Kuutazama Ulimwengu
Papa Asema Ni Watu Mmoja-Mmoja Wanaopasa Kulaumiwa, Si Kanisa
Katika barua iliyoandikiwa moja kwa moja viongozi wa kanisa, mamlaka za umma, na watu wa Rwanda, Papa John Paul 2 alijaribu kuondoa Kanisa Katoliki ya Kiroma hatiani kwa lawama la maangamizi ya jamii nzima-nzima huko katika 1994. “Kanisa lenyewe haliwezi kulaumika kwa makosa ya washiriki walo ambao wametenda dhidi ya sheria ya kievanjeli,” akadai. Hata hivyo, papa alitaarifu: “Washiriki wote wa kanisa ambao wametenda dhambi wakati wa maangamizi ya jamii nzima-nzima ni lazima wawe na moyo mkuu wa kukubali matokeo ya matendo waliyofanya.” Yaelekea hiyo ndiyo mara ya kwanza kwamba papa alizungumza hadharani kuhusu shtaka kwamba makasisi katika Rwanda walishiriki na kuchochea sana uchinjaji huo ambao uliua watu wapatao 500,000 na shtaka la kwamba viongozi wa Katoliki hawakuchukua hatua ya kuukomesha. Mwelezaji wa Vatikani Luigi Accattoli, akiandika katika gazeti la habari la Italia Corriere della Sera, alisema kwamba taarifa ya papa kwa Wakatoliki wasijaribu kuhepa kutekelezwa kwa haki “hugusa swala nyetivu,” kwa sababu “miongoni mwa wale wanaolaumiwa kwa maangamizi ya jamii nzima-nzima, pia mna makasisi ambao wametorokea ng’ambo.” Wengi wa watu walio Rwanda ni Wakatoliki.
“Familia Zapitia Badiliko”
“Familia ya kawaida ya Kanada imebadili muundo wayo kwa kutazamisha sana hivi kwamba wenzi waliooana walio na watoto huwa asilimia 44.5 tu ya familia zote,” laripoti The Globe and Mail. Kinyume cha hilo, “katika 1961, wenzi waliooana waliokuwa na watoto walikuwa karibu asilimia 65 ya familia zote za Kanada.” Tarakimu nyingine yenye kushangaza ni ongezeko la idadi ya ndoa zisizohalalishwa, ambazo ziliongezeka karibu mara tatu, kutoka 355,000 katika 1981 hadi 997,000 katika 1995. Uchunguzi huo, ambao ulifanywa na Statistics Canada, ulitaja hivi pia: “Ikiwa matukio ya talaka, kufunga ndoa tena na mahusiano ya ndoa zisizohalalishwa yaendelea kuwa juu, badiliko kubwa sana katika muundo wa familia laweza kutazamiwa.”
Upendezi wa Ufaransa Katika Mambo ya Kifumbo
“Kwa nini Wafaransa wanatumia wakati mwingi sana pamoja na waaguzi na wawasiliani-roho siku-hizi?” lauliza The New York Times. “Yaripotiwa kwamba Wafaransa wengi zaidi wanawaendea watu waonao mambo yasiyoonwa na wengine na wastadi wa umaana wa kifumbo wa tarakimu kwa wingi kuliko wakati mwingineo wote. . . . Serikali ina uthibitisho kwamba uchawi unanawiri. Mwaka uliopita, mamlaka za kodi zilisema kwamba walipa-kodi karibu 50,000, idadi kubwa kuliko zote, walisema kwamba walichuma mapato yao kwa kufanya kazi wakiwa wanajimu, waponyaji, wawasiliani-roho na kazi kama hizo. Kwa kulinganisha, nchi hiyo ilikuwa na makasisi wa Katoliki ya Kiroma wasiozidi 36,000 na wataalamu wa matatizo ya akili wapatao 6,000.” Kwa wengine, utendaji huo huonyesha hofu ya kile ambacho huenda kitukie mwishoni mwa mileani. Wengine wanauona kuwa tokeo la kuzorota kwa mashirika yaliyositawishwa, kama vile dini. Watu wenye kufanya utendaji huu husema kwamba wateja wao wamebadilika sana katika miaka ya majuzi. Wakati uliopita, wateja wengi walikuwa wanawake. Sasa kuna idadi inayotoshana ya jinsia zote mbili. Na badala ya kuuliza juu ya ugonjwa na mambo ya mapenzi, watu sasa wanauliza kuhusu kazi zao.
Mashine za Kuuzia za Japani
“Karibu kila kitu kinapatikana katika mashine ya kuuzia katika Japani,” lasema The Washington Post. Mashine za kuuzia hutoa vitu vilivyofungwa kwa karatasi ya zawadi, diski songamano, bia, kaptula za wanandondi, mayai, lulu, vichezeo vya tembo waliojazwa sufu, soksi ndefu za kike zilizoshikanishwa na chupi, kamera za kutumiwa mara moja na kutupwa, na karibu kila kitu uwezacho kukifikiria. Kuna “mashine za kuuzia ambazo hazihitaji uiname” ambazo hutoa vitu kwenye kimo cha kufikia kifuani, mashine zilizo chini ambazo hazitazuia mandhari, na hata mashine ambazo zimerembeshwa kwa maua na ubuni mwingineo uliorudiwa-rudiwa. “Japani ina ukubwa wa Montana tu, lakini kuna karibu mashine nyingi za kuuzia kama zilivyo katika Marekani yote,” makala hiyo yaongeza. “Mashine nyingi za kuuzia za Japani huwekwa nje; hata kuna moja juu ya Mlima Fuji wenye barafu.” Vitu vya gharama kubwa vyaweza kutolewa nje kwa sababu viwango vya kuharibu vitu kimakusudi viko chini sana Japani. Nafasi ni ghali, kwa hiyo wenye maduka hutumia mashine za kuuzia ili kuonyesha bidhaa zao zaidi ya kuzionyesha kwenye rafu. Hizo zaweza kupatikana katika karibu kila pembe ya barabara katika Tokyo. Hata hivyo, vikundi fulani vinakasirika kwamba, vinywaji vya alkoholi, bia, na sigareti zaweza kupatikana na mtoto yeyote awezaye kuingiza sarafu kadhaa.
Linalofuata Ni “Dhoruba ya Uhalifu” wa Matineja
“Uhalifu wenye jeuri Marekani ni jambo liwezalo kuwa hatari, ambalo litatokea katika miaka michache ijayo,” lataarifu The New York Times kuhusiana na ripoti iliyotolewa na Baraza la Uhalifu katika Marekani, shirika la mawakili wa mashtaka na wataalamu wa kutekeleza sheria. “Ingawa watu wazima wanatenda uhalifu usio na jeuri sana, kiwango cha uhalifu wenye jeuri miongoni mwa matineja kimepanda sana kwa mwongo uliopita. . . . Kila kizazi cha matineja tangu 1950 kimekuwa chenye jeuri kuliko kilichopita.” Kufikia mwaka 2005, idadi ya wanaume wenye umri wa miaka 14 hadi 17 itaongezeka kwa asilimia 23, na ni ongezeko hili ambalo linatia wataalamu wasiwasi. Akihangaika kwamba wahalifu wabaya zaidi ni wanaume ambao huanza mwenendo wao wa uhalifu wanapokuwa na umri mchanga sana, John J. DiIulio, Jr., profesa wa siasa na mambo ya umma kwenye Chuo Kikuu cha Princeton, alitaarifu: “Tuko katika utulivu wa muda kabla ya dhoruba ya uhalifu.” Ripoti yake, iliyokusanywa kwa ajili ya Baraza la Uhalifu katika Marekani, ilitaja kwamba thuluthi hivi ya uhalifu wote wenye jeuri unatendwa na watu ambao walikuwa wameshikwa lakini ambao walikuwa wameachiliwa chini ya masharti, probesheni, au kuachiliwa kwa kabla ya kufanyiwa kesi. Serikali ina daraka la kulinda raia wayo, ripoti hiyo ikasema, lakini inakosa kufanya hivyo.
Upasuaji Usiotumia Damu Wapata Mwendo
Mwishoni-mwishoni mwa 1996 hospitali moja katika Hartford, Connecticut, Marekani, ilijiunga na nyinginezo 56 kotekote nchini zilizo na “vituo visivyotumia damu kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova,” likaripoti The Hartford Courant. “Baada ya kuchunguza wazo hilo, wenye mamlaka za hospitali walitambua kwamba matamanio ya Mashahidi wa Yehova hayakuwa tofauti sana na yale ya wagonjwa wengi.” Kwa msaada wa dawa na ufundi wa hali ya juu wa upasuaji, madaktari huatika viungo na kubadili vifundo na vilevile hufanya upasuaji wa moyo, kansa, na pasuaji nyinginezo—zote bila kutumia damu. Kwa kuongezea, wataalamu wengi wa utunzi wa afya sasa hukubali waziwazi hatari za utiaji-damu mishipani. Dakt. David Crombie, Jr., mkuu wa upasuaji kwenye Hartford Hospital, akiri waziwazi hivi: “Nilipata mazoezi yangu ya tiba wakati ambapo damu ilifikiriwa kuwa dawa ya kutia afya na nguvu. Sasa yafikiriwa kuwa sumu.” Biblia kwa upatanifu hukataza kuingiza damu mwilini.—Mwanzo 9:4; Mambo ya Walawi 17:14; Matendo 15:28, 29; 21:25.
Je, Una Mkazo Utokanao na Tekinolojia?
Simu zenye kuchukulika, bipa, mashine za faksi, kompyuta za nyumbani, na modem zimebadili sana mawasiliano. Hata hivyo, Dakt. Sanjay Sharma, ambaye ana upendezi wa kipekee katika kushughulikia mkazo, ahisi kwamba aina hii mpya ya tekinolojia pia imeingilia usiri na wakati wa mapumziko wa watu. Tokeo ni mkazo utokanao na tekinolojia. Kama ilivyoripotiwa katika The Toronto Star, “mkazo huchangia sana ugonjwa, ukosefu wa utokezaji na kifo cha mapema.” Athari hutia ndani msongo wa juu wa damu, maradhi ya moyo, kubadilika-badilika kwa hali ya moyoni, kuumwa kichwa, mkazo wa misuli, tatizo la kupata usingizi, mshuko wa moyo, na kudhoofika kwa mfumo wa kinga. Waweza kuepukaje kupatwa na mkazo utokanao na tekinolojia? Bila shaka, sikuzote ni jambo la hekima kumwona daktari wako. Kwa kuongezea ripoti hiyo hupendekeza mazoezi ya mwili ya kawaida, kuchukua likizo ya mwisho-juma, na kupata nuru ya jua kila siku, ambayo “huchochea kutolewa kwa homoni zinazopambana na mshuko-moyo na mkazo.” Mwishowe, “zima wapigaji simu kwenye simu au mashine yako ya faksi. Acha mashine ya kujibia simu ijibu.”
King’ora cha Gari cha Mkesha-Mweusi
Mikesha-weusi wanasababisha tatizo lisilo la kawaida katika mji wa Guisborough wa North Yorkshire ya Uingereza—wanashtua watu kutoka kwenye usingizi wao wa mapema asubuhi kwa kuigiza ving’ora vya gari. “Wenye magari wanapokimbia nje kukabiliana na wezi, mara nyingi wao hupata mkesha-mweusi akiwa katikati ya wimbo,” laripoti The Times la London. “Alikuwa ameigiza kabisa namna na kadiri ya sauti,” akasema mkazi mmoja. “Tutatiwa kichaa sote.” Na hakutakuwa pumziko jingi. Kwa kuwa ndege mmoja hupitishia ndege mwingine wimbo mpya, sauti hiyo yaweza kuja kuwa ya kawaida sana. Kwa hakika, spishi 30 hivi kati ya spishi za Uingereza zaweza kuigiza sauti nyinginezo. Kwezi wa kawaida ndiye mwenye kipawa kuliko wote na aweza kuigiza miito ya ndege wengine. Mmoja alijulikana kuigiza mlio wa simu kwa njia ya kusadikisha sana hivi kwamba ilikuwa vigumu kutofautisha mwigo huo na mlio halisi wa simu.
Karamu ya Kipagani Bado Yapendwa Sana
Siku ya Mtakatifu Yohana Mbatizaji “haihusiani sana na mtakatifu huyo wa Katoliki kama mtu afikirivyo,” laripoti gazeti la Brazili Folha de S. Paulo. Ingawa karamu hiyo, “huangukia kwa sadfa kwenye siku ambayo yasemekana mtakatifu huyo alizaliwa, . . . mwadhimisho wenyewe huwa wa kilimo na kipagani.” Likijumlisha matokeo ya mwanthropolojia Câmara Cascudo, jarida hilo husema kwamba “madhehebu ya jua ya Kijerumani na Kiselti” yalisherehekea karamu hiyo wakati wa mavuno “ili kufukuza roho waovu wa ukosefu wa rutuba, tauni za nafaka, na ukame.” Miaka mingi baadaye, karamu hiyo ililetwa Brazili na Wareno. Sehemu moja ya karamu hiyo ambayo huendelea katika nchi fulani ni kuwashwa kwa mioto ya Mtakatifu Yohana. Zoea hili lilitoka wapi? “Desturi hiyo . . . yahusiana na ibada ya mungu-jua, akistahiwa ili asiende mbali sana na dunia ili kusiwe na kipupwe kibaya sana,” lasema gazeti hilo.