Waromani—Miaka Elfu ya Shangwe na Majonzi
INAFANANA na sherehe kubwa ya arusi ya kitamaduni. Kuna vyakula na vinywaji vingi nao muziki unadunda ndani ya nyumba. Watu wa ukoo wanasongamana ili kuwapongeza bwana na bibi arusi wake aliyejawa furaha. Lakini hii si arusi—ni sherehe ya uchumba inayofanywa katika mkesha wa arusi. Zaidi ya wageni 600 wamekuja kuwatakia kila la heri wachumba hao wawili. Katika sherehe hiyo jamaa ya mwanamume inawapa mahari wazazi wa msichana atakayeolewa. Kesho yake jamaa ya msichana itampeleka kwa mume wake, ambako sherehe nyingine itafanyika kutia ndani arusi yenyewe.
Watu wote wa ukoo wa maharusi wanazungumza Kiromani, lugha ambayo huonwa kuwa ya kigeni kokote watu wa jamii hiyo wanakoishi. Lugha hiyo na lahaja zake, tamaduni nyingi za kale, na mila za arusi, ndizo urithi wa jamii hiyo. Watu wa jamii hiyo wanaishi katika pembe zote za dunia, lakini hawana nchi wala serikali yao wenyewe. Watu hao huitwa Waromani.a
Waromani Ni Nani?
Ili kufahamu lugha, tamaduni, na jamii ya Waromani ilivyoanza tunahitaji kurudi nyuma miaka 1,000 hivi huko India kaskazini. Lugha yao, bila kutia ndani maneno ambayo yamekopwa hivi karibuni, ni ya asili ya Kihindi. Haijulikani vizuri kilichowafanya wahame India. Wasomi fulani wanaamini kwamba mababu zao walikuwa mafundi na watumbuizaji katika vikosi vya askari waliohama makwao baada ya vita kukomeshwa. Vyovyote vile, Waromani walifika Ulaya kupitia Uajemi na Uturuki kabla ya mwaka wa 1300 W.K.
Huko Ulaya, watu wengi wana maoni yanayotofautiana sana kuhusu Waromani. Kwa upande mmoja, wametukuzwa sana katika vitabu vya hadithi na sinema wakisemwa kuwa wakaribishaji, wasio na mahangaiko, na wazururaji ambao huonyesha waziwazi shangwe na majonzi yao kupitia nyimbo na dansi zao. Kwa upande mwingine, wameshutumiwa wakisemwa kuwa wasioaminika, watu wa kiajabu-ajabu, na wajanja—wageni wa kudumu, wanaojitenga na jamii jirani. Ili kuelewa kwa nini watu wana maoni hayo kuwahusu, acheni tuzungumzie maisha ya Waromani wa kale.
Kipindi cha Kubaguliwa
Katika Enzi za Kati, Wazungu wengi waliona vijiji au miji yao kuwa ndio ulimwengu mzima. Wazia jinsi walivyofikiri walipoona familia za Waromani zikiingia vijijini mwao kwa mara ya kwanza. Bila shaka, mambo mengi sana yaliwashangaza. Mbali na kuwa na ngozi, macho, na nywele nyeusi, wageni hao walikuwa na mavazi, tabia, na lugha tofauti kabisa na ya wenyeji nao walipenda kujitenga na watu wengine—tabia ambayo huenda ilianza walipokuwa wakiishi katika jamii zilizogawanywa kitabaka huko India. Makumi ya miaka baadaye, wenyeji wa Ulaya ambao mwanzoni walishangazwa na Waromani walianza kuwashuku.
Waromani walitengwa kabisa na jamii, hivyo walilazimika kupiga kambi kandokando ya vijiji nao wakakatazwa wasiingie vijijini hata ikiwa walitaka tu kununua vitu au kuteka maji. Uvumi ulienezwa kwamba wao “huiba watoto na hata kuwala!” Kulingana na sheria za sehemu fulani Waromani walihitajiwa kupikia nje ili yeyote aliyetaka aweze kuchunguza kilichokuwa katika vyungu vyao. Mara nyingi uchunguzi huo ulifanywa kwa kumwaga chakula chote ardhini. Haishangazi kwamba Waromani wengi waliiba chakula ili waendelee kuishi.
Ili kukabiliana na ubaguzi huo, Waromani walikuwa na mahusiano ya karibu sana. Kwa karne kadhaa, Waromani wamepata utegemezo na shangwe katika vifungo vya familia. Kulingana na mila za Waromani, wazazi huwajali sana watoto wao, nao watoto huwajali sana wazazi wao na kuwatunza wanapokuwa wazee. Pia wengi wao hushikilia sana viwango vya kitamaduni kuhusu mwenendo na tabia.
Kuhamahama
Kwa kuwa mara nyingi Waromani hawakukaribishwa, iliwabidi wahamehame. Maisha hayo ya kuhamahama yaliwawezesha kujifunza taaluma nyingi kama vile uhunzi, biashara, na utumbuizaji. Walifaulu kuruzuku familia zao kwa kufanya kazi hizo. Baadhi ya wanawake Waromani walisemwa kuwa wana uwezo wa kusoma akili za watu nao wakajifanya kuwa wana uwezo huo ili wajinufaishe kifedha. Pia, maisha yao ya kuhamahama yalipunguza uwezekano wa kufisidiwa kitamaduni au kimaadili kwa kushirikiana sana na gadje. Waromani huwaita watu ambao si wa jamii yao gadje.b
Wakati huohuo, Waromani walianza kuteswa kwa sababu ya ubaguzi. Walifukuzwa kutoka maeneo fulani ya Ulaya. Katika maeneo mengine, kwa karne kadhaa walifanywa kuwa watumwa. Katika miaka ya 1860, utumwa huo ulikomeshwa nao wakatapakaa katika maeneo mengi, wengi wao wakihamia Ulaya kaskazini na Marekani. Kokote walikoenda, waliendeleza lugha, utamaduni, na vipawa vyao.
Wajapodharauliwa, kwa kadiri fulani Waromani walipata uradhi kwa kucheza michezo ya kuigiza, dansi, na kuimba. Huko Hispania mchanganyiko wa utamaduni wao na wa jamii nyinginezo ulitokeza muziki na dansi ya flamenko, ilhali huko Ulaya Mashariki, wanamuziki Waromani waliimba nyimbo za kitamaduni za eneo hilo kwa mtindo wao wa pekee. Sauti zenye hisia za muziki wa Waromani ziliwaathiri hata watungaji wa muziki wa klasiki kama vile Beethoven, Brahms, Dvořák, Haydn, Liszt, Mozart, Rachmaninoff, Ravel, Rossini, Saint-Saëns, na Sarasate.
Waromani Katika Ulimwengu wa Leo
Leo kati ya Waromani milioni mbili hadi tano, au zaidi kulingana na maoni ya wengi, wanaishi katika karibu kila pembe ya dunia. Wengi wanaishi Ulaya. Wengi wao hawahamihami, na baadhi yao ni matajiri. Lakini katika maeneo mengi, Waromani ni maskini na wenye uhitaji, na mara nyingi wao hawana makao mazuri.
Wakati wa utawala wa Kikomunisti huko Ulaya Mashariki, sera za kisiasa zilisisitiza raia wote wawe na usawa. Serikali zilijitahidi na kufaulu kwa kadiri fulani kuwazuia Waromani wasihamehame kwa kuwapa kazi na nyumba zilizojengwa na serikali. Nyakati nyingine hatua hiyo iliboresha afya na maisha ya watu. Lakini hisia na maoni mabaya ambayo yalikuwapo kwa karne nyingi kati ya Waromani na watu wasio Waromani hayakubadilika.
Katika miaka ya 1990, mabadiliko ya kisiasa huko Ulaya Mashariki yaliwafanya watu watarajie mema. Lakini mabadiliko hayo yalitonesha majeraha ya zamani kwani misaada ya serikali ilipunguzwa na sheria dhidi ya ubaguzi zikaachiliwa, na hivyo Waromani wakajikuta tena katika hali ngumu kijamii na kiuchumi.
Kupata Tumaini na Maisha Mazuri
Hali ilikuwa hivyo Andrea, msichana mwenye nywele nyeusi zinazong’aa alipoenda shule huko Ulaya Mashariki. Alikuwa mwanafunzi wa pekee mwenye asili ya Kiromani katika darasa lao. Ajapokuwa jasiri, anajitahidi bila mafanikio kuzuia machozi yake anapokumbuka jinsi alivyodhihakiwa na kubaguliwa. “Kila mara ningekuwa wa mwisho kuchaguliwa timu ya michezo ilipokuwa ikiundwa,” Andrea anakumbuka. “Nilitaka kukimbilia India ambako ningefanana na wengine. Siku moja mtu fulani alimwambia rafiki yangu hivi kwa sauti, ‘Rudi India!’ Rafiki yangu akajibu, ‘Ningerudi ikiwa ningekuwa na pesa.’ Hakuna mahali palipokuwa salama kama nyumbani. Hatukukaribishwa popote.” Andrea aliyekuwa na kipawa cha kucheza dansi, alitarajiwa kuwa mashuhuri, na hivyo kukubaliwa na wengine. Lakini akiwa kijana, alipata kitu kizuri zaidi.
“Siku moja msichana fulani anayeitwa Piroska, ambaye ni Shahidi wa Yehova, alikuja nyumbani kwetu,” Andrea anasema. “Alinionyesha kupitia Biblia kwamba mbali na kuwapenda wanadamu kwa ujumla Yehova anampenda mtu mmojammoja. Alinieleza kwamba ninaweza kuwa na uhusiano mzuri na Mungu ikiwa ningetaka. Hilo lilinifanya nihisi ninathaminiwa sana na mtu fulani. Kujua kwamba watu wote ni sawa machoni pa Mungu kulinifanya nijiamini zaidi.
“Piroska alinipeleka kwenye mikutano ya Mashahidi, ambako nilikutana na Waromani na watu wasio Waromani na niliweza kuhisi kuwa wana umoja miongoni mwao. Nilipata marafiki wazuri miongoni mwa Mashahidi wa jamii zote mbili. Baada ya kujifunza Biblia na Piroska kwa karibu mwaka mmoja na nusu, mimi pia nikawa Shahidi wa Yehova.” Leo Andrea na mume wake ni wahubiri wa Injili wa wakati wote, wanaofundisha wengine kuhusu jinsi Mungu anavyowapenda sana watu wa mataifa yote.
“Waliniona Kuwa Sawa Nao”
Anapofikiria siku zake za ujana, Hajro, ambaye ni mwanamume Mromani anasema hivi: “Urafiki pamoja na wavulana ambao hawakutii sheria ulinitia mashakani mara nyingi. Siku moja polisi walinitia nguvuni kwa kuwa niliiba kitu fulani nikiwa na vijana hao. Waliponipeleka nyumbani, nilimwogopa mama yangu zaidi ya nilivyowaogopa polisi, kwani kama kawaida ya familia za Waromani, nilifundishwa kwamba ni kosa kumwibia mtu.”
Alipokuwa mtu mzima, Hajro na familia yake walikutana na Mashahidi wa Yehova. Ahadi ya Biblia kwamba Ufalme wa Mungu utawaondolea wanadamu matatizo kama vile chuki na ubaguzi, iligusa sana moyo wa Hajro. “Waromani hawajawahi kuwa na serikali yao wenyewe ili kushughulikia masilahi yao,” anasema. “Hiyo ndiyo sababu ninahisi Waromani wanaweza kuthamini zaidi jinsi Ufalme wa Mungu utakavyowafaidi wanadamu wote. Hata sasa ninafaidika. Tangu nilipoingia ndani ya Jumba la Ufalme, nilihisi kama mtume Petro aliposema: ‘Kwa hakika ninaona kwamba Mungu hana ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye anamwogopa na kutenda uadilifu anakubalika kwake.’ (Mdo. 10:34, 35) Wote waliniona kuwa sawa nao. Sikuamini masikio yangu watu wasio Waromani waliponiita phrala, yaani, ‘ndugu’ katika Kiromani!
“Mwanzoni, wengine katika jamaa yetu walinipinga. Hawangeweza kuelewa mabadiliko niliyofanya ili maisha yangu yapatane na kanuni za Biblia. Lakini watu wetu wa ukoo na Waromani wameona kwamba kushikamana kwa uthabiti na viwango vya Mungu, kumeniletea furaha na kutokeza mambo mengi mazuri. Wengi wao wangetaka kuboresha maisha yao pia.” Sasa Hajro ni mzee Mkristo na mhubiri wa Injili wa wakati wote. Pia Meghan, mke wake ambaye si Mromani, anawafundisha Waromani na wengine jinsi Biblia inavyoweza kuwasaidia kuwa na maisha yenye furaha, sasa na wakati ujao. “Nimekubaliwa kabisa katika jamaa na jamii ya mume wangu,” anasema. “Wanafurahi kwamba mtu asiye Mromani anawajali sana.”
[Maelezo ya Chini]
a Katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, Waromani wamepewa majina kama vile Wajipsi, Zigeuner, Tsigani, Cigány, na Gitanos. Hayo yote huonwa kuwa majina ya dharau. Waromani wengi hujiita Rom (wingi ni roma), neno linalomaanisha “mwanamume” katika lugha yao. Baadhi ya watu wanaozungumza Kiromani wanaitwa kwa majina tofauti kama vile Sinti.
b Ijapokuwa Waromani fulani hushikilia sana mambo mengi ya kitamaduni, mara nyingi wamefuata dini za walio wengi katika maeneo wanamoishi.
[Blabu katika ukurasa wa 24]
Leo Waromani wanaishi katika karibu kila pembe ya dunia
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Wakati wa utawala wa Nazi huko Ulaya, inakadiriwa kwamba Hitler aliua Waromani 400,000 au zaidi katika kambi zake za vifo, na pia aliua Wayahudi, Mashahidi wa Yehova, na watu wengine. Katika 1940, kabla hata habari za jitihada za maangamizi za Hitler hazijaenea sana, Charlie Chaplin, mwigizaji ambaye ana asili ya Kiromani, alitengeneza sinema iitwayo The Great Dictator, ambayo ilimkashifu kwa dhihaka Hitler na serikali yake ya Nazi. Wasanii wengine maarufu wanaodai kwamba wana asili ya Kiroma wanatia ndani waigizaji Yul Brynner, Rita Hayworth (chini), mpaka rangi Pablo Picasso (chini), mwanamuziki wa jazi Django Reinhardt, na mwimbaji Mmakedonia Esma Redžepova. Isitoshe, Waromani wamekuwa mainjinia, madaktari, maprofesa, na wabunge.
[Hisani]
AFP/Getty Images
Photo by Tony Vaccaro/Getty Images
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Mashahidi Waromani
Waromani wengi wamekuwa Mashahidi wa Yehova. Baadhi yao ni wazee wa makutaniko na pia mapainia, yaani, wahubiri wa wakati wote. Wakuu wa serikali katika maeneo yao na watu wengine ambao si Waromani huwaona kuwa mifano mizuri. Shahidi Mromani huko Slovakia anasema hivi: “Siku moja jirani fulani ambaye si Mromani alibisha hodi mlangoni petu. ‘Ndoa yangu imo mashakani, lakini nina hakika kwamba mnaweza kunisaidia,’ akasema. ‘Kwa nini sisi?’ tukamwuliza. Akajibu, ‘Ikiwa Mungu mnayemwabudu anaweza kuwasaidia ninyi Waromani kuboresha maisha yenu, yaelekea anaweza kutusaidia sisi pia.’ Tulimpa kitabu fulani kinachotegemea Biblia kuhusu familia ambacho kimechapishwa na Mashahidi wa Yehova.
“Baadaye mke wake alibisha hodi mlangoni na kutoa ombi lilelile, bila kujua kwamba mume wake alikuwa amemtangulia. ‘Hakuna mtu mwingine yeyote katika jengo hili anayeweza kutusaidia,’ akasema. Tulimpa kitabu kilekile. Kila mmoja wao alitusihi tusimwambie mwenzake kwamba alitutembelea. Mwezi mmoja na nusu baadaye, tulianza kujifunza Biblia na mtu huyo na mke wake. Kuishi kulingana na kweli za Biblia kumewafanya watu watuheshimu sana hivi kwamba wao hutujia ili kupata msaada wa kiroho.”
[Picha]
Narbonne, Ufaransa
Granada, Hispania
“Waromani wanaweza kuthamini zaidi jinsi Ufalme wa Mungu utakavyowafaidi wanadamu wote.”—Hajro
[Picha katika ukurasa wa 22]
Poland
[Hisani]
© Clive Shirley/Panos Pictures
[Picha katika ukurasa wa 22]
Mromani huko Uingereza, 1911
[Hisani]
By courtesy of the University of Liverpool Library
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
Slovakia
[Picha katika ukurasa wa 23]
Makedonia
[Hisani]
© Mikkel Ostergaard/Panos Pictures
[Picha katika ukurasa wa 24]
Rumania
[Picha katika ukurasa wa 24]
Makedonia
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Jamhuri ya Cheki
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Hispania
[Picha katika ukurasa wa 25]
Andrea alitarajia kuwa mashuhuri na kukubaliwa na wengine kwa kuwa mchezaji dansi
[Picha katika ukurasa wa 24 zimeandalia na]
Romania: © Karen Robinson/Panos Pictures; Macedonia: © Mikkel Ostergaard/Panos Pictures; Czech Republic: © Julie Denesha/Panos Pictures