya maji ambamo aligeta waliishi yalianza kukauka wakati wa ukame. Mvua ilipokuja na maeneo hayo kufurika, matundu yao na mayai yalifagiliwa mbali. Sasa idadi yao inapunguka haraka sana. Inaripotiwa kwamba wanakula watoto wao. Ndege maridadi wa maji ambao pindi fulani walikuwa zaidi ya milioni moja katika eneo hilo wamepunguka hadi maelfu tu—upungufu wa asilimia 90. Wale domokijiko-roseati walio warembo ambao pindi moja walijaa kama wingu angani walipokuwa wakirudi kwenye viota vyao sasa wamekuwa wachache sana kwa kulinganisha. Tangu miaka ya 1960, idadi ya korongo-miti imepunguka toka 6,000 hadi 500 tu, jambo linalohatarisha spishi hiyo. Vidimbwi vyenye ufanisi vya kukuza samaki vya Ghuba ya Florida kwa ajili ya biashara ya serikali ya makombe ya bahari pia vimo hatarini. Idadi ya wanyama wote wenye uti wa mgongo, tokea dia hadi kasa, imepunguka kwa asilimia 75 hadi 95, akaripoti mwanabiolojia mmoja.

Pamoja na mwingilio wa utaratibu wa kilimo na utendaji mwingine wa wanadamu vikaja pia vichafuzi vya mbolea na dawa za kuua wadudu ambazo polepole zilichafua ardhi na maji. Viwango vya juu vya zebaki vimepatikana katika tabaka zote za mtungo wa chakula, tokea samaki walio katika mabwawa hadi rakuni na aligeta na kasa. Wavuvi wanashauriwa wasile besi na kambare wanaovuliwa katika maji fulani yenye zebaki zilizotoka ardhini. Puma pia wameathiriwa na mwingilio wa mwanadamu, wakiuawa na sumu za zebaki na vilevile na wawindaji haramu. Mnyama huyu yumo hatarini mwa kutoweka hivi kwamba inaaminiwa kunao wachache kuliko 30 katika jimbo zima na 10 katika hifadhi hiyo. Mimea kadhaa ya asili ya Everglades pia imo hatarini mwa kutoweka.

Wachunguzi fulani na wanamazingira waamini kwamba huenda Everglades imefikia hali ambayo haiwezi kurekebishwa. Lakini serikali na maofisa wa mbuga na wanamazingira wengi waamini kwamba fedha zikipatikana na hatua ya dharura ikichukuliwa na mashirika ya jimbo na ya serikali, Everglades inaweza kuokolewa. “Hakuna mtu ajuaye kwa hakika wakati kitu kikubwa na chenye kutatanisha kama hiki kifikiapo hali ambayo hakiwezi kurekebishwa,” akasema ofisa mmoja. “Huenda tayari imetendeka.” Mwanabiolojia John Ogden akiri kwamba uwezekano wa kufanyiza upya Everglades hauonekani kama utafaulu, lakini yeye ana matumaini mazuri. “Ni lazima nitumainie mazuri,” akasema. “La sivyo, tokeo ni jangwa la viumbe, huku mabaki ya hifadhi yakiwa na aligeta wachache hapa, na viota kadhaa vya ndege pale na jumba zuri la kuhifadhi vitu vya kale lenye puma aliyejazwa sufu akiwa jambo kuu.”

Vilio vya maofisa wa Florida, wanabiolojia, na wanamazingira katika taifa zima vimesikiwa na maofisa wa serikali na wanasiasa wa serikali ya Marekani, kutia ndani rais na makamu wa rais wa Marekani. Sasa mipango inafanywa na Kikosi cha Uhandisi cha Jeshi la Marekani, ambacho watangulizi wacho waliharibu kazi waliyofanya miaka mingi iliyopita. Tamaa yao ni kuokoa Everglades na maisha yaliyomo, badala ya kuiondolea maji, kuiziba na kugeuza mkondo wa maji.

Kwa wazi, suala muhimu ni maji. “Msingi wa kupata mafanikio ni maji safi—na kwa wingi,” likaandika U.S.News & World Report, “na hayo yaweza kupatikana tu kwa kupunguza maji ya kilimo au ya maeneo ya miji. Mashamba makubwa ya miwa ya Florida Kusini na mashamba ya mboga yaelekea kuwa shabaha.” “Kugawanya maji kutakuwa jambo gumu, lakini tumetoa maji ya kutosha, na hatuwezi kutoa maji zaidi,” akatangaza msimamizi wa Hifadhi ya Everglades Robert Chandler. “Lazima wengine wawe wahifadhi waangalifu,” akasema. Wenye kuunga mkono pendekezo la kufanyiza upya Everglades wanahofu kwamba pigano lao kubwa zaidi dhidi ya mradi huo litakuwa dhidi ya wakulima wa miwa wa Florida na wakulima ambao wana mashamba makubwa katika Everglades. Kwa hasara ya maisha katika Everglades, kiasi kingi cha maji kinatumiwa ili kutegemeza mahitaji ya wakulima.

Kufanyiza upya na kuokoa Everglades kunaweza kuwa mpango wa utengenezaji upya wenye ujasiri zaidi na ulio ghali zaidi katika historia. “Tunazungumzia pesa nyingi, tunazungumzia ardhi kubwa sana, na tunazungumzia utengenezaji upya wa mfumo wa ikolojia kwa kiwango ambacho hatujapata kuona mahali popote ulimwenguni,” akasema ofisa anayesimamia mradi wa Everglades katika Hazina ya Ulimwengu ya Wanyama wa Pori. “Kwa miaka 15 hadi 20 ijayo, kwa gharama ipatayo dola bilioni 2,” likaeleza gazeti Science, “Kikosi cha jeshi na serikali ya jimbo na mashirika mengine ya serikali wanapanga kurekebisha mtiririko wa maji katika mfumo wote wa ikolojia wa Florida Everglades, kutia ndani kilometa 14,000 za mraba za mabwawa na mifereji iliyotengenezwa.”

Kwa kuongezea, mipango inahitaji kununuliwa kwa karibu hektari 40,000 za mashamba karibu na Ziwa Okeechobee na kuyageuza kuwa bwawa ambalo litachuja vichafuzi vinavyotoka katika mashamba yanayobaki. Wakuzaji wa miwa wanateta vikali juu ya mpango wa serikali wa kukata senti moja kwa kila nusu kilo ya sukari ili kupata fedha zaidi za kusafisha Everglades. “Kufanyiza upya mahali hapo kwapaswa kugharimiwa kifedha na wale walionufaika na kuharibika kwa mahali hapo: yaani wakuzaji na wasagaji wa miwa wa Florida,” wasema uhariri wa gazeti la kila siku USA Today. Inakadiriwa kwamba uchanganuzi huo wa kukatwa kwa senti moja kwa kila nusu kilo ya sukari ya Florida utatokeza dola milioni 35 kila mwaka.

Inatarajiwa kwamba vita hiyo—wakulima na wakuzaji wa miwa dhidi ya wanabiolojia, wanamazingira, na wapendao mambo ya asili—itaendelea kama ambavyo imeendelea katika sehemu nyingine za Marekani ambako vikundi hivyo vinazozana. Makamu wa rais wa Marekani Gore aliomba kuwe na ushirikiano. “Kwa kufanya kazi kwa ushirikiano,” alisema, “tunaweza kuziba mgawanyiko huo na kuhakikisha kuna mazingira mazuri na uchumi wenye nguvu. Lakini huu ndio wakati wa kuchukua hatua. Hakuna Everglades nyingine ulimwenguni.”

[Picha katika ukurasa wa 13]

Aligeta

[Hisani]

USDA Forest Service

[Picha katika ukurasa wa 14]

Furukombe

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kwarara-mweupe

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mbizi, au ndege-nyoka, wawili wenye kiota

[Picha katika ukurasa wa 16]

Rakuni watatu wanaotembea majini

[Picha katika ukurasa wa 16]

Yangeyange

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kulasitara-mkubwa-buluu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Limpkini, aitwaye pia ndege-mliaji

[Picha katika ukurasa wa 17]

Makinda ya mnandi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki