Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kukadiria Thamani ya Kitu Chenye Thamani Sana
  • Papa Azuru Kuba
  • Nywele Ndefu Zaidi Ulimwenguni
  • Maoni Aina Tatu ya Historia
  • Nyasi za Stediamu za Kijani Kibichi Zaidi
  • Majeraha ya Turubali
  • Upendo Haushindwi Kamwe
  • Wahifadhi Walio Bora
  • Michezo ya Kompyuta Yenye Jeuri
  • Biblia Bila Mungu
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?
    Amkeni!—2002
  • Je, Kuna Hatari kwa Wachezaji?
    Amkeni!—2002
  • Habari Za Kitheokrasi
    Huduma Yetu ya Ufalme—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kukadiria Thamani ya Kitu Chenye Thamani Sana

Wanasayansi 13 kutoka nchi mbalimbali wamekusanya ripoti ya kukadiria thamani ya vitu vya asili kwa dola. Wanasayansi hao walichunguza uchunguzi zaidi ya 100 uliochapishwa ili kukadiria gharama ya kulipia huduma mbalimbali zinazoandaliwa na dunia katika kila hekta. (Hekta moja ni sawa na ekari zipatazo 2.5.) Kwa kielelezo, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kwa kila hekta ya bwawa iliyotumiwa kwa ukuzi katika Marekani, “kulikuwa na ongezeko la hasara kwa kutoweza kudhibiti mafuriko ya kila mwaka ya kati ya dola 3,300 hadi dola 11,000,” lataarifu gazeti Science. Ingawa wengi huchukulia bidhaa za asili za dunia na huduma zake kivivi hivi, wanasayansi wanakadiria thamani yake ya kifedha ya kila mwaka kufikia dola 33,300,000,000,000—karibu mara mbili ya jumla ya pato la mataifa ulimwenguni mzima.

Papa Azuru Kuba

Kwenye ziara yake nchini Kuba Januari iliyopita, Papa John Paul wa Pili alieleza matumaini ya Kanisa Katoliki ya kushiriki fungu kubwa zaidi katika jamii ya Kuba. Kulingana na L’Osservatore Romano, alitaarifu kwamba wazazi “wanapaswa kuwachagulia watoto wao . . . mambo yahusuyo maadili na uraia na mambo ya kidini ambayo yatawawezesha kupata elimu muhimu.” Ingawa papa anataka kufungua tena shule za Kikatoliki katika nchi hiyo, maofisa wa Kuba wanasema kwamba wanataka Serikali iendelee kusimamia elimu ya umma. Kwa habari ya maoni ya serikali ya Kuba kuhusu ziara ya papa, gazeti la Kifaransa Le Monde Diplomatique laeleza hivi: “Fidel Castro anaiona ziara hiyo kuwa ushindi juu ya kutengwa kwa serikali yake ambako kumetukia.” Ijapokuwa baadhi ya taarifa za papa alipokuwa Kuba zilidokeza mambo ya kisiasa, Mashahidi wa Yehova wanadumisha kutokuwamo katika mambo ya kisiasa katika utendaji wao wa kidini.

Nywele Ndefu Zaidi Ulimwenguni

Hoo Sateow, jamaa mwenye miaka 85 wa kabila la Hmong katika kaskazini mwa Thailand, hajanyoa nywele zake kwa miaka ipatayo 70. “Nilizinyoa nilipokuwa na umri wa miaka 18, nikawa mgonjwa sana,” akasema Hoo. Hivi karibuni nywele zake zilipimwa na mwamuzi wa Guinness Book of World Records, zikawa na urefu wa sentimeta 520, na sasa nywele zake zaaminiwa kuwa ndefu zaidi ulimwenguni, laripoti Shirika la Habari la Associated Press. Hoo huosha nywele zake mara moja kwa mwaka na kuziangika juu ya fito ili zikauke. Mpinzani wake wa karibu zaidi ni ndugu yake mwenye umri wa miaka 87 anayeitwa Yi, ambaye alizinyoa nywele zake mara ya mwisho katika mwaka wa 1957. Na bado nywele za Yi ni ndefu kuliko za mtu aliyeshikilia rekodi ya hapo awali, mwanamke mmoja Mhindi ambaye nywele zake zilikuwa na urefu wa sentimeta 420. Hoo hufaidika kuwa na nywele ndefu hivyo, hasa juu kwenye milima yenye baridi ya Thailand. “Zinasaidia kunipasha joto,” asema.

Maoni Aina Tatu ya Historia

Watoto wa shule katika Bosnia wanafunzwa masimulizi aina tatu ya historia, sanaa, na lugha ya eneo hilo. Wanachosikia hutegemea ni kabila jipi katika makabila matatu makubwa linalosimamia masomo yao, laripoti The New York Times. Mathalani, wanafunzi katika eneo linalotawalwa na Waserbia la Othodoksi ya Mashariki wanajifunza kwamba mtu aliyeua Dyuki-Mkuu Ferdinand katika 1914 na kuanzisha vita ya ulimwengu ya kwanza alikuwa “shujaa na mshairi.” Wanafunzi Wakroatia wa Katoliki ya Kiroma wanaambiwa kwamba alikuwa “mwuaji aliyezoezwa na kuagizwa na Waserbia kufanya tendo hilo la ugaidi.” Masimulizi ya Kiislamu ya tukio hili humfafanua kuwa “mzalendo ambaye tendo lake lilichochea ghasia dhidi ya Waserbia na ambazo zilikomeshwa na polisi kutoka makabila yote matatu.” Wanafunzi wanaombwa wajitambulishe kuwa Waserbia, Waislamu, au Wakroatia ili watenganishwe katika madarasa yaliyo tofauti kikabila, yataarifu ripoti hiyo.

Nyasi za Stediamu za Kijani Kibichi Zaidi

Stediamu yenye viti 28,000 iliyojengewa kilabu ya kandanda ya Vitesse Arnhem ya Uholanzi yajisifia uwanja mzuri wa nyasi na pia paa lililofunikwa. Ni vigumu kupatanisha vitu hivi viwili, kwa kuwa nyasi hukua vyema zaidi ipatapo nuru nzuri ya asili na mvua. Bila vitu hivyo, nyasi hugeuka kuwa ya rangi ya kimanjano na kunyauka. Tatizo hili lilitatuliwa wakati jengo hili lilipokuwa likibuniwa, laripoti gazeti New Scientist. Uwanja wa michezo unakalia bamba lililojengwa kwa saruji ambalo huteleza juu ya magurudumu ya plastiki. Wakati hautumiwi, uwanja wote wa michezo wenye uzito wa tani 11,000 waweza kuhamishwa nje ya stediamu na mitambo minne inayoendeshwa kwa maji. Faida nyingine ya mpango huu ni kwamba sakafu ngumu ya stediamu hii yaweza kutumiwa kwa maonyesho ya muziki na matukio kama hayo.

Majeraha ya Turubali

Katika miaka ya hivi majuzi turubali zimezidi kupendwa, lakini hili limeongeza kujeruhiwa kwa watoto, lataarifu gazeti The New York Times. “Watu huzielewa vibaya turubali kuwa nyororo na kama mito,” asema Dakt. Gary A. Smith, wa Hospitali ya Watoto katika Columbus, Ohio, Marekani. Dakt. Smith alisema kwamba watoto wanajeruhiwa kwa kuanguka kutoka kwenye turubali, kuangukia mkeka kwa upande mbaya, kugongana na mtoto mwingine anayeruka wakati huo huo, au kugonga sakafu kavu. Aliongezea kwamba turubali zenye ngazi ndizo zilizo hatari hasa kwa sababu zinafanya turubali zipatikane kwa watoto wachanga, na mara nyingi wao ndio hujeruhiwa kwa urahisi zaidi. Ann Brown, wa Tume ya Usalama wa Bidhaa za Matumizi, anapendekeza kwamba watoto walio na umri unaopungua miaka sita hawapaswi kuruka kwenye turubali na kwamba ni mtoto mmoja tu anayepaswa kuruka kwa wakati mmoja. Alieleza hivi: “Kama ilivyo na dimbwi la kuogelea, mtoto aliye juu ya turubali huhitaji uangalizi wa daima.”

Upendo Haushindwi Kamwe

“Matineja walio na ukaribu sana wa kihisia-moyo na wazazi na walimu wao wana mwelekeo mdogo sana wa kutumia dawa za kulevya na vileo, kujaribu kujiua, kushiriki katika jeuri au kuwa wenye kufanya ngono wanapokuwa na umri mchanga,” laripoti The Washington Post. Watafiti katika Chuo Kikuu cha Minnesota na Chuo Kikuu cha North Carolina katika Chapel Hill pia walipata kwamba ndivyo ilivyo hata iwe mtoto anaishi katika nyumba ya mzazi mmoja au ya wazazi wawili. Jambo la maana ni kwamba mtoto ahisi anapendwa, anathaminiwa, na anaeleweka. Jambo jingine ambalo uchunguzi huu ulikazia ni “umaana wa wazazi kujihusisha sana katika maisha ya watoto wao katika miaka ya utineja, hata wanapohisi kwamba daraka lao linapungua,” lasema gazeti Post.

Wahifadhi Walio Bora

Jeshi la Wanamaji la Uingereza linatumia mbuzi kusaidia kuhifadhi mawe ya ngome ya kihistoria ya mwambao, laripoti The Sunday Telegraph. Mizizi ya mikwamba, miti, na magugu ilikuwa ikiharibu matofali na mchanganyiko wa sementi na mchanga. Njia za kawaida za kuiondoa zilitia ndani misumeno ya umeme iliyo ghali na dawa za kuua magugu, ambazo zaweza kuwa hatari. Kwa kuongezea, njia hizi huharibu mimea adimu, kuvu na wadudu. Hata hivyo, mbuzi hao wepesi si wa gharama ya chini tu; bali pia wanapunguza madhara kwa mimea na wanyama wa pori walio hatarini mwa kutoweka. Mshauri wa mpango huo, Mike Beauchamp asema hivi: “Katika miaka 10, mashirika mengi ya uhifadhi yatakuwa yakitumia mbuzi ili kurudisha ardhi iliyo na vichaka.”

Michezo ya Kompyuta Yenye Jeuri

Moja ya michezo ya kompyuta yenye jeuri zaidi iliyopata kutokezwa, Quake II, umerekebishwa ili uwe wenye jeuri hata zaidi. Programu hiyo “imevutia sana kikundi fulani cha watu kwa kutapanya damu na sehemu za mwili kwenye viwambo vyote vya kompyuta vya wachezaji,” laripoti The Wall Street Journal. “Majibu tuliyopata kutoka kwa wachezaji yalionyesha kwamba hakukuwa na damu ya kutosha,” asema kiongozi wa programu hiyo John Carmack, “kwa hiyo tuliongeza nyingine.” Mchezo wa Quake II huruhusu wachezaji “wachinjane-chinjane” na makumi ya wachezaji wenye vita katika Internet katika mashindano yaitwayo michuano ya kifo. Mchezo huu una sehemu ambayo huruhusu wachezaji watoe ishara za mwili za matusi kwa wapinzani wao. Wenye programu hii na mafundi ambao walitokeza mchezo huu “hufanya kazi katika mahali penye kupendeza sana wachezaji hao panapotia ndani chumba cha kuinulia uzani na jiko lililojaa vyakula visivyofaa mwili. Nambari ya mahali hapo ni 666, ambayo ni rejezo . . . katika Kitabu cha Biblia cha Ufunuo.”

Biblia Bila Mungu

Tabibu mmoja katika Denmark amechapisha tafsiri iliyoandikwa upya ya Maandiko ya Kiebrania—bila kutaja marejezo yote kwa Mungu. Dakt. Svend Lings aamini kwamba Mungu na imani “ni mambo ya kale ambayo yanaweza tu kutunyima uhuru,” laripoti gazeti la habari la Denmark Kristeligt Dagblad. Lings alisema kwamba watu wengi hawana furaha na ni wapweke. “Tunaishi katika utamaduni wa Kiyahudi na Kikristo,” asema Lings. “Kwa hiyo utamaduni wa Kiyahudi na Kikristo ndio umesababisha ukosefu wetu wa furaha.” Akiwa na tafsiri yake mpya ya Biblia, kulingana na gazeti hilo la habari, Lings akusudia, “kudhoofisha utamaduni wetu.” Katika tafsiri ya Lings, Bible Without God, Mwanzo 3:12 husema: “Adamu akafikiria yeye mwenyewe: ‘Mwanamke aliye kando yangu alinipa tunda kutoka kwenye mti huo, kisha nikala.’” Gazeti la habari Kristeligt Dagblad lauliza hivi: “Je, hii si sawa na kujaribu kuondoa maji kutoka kwa theluji na kuona ni nini kinachobakia?”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki