Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g01 6/22 kur. 14-15
  • Biblia ya Dalmatin Haipatikani Sana Lakini Haijasahaulika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Biblia ya Dalmatin Haipatikani Sana Lakini Haijasahaulika
  • Amkeni!—2001
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mtafsiri Aibuka
  • Malezi ya Dalmatin
  • Kazi ya Kutafsiri Yaanza
  • Matatizo Yaliyozuka
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2002
  • Ukurasa wa Pili
    Amkeni!—2001
  • Bidii Kama ya Nyuki wa Carniola
    Amkeni!—2004
  • Hatua Muhimu kwa Wapendao Neno la Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2001
g01 6/22 kur. 14-15

Biblia ya Dalmatin Haipatikani Sana Lakini Haijasahaulika

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SLOVENIA

MAPIPA ya mwisho yenye vitu fulani muhimu yalifika Slovenia mwishoni mwa miaka ya 1500. Yalisafirishwa kupitia sehemu mbalimbali kwa muda wa miaka miwili. Ili kuficha vitu vilivyokuwamo, mapipa hayo yalikuwa na vibandiko vilivyoandikwa “karata” au “bidhaa za dukani.” Mabuku ya kwanza kabisa ya Biblia nzima ya Kislovenia yenye majalada ya ngozi yalifichwa mapipani.

Shehena hiyo muhimu ilitokana na jitihada za wanaume wawili wenye bidii—Jurij Dalmatin na Primož Trubar, ambao walijitoa mhanga kutafsiri Biblia katika lugha ya kawaida ya watu wao. Ijapokuwa huenda wanaume hao hawatajwi na vitabu vingi vya kihistoria, majina yao yanaweza kuorodheshwa pamoja na majina ya watu waliochangia sana kazi ya kutafsiri Biblia hapo awali.

Dalmatin, aliyesafirisha Biblia hizo kisiri, alimtumia mshauri na rafikiye aliyeitwa Trubar, nakala ya Biblia yenye jalada la pekee sana. Acheni tuone magumu ambayo wanaume hao wawili walikabili walipokuwa wakitafsiri Biblia katika lugha ya kawaida ya wananchi wenzao.

Mtafsiri Aibuka

Katika karne ya 16, Milki Takatifu ya Roma, ambayo ilihusiana sana na Kanisa Katoliki, bado ilikuwa inamiliki sehemu kubwa ya Ulaya. Hata hivyo, Mapinduzi ya Kiprotestanti yalikuwa yamepamba moto, na harakati hizo ziliathiri miji na vijiji katika nchi ambayo leo inaitwa Slovenia. Trubar, kasisi katika Slovenia, alikuwa miongoni mwa wafuasi wa kwanza wa Uprotestanti.

Kwa kuwa Kanisa Katoliki lilitumia lugha ya kale ya Kilatini, watu wengi hawakuelewa mafundisho ya kanisa na Biblia ila watu wachache waliokuwa wamejifunza lugha hiyo. Lakini, Wanamapinduzi walisema kwamba ibada ya kanisa inahitaji kufanywa katika lugha ambayo kila mtu anaelewa. Kwa hiyo, kufikia katikati ya miaka ya 1500, sura kadhaa za Biblia zilisomwa katika Kislovenia wakati wa ibada ya kanisa. Ilikuwa rahisi kufanya hivyo kwa sababu maandiko kadhaa ya Kislovenia yaliandikwa pambizoni mwa Kitabu cha Misa cha Kilatini kilichotumiwa na makasisi.

Hata hivyo, Trubar alitaka kuwa na Biblia nzima ya Kislovenia. Trubar alibuni alfabeti ya Kislovenia kwa kuwa haikuwako, na mnamo mwaka wa 1550 aliandika kitabu cha kwanza kuchapishwa katika Kislovenia. Kitabu hicho kilikuwa na mistari kadhaa ya Biblia kutoka kitabu cha Mwanzo. Baadaye, alitafsiri pia Zaburi katika Kislovenia na mwishowe Agano Jipya, au Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.

Hata hivyo, Trubar alitambua kwamba hakuwa na ustadi wa lugha uliohitajiwa ili kutimiza mradi wake wa kutafsiri Biblia nzima katika Kislovenia. Aling’amua kwamba Jurij Dalmatin, mwanafunzi kijana mwenye kipawa, angeweza kumsaidia kutimiza mradi wake.

Malezi ya Dalmatin

Dalmatin alizaliwa katika familia maskini mnamo mwaka wa 1547 katika kijiji kimoja kilicho kusini mwa Slovenia leo. Akiwa kivulana, alihudhuria shule moja ya karibu iliyosimamiwa na mfuasi wa mapema wa Uprotestanti, na hilo liliathiri sana mwelekeo wake wa kidini baadaye. Dalmatin alihudhuria shule ya kidini na baadaye chuo kikuu nchini Ujerumani kwa msaada wa Trubar, vilevile mwalimu mmoja na pia parokia ya mji wao. Masomo hayo yalimsaidia kuelewa Kilatini na Kijerumani vyema zaidi na kujifunza Kiebrania na Kigiriki, kisha akakamilisha masomo yake ya falsafa na theolojia.

Ingawa Dalmatin alisomea Ulaya, alitiwa moyo na Trubar kuthamini na kusitawisha lugha yake ya asili ya Kislovenia. Dalmatin alipokuwa katika miaka yake ya 20 akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu, alianza kazi ngumu sana ya kutafsiri Biblia katika lugha yao ya asili. Mradi muhimu zaidi wa Dalmatin ulikuwa kuitafsiri Biblia nzima katika Kislovenia kama Trubar alivyotamani sana.

Kazi ya Kutafsiri Yaanza

Dalmatin alianza kazi hiyo kwa bidii sana, akitafsiri kwanza Maandiko ya Kiebrania. Yaonekana kwamba alitafsiri kutokana na lugha za awali huku akirejezea kwa ukaribu tafsiri ya Kijerumani ya Biblia ya Kilatini ya Vulgate ya Martin Luther. Kufikia mwaka wa 1577, Trubar alikuwa ametafsiri Maandiko yote ya Kigiriki ya Kikristo katika Kislovenia. Kisha Dalmatin akaanza kusahihisha na kuboresha tafsiri ya Trubar kwa msaada wa tafsiri ya Biblia ya Kijerumani ya Luther. Aliondoa athari nyingi za Kijerumani na kuifanya tafsiri hiyo iwe na upatano zaidi. Huenda Dalmatin alitumia ujuzi wake wa Kigiriki katika kazi yake ya kutafsiri, lakini bado wasomi hawajui iwapo alitumia maandishi ya kale ya Kigiriki au la.

Matatizo Yaliyozuka

Dalmatin alikuwa na kibarua kigumu sana kwa sababu alfabeti ya Kislovenia ilikuwa imebuniwa miongo michache tu mapema. Isitoshe, lugha hiyo ilikuwa na maneno machache tu, na vitabu vya Kislovenia vya marejeo havikuwapo. Kwa hiyo, alihitaji kuwa mbunifu sana ili kutafsiri katika Kislovenia kinachoeleweka.

Harakati za Kupinga Mapinduzi zilitokeza matatizo zaidi. Uchapishaji wa Biblia ulihitaji kufanywa katika nchi nyingine kwa sababu mchapishaji wa Slovenia alikuwa amepelekwa uhamishoni. Ndiyo sababu walihitaji kuficha Biblia walipokuwa wakizileta nchini humo. Lakini licha ya matatizo hayo, Dalmatin alifaulu kutimiza mradi wake katika kipindi cha miaka kumi tu, na yaelekea wakati huo bado alikuwa na umri wa miaka 30 hivi.

Chini ya usimamizi wa Dalmatin, uchapishaji wa kwanza wa nakala 1,500 za Biblia ulifanywa kwa muda wa miezi saba. Watu wengi waliiita Biblia hiyo kitabu bora na maridadi sana kupita vyote, kwa kuwa ilikuwa na picha maridadi 222 zilizochorwa kwa kutumia mihuri ya vipande vya mti. Biblia nyingi za awali bado zipo, na tafsiri hiyo imetumiwa kutafsiri Biblia za kisasa za Kislovenia. Kazi ya wanaume hao wawili imewasaidia sana wenyeji wa Slovenia leo kwa sababu wanaweza kusoma Neno la Mungu katika lugha yao ya asili.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

JINA LA MUNGU

Dalmatin aliandika hivi katika utangulizi wa Biblia Takatifu aliyotafsiri: “Popote ambapo neno BWANA limeandikwa katika herufi kubwa, lamaanisha BWANA Mungu peke yake ambaye jina lake ni יהזה, Yehova, katika lugha ya Kiyahudi. Hilo ni jina la BWANA Mungu peke yake wala si la mwingine.”

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Primož Trubar

Ukurasa wa kwanza wa Biblia ya Kislovenia

[Hisani]

Picha zote isipokuwa jina la Mungu katika Kiebrania: Narodna in univerzitetna knjižnica—Slovenija—Ljubljana

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki