Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w75 4/1 kur. 162-166
  • Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa —Ujeremani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa —Ujeremani
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Vichwa vidogo
  • MATUKIO YA KWANZA YA KIDINI
  • WENGINE WALIKUWA WAKIITAFUTA KWELI
  • KUSHIKAMANA NA KWELI KWA IMARA
  • NDUGU RUSSELL AZURU UJEREMANI TENA
  • MAGUMU JUU YA UANGALIZI WA KAZI
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
w75 4/1 kur. 162-166

Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa

​—Ujeremani

UJEREMANI imetumia maongozi makubwa katika historia. Watu wake wana sifa ya kuwa wafanya kazi wenye bidii na watiifu kwa mamlaka. Sifa hizi zimesaidia sana kukuza uchumi wa taifa, hata leo Ujeremani ya Magharibi, ikiwa na idadi yake ya zaidi ya watu milioni 60, ni mojawapo ya nchi za ulimwengu zenye viwanda vikubwa sana. Inaendesha biashara yake katika sehemu zote za dunia. Na ili kutimiza mahitaji ya uchumi wake unaositawi, katika miaka ya karibuni imekuwa lazima kuingiza nchini zaidi ya wafanya kazi wageni milioni tatu kutoka Ugiriki, Yugoslavia, Italia, Spania, Ureno, Uturuki na nchi nyingine.

Maongozi ya Ujeremani yameonwa kwa njia nyingine pia. Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, tangu 1914 mpaka 1918, majeshi ya Kijeremani yalisonga mashariki na kuingia Urusi, na magharibi kupitia Ubelgiji na kuingia Ufaransa. Kabla ya vita kwisha, yalikuwamo vitani kushindana na mwungano wa mataifa 24 kuzunguka dunia. Ujeremani ilishindwa. Lakini muda mfupi kabla yake askari mwenye maarifa wa vita hiyo, Adolf Hitler, alianza kupata mamlaka. Kufikia 1933 yeye alifanywa mkuu wa Ujeremani, akiwa mkuu wa National Socialist Party. Baada ya kuwa cheoni muda mfupi alitiisha watu wa Ujeremani kwa utawala wa kuogofya, na 1939 akaingiza ulimwengu katika vita nyingine ya dunia, yenye kutia mataifa mengi zaidi na yenye uharibifu mwingi zaidi kuliko ya kwanza.

Makanisa yalikuwa yanafanya nini haya yote yalipokuwa yakitokea? Kila Jumapili viongozi wa dini wa Katoliki waliomba baraka za Mbingu juu ya Milki ya Ujeremani. Je! viongozi wa dini wa Kiprotestanti waliteta? Badala yake, mwaka wa 1933 wote pamoja waliapa kuunga mkono Serikali ya Nazi kabisa. Na katika mwaka wa 1941, muda mrefu baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili kuendelea, Protestant Evangelical Church (kanisa la Kiprotestanti) katika Mainz, Ujeremani, lilimshukuru Mungu kwa kuwapa watu mtu aitwaye Adolf Hitler.

MATUKIO YA KWANZA YA KIDINI

Kwa kupendeza, hapa Ujeremani, ndipo Martin Luther alipogongomea mlango wa kanisa katika Wittenburg maneno ya ubishi Oktoba 31, 1517, kwa kupinga mazoea aliyoamini yalikuwa hayapatani na Neno la Mungu. Lakini karibuni mateto ya kidini yalikingamana na mapendezi ya kisasa, na kabla sana ya karne ya 20, matengenezo ya Kiprotestanti na Kanisa la Katoliki pia yalikuwa yamejitambua kuwa sehemu ya ulimwengu.

Ikiujua ubora wa kueneza habari njema kwenye sehemu za mbali zaidi za dunia, katika mwaka wa 1891 Watch Tower Society ilifanya mipango Ndugu Russell asafiri kwenye nchi nyingine kuamua uwezekano wa kupanua kazi. (Matendo 1:8) Wakati wa safari yake Ndugu Russell alizuru Berlin na Leipzig. Lakini baadaye alitoa habari hizi: “Hatuoni lo lote la kututia moyo tuvune katika Italia wala Austria wala Ujeremani.” Hata hivyo, baada ya kurudi kwake, mipango ilifanywa kuchapa vitabu na vikaratasi kadha katika Kijeremani. Watu waliokuwa wamehamia United States kutoka Ujeremani na waliokuwa wamesoma vitabu vya Sosaiti walivituma kwa jamaa na rafiki zao katika Ujeremani, wakiwatia moyo wavitumie katika mafunzo yao ya Biblia.

WENGINE WALIKUWA WAKIITAFUTA KWELI

Mwaka wa 1905 Ndugu Lauper aliacha nakala yake ya mwisho katika nyumba ya mwanamume mzee wa Kibaptist aitwaye Kujath alipokuwa akifanya kazi karibu na Berlin akigawa matoleo ya The Watch Tower. Mwanawe Gustav majuzi alikuwa amerudi kutoka kusanyiko la Kibaptist akiwa amechukizwa sana na onyo kali alilopewa mhubiri wa Kibaptist aitwaye Kradolfer, ambaye kwa ghafula alikuwa ameanza kufundisha kwamba nafsi yaweza kufa. Kwa kuona hivyo, Gustav alianza kuichunguza Biblia, akamkaribisha baba yake na rafiki zake wachunguze ukweli wa shauri hili pamoja naye. Katika Agosti wa mwaka wa 1905 Gustav Kujath alimzuru baba yake, aliyeishi umbali wa safari ya saa moja, na baba yake akakaza fikira zake kwenye nakala hii ya pekee ya The Watch Tower aliyokuwa ameiacha Ndugu Lauper. Hiki ndicho kitu walichokuwa wamekuwa wakitafuta hasa. Kilikuwa “chakula kwa wakati wake.”​—Mt. 24:45.

Kujath aliandikisha nakala za The Watch Tower mara hiyo na kuanza kukopesha wengine mafungu matano yake. Baada ya muda fulani watoto wake wakawa wanachukua nakala moja moja tena, ndipo yeye akawapa watu wengine wenye kupendezwa. Hivyo watu wengi walipata ujumbe. Kwa vyepesi alichukiwa na Wabaptist, akafukuzwa nao mwanzoni mwa mwaka mpya wa 1905, kwa maneno haya: “Wewe unafuata njia ya Ibilisi.” Baadaye, zaidi ya jamaa zake kumi waliliacha Kanisa la Baptist.

Kujath mdogo alikuwa ameelewa pia kwamba haiwapasi Wakristo waache kukutana pamoja. Kwa hiyo, aliiandikia afisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Elberfeld akiomba anwani za wengine ambao angeweza kukutana nao na kujifunza nao. Ndugu Kotitz aliweza kumpa anwani ya Bernhard Buchholz tu mwenye umri wa miaka kumi na tisa katika Berlin, ambaye Kujath alionana naye mara moja. Wakati huo Buchholz alikuwa wa kikundi kiitwacho “Kundi la Mwokozi.” Alikuwa amemaliza tu kuchoma vitabu Millenial Dawn akiwa na maoni ya kwamba yeye hakuwa mtu wa pekee katika Berlin aliyestahili kupata kweli, kwa kuwa alikuwa yatima na mkosa kazi kwa sababu ya uasi mdogo. Lakini Kujath alimtia moyo ajifunze vitabu hivyo naye, na hata alimtia moyo awe kolpota, kama mapainia walivyokuwa wakiitwa zamani. Muda mfupi baadaye Kujath alimpeleka nyumbani mwake.

Ili aweze kupata fedha ya kuenezea habari njema katika eneo hili, Kujath aliacha mipango ya kujenga nyumba mpya. Aliuza mali iliyokuwa ambapo nyumba hiyo ingalijengwa akazitumia fedha zilizopatikana kwa njia hii kugeuza vyumba viwili katika nyumba ya baba yake viwe chumba ambamo mikutano ingeweza kufanyiwa. Kufikia mwaka wa 1908 iliwezekana kufanyiza kikundi kidogo cha kuanzia watu 20 mpaka 30.

Karibu wakati ule ule mheshimiwa aitwaye von Tornow mwenye mashamba makubwa katika Urusi alianza kutafuta kweli. Akiwa amechukizwa na maisha ya ufisadi kati ya matajiri wa Urusi, alikuwa ameamua kwenda Afrika kupitia Switzerland na kutumikia huko kama mmisionari. Alipokuwa akiondoka, mtu fulani alimtolea mojawapo ya trakiti za Watch Tower Society. Sasa, badala ya kuelekea Afrika, kesho yake aliondoka akapate vitabu zaidi vya namna hii. Hii ilikuwa karibu mwaka wa 1907.

Katika mwaka wa 1909 alitokea katika kundi la Berlin amevalia mavazi yake bora akifuatana na mtumishi wake mwenyewe. Alikata tamaa alipoona namna mahali pa kukutania palivyokuwa hafifu na namna watu aliokutana nao huko wasivyojidai makuu wala kujivuna, kwa maana alikuwa na maoni ya kwamba kweli hizo zenye thamani kubwa sana zilistahili pia watu wawe na sura ifaayo ya nje. Lakini aliyosikia yalimvuta. Miezi mingi baadaye, alirudi alipokwisha kuondoa maono yake; walakini, sura yake sasa haikuwa ya kutokeza sana, kwa maana alikuja bila mtumishi wake na alivalia kwa kiasi zaidi. Baadaye alikubali kwamba pengine asingalirudi kama asingalisoma katika Biblia hivi: “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia . . . mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”​—1 Kor. 1:26-29.

Akiwa amesadiki sasa kwamba alikuwa ameiona kweli, alirudi Urusi, akauza mali yake yote, na kukaa Dresden. Akiwa na nia ya kuishi maisha ya kiasi, alikuwa tayari kutoa utajiri wake wote kwa utumishi wa Yehova.

KUSHIKAMANA NA KWELI KWA IMARA

Herman Herkendell alifahamu kweli mwaka wa 1905 kupitia kwa trakiti aliyokuwa ameiona katika chumba cha garimoshi. Yeye alikuwa mwalimu kijana na alikuwa akielekea Jena akaendelee na masomo yake katika chuo kikuu huko. Walakini, yaliyokuwamo katika trakiti hii yalimvuta sana hata karibuni akaliacha Kanisa la Kilutheri. Hii ilifanya akatazwe asifundishe dini shuleni. Karibuni baadaye alifutwa kutoka cheo chake cha ualimu.

Katika mwaka wa 1909 Ndugu Herkendell alikuwa tayari anatumikia kama badala ya Ndugu Kotitz kwa kutembelea makundi, na, mwishoni mwa mwaka, jina lake lilitokea kwa mara ya kwanza katika The Watch Tower kwa habari ya safari iliyoshauriwa aiwakilishe Sosaiti kama mmoja wa “wahaji.” Mwaka wa 1911 alioa binti wa Ndugu Jander, mwenyeji tajiri wa kiwanda cha ufinyanzi. Dada Herkendell mdogo alimwomba baba yake awape pesa za safari isiyo ya kawaida ya fungate. Walitaka kuzitumia wakiuhubiri ujumbe wa Ufalme kwa watu wa Urusi wenye kusema Kijeremani. Afisi ya Barmen iliwapa anwani zilizopatikana za Warusi-Wajeremani. Safari hii ilikuwa ya miezi mingi na ilikuwa ya kujitahidi kweli, kwa maana mara nyingi ilichukua saa nyingi kutoka kituo cha magari-moshi kufika walikoishi ndugu na watu wenye kupendezwa. Hawakuwa na gari lao wenyewe, na mawasiliano kwa barua na habari kwa simu yalikuwa hayategemeki. Kwa hiyo ni mara chache sana walipochukuliwa kutoka kituo cha magari-moshi. Ni vijana wangapi waliooana leo wawezao kufunga safari kama hiyo ya fungate?

Kwa muda mfupi wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza Ndugu Herkendell alipendelewa achukue madaraka ya Afisi ya Barmen. Halafu baada ya vita alitumikia tena kama mhaji, akafa mwaka wa 1926 akiwa uhajini (katika safari).

Ripoti ya kila mwaka ya 1908 ilipokusanywa, ilitia moyo kuona kwamba kwa mara ya kwanza trakiti nyingi zilizogawa zilikuwa zimetolewa kwa kipekee na wasomaji wa Watch Tower wenyewe na chache sana kwa njia ya magazeti. Walakini, ni kwa njia hii iliyotajwa mwisho kijana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na minane alivyopata kweli katika Hamburg. Alipomaliza shule alianza kusoma Biblia kila siku, akiwa na tamaa nyofu ya kuielewa. Miaka mingi ilipita na katika mwaka wa 1908 alipata trakiti yenye kichwa “Uuzaji wa Haki ya Uzaliwa.” Hii ilimpendeza kijana huyo sana. Bila ya kusikiliza dhihaka za wafanya kazi wengine, aliiandikia Sosaiti mara hiyo katika Barmen akiomba vitabu sita vile vya Studies in the Scriptures. Muda mfupi baada ya hapo alipata nafasi ya kukutana na Ndugu Kotitz, aliyemkaribisha aje Barmen wakati fulani. Kijana huyo aliukubali ukaribishaji, akieleza kwamba ziara ya Barmen ingekuwa siku ya ubatizo wake. Hii ilitukia wakati huo, mwanzoni mwa mwaka wa 1909. Mwangalizi wa tawi alimchukua rafiki huyo kijana, sasa akiwa ndugu yetu, kwenye kituo cha magari-moshi na kumwuliza kabla hajapanda gari-moshi kama angependa kufanya upainia. Ndugu yetu kijana alisema kwamba Sosaiti ingepata habari kwake akifika.

Ndugu huyu kijana alikuwa Heinrich Dwenger. Karibuni alipanga mambo yake aweze kuanza upainia Oktoba 1, 1910. Makumi ya miaka iliyofuata amekuwa na pendeleo la kutumikia katika karibu kila idara ya karibu kila makao ya Betheli ya Watch Tower Society Ulaya. Pindi kwa pindi alifurahia kusafiri kwa niaba ya Sosaiti na mara nyingi akawa badala ya waangalizi wa tawi nyakati zenye magumu. Wengi wamepata kumpenda nao wamjua yeye kama mfanya kazi mwenye mafaa. Kwa sasa ana umri wa miaka 86 naye afurahia kuwa na afya njema kiroho na kimwili pia baada ya kipindi kisichokatizwa cha zaidi ya miaka 60 ya utumishi wa wakati wote.

NDUGU RUSSELL AZURU UJEREMANI TENA

Katika mwaka wa 1909 maendeleo zaidi ya tengenezo yalifanywa afisi ilipohamishwa kwenye makao makubwa zaidi katika Barmen. Hii ilimaanisha kwa vyepesi gharama zingeongezeka. Bila kukawia Ndugu Cunow aliuza mali yake akazitumia pesa kununua vifaa vya makao ya Betheli. Mengi pia yalifanywa mwaka wa 1909 kwa ujenzi wa kiroho. Katika Februari akina ndugu katika Saxony walipanga Ndugu Kotitz atoe hotuba nyingi za watu wote. Aliweza kutoa ushuhuda kwa walau watu 250 kufikia 300 mara sita.

Lakini tukio lililokuwa zuri zaidi la mwaka wa 1909 bila shaka ni ziara iliyotazamiwa kwa muda mrefu ya Ndugu Russell ya Ujeremani. Baada ya kutua katika Hamburg kidogo, alifika Berlin akalakiwa na kikundi cha ndugu. Mara hiyo walikwenda kwenye chumba cha kusanyiko kilichopambwa vizuri, ambako ndugu 50 kufikia 60 hivi walikuwa wamekuwa wakingojea kufika kwa Ndugu Russell. Ndugu Russell alisema juu ya kurudishwa kwa alichopoteza Adamu, hasa akionyesha pendeleo ambalo wale wenye matumaini ya kuwa washiriki wa mwili wa Kristo wangepokea. Walipoisha kula pamoja, walikwenda Hohenzollern Hall, ambako hotuba ya watu wote ilipaswa itolewe. Ilijaa pomoni! Kundi la watu 500 liliisikiliza hotuba “Wafu Wako Wapi?” Ililazimu karibu watu 100 wasimame. Wengine 400 walizuiwa kwa sababu ya ukosefu wa nafasi, lakini walipewa trakiti nje ya jumba. Baadaye, katika Dresden, walau watu 900 kufikia 1,000 hivi waliisikia hotuba ya watu wote ya saa mbili ya Ndugu Russell. Aliendelea na safari akafika Barmen, ambako karibu watu elfu moja waliisikia hotuba yake. Alasiri iliyofuata ndugu 120 walikusanyika katika Bible House, na jioni hiyo watu 300 wakakusanyika kumsikia Ndugu Russell akijibu maulizo ya Biblia. Hii ilimalizia ziara ya Ndugu Russell ya Ujeremani, na muda mfupi baada ya saa 5 usiku huo akapanda gari-moshi kwenda Switzerland, ambako kusanyiko la siku mbili lilipaswa lifanywe Zurich.

Mwaka huo akina ndugu katika Ujeremani walitiwa moyo watumie mali zao na nguvu zao kuitegemeza kazi ya Ufalme katika Ujeremani bila ya msaada wa kutoka nje. Mwishoni mwa mwaka gharama (bei) za uchapaji, usafirishaji, shehena, vitu vilivyoingizwa, gharama za hotuba za watu wote na za kusafiria, kodi ya nyumba, taa, vifaa vya kupasha nyumba moto, na gharama nyingine, zilikuwa zimejumlika kuwa mark 41,490.60, hali michango ilijumlika kuwa mark 9,841.89 tu, ikiacha hasara ya mark 31,648.71, iliyolipwa kwa pesa zilizotoka makao makuu ya Brooklyn. Hii ilimfanya Ndugu Russell aseme yafuatayo katika ripoti yake ya kila mwaka: “Lo! Sosaiti imetumia kiasi kikubwa namna gani kujulisha kweli katika Ujeremani. . . . Jitihada zilizotiwa katika Ujeremani ni kubwa zaidi kuliko katika nchi nyingine yo yote. Imetupasa tutazamie matokeo ya kiasi icho hicho​—isipokuwa kama wingi wa Wajeremani walio wakf wamekwisha hamia United States.”

Ndugu Russell alitua kidogo kwa saa kumi katika Berlin akiwa katika safari yake ya ulimwengu ya mwaka wa 1910 na kuhutubia watu 200 waliokuwa wanamngoja alipofika.

Karibu wakati huu Emil Zellmann, kondakta wa gari, kutoka Berlin, alianza kuvuta fikira za watu sana. Alitumia vema kila nafasi kusoma Biblia au kutolea abiria wake ushuhuda, nyakati nyingine hata katikati ya vituo vya gari; wakati mmoja alipokuwa na shughuli ya kusoma alifurahisha abiria wake kwa kupaza sauti, si kutaja kituo cha gari kilichofuata, bali “Zaburi 91,” aliyokuwa amekuwa akiisoma wakati huo. Karibuni zaidi ya makondakta kumi wenzake na jamaa zao walikuwa wanahudhuria mikutano. Kikundi hiki kidogo lakini chenye kutenda sana kilifanya mengi katika kueneza habari njema katika Berlin. Ingawa ndugu hawa walianza kufanya kazi asubuhi saa 11, mara nyingi bidii yao bora iliwafanya waende kwenye kituo kikuu cha magari ya kusafiria saa mbili mapema wakaangushe trakiti juu ya viti vya magari ya kusafiria yaliyokuwa yakichunguzwa.

Uliokuwa wenye kufurahisha sana mwishoni mwa mwaka ulikuwa uhakika wa kwamba gharama za kazi zingeweza kulipwa kwa michango ya kujitolea, hata kiasi kidogo kikawa kinabaki. Hivyo akina ndugu katika Ujeremani walifikia mwisho wa mwaka wenye baraka tele wakisadiki kwamba mwaka mwingine wa utendaji wenye bidii ulikuwa mbele, mwaka ambao wengi walifikiri ungekuwa ‘mwaka wa mwisho wa mavuno.’

Lakini vita ilileta magumu, ya kwanza yakatokea mawasiliano na Amerika yalipokatizwa kwa muda.

MAGUMU JUU YA UANGALIZI WA KAZI

Sasa watu wa Mungu katika Ujeremani walikuwa wanaingia katika kipindi cha mikazo mikubwa, chenye magumu juu ya uangalizi wa kazi. Kuelekea mwisho wa mwaka wa 1914, karibu miaka kumi na mmoja baada ya Ndugu Russell kumpa Ndugu Kotitz mamlaka ya kuja Ujeremani akaangalie kazi hapa, alishambuliwa kwa ghafula tokea pande mbalimbali na kushtakiwa juu ya mambo yasiyofaa. Hii ilileta wasiwasi kati ya akina ndugu na kumfanya Ndugu Russell amwondolee cheo chake cha utumishi.

Uhitaji wa ndugu zaidi wahaji katika Ujeremani ulikuwa umemfanya Ndugu Russell atume ndugu aitwaye Conrad Binkele kutoka United States, aliyekuwa mhubiri wa Kimethodist hapo kwanza na aliyekuwa amefahamiana na The Watch Tower karibu mwaka mmoja tu, atumikie katika cheo hiki, ingawa Ndugu Russell alikuwa amefanya hivyo akisita-sita tu. Ndugu Binkele alifika Ujeremani wakati tu magumu kati ya watumishi yalipoanza kuwa mazito, na katika mwaka wa 1915 alikabidhiwa uangalizi wa kazi katika Ujeremani.

Walakini, karibuni Ndugu na Dada Binkele walirudi United States. Maneno yao ya kwa heri yalionyeshwa kwa herufi kubwa katika ukurasa wa mwisho wa Watch Tower la Oktoba, yakiwa na maelezo ya kwamba ‘hali zilikuwa zimelemea nguvu zao kufikia upeo.’ “Hali” hizi pengine zilikuwa magumu yaliyoendelea kuongezeka wakati wa mwaka wa 1915. Katika Oktoba Ndugu Russell alijiona alikuwa na lazima ya kuuangalia ugumu kwa pekee na kuushughulikia ilivyo lazima. Barua yenye kichwa “Barua ya Kipekee kutoka kwa Ndugu Russell kwa Wanafunzi wa Biblia wa Ujeremani” ilisema ifuatavyo:

“Brooklyn, Oktoba 1915

“Ndugu Wapenzi:

“Mimi nawafikirieni katika sala zangu na tamaa yangu yenye shauku ni kwamba Bwana apate kuwabariki. Twawasikitikieni katika dhiki za vita zinazowapata moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Pia twataka kuonyesha masikitiko yetu kwenu kwa habari ya dhiki mlizozipata kwa kutafuta faida za kweli katika Ujeremani. Si juu yetu kuhukumiana wala kuadhibu kwa kutangaza hukumu ya mwisho. Ndugu wenye kukosa wakitubu, lazima turidhishwe na kumwachia Bwana hukumu ya mwisho na adhabu ambaye amesema hivi: ‘Bwana atawahukumu watu wake.’ Ebr. 10:30.

“Hata hivyo kwa faida za kweli, haki na mwenendo ufaao, na kwa ajili ya maongozi yanayotumiwa na wajumbe wa Sosaiti yaelekea kuwa lazima kuweka wajumbe wapya wa Sosaiti katika Ujeremani. Vita imesababisha mambo fulani yasiyofaa, utumishi wa usafirishaji na wa habari za simu si wa kawaida na yafahamika kwamba kutoelewana fulani juu ya uongozi katika Barmen kulitokea kwa muda. Sisi twaamini kwamba Ndugu yetu mpenzi Binkele alifanya yote aliyoweza na kushughulika na mambo ifaavyo chini ya hali zenyewe. Lakini kama mjuavyo Ndugu Binkele amerudi Amerika.

“Twataka kuwafahamisha ndugu wa Ujeremani kwamba tangu sasa na kuendelea mambo ya Sosaiti yatasimamiwa na halmashauri ya ndugu watatu; Ernst Haendeler, Fritz Christmann na Reinhard Blochmann. . . .

“Ndugu wapenzi, napendekeza katika kila jambo mshirikiane na kuunga mkono uongozi mpya katika Barmen. Mwili wa Kristo ni mmoja, msiruhusu migawanyiko katika mwili, hata kama vile Mtume atuonyavyo kwa upole.”

Lakini mpango huu haukufanyika kama ulivyopangwa, kwa maana Ndugu Blochmann alikuwa amelazimishwa kuondoka Barmen, na Ndugu Haendeler alikuwa amekufa hata kabla barua ya Ndugu Russell kufika Ujeremani. Kwa kuwa msukosuko haukwisha miezi iliyofuata, katika Februari wa mwaka wa 1916 Ndugu Russell aliweka “halmashauri ya uangalizi” yenye ndugu watano, H. Herkendell, O. A. Kotitz, F. Christmann, C. Stohlmann na E. Hoeckle.

“Mpango huu wa halmashauri ya uangalizi” haukuendelea kwa muda mrefu hata hivyo. Miezi michache tu baada ya halmashauri kukusanywa tena, Ndugu Binkele, ambaye kwa sasa alikuwa amerudi Ulaya na kuanza kukaa Zurich, Switzerland, aliwekwa atumikie kama mjumbe wa kisheria wa Ujeremani, Switzerland na Netherlands, naye Ndugu Herkendell akapewa daraka la kazi ya usimamizi wa habari za kuandikwa magazetini.

Ndugu Kotitz, ambaye nafasi yake ilikuwa imechukuliwa mwaka wa 1914 na Ndugu Binkele, alikuwa amekuwa akionyesha Photo-Drama (sinema) tangu wakati huo. Walakini, aliendelea kuwa lengo la shambulio kutoka kwa akina ndugu wakiwa na kusudi la kutimiza tamaa zao za kichoyo, badala ya kushiriki kuleta amani ya ndani ya tengenezo. Elisabeth Lang, ambaye kwa miaka mingi alikuwa amefanya kazi na Ndugu Kotitz, alimwona wakati mmoja amekalia kiti cha bustani akiwa mwenye huzuni karibu na jumba ambako Photo-Drama ilikuwa ikionyeshwa. Alimwambia kwamba kwa mara nyingine alipokea barua yenye mashtaka kwa wazi ikiwa na kusudi la kumnyang’anya mapendeleo yake ya mwisho ya utumishi yaliyokuwa yamebaki. Alieleza namna alivyokuwa amekuwa na pendeleo la kufanya kazi kando ya Ndugu Russell kwa karibu miaka kumi kabla hajagawiwa daraka la kusimamia kazi katika Ujeremani. Walakini, sasa alijichunguza sana mara nyingi aone kama alikuwa amestahili kabidhi hii. Walakini, alijifariji kwa wazo hili: “Ikiwa nimesaidia mtu mmoja tu astahili kuwa mmoja wa 144,000 kwa sababu ya miaka yangu 24 ya utendaji, basi nimekuwa na pendeleo la kufanya sehemu moja kwa 144,000 ya kazi.”

Yaeleweka kwamba mashambulio haya yaliyoendelea kufanywa yaliidhuru afya yake, iliyokuwa imedhoofishwa sana na pafu lililopasukia Berlin. Hivyo ikawa kwamba Septemba 24, 1916 alikufa akiwa mwenye umri wa miaka 43. Tangazo la Sosaiti katika The Watch Tower lilitaja “uaminifu” wake na kusema kwamba “bidii yake, uvumilivu wake, uthabiti wake, imani yake na nia yenye nguvu, wakf wake na utimizo mwaminifu wa wajibu vinashukuriwa na kuthaminiwa na ndugu wote wapenzi.”

Muda mfupi baadaye ndugu Wajeremani walipata habari kwamba Oktoba 31, karibu juma tano baada ya Ndugu Kotitz kufa, Ndugu Russell pia alikuwa amemaliza mwendo wake wa kidunia. Wengine walihuzunishwa sana na jambo hili hata wakauacha mwendo wao na kuacha imani. Lakini walio wengi waliziona habari za kufa kwa Ndugu Russell kama kitia moyo cha kutumia nguvu zao na wakati wao kwa wingi zaidi waendeshe kazi waliyokuwa wameianza.

Vita ilifanya iwe lazima kufanya mabadiliko mengine katika uangalizi. Kuanzia Oktoba 1916 mpaka Februari 1917, Paul Balzereit alitumikia katika cheo hiki; kuanzia Februari 1917 mpaka Januari 1918, Ndugu Herkendell; na kuanzia Januari 1918 mpaka Januari 1920, Ndugu M. Cunow, ambaye ndipo nafasi yake ilipochukuliwa na Ndugu Balzereit.

Habari hii itaendelea katika toleo lifuatalo la Mnara wa Mlinzi.​—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki