Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 1/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nyumba za Hifadhi Zimo Hatarini
  • Hali ya Kindoto au Kifo?
  • Muziki na Uuaji wa Kukusudia
  • Utibabu Mwingineo
  • Bima ya Kanisa Dhidi ya Madai ya Kutenda Vibaya
  • Jinsi ya Kuwa Kasisi
  • Matatizo ya Moyo Miongoni mwa Wanawake Waarjentina
  • Mfadhaiko wa Akili Katika Nyumba ya Watawa?
  • Vita Vingali Vyaendelea
  • Barabara Yaitwa kwa Jina la Shahidi Mfia-Imani
  • Tatizo la Kusoma?
  • Mkutano Wenye Kutokeza Kuhusu Upasuaji Bila Damu Wafanywa Moscow
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Jilinde na Muziki Usiofaa!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 1/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Nyumba za Hifadhi Zimo Hatarini

Je! nyumba za hifadhi zimo katika hatari ya kutoweka? Katika Italia, taifa lililokirimiwa mojawapo urithi wa kitamaduni ulio mkubwa zaidi ulimwenguni, kiasi kilicho sawa na nyumba nzima ya hifadhi iliyojaa hazina za kisanii hutoweka kila mwaka. “Nyumba ya hifadhi ya Italia iliyo na vitu vingi zaidi ni ile usiyoweza kuona,” laripoti gazeti Il Messaggero. Katika 1992 pekee, karibu sanaa 35,000, zenye thamani ya zaidi ya lire bilioni 200 (dola milioni 123 za U.S.), ziliibwa katika nyumba za hifadhi, makanisa, taasisi za umma na za watu binafsi, na makao. Ni 1,971 pekee zilizopatikana. Kulingana na makadirio, kati ya 1970 na 1992, wastani wa sanaa 30,000 zimekuwa zikitoweka kila mwaka—hali ya dharura ya kitaifa, wasema wenye mamlaka. Ni nini hutukia kwa hazina hizo zote zilizoibwa? Yaripotiwa kwamba, nyingi zazo huishilia kwenye maficho ya siri ya wauzaji madawa ya kulevya na viongozi wa magenge ya uhalifu.

Hali ya Kindoto au Kifo?

Ingawa wafuasi wa Balak Brahmachari, wamejitoa kwa guru wao, yaonekana hawakupatwa na mtamauko mkubwa wakati madaktari walipojulisha kwamba amekufa, India Today laripoti. Wafuasi hao, waitwao Wasantani, walisisitiza kwamba madaktari walikosea na kwamba kiongozi wao wa miaka 73 alikuwa tu ameingia katika “hali ya kindoto ya kutafakari.” Waliomba kwamba yeye awekwe katika sehemu ya hospitali ya kutunzia wagonjwa mahututi. Madaktari walipokataa, Wasantani waliurudisha mwili kwenye ashramu yao, au makao ya dhehebu hilo, karibu Calcutta, na wakauweka uweze kuonwa katika kitanda cha barafu katika chumba kilichotiwa baridi. Wenye mamlaka wa manispaa ya mji walisisitiza kwamba mwili huo uchomwe ili kuzuia maambukizo yoyote, lakini Wasantani walikatalia mbali maombi hayo kuwa propaganda, wakitoa hoja kwamba mwili huo haukuonyesha “ishara yoyote ya kuoza.” Majuma yakapita. Hatimaye, wenye mamlaka walilazimika kuchukua hatua na kuiondolea mbali maiti hiyo.

Muziki na Uuaji wa Kukusudia

Huenda muziki ulikuwa na sehemu ya maana katika visa viwili vya uuaji kimakusudi katika Texas, U.S.A. Katika kisa kimoja, dereva wa miaka 19 alipiga risasi na kuua polisi aliyekuwa amemsimamisha katika njia kuu ili kumkabidhi shtaka la trafiki. Wakili wa kijana huyo hakudai tu kwamba kijana huyo alikuwa akisikiliza muziki wenye jeuri wa rapu alipomfyatua risasi ofisa huyo bali pia alidai kuwa kuzamishwa kwake kwa muda mrefu katika muziki wa aina hiyo ‘kulikuwa kumemchochea’ aue kimakusudi. Mahakimu waripotiwa kuwa walikubali kwamba muziki huo ulikuwa na fungu la maana katika vitendo vya kijana huyo. Lakini kulingana na wakili wa mashtaka katika kesi hiyo, “wao hawakuhisi kwamba muziki huo ulipunguza hali [yake] ya kulaumika kwa ajili ya uhalifu huo.” Kijana huyo alihukumiwa kifo. Katika kisa kama hicho, kijana mwenye miaka 15 aliyekiri kumpiga risasi na kumuua mama yake alidai kwamba wimbo wa kikundi cha Megadeth wenye mdundo mzito ulikuwa umempa maagizo kutoka kwa mashetani ili aweze kuua.

Utibabu Mwingineo

Wakitafuta kupunguza hatari ya wagonjwa wao kuambukizwa UKIMWI au mchochota-ini, madaktari katika Brazili wanatafuta njia nyingine isiyohusu mitio ya damu mishipani, laripoti gazeti O Estado de S. Paulo. Gazeti hilo lilieleza hivi zaidi: “Madaktari wa Brazili tayari hutumia njia nyinginezo za upasuaji kwa Mashahidi wa Yehova. Kwa kutumia erythropoietin—[homoni] itokezwayo na figo—wameweza kuongeza hesabu ya chembe nyekundu za damu kufikia kiwango cha kutosha, katika visa fulani, ili kuepuka kutia damu baada ya upasuaji.” Hivyo, baada ya kuwapasua Mashahidi 91, Dakt. Sergio A. de Oliveira wa Hospitali ya Hali-Njema ya Ureno, São Paulo, asema: “Twapata kwamba wagonjwa ambao ni Mashahidi wa Yehova waweza kupata upasuaji wa moyo bila damu au vitu vilivyofanyizwa kwa damu, kukiwa na usalama wa kutosha.”

Bima ya Kanisa Dhidi ya Madai ya Kutenda Vibaya

“Kanisa Katoliki la Australia limechukua bima ya mamilioni ya dola ili kujilinda dhidi ya madai ya kutenda vibaya kingono kunakofanywa na makasisi,” laripoti The Sunday Telegraph la Sydney, New South Wales. “Tunakubali kwamba kutenda vibaya kingono kwaendelea,” akasema askofu Mkatoliki katika Melbourne, Australia. Yeye adai kwamba bima hiyo kubwa hivyo ni jambo la kawaida “kwa shtaka la aina hiyo.” Kulingana na kikundi cha kutegemeza waliotendwa vibaya, kutenda vibaya kingono kwa makasisi kumeenea zaidi ya vile kanisa linavyokiri. Msemaji mmoja wa kikundi hicho alisema ya kuwa anaamini kwamba uangalifu wa kanisa umeelekezwa zaidi katika kulinda makasisi kuliko kusaidia watendwa vibaya. Yeye aliongeza kwamba ujumbe “ulio katika hati za bima za kanisa ni, usiseme kweli.”

Jinsi ya Kuwa Kasisi

“Sikuhizi vijana Wajapani wanaitwa ‘kizazi cha kitabu-mwongozo’ —wao husoma ‘vitabu vya jinsi ya kufanya mambo’ kabla ya kufanya lolote. Sasa makasisi watiwa ndani.” Ndivyo linavyoripoti gazeti la Tokyo The Daily Yomiuri. Ili kufundisha makasisi wachanga wa leo juu ya desturi na mapokeo ya kikasisi, Taasisi ya Kyoto ya Mafunzo ya Zen ilielekeza kwamba kitabu-mwongozo cha jinsi-ya-kuwa-kasisi kifanyizwe. Ilihali iliwabidi makasisi wa Zen wa kale wabaki bila kuoa na walisifiwa kwa ajili ya mazoezi yao makali, wengi leo hurithi tu kazi ya baba zao au za babu zao. Lakini gazeti hilo lasema kwamba mara nyingi akina baba hushindwa kufundisha wanao adabu zifaazo makasisi, na vijana wenyewe ni wenye shughuli mno wasiweze kujifunza desturi za Zen kwa sababu ya kujifunza kwa ajili ya mitihani ya chuo. Baadhi yao waripotiwa kuwa wapata kuwa vigumu kusoma sutras, au hotuba za Buddha.

Matatizo ya Moyo Miongoni mwa Wanawake Waarjentina

Tarakimu za hivi karibuni zaonyesha kwamba idadi ya maradhi ya moyo yapanda miongoni mwa wanawake wa umri wote katika Arjentina. Gazeti Clarín lilichapisha matokeo ya uchunguzi mmoja juu ya jambo hilo uliofanywa na Sociedad Arjentina de Cardiología (Shirika la Arjentina la Kardiolojia). Lilifanya uchunguzi wa sehemu 82 za wagonjwa mahututi na wagonjwa wa moyo 521 kotekote nchini. Ripoti hiyo yasema kwamba idadi ya wanawake waliolazwa katika hospitali za Arjentina kwa sababu ya maradhi ya moyo iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 56 katika muda unaopungua mwaka mmoja. Na ilihali katika 1991 ni asilimia 25 tu ya wagonjwa wa maradhi ya moyo waliokuwa wanawake, kwa wakati huu wao wawakilisha karibu asilimia 40. Mambo yenye kuchochea maradhi ya moyo yatia ndani msongo mkubwa wa damu, unene wa kupita kiasi, mafuta mengi kupita kiasi katika damu, ulevi, na utumizi wa tumbaku. Hata hivyo, uchunguzi huo haukupata uhusiano wa moja kwa moja kati ya umri na kadiri ya kufa kwa wagonjwa wa moyo.

Mfadhaiko wa Akili Katika Nyumba ya Watawa?

Mara nyingi nyumba za watawa wa kike na wa kiume hufikiriwa kuwa mahali pafaapo kwa ajili ya kutafakari. Hata hivyo, Bruno Giordani, kasisi anayefunza elimu ya akili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran katika Roma, ametokeza “uchanganuzi wenye kusikitisha” wa makao ya watawa wa kike na wa kiume, laripoti gazeti la Italia Corriere della Sera. Kulingana na ripoti yake, “watawa wengi wa kike waonekana kuwa wagonjwa” wa “hesabu kubwa ya matatizo mabaya ya akili.” Yeye aorodhesha tabia za “mtawa wa kike mwenye matatizo ya akili,” ambaye “hupatwa mara kwa mara na hisia za hatia za kimawazo au sivyo kutokuwa na hisia yote ya maadili.” Baadhi yao husumbuka kwa “upweke, kukosa kueleweka, na tabia za kujipenda kupita kiasi,” athibitisha Giordani. Basi si ajabu kwamba mkutano wa ulimwengu utakaofuata wa maaskofu wa Kikatoliki, utakaofanywa katika 1994, utashughulikia matatizo hususa yanayokabiliwa na makasisi.

Vita Vingali Vyaendelea

Ingawa matumizi ya gharama za kijeshi ulimwenguni pote yanapunguzwa, hesabu ya vita vinavyopiganwa haipungui. “Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) katika Swedeni ilirekodi mapigano makali 30 katika mwaka uliopita [1992],” laripoti gazeti la Ujerumani Nassauische Neue Presse. Kulingana na taasisi hiyo, hiyo ilikuwa hesabu sawa na ya 1991. Hata ingawa mapigano yalikwisha katika sehemu za vita, “Bosnia ilishuhudia mwanzo wa mapigano yenye umwagikaji mwingi zaidi wa damu, ambamo watu zaidi ya 100,000 waliuawa kufikia mwishoni mwa mwaka huo.” SIPRI yatabiri kwamba “hesabu ya makabiliano yanayozidi kuwa ya jeuri itapungua kidato kwa kidato tu.”

Barabara Yaitwa kwa Jina la Shahidi Mfia-Imani

Ulipowadia wakati wa kuipa jina barabara mpya katika mji mdogo wa Baltmannsweiler wa Ujerumani, Baraza la Jumuiya liliteua jina Bernhard Grimm. Kwa nini? Gazeti Esslinger Zeitung laripoti: “Grimm, aliyezaliwa katika 1923, aliishi katika Barabara ya 30 Reichenbacher. Akiwa Shahidi wa Yehova mwenye kuamini, alikataa kutumikia jeshini aliposajiliwa. Alifungwa mara hiyo na kupelekwa Berlin. Mahakama ya kijeshi ilimhukumu kifo kwa ‘kuvunja moyo majeshi.’ Mnamo Agosti 21, 1942, hukumu ya kifo ilitekelezwa dhidi yake akiwa mwenye miaka 19 katika Berlin-Plötzensee.” Kwa sababu ilikuwa miaka zaidi ya 50 tu tangu kijana huyo afie-imani, diwani wa jumuiya alifikiri kuwa wakati ufaao kuita barabara hiyo kwa jina lake.

Tatizo la Kusoma?

“Magazeti na nyusipepa zina wasomaji wachache zaidi,” lasema Gazeta Mercantil. Gazeti hilo la Brazili laripoti kwamba wajumbe katika Berlin, Ujerumani, waliohudhuria mkusanyiko wa 46 wa Muungano wa Kimataifa wa Wahariri wa Magazeti walihangaikia kuongezeka kwa hali ya “ukosefu wa upendezi katika kusoma vichapo na upendeleo wa [vyombo vya habari] vyenye sauti na picha.” Kwa maoni ya msimamizi wa Shirika la Waeneza Habari la Amerika, Alejandro Junco de la Vega, wengi “hawajui umaana wa vichapo . . . Wengi bado waamini kwamba televisheni ndiyo ifaayo zaidi.” Horácio Aguirre, mkurugenzi wa gazeti Las Americas katika Miami, atoa maoni ambayo bila shaka yashirikiwa na wanamagazeti wengi, kwamba gazeti “hutokeza picha iliyo kamili zaidi juu ya yale yanayotukia ulimwenguni.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki