Kuutazama Ulimwengu
Mwaka wa 2000 na Kristo
“Uchunguzi waonyesha ni Waingereza wasiozidi sudusi moja tu wanaohusianisha mwaka wa 2000 na Kristo,” chataarifu kichapo ENI Bulletin. Uchunguzi wa Gallup “ulifunua kiasi kikubwa cha ukosefu wa ujuzi juu ya Milenia, kukiwa na asilimia 37 ya waliohojiwa wakisema hawakufahamu ilikuwa kumbukumbu ya nini . . . , asilimia 18 wakisema sherehe hizo zilitia alama karne mpya, na asilimia 17 kwamba zilitia alama mwaka wa 2000.” Ni asilimia 15 tu wanaoona uhusiano uliopo kati ya mwaka wa 2000 na kuzaliwa kwa Kristo. Kulingana na Profesa Anthony King, wa Chuo Kikuu cha Essex, kwa watu wengi milenia ilikuwa “fursa ya kucheza dansi, kunywa shampeni, kukesha pamoja na marafiki au kusafiri ng’ambo tu.” Askofu wa Kianglikana Gavin Reid alielezea hivi: “Tunaishi katika jamii ambayo imepoteza kumbukumbu lake la kitamaduni na la kiroho.”
Tahadhari juu ya “Vijidudu-Maradhi”
“Usugu wa ‘vijidudu-maradhi’ kwa viuavijasumu vyenye nguvu zaidi wapaswa kuwatahadharisha watu wote si wataalamu wa kitiba tu bali watumiaji pia,” lasema gazeti la habari Star la Afrika Kusini. Mwanapatholojia Mike Dove aonya kwamba “maradhi ambayo wakati mmoja yalionekana kuzuiwa au kumalizwa kabisa yamebadilika na yanarudi.” Kutumia viuavijasumu kupita kiasi kumetokeza namna mpya za magonjwa ya kifua kikuu (TB), malaria, homa ya matumbo, kisonono, utanda bongo, na nimonia ambayo yazidi kuwa vigumu kutibu na yamekuwa sugu kwa dawa za kisasa. Zaidi ya watu milioni tatu hufa kila mwaka kutokana na TB peke yake. Wagonjwa wanaweza kusaidia kwa kukumbuka yafuatayo: Kwanza kabisa, jaribu kutumia tiba ya kunywa vinywaji vingi, kupata pumziko linalohitajiwa, na kusukutua umio lako kwa maji yenye chumvi iwapo una vidonda vya koo. Usimlazimishe daktari wako akupe viuavijasumu—mwache yeye aamue iwapo ni vya lazima kikweli. Iwapo waagizwa na daktari, daima zitumie kwa siku zote zilizoonyeshwa hata iwapo wapata nafuu. Kumbuka, viuavijasumu haviwezi kutibu homa na mafua yanayosababishwa na virusi, na si bakteria. “Kila mtu,” akasema Dove, “apaswa kushirikiana ili kukabili tatizo hili la tufeni pote lenye kutia wasiwasi ambalo laweza kutokeza msiba mkuu wa kiafya.”
Gharama Kubwa ya Mshuko-Moyo
“Mshuko-moyo—unaozidi sana maradhi ya kimwili—ndio kisababishi kikuu cha kutokufika kazini na cha matokeo hafifu ya kazi ulimwenguni,” lasema gazeti la habari la Brazili O Globo. Ripoti moja ya Shirika la Afya Ulimwenguni yaonyesha kwamba maradhi ya akili ndiyo yaliyokuwa visababishi vya vifo 200,000 katika 1997. Kwa kuongezea, vurugu ndogondogo za kiakili, kama vile hali ya kubadilika-badilika ya mtu, zilikuwa na matokeo mabaya juu ya utendaji wa kazi ya watu wasiopungua milioni 146 ulimwenguni pote—idadi inayozidi kidogo wafanyakazi zaidi ya milioni 123 waliopatwa na tatizo la kusikia au milioni 25 ya waliopatwa na aksidenti kazini. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na profesa Guy Goodwyn wa Chuo Kikuu cha Oxford, tatizo la mshuko-moyo litaongezeka katika miaka ijayo, likitokezea jamii mzigo mkubwa wenye kulemea kwa sababu ya matokeo ya uzalishaji hafifu na gharama zinazopanda za matibabu. Katika Marekani pekee, hasara za kila mwaka zinazotokana na mshuko-moyo, tayari zimefikia dola bilioni 53.
Ni Rahisi Kusoma Kwenye Karatasi
“Hakuna kiwambo kiwezacho kusomeka vyema kama maandishi yaliyochapwa kwenye karatasi,” shirika la habari la Ujerumani dpa-Basisdienst laripoti. Kusoma kutoka kwenye karatasi hutokeza makosa madogo na usomaji ni wa haraka kwa kulinganishwa na kusoma kutoka kwenye kiwambo. Majaribio huonyesha kwamba, kusoma maandishi kwenye kiwambo huchukua urefu wa wastani wa asilimia 10 zaidi kukilinganishwa na kusoma kutoka kwenye karatasi. Ijapokuwa matokeo yaliimarika viwambo vya hali bora zaidi na vyenye uwezo wa kurekebisha tofauti za wangavu vilipotumiwa, bado havikulingana na matokeo ya kusoma kutoka kwenye karatasi. “Yeyote afanyaye kazi kwenye kiwambo hutumia muda wake wote akitazama moja kwa moja kwenye chanzo cha mwanga wenye kung’aa, unaowakawaka, na unaorudisha mwangaza,” akasema mwanasaikolojia Martina Ziefle, kutoka Aachen, Ujerumani. “Mistari inayoonyesha umbo la maneno haiko wazi, na viwango vya tofauti za wangavu si vyenye nguvu.” Mkataa wa dpa ni: “Ununuapo kompyuta, wapaswa kukazia uangalifu mwingi juu ya ubora wa kiwambo.”
Ishara za Nyakati
“Jambo moja la kale lisilo la kawaida lililosalia la utamaduni wa Kanada litakwisha majuma machache yajayo polisi [katika Newfoundland] waanzapo kubeba bunduki kwa mara ya kwanza,” charipoti kichapo The Toronto Star. Kikundi cha polisi kiitwacho The Royal Newfoundland Constabulary, kilichoundwa mwaka wa 1729, “ndicho kilichokuwa cha mwisho katika Amerika Kaskazini kushika doria bila bunduki mkononi.” Sheria mpya iliyopitishwa ilibatilisha sera ya awali. Ilibidi askari wamwombe msimamizi ruhusa ili kuwa na silaha. Iwapo ruhusa ingetolewa, ofisa wa polisi angeifungia silaha yake ndani ya sanduku katika buti la gari lake. Kisha, ilipohitajika, kwa mwito wa dharura, alihitaji kuegesha gari lake, afungue buti la gari, afungue sanduku, na kuitia risasi silaha yake. “Ni sera ya kikale na tena ya kuvutia, lakini, kwa vyovyote, haiwezi kusemwa kwamba askari waliozoezwa wa kikosi cha polisi katika 1998 hawawezi kuzipata silaha zao,” akasema Waziri Mkuu Brian Tobin. Mwamba, sawa na lijulikanavyo jimbo la Newfoundland kwa njia yenye shauku, lingali lajivunia kiwango cha uhalifu cha chini zaidi nchini na halijawa na askari aliyepigwa risasi akiwa kazini.
Kulipiza Kisasi Ndiyo Shughuli Yao
Ikiahidi “kuweka siri kabisa” na uwezo wa kutoa utumishi popote Japani, kampuni moja ya Tokyo inatangaza hivi: “Tutakulipizia kisasi.” Wazo la msingi ni “kumtesa mtu sawasawa na alivyomtesa mteja mwanzoni,” asema mwenye kampuni hiyo. Kama ilivyoripotiwa katika kichapo Asahi Evening News, kampuni hiyo “itafanyiza vitendo vya kisheria vya kupatiliza adhabu,” kama vile kuhakikisha “mtu amepoteza kazi na familia yake,” kuvunja mahusiano, na “kuhakikisha mfanyakazi mwenzi apoteza kazi yake au mwajiri wa kazi aliyesumbua kingono atwezwa.” Kati ya watu wapatao 50 wanaoipigia kampuni hiyo simu kila siku, 20 huuliza juu ya kandarasi za mauaji; lakini kanuni ya kawaida ya kampuni hiyo si kutumia nguvu au kuvunja sheria, “ijapokuwa nyakati nyingine hukaribia kufanya hivyo.” Kampuni hiyo huwaajiri wafanyakazi wengi, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa siku nzima wa kazi nyingine. Wengine wao ni watu walioteseka na wanaotaka kusaidia wengine walipize kisasi. “Huwezi kujua iwapo ulilotenda wakati uliopita limewafanya wengine kuwa na kinyongo nawe. Jihadhari,” akatahadharisha mwenye kampuni.
Kaa wa Nchi Kavu na Ikolojia
Chungu, mchwa, na minyoo huozesha majani na vifusi sakafuni mwa misitu, lakini huwaje katika misitu ya mvua ya kitropiki igarikishwayo na maji pindi kwa pindi? Kaa wa nchi kavu hufanya kazi hiyo. Mwanaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani, alishangaa kupata eneo kubwa la msitu kwenye Pwani ya Pasifiki ya Kosta Rika ambalo badala ya kuwa na matawi sakafuni lilikuwa na mashimo mengi makubwa. Usiku, alitazama kaa wa nchi kavu—waliokadiriwa kuwa 24,000 kwa eka moja—wakijitokeza kutafuta matawi yaliyooza, matunda, na mbegu, walizozisafirisha hadi kwenye sehemu ya chini ya mashimo yao yenye urefu wa meta moja. Kaa hawa wenye ukubwa wa sentimeta 20, wenye mashavu ya kupumua yaliyorekebika ambao hufanya ziara za pindi kwa pindi tu hadi pwani ili kuzaana, husaidia kuilisha miti yenye mizizi yenye vina sana. Ikolojia yote ya msitu huo hutegemea yale viumbe hawa hufanya, laripoti gazeti Times la London.
Mbali Zaidi Katika Anga
“Voyager 1 [chombo cha angani kinachochunguza mambo ya kisayari] kimekuja kutambuliwa kuwa chombo cha kibinadamu ambacho kimesafiri mbali zaidi ya vyote,” lataarifu gazeti Astronomy. “Rekodi ya awali ilishikiliwa na Pioneer 10, ambacho chaonekana kuelekea upande ulio kinyume na katika mwendo uliopungua.” Voyager 1 kimefikia umbali gani kutoka duniani? Umbali wa kilometa bilioni 10.4 kufikia Februari 17, 1998. Chombo hicho kilirushwa Septemba 5, 1977; kikapita sayari ya Sumbula Machi 5, 1979; na kikaruka juu ya sayari ya Sarateni Novemba 12, 1980. Hicho huendelea kupeleka habari kupitia mfululizo wa visehemu vinavyotoka kwenye jua na kupitia kwa ugasumaku. “Hatimaye, vifaa vyake huenda vikawa vya kwanza vya chombo chochote cha anga la juu kugundua lile eneo la mpaka kati ya uvutano wa ugasumaku wa Jua, na mwanzo wa uvukwe wa anga la kinyota,” lasema Shirika la National Aeronautics and Space Administration.
Watoto Wasioandikishwa
“Labda thuluthi moja ya watoto wachanga wote, hawaandikishwi wanapozaliwa, wakiachwa katika hali ya kutotunzwa ambayo yaweza kumaanisha kukosa nafasi za kielimu na matibabu,” laripoti gazeti The New York Times. Karibu na Sahara ya Afrika, na nchi fulani za Asia kama vile Kambodia, India, Myanmar, na Vietnam ndiko kulikokuwa na kiasi cha chini zaidi cha kuandikishwa kuzaliwa kwa watoto. “Kutokuwa na cheti cha kuzaliwa ni kama kusema hukuzaliwa kamwe,” asema Carol Bellamy, mkurugenzi mkuu wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, shirika lililofanya uchunguzi huo ulimwenguni pote. Mataifa mengi hutaka cheti cha kuzaliwa kwa mtoto kabla hajatibiwa hospitalini au kuandikishwa shuleni, na watoto wanaokosa vyeti hivi huelekea kulazimika kufanyishwa kazi ngumu au kutumiwa kufaidi watu wengine kingono. Makala hiyo iliongeza hivi: “Kiwango cha kujiandikisha hakitokani na umaskini, ikipata viwango vingi vya kuandikishwa katika sehemu nyingi za Amerika ya Latini, Asia ya kati na Afrika Kaskazini.”