Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wahamiaji Wajasiria Kifo
  • Hali Mbaya ya Watoto Wanaoishi Katika Maeneo ya Vita
  • Wanyama “Wapya” Wagunduliwa
  • Dini Yalazimika Kufanya Maamuzi
  • Je, Milenia Imeisha Tayari?
  • Sasa Paka Watiwa Ndani
  • “Mlipuko wa Ugonjwa wa Unene wa kupita Kiasi”
  • Ujitoaji Ulioelekezwa Vibaya?
  • Kupata Faida Kutokana na Uraibu
  • Watoto Wanene Kupita Kiasi—Suluhisho ni Nini?
    Amkeni!—2009
  • Je, Kunenepa Kupita Kiasi Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote?
    Amkeni!—2003
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Je, Kunenepa Kupita Kiasi ni Tatizo?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Wahamiaji Wajasiria Kifo

Kila mwaka maelfu ya wahamiaji haramu huhatarisha uhai wao katika kutafuta kazi za kuajiriwa na kiwango cha maisha kilicho bora katika Afrika Kusini. Yasemekana kwamba mamia ya wahamiaji haramu wameliwa na mamba wakiogelea kuvuka Mto Limpopo. Wengine hukanyagwa-kanyagwa na tembo au kuuawa na simba wanapovuka kwa miguu Mbuga ya Kitaifa ya Kruger. Hivi karibuni maofisa wa mbuga waliwapiga risasi simba watano ambao waligeuka kuwa wala-watu. “Uchunguzi wa maiti ya simba hao watano,” laripoti gazeti la habari la Johannesburg The Star, “ulifunua mabaki ya binadamu ndani ya mifumo ya umeng’enyaji ya wanyama hao.” Idadi barabara ya wahamiaji haramu wanaouawa na wanyama wa mwitu haijulikani. “Doria za kawaida zimepata alama za binadamu ambazo hupotea kabisa, bila kuacha dalili,” lasema hilo gazeti la habari. “[Simba] wa kiume aliyekomaa anaweza kula kilo 70 za nyama kwa wakati mmoja. Uwezekano wa kuonekana kwa mabaki ya binadamu ili yawe ushuhuda ni kidogo sana, hasa wakati fisi na mbweha wanapowasili mahali ambapo simba ameua windo.”

Hali Mbaya ya Watoto Wanaoishi Katika Maeneo ya Vita

Mashirika ya Terre des Hommes hushughulikia watoto walio na uhitaji. Kulingana na Petra Boxler, kinara wa shirika hilo katika Ujerumani, “karibu watoto milioni mbili wamepoteza uhai wao katika miaka kumi iliyopita katika vita, mapigano madogo-madogo, na mapigano ya mitaani.” Zaidi ya hilo, laripoti Süddeutsche Zeitung, watoto wengine milioni sita wameteseka kutokana na majeraha mabaya ya mwili, na milioni kumi wana mfadhaiko mkubwa wa kihisia-moyo. Boxler aomboleza kwamba kwa watoto, hivi karibuni vita vimekuwa kitu kibaya zaidi. Katika nchi fulani watoto wanazoezwa kwa nguvu kuwa wauaji, na katika nchi nyinginezo “wanatumiwa kutafuta mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi.”

Wanyama “Wapya” Wagunduliwa

“Miongo michache tu iliyopita, maarifa ya kawaida yalionyesha ya kwamba wengi wa mamalia wa ulimwengu—viumbe wenye manyoya, wenye damu moto, watoao maziwa—tayari walijulikana. Hili si kweli tena,” lasema U.S.News & World Report. “Kati ya matoleo ya 1983 na 1993 ya Mammal Species of the World, wanyama 459 waliongezwa. Katika miaka minne iliyopita, wanabiolojia wamegundua wengi zaidi—wanyama-wagugunaji, popo, mbawala, paa, ng’ombe-mwitu, na hata tumbili.” Inatabiriwa kuwa zile spishi 4,600 zinazojulikana sasa zitaongezeka zifikie karibu 8,000. Baadhi ya ‘mavumbuzi’ ya “mamalia hufanywa katika majumba ya makumbusho, wakati wanasayansi wafanyapo utafiti kwa makini zaidi kwenye violezo vilivyokusanywa miaka iliyopita.” Kwa kuongezea, “spishi nyingi mpya hutegemeza jumuiya ya vimelea na viumbe vingine vidogo mno ambavyo havijapata kuonwa na sayansi,” makala hiyo yataarifu, na “1 kati ya mamalia 3 waliofafanuliwa upya ni mnyama ambaye hajapata kuonwa kamwe na mwanasayansi.” Mavumbuzi mengi mapya zaidi yanafanywa katika misitu ya kitropiki na maeneo mengine yaliyojitenga ya ulimwengu. Mstadi wa mamalia George Schaller asema: “Ninashangaa kuona watu wakisisimuka kupita kiasi kuhusu kuwezekana kuwapo kwa bakteria huko Mihiri wakati ambapo sayari yetu imejaa spishi zisizogunduliwa.”

Dini Yalazimika Kufanya Maamuzi

“Tunapokaribia mwisho wa karne hii na mwisho wa milenia hii, kuna hisi ya kwamba milenia si mwanzo wa ufananisho tu, kwamba kuna badiliko maalumu linalotukia,” akasema Konrad Raiser, katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. “Tatizo ni kwamba hatuelewi kabisa jinsi badiliko hili litakavyotuathiri. Kwa hiyo tunazuiwa kwa njia fulani kupanga vizuri hatua ya badiliko hili badala ya ku[li]kubali tu na kuitikia.” Dakt. Raiser aliorodhesha “wingi wa dini” kuwa suala la kukabiliwa. Alinukuliwa na ENI Bulletin akisema kwamba Jumuiya ya Wakristo “bado inachangia kwa sehemu kubwa tatizo hilo badala ya kutokeza suluhisho.” Aliongezea: “Bado hatujasitawisha njia ambazo mtu na mwenzake wanaweza kuishi kama majirani bila kuendelea kuona mwingine, yule ambaye ana masadikisho na mazoea ya kidini yaliyo tofauti na yetu, kuwa tisho badala ya . . . chanzo kiwezacho kufaidi.”

Je, Milenia Imeisha Tayari?

Kulingana na wasomi, “kwa kweli milenia iliisha miaka kadhaa iliyopita. Pole sana, lakini sote tulikosa kuifahamu,” lataarifu gazeti Newsweek. Sababu? Kalenda yetu “inategemea mgawanyo tuliochagua wa wakati,” unaosemekana unategemea kuzaliwa kwa Kristo. Lakini, makala hiyo yasema, wasomi wa kisasa huitikadi kwamba kwa kweli Yesu alizaliwa miaka kadhaa “kabla ya Kristo.” Kulingana na Newsweek, hilo “lamaanisha kwamba tayari tuko katika milenia ya tatu.” Kosa lilifanywa na Dionysius Mfupi, ambaye, katika 525 W.K., aliagizwa na Papa John wa Kwanza atengeneze kalenda ya kawaida ya kanisa. Dionysius aliamua kutumia kuzaliwa kwa Yesu kuwa tarehe ya msingi lakini akakosea katika kupiga hesabu. “Kwa kweli wanahistoria hawatapata kujua kamwe wakati barabara ambapo Yesu alizaliwa,” lasema Newsweek. “Hata tarehe ya Krismasi, ambayo husherehekea kuzaliwa kwake, imechaguliwa tu. Wasomi wanaamini kwamba, kanisa liliteua Desemba 25, ili ilingane na—na kupinga kidini—sherehe za kipagani za majira ya baridi kali ya solistisi.” Kronolojia ya Biblia huonyesha kwamba Yesu alizaliwa katika mwaka wa 2 K.W.K.

Sasa Paka Watiwa Ndani

Kwa karne kadhaa katika Jimbo la New York limekuwa kosa kuondoka mahali pa aksidenti iliyohusisha ng’ombe, farasi, au mbwa, bila kutafuta mwenyewe au angalau kuwajulisha polisi wa hapo. Paka hawakutiwa ndani. Hata hivyo, jambo hilo sasa limeshughulikiwa na mswada mpya ambao ulipitishwa na kutiwa sahihi na wengi uwe sheria. Ukiitwa mswada wa “Paka Bapa,” sheria hii hulifanya kuwa kosa kuondoka mahali pa aksidenti ambayo inamjeruhi paka, bila kujulisha angalau polisi juu ya jeraha hilo. Kukosa kuripoti kungeweza kutokeza faini ya dola 100 kwa madereva “wenye kuwajeruhi paka kwa kuwagonga na kukimbia.” “Kwa wale wapendao paka, inaonyesha uwezekano ulio wa kipekee kwamba udhihirisho mmoja wa kubaguliwa kwa spishi waweza kukomeshwa,” likaeleza The New York Times.

“Mlipuko wa Ugonjwa wa Unene wa kupita Kiasi”

“Ongezeko la mlipuko wa ugonjwa wa unene wa kupita kiasi linatisha afya ya mamilioni ulimwenguni,” laripoti The Journal of the American Medical Association, likitaja onyo lililotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni. “Wataalamu wa lishe na wa afya kutoka nchi 25 walisema kwamba kuenea kwa unene wa kupita kiasi miongoni mwa watu wazima kunafikia asilimia 25 katika nchi fulani katika magharibi mwa Ulaya na sehemu za Amerika. Tarakimu hii huongezeka kufikia asilimia 40 kwa wanawake katika mashariki mwa Ulaya na nchi za Mediterania na kwa wanawake weusi katika Marekani. Melanesia, Mikronesia, na Polinesia, zina mweneo wa juu zaidi wa unene wa kupita kiasi—unaofikia asilimia 70 katika maeneo fulani.” Wataalamu walionya kwamba mielekeo isipobadilishwa kuelekea milo yenye mafuta kidogo na kuelekea mitindo-maisha yenye utendaji mwingi, nchi nyingi zitakabili idadi kubwa zaidi za watu walio na maradhi ya mishipa ya moyo, matatizo ya kupumua, mshtuko wa akili, ugonjwa wa nyongo, kansa, ugonjwa wa kisukari, na matatizo yanayohusiana na misuli na kiunzi cha mifupa. “Unene wa kupita kiasi ‘wapasa kuonwa kuwa mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya afya ya umma yaliyopuuzwa katika wakati wetu, yaliyo na madhara mabaya kwa afya [ambayo] yanaweza kuthibitika kuwa makubwa kama lile la uvutaji wa sigareti,’ wataalamu hao walisema.”

Ujitoaji Ulioelekezwa Vibaya?

Katika Juni 1, 1997, umbo—lililoonekana kuwa lilisababishwa na unyevuanga—lilitokea ukutani katika moja ya stesheni za Metro za Mexico City. Kwa Wakatoliki wengi wenye kujitoa, hili lilikuwa umbo lipitalo nguvu za binadamu la Bikira wa Guadalupe—jina lililopewa Bikira Maria katika Mexico. “Kanisa Katoliki halioni kutokea kwa umbo la Bikira wa Metro kuwa muujiza halisi bali tokeo la asili la upenyaji wa maji ndani ya kuta za stesheni,” lilitaarifu gazeti la habari El Universal. Hata hivyo, watu wengi husimama mbele yake na kuuabudu, na “watu elfu moja kwa saa wamezuru” mfano huo. Pembe ndogo ilijengwa kwa ajili ya mfano huo na ilizinduliwa na kasisi Mkatoliki.

Kupata Faida Kutokana na Uraibu

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, inakadiriwa kwamba kuna waraibu wa madawa ya kulevya milioni 340 hivi ulimwenguni pote. Kama ilivyoripotiwa katika Jornal da Tarde, “kutegemea dawa za kutuliza na kupoza maumivu huchukua nafasi ya kwanza, kukiwa na watumizi milioni 227.5 au karibu asilimia 4 ya idadi ya watu wote ulimwenguni. Kisha hufuata bangi, ikiwa na waraibu milioni 141, wakijumlika kuwa asilimia 2.5 ya idadi ya watu tufeni pote.” Pia inakadiriwa kwamba ni asilimia 5 hadi 10 tu ya madawa ya kulevya ambayo hunaswa na polisi. Uuzaji wa madawa ya kulevya huzalisha dola zinazofikia bilioni 400 kila mwaka. Katika visa fulani, wauzaji hao wa madawa ya kulevya hupata faida zinazofikia asilimia 300—“faida ambazo hazipatikani kamwe katika biashara ya aina yoyote,” lasema hilo gazeti la habari.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki