Kuutazama Ulimwengu
Chakula cha Brazili Kinachotupwa
Kulingana na Wizara ya Kilimo ya Brazili, “nchi hiyo kila mwaka hutupa dola bilioni 2.34 (za Marekani) katika mchele, maharagwe, mahindi, soya, ngano, mboga, na matunda,” lasema O Estado de S. Paulo. “Ukihesabu hasara za mazao mengine [ya kilimo] na utumizi mbaya wa wanunuzi, hicho kiasi chajumlika kuwa dola bilioni 4 (za Marekani).” Lakini kwa nini asilimia 20 ya mapato ya kilimo na asilimia 30 ya mazao ya matunda hutupwa? Miongoni mwa sababu zilizotolewa ni ‘nafasi ndogo ya kuhifadhi mashambani, tekinolojia ya kutokeza mazao isiyotosha, ukosefu wa usalama kwenye barabara kuu, na usimamizi mbaya wa mimea.’ Akisikitikia ukosefu wa kanuni kudhibiti huo utupwaji, Benedito Rosa wa Wizara ya Kilimo anukuliwa akisema hivi: “Chakula hicho kinachotupwa kingeweza kulisha watu ambao wanakihitaji.”
Ugonjwa wa Jumatatu Asubuhi
“Ule mkazo wa kurudi kazini Jumatatu asubuhi huongeza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo kwa asilimia 33,” laripoti Jornal do Brasil. Uchunguzi wa Ujerumani wa visa 2,636 “ulifunua kwamba hatari ya kupatwa na kushindwa kwa moyo kutenda hutofautiana kulingana na siku na saa ya juma.” Hata hivyo, ilipatikana kwamba siku za Jumatatu hasa zilikuwa hatari na kwamba mshiko wa moyo una uelekeo wa mara tatu zaidi kutukia wakati wa asubuhi kuliko wakati uliosalia wa siku. Wafanyakazi wa viwandani wanaathiriwa zaidi na ugonjwa wa Jumatatu asubuhi kuliko wataalamu na wafanyakazi wa ofisini. “Twadadisi kwamba lile badiliko la utendaji zaidi, mara baada ya pumziko la mwisho-juma, husababisha mshiko [wa moyo],” akasema profesa Stefan Willich, aliyeelekeza huo utafiti. Ilidokezwa kwamba watu walio na tatizo la moyo wanapaswa kuanza kazi mwanzoni mwa juma katika njia ya utulivu.
“Taifa Linaloongoza Ulimwenguni Katika Kucheza Kamari”
“Japani imekuja kuwa taifa liongozalo ulimwenguni katika kucheza kamari,” lasema Asahi Evening News. Fedha zilizo nyingi (asilimia 65) zikichezwa kamari kwenye pachinko, kwa kutumia mashine zenye waya zichezazo mpira. Wajapani pia hutumia fedha zaidi kuliko taifa jinginelo kwenye mashindano ya farasi ya kwao. Mauzo katika 1992 yalikuwa zaidi ya maradufu yale ya Marekani na zaidi ya mara nne yale ya Hong Kong, Ufaransa, na Uingereza. Ili kuongeza mauzo, wanawake wachanga sasa wanalengwa shabaha. Alisema mwanamke mmoja mchanga kutoka Nagoya hivi: “Wazazi wangu hulalamika lakini sikuzote mimi huwaambia, ‘Serikali za kitaifa na za mitaa zinafanya mipango kwa ajili ya kucheza kamari. Zaweza kuwaje mbaya?’” Kwa hakika, sheria ya Kijapani hukataza kucheza kamari kwa maandishi, lakini kucheza kamari kwa hadharani huwapo kama “sheria iliyowekwa kutegemeza uchumi,” asema mtafiti Hiroshi Takeuchi. Yeye ahisi kwamba uchezaji kamari uendeleapo kupita asilimia 4 ya mazao ghafi ya taifa, huja kuwa tatizo la kijamii. Japani sasa yasimama kwenye asilimia 5.7.
Makanisa Yahisi Mkumbo wa Uhalifu
Hadi miaka ya majuzi, makanisa ya Australia kwa ujumla yaliachwa bila kutiwa kufuli, hata wakati hakukuwa na huduma zozote zilizokuwa zikifanywa. Lakini mambo yamebadilika sasa, laripoti gazeti la habari The Weekend Australian, kwa sababu ya uhalifu, kuvunja makanisa, uharabu kwenye majengo ya kanisa, na katika visa kadhaa kati ya hivyo mapadri wameshambuliwa. “Nyingi za parishi zetu sasa zinatia kufuli makanisa yazo, nahofia. Nadhani hilo lasikitisha sana,” akasema askofu mkuu wa Katoliki John Bathersby. “Nadhani kumekuwa na kudhoofika katika staha kwa ajili ya dini. Nafikiri kujiingiza katika ulimwengu kwa jamii nzima kwa kweli kumetokeza mazingira ambayo watu hawatambui Kanisa kuwa tofauti na vyuo vinginevyo vyote katika jamii, na hivyo basi hali ya staha ya kipekee kwalo imepotea. Watu wengine huona kanisa kama jengo jinginelo tu.”
Papa Mwenye Kubadilikana
Si kwamba tu Papa John Paul 2 ni kichwa cha kiroho cha Kanisa Katoliki la Roma bali pia ni mwanatamthilia, mtungaji vitabu, na stadi wa kurekodi. Kitabu chake cha hivi majuzi, Crossing the Threshold of Hope, kilikuwa katika orodha ya vitabu viuzwavyo sana kwa majuma mengi. Ile tamthilia, drama ya kimuziki iitwayo The Jeweler’s Shop, ilifunguliwa Desemba uliopita katika New York City kwa utumbuizo wa muda mfupi. Iliandikwa na papa katika 1960 chini ya jina Andrzej Jawien. “Papa alikuwa mwanatamthilia, mwigizaji, mwelekezi, mtafsiri na mchambua drama kwa ajili ya gazeti lenyeji katika Cracow,” akaeleza mtokezaji wa hiyo tamthilia. Pia kuna diski songamano iliyo maarufu yenye mrekodio wa papa akikariri Rozari. Na papa ni msafiri ajulikanaye sana wa ulimwenguni pote, akiwa na mipango ya kutembelea mabara matano mwaka huu. Safari yake ya 63, katika Januari ilifafanuliwa na The New York Times kuwa “jaribio la Papa mwenye umri wa miaka 74 kuumbua lile wazo la kwamba upapa unadidimia na kutokeza wazo kwamba wala afya yake wala umri wake hautamzuia kutoa maoni yake ya maadili katika shughuli za ulimwengu.”
Damu—“Dawa” Hatari
“Ingeweza kuwa kwamba Mashahidi wa Yehova wana haki kwa kukataa utiaji-damu mishipani?” likauliza Sunday Telegraph la Uingereza. Tisho la sasa la utiaji-damu hutia ndani damu iliyoambukizwa na virusi ya mchochota wa ini C na UKIMWI. “Lakini ambukizo ni moja tu ya idadi ya hatari ambazo zimepata kufafanuliwa katika majarida ya kitaalamu,” lasema Telegraph. “Machunguo kama lile moja ambalo lilikadiria uwezekano wa tendo-itikio la kupita kiasi kutokana na utiaji-damu kuwa wa juu kufikia asilimia 20 yajulikana kidogo mno kwa umma. Sawa na hayo ni machunguo yasiyojulikana na ambayo yamepata kwamba utiaji-damu ni kitangulio bora zaidi cha upataji-nafuu usio mzuri baada ya upasuaji wa fumbatio ama utumbompana.” Machunguo pia yaonyesha kwamba asilimia kubwa ya utiaji-damu mishipani hupendekezwa isivyo lazima na kwamba mazoea ya utiaji-damu hutofautiana sana na hutegemezwa zaidi na mazoea kuliko tarakimu za kisayansi. Akiita damu “dawa yenye nguvu sana” ambayo kwa hiyo “wapasuaji wengi waipendekeza zaidi,” Tom Lennard, mpasuaji wa kutoa mashauri kwenye Royal Victoria Infirmary, alisema hivi: “Ikiwa damu ilikuwa dawa mpya haingepata leseni ya kutumiwa.”
Linda Vitoto Vyako Kutokana na Kelele
“Kelele nyingi mno zaweza kuwa zenye kudhuru kwa vitoto ambavyo havijazaliwa bado na vilivyozaliwa majuzi,” ikasema idhaa ya habari ya Radio France Internationale. Kitoto katika tumbo la uzazi la mama yacho hasa kina uelekeo wa kudhuriwa na makelele yoyote ambayo yanampata mama yacho. Kwa sababu ukuta wa fumbatio la mama na umajimaji wa omnioni huandaa ulinzi mchache sana kutokana na makelele yatokayo nje, mtoto huenda alemae kabla ya kuzaliwa. Kwa kielelezo, ile hatari ya kupoteza usikiaji wa kasimawimbi za juu ni mara tatu zaidi miongoni mwa watoto ambao mama zao walipatwa na viwango vya kelele vya decibels kati ya 85 na 95—viwango ambavyo ni vya kawaida mno katika maonyesho ya roki na majumba ya disko. Zaidi ya kusababisha madhara ya kusikia, watafiti wengine waonya kwamba, kupatwa na makelele ya juu kwa ukawaida, hasa wakati wa mwezi wa mwisho wa mama kuwa mjamzito, kwaweza pia kuongeza kiwango cha mpigo wa moyo wa kitoto ambacho hakijazaliwa bado.
“Huduma ya Kwanza ya Kihisia-Moyo”
Huduma ya kwanza kwenye eneo la aksidenti yapasa kutia ndani zaidi ya uangalifu kwa majeraha ya kimwili. Watu waliojeruhiwa pia huhitaji msaada wa kihisia-moyo, laripoti gazeti la Kijerumani Süddeutsche Zeitung. Msaada wa aina gani? Shirika la Wataalamu wa Saikolojia la Ujerumani ladokeza hatua nne sahili kwa ajili ya kutoa “huduma ya kwanza ya kihisia-moyo.” Hayo madokezo yalikuwa matokeo ya mahojiano kati ya majeruhi wa aksidenti na wataalamu. Mapendekezo ni: “Sema kwamba uko pale. Mlinde mtu aliyejeruhiwa kutokana na visumbuaji. Wasiliana naye kwa mguso. Sema na usikilize.” Jitihada zinafanywa ili kuhakikisha hizo hatua zimekuzwa kupitia madaktari na taaluma za uendeshaji magari na kuhakikisha zitatiwa ndani ya taaluma za huduma ya kwanza.
“‘Hayawani Wadogo wa Mizigo’ wa India”
Hivyo ndivyo ripoti ya Times of India iliita watoto milioni 17 hadi milioni 44 wafanyao kazi sugu. Licha ya kuwako kwa watu wazima wapatao milioni 23 wenye nguvu na wasioajiriwa, wenye viwanda mara nyingi huchagua kuajiri watoto, ambao hufanya kazi bila kugoma kwa nusu ya mshahara wa mtu mzima na mara haba mno wao hunung’unika kuhusu hatari za kiafya kazini mwao. Ilikuwa tu baadhi ya mataifa ya Magharibi yalipokataa bidhaa za kuingizwa kutoka nje zilizotokezwa na watoto kwamba baadhi ya watokezaji walibadilisha watoto na watu wazima. Serikali ya India imeahidi kuweka sheria thabiti zaidi ili kuzuia kutendwa vibaya kwa aina hiyo na kulazimisha wazazi kuwapa watoto wao elimu ya msingi. Akasema Rais wa India, Dakt. Shankar Dayal Sharma: “Wala mahitaji ya kitamaduni wala ya kiuchumi hayawezi kutetea kufanya kazi kwa mtoto na kuondoa dhuluma kama hiyo ni moja ya magumu makubwa leo.” Hata hivyo, wengi hutetea hilo zoea juu ya msingi wa kwamba umaskini kabisa ni “uhalisi mkali” na kwamba mishahara ipatwayo na mtoto hutoa utegemezo unaohitajiwa mno kwa familia.