Linda Mtoto Wako na Aksidenti
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SWEDEN
HANNA, ambaye ana umri wa miaka mitatu hivi, alikuwa pamoja na wazazi wake, Karl-Erik na Birgitta, huku wakisafisha nyumba ya jirani aliyekuwa amekufa. Baada ya muda, Hanna alitoka chumbani akiwa na chupa ya tembe mkononi mwake. Alikuwa amekula baadhi yake. Akiichunguza chupa hiyo, Birgitta alishtuka vibaya sana. Ilikuwa chupa ya dawa za moyo za jirani.
Upesi, Hanna alipelekwa hospitali, ambapo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi usiku mzima. Licha ya kunywa dawa hizo ambazo zingeharibu afya yake daima, hakupatwa na athari zozote. Kwa nini? Kwa sababu alikuwa amekula nafaka iliyopikwa kabla ya kumeza tembe hizo. Kiasi fulani cha sumu hiyo kilifyonzwa na nafaka, na sumu hiyo ilitoka alipotapika.
Jambo lililompata Hanna si la pekee hata kidogo. Kila siku, maelfu ya watoto hupatwa na aksidenti ambazo hufanya iwe lazima wapelekwe kwa daktari au hospitali. Kila mwaka mtoto 1 kati ya watoto 8 huko Sweden hupokea matibabu baada ya aksidenti. Kwa sababu hiyo, ikiwa wewe ni mzazi, kuna uwezekano mkubwa kwamba jambo linalofanana na hilo lingeweza kumpata mtoto wako.
Ni jambo la kawaida mara nyingi watoto kujeruhiwa katika mazingira ambayo wameyazoea, kama vile nyumbani na sehemu zinazoizingira. Aina ya majeraha wanayopata hubadilika wanapokuwa na umri mkubwa zaidi. Kitoto kichanga kinaweza kuanguka kutoka kitandani au kusongwa na kipande cha chakula au kitu kidogo kinachokwama kwenye koo lake. Mara nyingi watoto wachanga huanguka wanapopanda au huchomeka au kutiwa sumu wanapogusa au kuonja vitu vilivyo karibu. Watoto wenye umri wa kwenda shuleni mara nyingi hujeruhiwa katika aksidenti za magari au wanapocheza nje.
Nyingi za aksidenti hizi zaweza kuzuiwa. Kwa kutumia busara kidogo na kufahamu kiwango cha ukuzi wa mtoto wako, unaweza kuzuia majeraha au hata aksidenti zenye kufisha. Jambo hilo limethibitishwa na programu inayohusu usalama wa watoto ambayo imetekelezwa huko Sweden tangu mwaka wa 1954. Kabla ya wakati huo, zaidi ya watoto 450 walikufa kila mwaka katika aksidenti. Leo, idadi ya vifo kila mwaka imepungua na kufikia takriban 70.
Ndani ya Nyumba
“Huwezi kumfundisha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, miaka miwili, au miaka mitatu kuepuka hatari na kutarajia wakumbuke,” asema mwanasaikolojia wa watoto Kerstin Bäckström. Kwa sababu hiyo, daraka la kumsaidia mtoto wako aepuke aksidenti ni lako ukiwa mzazi—au ni la watu wazima wanaokaa na mtoto pindi kwa pindi.
Kwa kuanza, tazama huku na huku katika nyumba yako. Tumia orodha ya kukagulia kwenye sanduku lililo kando ya makala hii. Labda vifaa fulani vya usalama havipatikani katika nchi zote au havipatikani kwa bei nafuu. Hata hivyo kwa kutumia ustadi kidogo na ubunifu, labda unaweza kufikiria suluhisho unaloweza kutumia katika hali zako hususa.
Kwa kielelezo, ikiwa saraka za jiko lako zina vipete aina ya kitanzi, unaweza kuvifunga kwa kuweka kijiti kwenye vipete hivyo. Unaweza kutumia mbinu hiyo hiyo kufunga mlango wa joko. Mifuko ya plastiki haiwi hatari sana unapoifunga kwa kuweka kifundo wakati wa kuihifadhi.
Labda unaweza kufikiria njia nyingine sahili za kuzuia aksidenti ndani na nje ya nyumba yako na kuwaeleza marafiki na wajuani wako walio na watoto wadogo.
Nje ya Nyumba
Chunguza maeneo ambayo mtoto wako huchezea. Watoto wenye umri unaozidi miaka minne mara nyingi hujeruhiwa wanapocheza nje ya nyumba. Wao huanguka na kujeruhiwa au labda huanguka kutoka kwenye baiskeli zao. Aksidenti zenye kufisha zilizo za kawaida zaidi kwa watoto walio na umri wa kati ya miaka mitatu na saba ni aksidenti za magari na kufa maji.
Unapochunguza viwanja vya kuchezea, chunguza uone ikiwa vifaa viko katika hali nzuri ili mtoto asijeruhiwe anapovitumia. Je, ardhi iliyo chini ya vibembeo, ngazi za kubembea, na vifaa kama hivyo ni laini, kama vile mchanga, ili mtoto asijeruhiwe iwapo ataanguka?
Je, kuna vidimbwi vya maji au vijito karibu na nyumbani mwako? Maji yenye kina cha sentimeta chache yanatosha kufisha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja au miaka miwili. “Mtoto mdogo anapoanguka kifudifudi ndani ya kidimbwi cha maji, hupoteza fahamu kuhusu kitu kilicho juu na kilicho chini,” asema mwanasaikolojia wa watoto Bäckström. “Mtoto hawezi kujiinua tena.”
Kwa hiyo, kanuni ya msingi ni hii: Usiruhusu kamwe mtoto mwenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka mitatu acheze nje ya nyumba akiwa peke yake bila uangalizi wa mtu mzima. Ikiwa kuna maji kiasi fulani kwenye ujirani, subiri hadi mtoto anapokuwa na umri mkubwa zaidi kabla ya kumruhusu acheze nje ya nyumba bila uangalizi.
Mahali Penye Magari
Hali ni namna moja ikiwa kuna magari karibu na nyumba yako. “Mtoto ambaye hajaanza kwenda shuleni anaweza kuelewa tu ishara iliyo wazi na hususa na kukazia fikira jambo moja kwa wakati,” asema Bäckström. “Lakini magari yamejaa dhana zilizo ngumu kueleweka na jumbe zilizo tata.” Usimruhusu mtoto wako avuke barabara akiwa peke yake kabla hajafikia umri wa kwenda shuleni. Watoto hawaonwi kuwa wamekomaa vya kutosha kuendesha baiskeli wakiwa peke yao mahali penye magari mengi mpaka wanapofikia angalau umri wa miaka 12, kulingana na wataalamu.
Mfundishe mtoto wako kutumia kofia ya chuma ya usalama anapoendesha baiskeli, anapobebwa, anapotumia rolasketi au anapoteleza kwenye sileji. Ni vigumu kutibu majeraha ya kichwa na yanaweza kusababisha madhara ya kudumu—au hata ya kufisha! Kwenye kliniki moja ya watoto, asilimia 60 ya waliotibiwa kufuatia aksidenti za baiskeli walikuwa wamejeruhiwa kichwa na uso, lakini wale waliotumia kofia za chuma hawakujeruhiwa kichwa hata kidogo.
Pia, hakikisha kwamba mtoto wako yuko salama anaposafiri kwa gari. Nchi nyingi zina sheria ambazo hutaka watoto wadogo wafungwe kwenye viti maalum vilivyotengenezwa kwa ajili ya usalama. Viti hivyo vimepunguza sana majeraha na vifo miongoni mwa watoto waliohusika katika aksidenti za magari. Ikiwa kuna viti vya usalama mahali unapoishi, kutumia kimoja kwaweza kuandaa usalama kwa uhai. Lakini hakikisha kwamba muundo wake unakubalika. Ona kwamba viti vya vitoto vichanga ni tofauti na vile vya watoto wenye umri unaoanzia miaka mitatu hivi.
Watoto wetu ni zawadi zenye thamani kutoka kwa Yehova, na tunataka kuwatunza katika kila njia. (Zaburi 127:3, 4) Wakiwa wazazi wema, Karl-Erik na Birgitta wamekuwa wakihangaika daima kuhusu kulinda watoto wao—kabla na hata baada ya tukio lililompata Hanna. “Lakini bila shaka tulikuwa waangalifu hata zaidi baada ya tukio hilo,” akiri Karl-Erik. “Sasa tuna wajukuu, na sikuzote tunahakikisha kwamba dawa zetu zimefungiwa,” amalizia Birgitta.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Usalama Nyumbani Mwako
• Dawa: Ziweke mbali na watoto kwa kuzifungia kabatini. Fanya vivyo hivyo na dawa za kununuliwa dukani na mitishamba. Pia, waombe wageni wanaolala nyumbani mwako waweke dawa zao mbali na watoto.
• Kemikali za nyumbani: Ziweke mbali na watoto katika kabati. Ziweke katika vikasha vyao vya awali ili ziweze kutambuliwa waziwazi. Linda kwa makini bidhaa unazotumia, na ziweke mbali daima, hata ikiwa watoka chumbani kwa muda mfupi tu. Usiache mabaki ya sabuni ndani ya maji ya kuoshea vyombo.
• Jiko: Sikuzote geuza mikono ya vikaango ielekee upande wa ndani wa jiko. Shikiza kifaa cha kulinda sufuria, ikiwa kinapatikana. Shikiza kifaa cha kuzuia jiko lisiiname upande mmoja kwa ajili ya usalama iwapo mtoto atapanda kwenye mlango wa joko uliofunguliwa. Mlango wenyewe wa joko wapaswa kuwa na kufuli. Je, mtoto angeweza kuchomeka kwa kugusa mlango wa joko? Basi weka kifaa cha kuulinda ili asiweze kugusa mlango ulio moto.
• Vyombo vya nyumbani vilivyo hatari: Visu, makasi, na vyombo vingine hatari vyapasa kuwekwa ndani ya kabati au saraka zenye komeo au vifaa vya kuvizuia visisonge au viwekwe mbali na watoto. Unapotumia vyombo hivyo na kuviweka kando kwa muda, viweke mbali na pembe ya meza au kaunta, mbali na mtoto. Viberiti na mifuko ya plastiki ni hatari pia kwa watoto wadogo.
• Ngazi: Weka malango, angalau sentimeta 70 hadi 75 juu, kwenye miisho yote ya ngazi.
• Madirisha na milango ya roshani: Yaweke na vifaa vya kulinda usalama wa watoto au minyororo juu yake au vifaa vingine vya usalama ambavyo huzuia mtoto kuvifungua au kujipenyeza ndani yake vinapofunguliwa ili kuingiza hewa chumbani.
• Rafu za vitabu: Ikiwa mtoto anapenda kupanda na kuning’inia juu ya vitu, fungia rafu za vitabu na fanicha nyingine ndefu ukutani, ili kuzizuia zisianguke.
• Soketi za umeme na nyaya za stima: Soketi zisizotumiwa lazima ziwe na kufuli ya aina fulani. Nyaya za taa za mezani na nyingine kama hizo zapasa kufungiwa ukutani au kwenye fanicha, ili mtoto asivute taa na kuangukiwa nayo. Kama sivyo, ondoa taa za namna hiyo. Usiache kamwe pasi ya stima kwenye ubao wa kupigia pasi, na usiache waya ikining’inia.
• Maji moto: Ikiwa unaweza kurekebisha halijoto ya maji moto, unapaswa kuiweka digrii 50 Selsiasi ili mtoto asichomeke anapofungulia mfereji.
• Vichezeo: Tupa vichezeo vyenye ncha au pembe zilizochongoka. Tupa vichezeo vidogo au vichezeo vinavyoweza kutolewa katika vipande vidogo-vidogo, kwa kuwa vinaweza kumsonga mtoto anapovitia mdomoni. Macho na pua za vichezeo-dubu vya mtoto yapasa kuwa yamekazika. Wafundishe kaka na dada kuondoa vichezeo vyao vidogo mtoto anapokuwa sakafuni.
• Peremende na vitafuno: Usiache pipi na vitafuno, kama vile njugu karanga au peremende ngumu, karibu na mtoto. Zinaweza kusakama katika koo la mtoto.
[Hisani]
Chanzo: The Office of the Children’s Ombudsman
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Aksidenti Itokeapo
• Kutiwa sumu: Ikiwa mtoto amemeza sumu fulani, osha kinywa chake kwa maji safi kikamili na kumpa glasi moja au mbili za maji au maziwa anywe. Baada ya hapo, mwite daktari au piga simu kwenye kituo cha ushauri kuhusu sumu. Ikiwa mtoto ameingiwa na kitu kinachobambua ngozi ndani ya jicho lake, mwoshe mara moja kwa maji safi ya kutosha kwa angalau muda wa dakika kumi.
• Majeraha ya kuchomeka: Kwa majeraha madogo ya kuchomeka, tumia maji (si baridi sana) kwenye jeraha hilo kwa angalau dakika 20. Ikiwa jeraha ni kubwa kuliko kiganja cha mtoto au liko usoni, kwenye kiungo, au kwenye fumbatio ya chini au viungo vya uzazi, unapaswa kumpeleka mtoto kwenye chumba cha kushughulikia hali za dharura. Majeraha makubwa kwenye ngozi yapasa kutibiwa na daktari daima.
• Kusongwa: Ikiwa kitu fulani kimesakama ndani ya koromeo ya mtoto, fanya hima kutoa kitu hicho. Njia moja yenye matokeo unayoweza kutumia ni ile inayoitwa mbinu ya Heimlich (kuweka msongo kwenye tumbo la mtu aliyesakamwa ili kutoa kitu kilichokwama kwenye koromeo). Ikiwa hufahamu mbinu hiyo, mfikie daktari wako ili upate habari zaidi kuhusu mbinu hiyo, au hudhuria mtaala wa aksidenti za watoto au wa huduma ya kwanza mahali ambapo mbinu hiyo hufunzwa.
[Hisani]
Chanzo: The Swedish Red Cross
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kuvalia kofia ya chuma ya usalama ya baiskeli
[Picha katika ukurasa wa 23]
Akiwa salama katika kiti cha gari