Unamna-Namna wa Mimea Watoweka—Kwa Sababu Gani?
KATIKA China, karibu unamna-namna 10,000 wa ngano ulilimwa katika 1949. Hata hivyo, kufikia miaka ya 1970, ni 1,000 pekee uliokuwa ukitumika. Katika Marekani, kati ya unamna-namna 7,098 wa matofaa uliotumiwa kati ya mwaka wa 1804 na 1904, karibu asilimia 86 umepotezwa. Kwa kuongezea, kulingana na Report on the State of the World’s Plant Genetic Resources for Food and Agriculture, “asilimia 95 ya kabichi, asilimia 91 ya mahindi yanayokua shambani, asilimia 94 ya dengu, na asilimia 81 ya namna nyingi za nyanya zaonekana kuwa haziko tena.” Takwimu zinazofanana na hizo zinaripotiwa katika nchi zote za ulimwengu. Kwa sababu gani kuna huo upungufu wa ghafula? Wengine wanasema kwamba kisababishi kikuu ni kuenea kwa kilimo cha kibiashara cha kisasa na kuachwa kutumiwa baadaye kwa mashamba madogo, ambako kumetokeza kupotezwa kwa unamna-namna wenye kubadilika wa mazao ya kidesturi.
Kupotezwa kwa unamna-namna wa mimea kwaweza kuongezea kutofaulu katika mazao. Kwa kielelezo, fikiria njaa kuu ya viazi ya Ireland mwaka wa 1845 hadi 1849, wakati ambapo watu wapatao 750,000 walikufa kwa sababu ya kukosa chakula wakati maradhi ya mimea yalipoharibu mazao mengi ya viazi. Ni nini kilichokuwa kisababishi cha kibiolojia cha msiba huu? “Usawa katika jeni,” yasema ripoti moja ya Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya benki za jeni 1,000 zilijengwa ulimwenguni pote katika miaka ya 1970 na 1980 ili kukusanya na kuhifadhi rasilimali za jeni za mimea. Lakini benki kadhaa za jeni zinafifia haraka, na baadhi ya benki hizo zimefungwa tayari. Yaripotiwa kuwa, kwa sasa ni karibu nchi 30 pekee zilizo na vifaa vifaavyo kwa ajili ya kuhifadhi kwa usalama na kwa muda mrefu mbegu za mimea.
Biblia huahidi kwamba chini ya utawala wa Ufalme wa Kristo, Yehova ‘atawafanyia mataifa yote karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.’ (Isaya 25:6) Jinsi tunavyoweza kuwa wenye shukrani kwamba Yehova Mungu, ‘apaye kila chenye uhai chakula’ na Muumba wa jeni tofauti-tofauti, atatosheleza mahitaji yote ya mwanadamu ya chakula!—Zaburi 136:25; Mwanzo 1:29.