Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/22 kur. 20-24
  • Somo Kutokana na Chungu cha Mafuta

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Somo Kutokana na Chungu cha Mafuta
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Urithi wa Kiyahudi
  • Umiliki wa Nazi
  • Kuondoka kwa Wingi na kwa Hofu
  • Maisha Tukiwa Wakimbizi
  • Chaguo la Familia Yetu la Dini
  • Huduma Katika Nchi Mpya
  • Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu
    Amkeni!—1993
  • Ninaweza Kumlipa Yehova Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Nilichochewa na Uaminifu-Mshikamanifu wa Familia Yangu kwa Mungu
    Amkeni!—1998
  • “Jinsi Inavyotamanika Imani Isiyofifia”!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/22 kur. 20-24

Somo Kutokana na Chungu cha Mafuta

Maogofyo ya vita ndiyo baadhi ya kumbukumbu zangu za mapema zaidi, hasa zile za kutoroka ili kuokoa uhai wetu mwisho-mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, nilipokuwa na umri wa miaka minne tu. Familia yetu ya watu saba ilikuwa ikiishi Prussia Mashariki, ambayo wakati huo ilikuwa sehemu ya Ujerumani.

NILIKODOLEA macho giza lenye kutia hofu, nikisikiliza kikosi chenye kukaribia cha Warusi chenye kurusha mabomu. Ghafula, mimweko mikali sana na milipuko mikubwa sana iliwasha moto matangi ya kuhifadhia mafuta umbali wa meta mia kadhaa. Gari-moshi tulimokuwa ndani yake lilitikisika juu ya reli, watu wakapiga mayowe. Lakini muda si muda hao warusha-mabomu wakaondoka, na safari yetu ikaendelea.

Katika pindi nyingine niliamka kutoka usingizi wa vipindi-vipindi na kumwona mwanamke mwenye kupiga mayowe akijaribu kutoka nje ya behewa la kubebea ng’ombe tulimokuwa. Baba alimzuia na kumvuta ndani. Mwanamke huyo alikuwa ameshikwa na usingizi karibu na mlango, mtoto wake akiwa mikononi mwake. Alipoamka, aligundua kwamba mtoto huyo aliganda hadi akafa. Kisha wanaume wakautupa mzoga barafuni, na kwa sababu ya kushindwa na huzuni, mama huyo alikuwa akijaribu kufungua mlango ili aruke nje afe huko na mtoto wake.

Ili kupambana na baridi kali, jiko lenye kitako cha mviringo lilikuwa limewekwa katikati ya behewa letu la kubebea ng’ombe. Ugavi mchache wa kuni mwishoni mmoja wa behewa ulitumiwa kidogo-kidogo sana ili kupikia viazi. Magunia ya viazi pia yalitumika yakiwa vitanda vyetu, kwa kuwa kulala juu yake kuliandaa kinga dhidi ya mbao zilizoganda za sakafu ya behewa.

Kwa nini tulikuwa tukitoroka kuokoa uhai wetu? Familia yetu ilisalimikaje miezi mingi ikiwa watoro? Acheni niwaeleze.

Urithi wa Kiyahudi

Nilizaliwa Desemba 22, 1940—nikiwa kitinda-mimba kati ya watoto watano—katika Lyck, Prussia Mashariki (sasa Elk, Poland). Mnyanyaso wa kidini ulilazimisha wazazi wangu wa kale walio Wayahudi kuondoka Ujerumani mwishoni mwa miaka ya 1700. Walihamia Urusi katika mojawapo ya uhamiaji wa watu wengi sana katika historia. Kisha, katika 1917, ili kutoroka mnyanyaso wa wapinga-Wayahudi katika Urusi wakati huo, babu yangu Myahudi alihamia Prussia Mashariki kutoka kijiji chake karibu na Mto Volga.

Babu alipata uraia wa Ujerumani, na Prussia Mashariki palionekana kuwa mahali salama. Wale waliokuwa na majina ya kwanza ya Kiyahudi walichukua majina ya Kiarya. Hivyo, baba yangu, Friedrich Salomon, akaja kuitwa Fritz. Mama naye alikuwa Mprussia. Yeye na baba, ambaye alikuwa mwanamuziki, walioana katika 1929.

Maisha ya wazazi wangu yalionekana kuwa yenye furaha kamili na yenye matumaini. Nyanya Fredericke na nyanya-mkuu Wilhelmine (upande wa mama) walikuwa na shamba kubwa, ambalo lilikuja kuwa makao ya pili kwa wazazi wangu na sisi watoto. Muziki ulikuwa na sehemu kubwa katika maisha ya familia yetu. Mama alipiga ngoma katika bendi ya dansi ya baba.

Umiliki wa Nazi

Katika 1939, hali yenye kutisha ya kisiasa ilianza kuonekana. Lililoitwa eti suluhisho la mwisho la Adolf Hitler kwa tatizo la Wayahudi lilianza kuwahangaisha wazazi wangu. Sisi watoto hatukujua kuhusu urithi wetu wa Kiyahudi, nasi hatukujua hadi kifo cha mama katika 1978—miaka tisa baada ya baba kufa.

Ili mtu yeyote asimshuku kwamba alikuwa Myahudi, baba alijiunga na Jeshi la Ujerumani. Mwanzoni, alitumika katika kikosi cha muziki. Hata hivyo, mtu fulani ambaye yaelekea alijua kuhusu malezi yake alisema kwamba alikuwa Myahudi, kwa hiyo familia yetu yote ikahojiwa na kupigwa picha. Wataalamu wa Nazi walijaribu kupambanua kama sura zetu zilionekana kama za Kiyahudi. Ni lazima tulionekana vya kutosha kama Waarya kwao, kwa hiyo kwa uzuri, hatukukamatwa au kutiwa gerezani.

Ujerumani iliposhambulia Poland Septemba 1, 1939, hofu ilianza kujaa eneo letu ambalo hapo mwanzo lilikuwa lenye amani. Mama alitaka kuhama mara hiyo hadi mahali salama, lakini familia ililazimishwa na maofisa wa Nazi isifanye hivyo. Kisha, majeshi ya Urusi yalipokuwa yakisonga kuelekea Prussia Mashariki wakati wa kiangazi cha 1944, Wajerumani waliazimia kuondosha watu Lyck na maeneo yaliyo karibu. Siku moja katika Julai, tulipewa muda wa saa sita tu kuondoka nyumbani.

Kuondoka kwa Wingi na kwa Hofu

Mama alikuwa katika hali ya mshtuko. Tuchukue nini? Twende wapi? Tusafirije? Tungepata kurudi tena? Kila familia ingeweza kuchukua vitu vichache sana. Mama kwa hekima alichagua vitu vya msingi—kutia ndani chungu cha mafuta ya nyama ya ng’ombe pamoja na vipande vya bekoni—vya kutosha tu sisi kubeba bila kuchosha. Familia nyinginezo zilichagua kuchukua mali zao za kimwili zenye thamani.

Katika Oktoba 22, 1944, vikosi vya Urusi viliingia Prussia Mashariki. Mwandikaji mmoja aliandika hivi: “Halikuwa jambo la kushangaza kwamba askari-jeshi Warusi ambao walikuwa wameona familia zao wenyewe zikichinjwa-chinjwa na makao yao wenyewe na mimea ikichomwa kutaka kulipiza kisasi.” Uharibifu huo ulishtua Prussia Mashariki yote, na watu wakatoroka kwa hofu.

Wakati huo tulikuwa wakimbizi, tukiishi mbali upande wa magharibi katika Prussia Mashariki. Njia pekee ya kutorokea sasa ilikuwa kupitia Bahari ya Baltiki, kwa hiyo watu walitorokea bandari ya Danzig (sasa Gdansk, Poland). Huko, meli zilishurutishwa zitumike katika shughuli za dharura za uokoaji. Familia yetu ilikosa gari-moshi ambalo lingetupeleka kuingia meli ya abiria ya Ujerumani Wilhelm Gustloff, ambayo iliabiri kutoka Gdynia, karibu na Danzig, Januari 30, 1945. Tulipata kujua baadaye kwamba makombora ya Urusi yalizamisha meli hiyo na kwamba abiria wapatao 8,000 walikufa katika maji hayo ya barafu.

Njia ya kutorokea baharini ikiwa imefungwa, tulielekea magharibi. Alipokuwa katika likizo ya muda kutoka jeshini, baba alijiunga nasi kwa sehemu ya safari katika gari-moshi, kama ilivyofafanuliwa katika utangulizi. Baada ya muda mfupi alilazimika kurudi kwenye utumishi wa kijeshi, nasi tukaendelea na safari hiyo ndefu na yenye hatari tukiwa peke yetu. Mama alilinda chungu hicho cha mafuta, akiyagawa kidogo-kidogo kwa wakati mmoja. Yaliongezea vipande vyovyote vya chakula tulivyopata njiani, yakitusaidia kuendelea kuwa hai wakati wa majira marefu ya baridi kali. Chungu hicho cha mafuta kilithibitika kuwa chenye thamani zaidi ya dhahabu au fedha yoyote!

Hatimaye, tulifika kwenye mji wa Stargard, ambapo askari-jeshi Wajerumani na shirika la Msalaba Mwekundu walikuwa wametengeneza mahali pa supu karibu na kituo cha gari-moshi. Kwa mtoto mwenye njaa sana, supu hiyo ilikuwa yenye kupendeza sana. Baada ya muda, tulifika Hamburg, Ujerumani, tukiwa na njaa na kuchoka, lakini wenye shukrani kuwa hai. Tuliwekwa katika shamba moja karibu na mto Elbe, pamoja na wafungwa wa vita Warusi na Wapoland. Hali yetu ilikuwa mbaya sana, vita katika Ulaya ilipomalizika Mei 8, 1945.

Maisha Tukiwa Wakimbizi

Baba alikuwa amekamatwa na Wamarekani, nao walimtendea vizuri, hasa walipojua kwamba alikuwa mwanamuziki. Walitumia stadi zake za muziki katika sherehe zao za Siku ya Uhuru. Muda mfupi baada ya hapo, alifaulu kutoroka na kusafiri hadi Hamburg, ambapo tuliungana tena kwa furaha. Tulikaa katika nyumba ndogo, na baada ya muda mfupi nyanya zetu wakafika salama na wakaweza kujiunga nasi.

Hata hivyo, baadaye, wakazi wenyeji, kutia ndani Kanisa la Kilutheri letu wenyewe, walianza kuchukia wakimbizi wengi. Jioni moja mhudumu alizuru familia yetu. Ilionekana kwamba alisababisha udhia kimakusudi kwa kusema maneno ya kutukana kuhusu hali ya chini ya wakimbizi. Baba, aliyekuwa mwenye mwili kakawana, alikasirishwa na kumshambulia mhubiri huyo. Mama yetu na nyanya zetu walimzuia baba. Lakini alimnyanyua juu-juu kasisi huyo, akambeba hadi mlangoni na kumsukuma nje. Kuanzia wakati huo na kuendelea baba alikataza mazungumzo yoyote ya dini katika nyumba yake.

Muda mfupi baada ya tukio hilo, baba alipata kazi katika reli ya Ujerumani nasi tukahamia viunga vya Hamburg, ambapo tuliishi katika behewa lisilotumiwa. Baadaye, baba alitujengea nyumba nzuri. Lakini chuki dhidi ya wakimbizi iliendelea, na nikiwa mtoto mdogo, nilikuja kuwa shabaha ya kutendwa vibaya kwingi kwa kimwili na kihisia-moyo na watoto wenyeji.

Chaguo la Familia Yetu la Dini

Nikiwa mtoto, nililala katika chumba kimoja na nyanya zangu wawili. Japo amri za baba, alipokuwa hayuko, nyanya wote wawili mara nyingi waliongea nami kuhusu Mungu, wakaimba nyimbo, na kusoma Biblia zao. Upendezi wangu wa kiroho ukaamshwa. Kwa hiyo, nilipokuwa na umri wa miaka kumi, nilianza kutembea kilometa 11 hivi kwenda na kilometa 11 kurudi ili kuhudhuria kanisa Jumapili. Ingawa hivyo, ni lazima niseme kwamba nilikatishwa tamaa wakati maswali mengi niliyouliza hayakujibiwa kiasi cha kuniridhisha.

Kisha, katika kiangazi cha 1951, mwanamume aliyevalia kwa unadhifu alibisha mlango wetu na kumpa mama nakala ya gazeti la Mnara wa Mlinzi. “Mnara wa Mlinzi hutoa ufahamu wenye kina katika Ufalme wa Mungu,” akasema. Moyo wangu ulifurahi kwa kuwa hicho ndicho nilichotamani. Mama alikataa kwa upole, bila shaka kwa sababu ya upinzani wa baba dhidi ya dini. Hata hivyo, nilimsihi sana hivi kwamba alikubali na kunichukulia nakala moja. Wakati fulani baadaye, Ernest Hibbing alirudi na kuacha kitabu “Let God Be True.”

Karibu na wakati huo, baba alipata aksidenti kazini na kuvunjika mguu. Hilo lilimaanisha kwamba hangeweza kutoka nyumbani, jambo ambalo lilimkasirisha sana. Ingawa mguu wake uliwekwa plasta, aliweza kuchechemea hapa na pale. Tulishangaa kwamba alikuwa akitoweka mchana, akirudi tu wakati wa chakula. Hilo liliendelea kwa juma zima. Niligundua kwamba wakati wowote baba alipotoweka, kitabu changu kilitoweka pia. Kisha, wakati mmoja wa chakula baba akaniambia: “Mtu yule akija tena, nataka kumwona!”

Ndugu Hibbing aliporudi, kwa mshangao wetu baba alikipigisha kile kitabu mezani na kusema: “Kitabu hiki ndicho kweli!” Mara moja funzo la Biblia lilianzishwa, na baadaye washiriki wengine wa familia walijiunga na funzo hilo. Ndugu Hibbing akaja kuwa mshauri mwenye kutumainika na rafiki yangu wa kweli. Baada ya muda mfupi nilifukuzwa kutoka shule ya Jumapili kwa sababu ya kujaribu kushiriki itikadi zangu mpya. Kwa hiyo nilijiuzulu kutoka Kanisa la Kilutheri.

Katika Julai 1952, nilianza kushiriki na rafiki yangu mpendwa katika kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu kutoka nyumba hadi nyumba. Kila Jumapili, Ndugu Hibbing alikuwa akinishauri nisikilize kwa uangalifu jinsi alivyotoa ujumbe kwa wenye nyumba. Baada ya majuma machache, alinionyesha jengo kubwa na kusema: “Zote hizo ni zako uzifanyie kazi peke yako.” Baada ya muda, nilishinda wasiwasi wangu nikawa na mafanikio katika kuzungumza na watu na kuwaangushia fasihi za Biblia.

Baada ya muda mfupi, nilistahili kubatizwa katika ufananisho wa wakfu wangu kwa Yehova. Mimi na baba tulibatizwa Machi 29, 1953, na baadaye mwaka huo mama pia akabatizwa. Hatimaye, washiriki wote wa familia yetu walibatizwa, kutia ndani dada yangu Erika; ndugu zangu Heinz, Herbert, na Werner; na nyanya zetu wapendwa, ambao kufikia wakati huo walikuwa katika miaka yao ya 80. Kisha, katika Januari 1959, nikawa painia, kama wahudumu wa wakati wote waitwavyo.

Huduma Katika Nchi Mpya

Sikuzote baba alikuwa amenisihi niondoke Ujerumani, na kwa kuwazia naamini kwamba hiyo ilikuwa kwa sababu ya hofu zake zenye kuendelea juu ya uhasama kuelekea Wayahudi. Nilijaza maombi ya kuhamia Australia, nikitumaini kwamba hili lingekuwa hatua ya kunisaidia kutumikia nikiwa mishonari katika Papua New Guinea au katika kisiwa kinginecho cha Pasifiki. Ndugu yangu Werner nami tulifika pamoja katika Melbourne, Australia, Julai 21, 1959.

Kwa muda wa majuma machache, nilikutana na Melva Peters, ambaye alikuwa akitumikia akiwa mhudumu wa wakati wote katika Kutaniko la Footscray, nasi tukaoana katika 1960. Tulibarikiwa kupata mabinti wawili, ambao pia walikuja kumpenda Yehova Mungu na kuweka maisha zao wakfu kwake. Tumejaribu sana kufanya maisha yetu yawe sahili ili tukiwa familia tuweze kufuatia kikamili zaidi miradi ya kiroho. Kwa miaka mingi, hadi matatizo ya kiafya yalipomzuia kuendelea, Melva alitumikia akiwa painia. Kwa sasa mimi ni mzee na painia katika Kutaniko la Belconnen, katika jiji la Canberra.

Kutokana na maono yangu ya mapema utotoni, nimejifunza kuwa mwenye furaha na kuridhika na maandalizi ya Yehova. Kama ilivyotolewa kielezi na chungu cha mama cha mafuta, nimekuja kuthamini kwamba kusalimika hutegemea, si dhahabu wala fedha, bali vitu vya msingi vya kimwili na zaidi, funzo la Neno la Mungu, Biblia, na kutumia yale linayofundisha.—Mathayo 4:4.

Maneno yenye maana sana ya mama ya Yesu, Maria, hakika ni ya kweli: “[Yehova] ameshibisha kabisa wenye njaa kwa vitu vyema na wale waliokuwa na mali amewaacha waende bila kitu.” (Luka 1:53) Kwa kufurahisha, naweza kuhesabu washiriki 47 wa familia ambao wanatembea katika njia ya kweli ya Biblia, kutia ndani wajukuu saba. (3 Yohana 4) Kwa yote haya, na vilevile watoto na wajukuu wetu wengi wa kiroho, Melva nami twatazamia wakati ujao mzuri ajabu katika usalama chini ya utunzi mwanana wa Yehova na muungano mkuu pamoja na wapendwa wetu wengine watakapofufuliwa.—Kama ilivyosimuliwa na Kurt Hahn.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Vikosi vya Urusi vikisonga kuingia Prussia Mashariki, katika 1944

[Hisani]

Sovfoto

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ndugu yangu Heinz, dada yangu Erika, mama, ndugu zangu Herbert na Werner, na mimi mbele

[Picha katika ukurasa wa 24]

Nikiwa na mke wangu, Melva

[Picha katika ukurasa wa 24]

Chungu kama hiki, kikiwa kimejaa mafuta, kilitutegemeza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki