SEHEMU YA 6
Kuzaliwa Yesu Mpaka Kufa Kwake
Malaika Gabrieli alitumwa kwa msichana mzuri jina lake Mariamu (Maria). Akamwambia ya kuwa angezaa mtoto ambaye angetawala milele akiwa mfalme. Mtoto huyo, Yesu, alizaliwa katika boma la ng’ombe, ambamo wachungaji walimtembelea. Baadaye, nyota ikaongoza watu kutoka Mashariki mpaka kwenye mtoto mchanga. Twajifunza aliyeonyesha nyota hiyo, na namna Yesu alivyookolewa asiuawe.
Halafu, Yesu akiwa mwenye miaka 12, twamwona akizungumza na waalimu katika hekalu. Miaka kumi na minane baadaye Yesu anabatizwa, kisha aanza kazi ya kuhubiri Ufalme na kufundisha ambayo Mungu alimtuma duniani aifanye. Ili wamsaidie kazi hiyo, Yesu alichagua wanaume 12 akawafanya mitume wake.
Pia Yesu alifanya miujiza mingi. Alilisha maelfu ya watu samaki wachache na mikate michache. Aliponya wagonjwa na hata kufufua wafu. Mwishowe, twajifunza mambo mengi yaliyompata Yesu siku ya mwisho ya kuishi kwake, na namna alivyouawa. Yesu alihubiri muda wa miaka mitatu na nusu, basi Sehemu ya 6 inazungumza kipindi cha miaka mingi kidogo kuliko 34.