Kuutazama Ulimwengu
Mashine za Kuzuia UKIMWI
Halmashauri inayoshughulikia UKIMWI ya serikali ya Australia ilipewa mwelekezo itoe mapendekezo ya kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo. The Courier-Mail la Brisbane lilisema kwamba ilipendekezwa kwa dhati kwamba vijana wapate kwa urahisi zaidi njia za kujizuia na UKIMWI kwa kuwa, kama vile mwenyekiti Dakt. Charles Watson, alivyoeleza, wanafunzi wengi wa shule ya upili ni watendaji kingono. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kugawanywa kwa kondomu (nyuo au ala) kwa mashine zenye kuziuza katika shule za upili. Dakt. Watson haamini kwamba kupatikana kwa mashine hizo kutatia moyo wanafunzi wachanga kufanya ngono mapema zaidi. Hakuna mapendekezo yaliyotiwa ndani ya ripoti hiyo ya kujizuia kimaadili.
Helikopta za Kibinafsi?
Je! umepata kufadhaika ukingonjea katika milolongo ya magari mjini kwa saa nyingi? Je! umepata kufikiri jinsi inavyoweza kupendeza kuruka angani na kushuka chini katika mahali unapoenda? Namna gani kuhusu helikopta ya kibinafsi? Gazeti la Italia Il Messaggero linaripoti kwamba kutokezwa kwa helikopta ya kwanza yenye uzito mdogo sana ndiyo uvumbuzi wa karibuni zaidi katika shughuli ya urukaji wa ndege. Ina uzito wa kilogramu 230 tu, na ina mwendo wa kilometa 150 kwa saa. Itakugharimu dola 60,000 za U.S. kuinunua, na karibu dola 1 ya U.S. kuruka nayo kwa kilometa moja unusu. Ingawa ni ndogo kuliko helikopta kubwa, bado inaweza kuruka kwa umbali wa kwenda juu wa mita 4,000 na uwezo wa kwenda kilometa 330.
Kulalwa Kinguvu na Wanajeshi
Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2 maelfu ya wasichana na wanawake vijana walikamatwa katika nchi za Esia ya mashariki na majeshi ya Wajapan ili kutumikia askari vitani. Wakiitwa kwa tasifida (jina lisilo mwiko) “wanawake wa faraja,” wale ambao hawakufa kwa ugonjwa wa zinaa waliachwa wafe majeshi yaliporejea. Miaka hamsini baadaye mwanamume mmoja amejitokeza kukiri peupe kuhusika kwake na kuomba msamaha. Seiji Yoshida, wa miaka 78, “hawezi kuondolea mbali kumbukumbu la kupiga mateke watoto Wakorea wenye kung’ang’ania na kulia, huku watu wake wakiwaingiza mama zao wachanga ndani ya malori ili wakawe watumwa wa kingono kwa Jeshi la Kitaifa la Wajapani,” lasema Mainichi Daily News. Alipoulizwa jinsi alivyohisi wakati huo, gazeti hilo liliripoti Yoshida kuwa alijibu hivi: “Tulifuata tu maagizo. Kisaikolojia tulipungukiwa kabisa. Ilikuwa ni kazi tu. Wazo tofauti halikuwezekana. Sikuhisi kitu chochote. Nilikuwa mwenye shughuli, nilitamauka, nilizidiwa na mawazo.” Maofisa wa kijeshi wa mataifa mengi wamehakikisha kwamba askari wao waliandaliwa wanawake, ama kwa kutekwa ama wakiwa malaya wa kulipwa.
Muziki Wenye Kuumiza
“Punguza sauti ya huo muziki!” umekuwa ndio mlio wa wazazi wenye kusumbuliwa. Matineja wengi wanahisi hawawezi kufurahia muziki wao isipokuwa wahisi mpigo wao. Ingawa mara nyingi muziki wa sauti ya juu umefungamanishwa na kupoteza uwezo wa kusikia, ripoti ya hivi majuzi katika The Globe and Mail ya Toronto, Canada, ilieleza kwamba tatizo la kusikia kelele kwenye masikio (tinnitus) ni tokeo la kawaida pia. Tinnitus ni “kusikia sauti kama ya mlio wa kengele, mvumo, kishindo, au kama ile ya kuchatachata ndani ya kichwa, mara nyingi ikiathiri masikio yote mawili. Lakini [maelezo] hayo hayafafanui kikamili sauti hiyo,” gazeti hilo linasema. Unapoipata, “hupati tena amani kamili na utulivu” asema Elizabeth Eayrs, mratibu wa Shirika la Tinnitus la Canada. Hasa wale wanaoathiriwa ni wale wanaovaa vidude vya kusikizia masikioni wanaoongeza sauti ya juu sana hivi kwamba majirani wao waweza kuisikia. Uwezo wao wa kufurahia muziki au sauti nyingine yoyote mara nyingi huathirika vibaya katika miaka yao ya baadaye.
“Tulikuwa na Uvutano Mbaya Kwenu Watoto”
Watoto kutendwa vibaya? Si katika maana ya kawaida. Yaliyo juu ni maneno ya David Goerlitz, mwigizaji katika matangazo ya sigareti za Winston akiwa mkwea miamba ambaye angewasha sigareti huku akibembea kwenye genge. The Boston Globe laripoti kwamba Goerlitz na Wayne McLaren (walioigiza katika matangazo ya sigareti za aina ya Marlboro) wanatokea mbele ya vikundi vya watoto wa shule kuwasadikisha wasivute sigareti. “Tuliwafanya ninyi watoto mwamini kwamba ikiwa mngevuta sigareti, mgekuwa watu wa kiume” Goerlitz akaeleza. “Uhai wangu umefupizwa sana kwa sababu nilichagua kuvuta sigareti,” McLaren akaungama kwa huzuni, baada ya pafu lake moja kukosa kufanya kazi kwa ajili ya kansa.
Huduma ya Kwanza kwa Jino Lililong’olewa
Meno ambayo yameng’olewa yanaweza kurudishwa tena mahali payo hata siku kadhaa baada ya aksidenti, maadamu yanahifadhiwa vema,” laripoti gazeti la Ujerumani Frankfurter Allgemeine Zeitung. Sanduku la huduma ya kwanza limetokezwa ambamo jino lililong’olewa laweza kuwekwa. Sanduku hilo lina maji safi kabisa, pamoja na mchanganyiko wa vilishaji na viua-vijasumu, ambao huwekwa kando. Halafu vitu hivyo viwili vyaweza kuchanganywa pamoja kwa kubonyeza kidude. Kifaa hicho si ghali na chaweza kuwekwa bila kufanywa kuwa baridi kwa muda wa miaka mitatu hivi. Sanduku la huduma ya kwanza kama hilo laweza kuwa la manufaa hasa katika mahali ambapo aksidenti zinazohusisha meno hutokea mara kwa mara kwa kulinganisha, kama vile kwenye vidimbwi vya kuogelea, viwanja vya michezo, na shuleni.
Mkazo wa Likizo
Kubadili tabia fulani kwaweza kumnufaisha mtu aliye na mkazo kuliko kwenda likizo. Dakt. Sérgio Tufik, profesa wa Shule ya Utabibu ya São Paulo, Brazili alinukuliwa katika Veja akisema: “Mwendo wetu wa kibayolojia umefanyizwa kwenda kama saa. Badiliko lolote, hata liwe ni juma moja la ustarehe katika Karibea, laweza kuuchosha mwili.” Iwe kazi ni ngumu au la, ili kuepuka mkazo unaodhuru, yeye apendekeza hivi: “Ridhika na yale [u]nayofanya.” Badala ya kujaribu sikuzote kufanya jambo jingine ambalo laweza kuwa lenye kuleta mkazo kuliko kazi ya kila siku, daktari huyo adokeza: “Labda siri ni ‘kwenda likizoni’ kila siku. Yaani, zaidi ya kazi, kushiriki katika utendaji mbalimbali unaoleta uradhi.”
Upaji wa Damu Wenye Msiba
Watu zaidi ya elfu moja katika Ufaransa wameambukizwa UKIMWI kwa kutiwa damu mishipani. Kwa nini wawe na kiasi ambacho ni mara tano hadi kumi zaidi ya nchi nyinginezo za Ulaya ya magharibi? Le Monde laeleza kwamba wasimamizi wa magereza waliendelea kupokea upaji wa damu kutoka kwa wafungwa hadi 1985, miaka mitatu baada ya nchi jirani kukomesha zoea hilo. Ripoti hiyo ilisema zaidi kwamba upaji wa damu “ulikuwa zoea la muda mrefu ulioonwa kuwa ulisaidia kuwarekebisha tabia wafungwa. Kutoa damu kuna maana ya kukomboa, na tena kuliwapa wafungwa wenzi fursa . . . ya kunywa glasi ya divai, na kwa habari ya wazoevu wa dawa za kulevya, walipata msisimko baada ya kudungwa sindano.” Upaji wa damu pia ungeweza kusaidia wafungwa wapunguziwe muda wa kifungo chao.
Wonyesho wa Mitindo ya Mavazi Katika Kathedro
“Kukiwa na sauti za nyimbo za Kigregori, makofi mazito na kengele, katika hali ya karibu giza tititi, vivuli vya watawa saba wa kike vyatokea, vikiwa na majoho marefu yanayoficha nyuso zao. Kwa ghafula taa zawashwa, watawa hao waondoa majoho yao, [na] wanakuwa violezo vya mitindo.” Kwa maneno hayo, Jornal da Tarde laeleza wonyesho wa mitindo ya mavazi yaliyofanywa katika chumba cha siri cha Kathedro Kuu ya Porto Alegre, Brazili. Askofu mkuu aliyehudhuria alinukuliwa kuwa akisema: “Wakati wote nimefikiri kwamba mahali hapa papaswa kuwa jumba la matukio ya kisherehe na kijamii.” Ingawa wonyesho huo ulikusanya fedha za kusaidia wazoevu wa dawa za kulevya, askofu wa Novo Hamburgo hakubaliani na wazo hilo lote. Yeye alisema: “Njia inayotumiwa haiwezi kukubalika, hata ikiwa inatimiza matokeo yanayotakiwa.”
Tatizo Lenye Kuenea Sana la Utekaji Nyara
Kutekwa nyara kwa magari kwaweza kuwa ni tatizo la kimataifa, lakini katika Afrika Kusini “utekaji nyara wa magari umefikia kiasi chenye kuenea sana,” kulingana na Financial Mail la South Afrika. Unaweza kupunguzaje hatari ya kutekwa nyara kwa gari lako ikiwa unaishi mahali ambapo kuna tatizo hilo? Jaribu kubadilisha-badilisha zoea lako la kusafiri. Pitia njia tofauti, au uondoke mapema kidogo au baadaye kidogo. Acha milango na madirisha yakiwa yamefungwa. Usiwape watu lifti, na usisafiri peke yako, ikiwezekana. Kabla ya kusimama kwenye kizuizi cha barabarani, jiulize kama kinaonekana kuwa cha halali. Angalia kama kuna taa za manispaa, bendera, na uangalie mavazi ya wafanyakazi wa barabara. Ikiwa dereva anajikuta katika hali ya hatari, kanali wa polisi alishauri: “Likabidhi gari hilo ikiwa maisha yako yamo hatarini. Hakuna haja ya kuwa shujaa mfu.”
Wazazi Watendwa Vibaya Kimwili
Lile ambalo limeitwa “ogofyo lililofichwa la hasira ya utineja” juu ya wazazi linaongezeka katika Australia. Polisi na vikundi vinavyoshughulikia hali njema vinaripoti kwamba idadi ya matineja wanaopiga wazazi wao inaongezeka haraka katika nchi hiyo. Na ingawa mara nyingi wapigwao huwa akina mama, hata akina baba na babu na nyanya wameshambuliwa kikatili. Gazeti la Sydney Sunday Telegraph linamnukuu mkurugenzi wa shirika linaloshughulikia hali njema kuwa akisema: “Watu wanashangaa kusikia kwamba watoto wa umri mchanga kufikia miaka 10 wanaweza kuwa wenye jeuri—wakiwatisha mama zao na ndugu na dada zao wengine.” Shirika Linalohudumia Hali Njema ya Jumuiya limepokea simu nyingi sana kutoka kwa wazazi waliotendwa vibaya hivi kwamba linapanga programu ya pekee kwa ajili ya wapigwao na wakosaji.