Wakosa Kuvumiliwa kwa Mara Nyingine
APRILI 25, 1974 ilifika. Hali ya siasa katika Ureno na katika nchi zake za ng’ambo ilibadilika upesi sana. Mapinduzi Lisbon yalimaliza miaka 48 ya utawala wa kutumia nguvu yakatetemesha utawala wa Kireno.
Kulielekea kuwa na matumaini makubwa zaidi ya kupata uhuru katika Ureno na katika nchi zake za ng’ambo. Watu Msumbiji walifurahi. Mashahidi wa Yehova wenyewe walitaka kujua kama watatoka katika mateso ya karibu miaka 40.
Serikali ya muda iliwekwa Msumbiji kutayarisha kuyapa majeshi ya Frelimo utawala wote kufika Juni 1975. Wakati huo kulipokuwa na uhuru mdogo Mashahidi wa Yehova waliweza kujifunza Biblia hadharani. Hata walifanya makusanyiko makubwa na watu wote walikaribishwa kuhudhuria.
Kwa mara ya kwanza, Aprili mwaka wa 1975, waliweza kuwa na kusanyiko la mchanganyiko wa Waafrika na weupe katika Lourenço Marques. Hilo lisingaliwezekana chini ya utawala wa kutumia nguvu wa Kireno. Mashahidi walifurahi kuweza kushirikiana kwa njia ya Kikristo bila ya mtengano wo wote wa kikabila.
Lakini sasa majeshi ya kisiasa yalianza kutia mkazo watu waonyeshe hadharani kwamba wanaunga mkono siasa. Vikundi vya watu vilikwenda huko na kule vikiomba wote wahudhurie mikutano ya kisiasa nao wahudhuriaji walipaswa kupaza sauti wakisema “Viva Frelimo” (“Frelimo Kidumu”) na kuinua ngumi yao ya mkono wa kuume (kama inavyofanywa katika saluti ya Kikomunisti).
Mashahidi wa Yehova walichukua msimamo gani? Wao walibaki bila kuingilia siasa. Walichukua msimamo ule ule ambao Mashahidi wa Yehova walichukua Italia wakati wa utawala wa Mussolini watu walipotazamiwa kupaza sauti wakisema “Viva il Duce” (Kiongozi Aishi Maisha Marefu) na kumpa Mfasisti (mpinga Ukomunisti) huyo saluti. Walifanya kama Mashahidi wa Yehova wa Ujeremani walivyofanya walipotazamiwa kupaza sauti wote wakisema “Heil Hitler” (Mtukuze Hitler) kisha kumpa Mnazi huyo saluti. Walifanya kama ndugu zao katika nchi zenye kukaliwa na Wajapan walivyofanya wakati wa vita ya ulimwengu ya pili watu walipoamriwa wainame kwa kumwabudu mfalme wa Japan.
Naam, msimamo wao ulikuwa kama uliochukuliwa Uingereza, United States, Ureno, Spania na katika kila nchi nyingine iliyo katika uso wa dunia. Waliendeleza kutokuwamo kwao kwa Kikristo katika siasa bila kujali wangepatwa na magumu ya namna gani kwa sababu ya kukataa kupaza sauti wakitaja misemo ya kisiasa au kupiga saluti (kutoa salamu) za kisiasa. Maelfu walikaa miaka mingi katika kambi za mateso za Ujeremani au katika kambi za Siberia kulikokuwa na kazi ya ukatili.
Lakini Mashahidi wa Yehova wa Msumbiji, kama wa nchi nyingine zote ulimwenguni, waliendelea kuheshimu wakuu wa Serikali, kupatana na amri ya Biblia iliyo katika Warumi 13:1. Nao walionyesha heshima hiyo kwa kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu bila kujaribu kuepa, kwa kuendelea kuwa wafanya kazi wenye bidii na wenye kutegemeka, na kwa kuendelea kuwa raia wenye kutii sheria. Hawakukosa kutii sheria zo zote isipokuwa zile zilizopinga waziwazi sheria za Mungu mwenyewe zilizoandikwa katika Neno lake, Biblia. Matokeo yakawa nini?
Katika Katiba ya Msumbiji, iliyoanza kutumiwa Juni 25, 1975, kifungu cha 33 husema:
“Serikali imetoa uhakikisho kamili wa kuwapa raia wote wa Jamhuri ya Msumbiji uhuru wa kufanya mambo yao wenyewe. Uhuru huo unatia ndani kutoingiliwa nyumbani wala usiri wa barua nao hauwezi kupunguzwa, isipokuwa katika visa vya pekee vinavyoruhusiwa na sheria.
“Katika Jamhuri ya Msumbiji Serikali imehakikishia kabisa raia zake uhuru wa kufuata au wa kutofuata dini yao.”
Kifungu cha 25 cha Katibu hiyo chasema hivi:
“Katika Jamhuri ya Msumbiji hakuna mtu anayeweza kukamatwa wala kupelekwa ahukumiwe isipokuwa kwa sheria. Serikali hutoa uhakikisho kamili wa kumpa mshtakiwa haki ya kulindwa.”
Je! maneno haya yana ukweli? Yaliyowapata Mashahidi wa Yehova Msumbiji yafanya hilo liwe ulizo zito.
Karibu mwezi mmoja kabla ya kutangazwa kwa uhuru kamili wa nchi, kundi la Mashahidi wa Yehova la Chonguene, maili chache kutoka mji wa João Belo lilikutana Jumapili kujifunza Biblia kama kawaida. Kikundi cha watu, Wakatoliki na Waprotestanti, kikaja katika mkutano wa kujifunza Biblia kikielekea kwenye mkutano wao wa kisiasa, kikaukatiza na kuwauliza wahudhuriaji sababu ya kutohudhuria kwao mkutano wa kisiasa. Wakawaacha Mashahidi baada ya kuwatisha.
Siku chache baadaye, Mei 23, magari ya polisi yenye kuchukua askari wa Frelimo yalifika yakazingira wanaume sita waliokuwa wamehudhuria mkutano wa Mashahidi wa kujifunza Biblia. Amiri akaagiza watu wake wawachape na kuwapiga mateke wanaume sita hao kisha wawapeleke gerezani.
Huko gerezani wanaume hao walipigwa kila siku kujaribu kuwalazimisha waseme “Viva Frelimo.” Watatu kati yao walikuwa watu walioanza kupendezwa karibuni tu wala hawakuwa Mashahidi waliobatizwa. Watu hao watatu walikubali kufanya walivyoagizwa walipopigwa. Wale watatu waliokuwa Mashahidi waliobatizwa walikataa kabisa kutenda kinyume cha dhamiri zao za Kikristo. Ndipo walipotolewa nje wakaagizwa kuchimba shimo lenye urefu wa kutosha kuweza kusimama ndani. Wakalazimishwa kusimama ndani ya shimo hilo vichwa tu vikitokeza, wakaambiwa kwamba wakiendelea kukataa kutaja msemo ule wa kisiasa wangepigwa risasi na kuzikwa mumo humo. Lakini wao wakasimama imara wasitende kinyume cha dhamiri zao. Mwishowe walirudishwa gerezani.
Linalofurahisha ni kwamba, Waziri wa Ulinzi wa Lourenço Marques alipopashwa habari hizo alishangaa akampigia simu amiri wa Frelimo katika eneo hilo. Baada ya muda mfupi Mashahidi hao wakaachiliwa. Lakini hilo ni tendo moja tu lililo jema kati ya matendo mengine mabaya sana.
Siku ya Uhuru, Juni 25, 1975, katiba mpya ilianza kufuatwa kwa bidii nyingi. Je! mashambulio ya ukatili juu ya uhuru wa dini kama lile lililosimuliwa sasa hivi yangekwisha? Je! nia ya maendeleo na elimu ingeondolea mbali matendo ya upumbavu ya kutowavumilia watu hawa?
SHUGHULI YA JEURI YAANZWA
Jibu lilipatikana upesi, baada ya siku chache tu. Shughuli ilianzwa nchini mwote ya kusingizia Mashahidi wa Yehova. Mashambulio mengi yalifanywa kwa njia ya kutolewa kwa hotuba radioni na magavana wa wilaya na wanasiasa wengine.
Vikundi vya wenye kuchochea wengine wafuate siasa vilitia fitina Mashahidi wa Yehova wa sehemu mbalimbali wakakamatwa na kupelekwa kwenye makao makuu ya Frelimo wakahojiwe. Mara nyingi walipigwa. Kwa mfano, fikiria lililopata kundi la Mashahidi wa Yehova katika Choupal katika wilaya ya Lourenço Marques Septemba 13, 1975:
Mzee mgeni wa Mashahidi wa Yehova, Elias Mahenye, alikuwa akitolea watu karibu 300 hotuba ya Biblia katika Jumba la Ufalme la kundi hilo. Mwishoni mwa hotuba yake, wanachama wa mahali hapo wa kikundi cha kuchochea watu wafuate siasa waliingia jumbani wakajaribu kukatiza mkutano. Kwa imara na kwa uungwana wakaambiwa kwamba mkutano haujakwisha, wakaombwa wangoje.
Hata kabla kundi halijamaliza kusema “Amina” kwa sala ya mwisho wachochezi hao wakapanda jukwaani wakadai kundi lote lipaze sauti kusema “Viva Frelimo.” Wakadai mara tatu jambo hilo lifanywe lakini hawakuitikiwa. Kisha wakaagiza kundi libaki jumbani wanapokwenda kuita askari wa Frelimo.
Amiri wa askari alipofika, akauliza padre ni nani. Akaelezwa kwamba Mashahidi hawana padre; lakini, Mahenye akasema ndiye aliyekuwa akitoa hotuba. Yeye na wengine wanne wakasimamishwa jukwaani, wakavuliwa nguo kutoka viunoni kwenda juu na kuagizwa wapaze sauti wakisema “Viva Frelimo.” Walipokataa, walipigwa vibaya sana kisha wakafungwa kwa seng’enge za umeme. Mikono ya Mahenye hata sasa ina makovu katika sehemu za mikono yake zilizokatwa na seng’enge hizo.
Watu hao watano wakapelekwa kwenye makao ya majeshi ya karibu, naye Mahenye akashitakiwa kuwa aliambia watu waseme “Frelimo Chini”—uongo mtupu. Kisha askari wakampiga kwa ngumi na matako ya bunduki. Halafu wote watano wakapigwa kwa mishipi ya askari. Wakafungiwa katika choo kichafu-chafu usiku huo. Saa 10 alfajiri na mapema wakatolewa nje wakapigwa tena. Mahenye akashitakiwa kwa uongo kuwa alizoeza askari wapige Frelimo halafu akapigwa tena. Baadaye ilikubaliwa kwamba shtaka hilo halikuwa na msingi.
Wakati wa mchana, sergeant wa Frelimo alifika akahoji watu hao. Akawaambia: “Msiposema ‘Viva Frelimo,’ Frelimo hawatakubali mwendelee kukaa nchini. Kwa sababu wao walipigana miaka kumi, hawakumpigania Yehova, wala hawakupata msaada wo wote kutoka kwa Yehova. Yampasa kila mtu aseme ‘Viva Frelimo,’ kwa sababu Frelimo ndiye mungu wa Msumbiji kisha bunduki ndiye mungu wa pili wa Msumbiji. Sisi hatutaki kusikia lo lote juu ya Yehova.”
Namna gani juu ya wengine katika kundi, kutia na wanawake, wazee wa umri na watoto waliokuwa wameachwa katika Jumba la Ufalme? Walilazimishwa kubaki humo usiku kucha. Wengi walipigwa wakafungwa kwa seng’enge. Pamoja na hayo askari walipaza sauti wakisema: “Yehova huyu wenu ndiye nani? Mbona haji na kuwasaidieni?”
Wakati wa saa 24 hizo, hakuna mtu aliyeruhusiwa kulala, kunywa maji, kula wala kwenda kujisaidia, hata wanawake na watoto. Biblia na vitabu vya kusaidia kujifunza Biblia vilivyotumiwa mikutanoni vikachomwa. Ilikuwa kana kwamba Msumbiji imekuwa Ulaya ya zamani wakati watu waliponyang’anywa mali zao zikachomwa na wakati Baraza Kuu ya Kikatoliki ilipohukumu wazushi wa dini na kuwatesa vikali. (Nyakati hizo huitwa Middle Ages na Catholic Inquisition.) Mwishowe Mashahidi waliruhusiwa kuondoka, wakatishwa kwamba wasipojifunza kusema “Viva Frelimo” wangesumbuliwa zaidi.
Katika Magude, kaskazini ya Lourenço Marques, Mashahidi kumi na watatu walikamatwa, wakapigwa na kulazimishwa kuchimbua miti kwa vidole vyao. Halafu wakafungwa miguu na mikono yao wakabingirishwa-bingirishwa kama mapipa. Kama katika Rumi ya kale, wakaaji wa hapo waliombwa waje kuona Wakristo wakiteswa vibaya.
Karibu na Manjacaze, washiriki kadha wa makundi mawili madogo ya Mashahidi wa Yehova walifungwa. Halafu gavana wa wilaya ya Gaza akaja akaomba Mashahidi waliobaki wahudhurie mkutano wa watu wote. Wakakubali. Baada ya kuhutubu juu ya kazi za mashamba, gavana akawaomba Mashahidi wote kwa ghafula waje mbele. Wakafanya hivyo. Gavana akaagiza wakamatwe, wanaume na wanawake pia. Wakapigwa sana, wengine wakapigwa vibaya sana hata damu ikawatoka katika masikio na wengine katika macho. Wakapelekwa gerezani.
Katika wilaya iyo hiyo ya Gaza, kikundi cha mashahidi kilipigwa kila siku kwa zaidi ya miezi mwili, ili kujaribu kuvunja ukamilifu wao!
Lakini visa vyote hivyo vilikuwa mwanzo tu. Baada ya juma chache agizo rasmi lilitolewa: Mashahidi wa Yehova wote walio nchini wakamatwe.
Agizo hilo lilifuatwa kwa utaratibu na bila huruma. Wafuasi wa Frelimo walikwenda nyumba kwa nyumba wakadai wakaaji waseme “Viva Frelimo.” Waliokataa walichukuliwa kuwa Mashahidi wa Yehova nao walipelekwa gerezani. Jamaa nzima, watoto wakiwamo, ziliburutwa bila huruma.
Hii yamaanisha kwamba ni maelfu ya Mashahidi wa Yehova waliotiwa gerezani Msumbiji. Imekuwa vigumu sana kuonana nao wenyewe. Lakini, Mashahidi wengine waliweza kukimbilia nchi za ujirani. Wanasema kwamba jela za eneo la mji mkuu Lourenço Marques, sasa “zimejaa pomoni.” Kwa kuwa magereza yamejaa, Mashahidi wamewekewa kambi ya pekee karibu na kaburi liitwalo St. Jose’s Cemetery. Kwa kuwa hakuna mahali pa kukaliwa na watu wengi hivyo, wengi sana wamelazimika kulala nje bila blanketi. Hawapewi chakula. Wakuu wanaruhusu watu wa ukoo walete chakula siku za Alhamisi na Jumapili tu. Wageni hao wenye huruma wanakuwa katika hatari ya kukamatwa wakikataa kusema “Viva Frelimo.”
Kwa wazi wakuu wamepanga kupeleka Mashahidi wengi wanaume kwenye miji ya kaskazini kama Nampula na Quelimane. Huko watatumiwa kama watumwa wa kujenga majengo. Watoto watapelekwa kwenye shule za kisiasa wapate mafundisho ya chama cha Frelimo. Matangazo ya radio yasema kwamba Mashahidi walio na pesa benki watanyang’anywa. Nyumba na magari zitachukuliwa na serikali.
Kabla hawajaanza kukamatwa kwa wingi sana, washiriki karibu 30 wa kundi la Mashahidi wa Yehova la Xinavane waliitwa wakahutubiwa kwa saa kadha. Mashahidi walipotumia Biblia kueleza sababu yao ya kukataa kujitia katika siasa na kupaza sauti wakitaja misemo ya kisiasa, amiri wa Frelimo aliwafanyia mzaha, akisema: “Mimi nampa Yehova wenu dakika tano aibomoe nyumba hii.” Akaacha dakika tano zikapita, kisha akasema: “Mimi niko tayari kupambana na Yehova wenu kwa bunduki. Askari wa Kireno walisali wapate ushindi wakashindwa. Frelimo walipiga vita bila Yehova wakashinda. Sisi tutamshinda Yehova. Sisi hatulitaki jina lake Msumbiji.”
Hiyo ni sawa na vile farao wa Misri ya kale alivyosema kwa kujisifu: “[Yehova] ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa ruhusa waende zao? Mimi simjui [Yehova], wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.”—Kut. 5:2.
Basi, ulizo lenyewe hasa ni nini Msumbiji?
MAULIZO YANAYOPASWA KUJIBIWA UPESI
Serikali mpya ya Msumbiji imetangaza kwamba inapendelea mawazo bora mengi. Kati ya mawazo hayo bora kuna wazo la kuwapa watu elimu bora (wakoloni Wareno waliacha idadi ya watu 90 kwa mia bila kujua kusoma wala kuandika), wazo la kuondolea mbali umalaya na ulevi, kuondolea watu uonezi. Kwa kweli, Mashahidi wa Yehova husaidia sana katika mambo hayo.
Katika Mexico peke yake wamesaidia watu 48,000 wakajua kusoma na kuandika miaka 28 iliyopita. Katika Nigeria zaidi ya watu 5,000 walisaidiwa kwa njia hiyo miaka minne iliyopita. Na ndani ya Msumbiji yenyewe watu 3,930 walifundishwa kusoma na kuandika na Mashahidi wa Yehova miaka miwili tu iliyopita! Kwa hiyo, katika habari hii hakuna watu wanaofikiria elimu zaidi kuliko Mashahidi wa Yehova.
Je! watu wakisema misemo ya kisiasa na kutoa ishara, kanuni za adili za watu zitakuwa bora? Je! kufanya hivyo kulifanya kanuni hizo zikawa bora katika Ujeremani ya Nazi au katika Italia ya Ufasisti au katika sehemu nyingine yo yote ya dunia katika kipindi cho chote cha historia ya kibinadamu? Mambo ya hakika yaonyesha hakukufanya hivyo, na kufikiri kuzuri kwaonyesha isingaliwezekana.
Je! kunaweza kuwa na hakika kwamba kodi zitalipwa kwa sababu ya kusema misemo na kutoa ishara za kisiasa? Je! wenye kutoa sauti kubwa zaidi ndio waaminifu zaidi katika ulipaji wa kodi? Ukosefu wa kulipa kodi katika nchi nyingi waonyesha kwamba kuonyesha nje-nje tu kwamba mtu anatukuza taifa hakuhakikishi kabisa kwamba hataepa asilipe kodi. Tena, Mashahidi wa Yehova wameheshimiwa kabisa katika nchi zote kwa sababu ya kulipa kodi kwa uaminifu, kwa sababu ya uaminifu na kutegemeka kwao katika mambo ya biashara.
Namna gani wale wanaojaribu kupotoa mambo wakiyafunika yasionekane yalivyo hasa kwa porojo za kutaka wachache wachukiwe? Kwa hakika wao ndio wanaostahili kuitwa ‘wenye kupinga maendeleo na maenezi ya ujuzi, hasa kwa kutumia usemi wa kuvuruga sana, desturi, n.k.’ Wale wanaokosa kuvumilia uhuru wa msingi wa wengine hutumia njia za zamani sana kama ilivyo historia yenyewe ya matendo ya ukatili.
Wale wanaojaribu kufanya Serikali iendelee kuabudiwa kwa kuondolea wanadamu uhuru wao mbalimbali wanafuata kielelezo cha maelfu ya miaka iliyopita, cha nyakati za milki za Ashuru na Babeli ya kale. Kwa kweli mwendo huo unarudisha watu nyuma, hauwapi maendeleo ya kweli wala hauenezi ujuzi. Ukweli una nguvu za kutosha hata usihitaji kutumia njia hizo.
Je! wewe waamini kwamba Serikali imepaswa kuwa na haki ya kuongoza mawazo yote ya raia zake? Au waamini kwamba watu wamepaswa kuwa na haki ya kuabudu kulingana na dhamiri zao?
Ikiwa hukubaliani na jitihada za chama kimoja kutumia nguvu ili watu wafuate wazo la kisiasa, ikiwa wewe unahurumia wale wanaotaabika kwa sababu ya kushikamana na imani zao zinazoongozwa na dhamiri, unaweza kupeleka telegram au barua kwa mmoja au wengi wa wakuu wa serikali ya Frelimo katika Jamhuri ya Msumbiji.