Alitiwa Mafuta na Nani na kwa Kitu Gani?
(Funzo la Kitabu hs 5:20-37)
1. Mwana mzaliwa wa kwanza wa Mariamu alizaliwa wapi, na kwa sababu gani?
WAKATI wa utawala wa Kaisari Augusto, mtawala wa Milki ya Rumi ya upagani, Yesu alizaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi, kutimiza unabii wa Mika 5:2. Hiyo ilikuwa mapema katika vuli ya mwaka wa 2 kabla ya Wakati wetu wa Kawaida. Wakati Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu wakijiandikisha, “akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”—Luka 2:7.
2. Ni nani waliofanywa kuwa mashahidi wa kidunia waliojionea kwa macho yao, usiku wa kuzaliwa kwa Yesu, na kwa namna gani?
2 Masihi aliyekuwa akitazamiwa akawa amefika! Hizo ndizo habari zenye kusisimua ambazo malaika mtukufu wa Mungu alitangazia wachungaji waliokuwa wakichunga makundi yao usiku katika wanja karibu na Bethlehemu. “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo.” Ingawa Yesu aliyezaliwa karibuni katika hori Bethlehemu hakujua, “mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Halafu wachungaji waliopashwa habari hizo wakaenda wakimtafuta mtoto katika hori wakampata, na hivyo walithawabishwa kwa kuwa mashahidi wa kuzaliwa kwa Yesu usiku huo wenye maana sana.—Luka 2:8-20.
3. Yesu alipata kuwa vile malaika alivyomwita, “Kristo Bwana,” wakati gani na kwa namna gani?
3 Yesu huyu akawa “Kristo Bwana” wakati gani? Si siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake, alipotahiriwa. Hakutiwa mafuta siku hiyo. Alitiwa mafuta alipokuwa wa miaka 30. Alimwendea Yohana Mbatizaji, ambaye wakati huo alikuwa akibatiza watu katika Mto Yordani. Hakumwomba Yohana amtie mafuta rasmi ya halisi awe mfalme wa Kimasihi juu ya makabila yote kumi na mawili ya Israeli. Alimwomba ambatize katika maji, kama alivyokuwa amefanyia Wayahudi wengine wengi miezi ya utendaji wa Yohana hadharani. “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; [roho takatifu ikashuka] juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”—Luka 3:21-23.
4. Yohana Mbatizaji alitoaje ushuhuda kuhusiana na namna Yesu alivyofanywa kuwa Kristo?
4 Baadaye nabii Yohana alitolea ushuhuda wanafunzi wake juu ya hilo, alipowaambia: “Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye [utaona roho ikishuka] na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa [roho takatifu]. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.”—Yohana 1:33, 34.
5. Andrea alimwaambia ndugu yake kwamba alikuwa amemwona nani, naye Nathanaeli alikubali Yesu kuwa nani?
5 Karibu siku 40 baada ya Yesu kubatizwa katika Mto Yordani, Yohana alieelekeza fikira za wanafunzi wawili wake kwenye Yesu. Walimfuata wakakubali maagizo ya Biblia aliyowapa. Mmoja wao, Andrea, alipofurahi sana na jambo alilogundua, alimtafuta ndugu yake aliyeitwa Petro akamwambia: “Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo).” Muda mfupi baadaye mtu aitwaye Nathanaeli aliletwa kwa Yesu, Nathanaeli alimwambia: “Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.” Huo ulikuwa uhakikisho wa Nathanaeli kwamba Yesu aliyetiwa mafuta alikuwa ndiye Masihi, Kristo.—Yohana 1:35-49.
MASIHI AU KRISTO WA KIROHO
6. Ujapokuwa ubatizo wa Yohana ulikuwa kwa wenye dhambi, ni kwa sababu gani Yesu alibatizwa?
6 Kwa kuwa Yesu alipokuwa duniani alikuwa Mwana wa Mungu wa kibinadamu kabisa na hakuwa na dhambi za kutubia, kwa sababu gani alizamishwa na mwanadamu aliyekuwa akihubiri ubatizo wa toba na msamaha wa dhambi? Alifanya hivyo ili kutimiza unabii wa Zaburi 40:6-8. Ubatizo wake katika maji ulifananisha kujitoa kwake kabisa ‘kufanya mapenzi yako, Mungu,’ kwa sababu angefunuliwa mapenzi hayo tangu wakati huo. (Waebrania 10:5-10) Mapenzi hayo ya kimungu yangemwongoza jinsi ya kutenda kama Masihi au Kristo.
7. Yaliyosikiwa yakisemwa na sauti ya Mungu kutoka mbinguni yalionyesha badiliko gani katika maisha ya Yesu, na kwa sababu gani hili lilikuwa jambo la lazima kwake?
7 Yesu alipokuwa akitoka katika maji aliyobatizwa kwayo, sauti ya Mungu ilisikiwa kutoka mbinguni, ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (Mathayo 3:17) Hiyo ilionyesha badiliko katika maisha ya Yesu. Kwa njia gani? Tangazo la Mungu lilimaanisha kwamba sasa alikuwa amemzaa Yesu mwenye miaka 30 awe Mwana wa Mungu wa kiroho. Hivyo njia ilifunguliwa kwa Mwana wa Mungu huyu arudi mbinguni. Ilikuwa lazima hata Yesu azaliwe hivyo ndipo aweze kwenda mbinguni. Ni kama vile alivyomweleza Nikodemo baadaye aliyekuwa mtawala Myahudi: “Mtu asipozaliwa mara ya, pili hawezi kuuona ufalme wa Mungu. . . . Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa [roho], hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa [roho] ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.”—Yohana 3:3-7.
8. Tangazo la Mungu kutoka mbinguni kuhusu Mwana wake, lilionyesha jambo gani kuhusiana na Yesu, nao uhusiano wa Yesu na Mariamu ulibadilikaje sasa?
8 Kupitia kwa tangazo lililofanyiwa mbinguni Yehova Mungu alitangaza kwamba alikuwa amezaa Mwana wa kiroho mwenye tumaini la kuingia katika ufalme wa Mungu wa mbinguni. Mariamu mama ya kilichokuwa mwili, hakuwa mama ya huyu Mwana wa Mungu wa kiroho, na tangu wakati huo Yesu hatajwi tena akimwita “mama.” Kwa hiyo Yesu anatajwa kuwa “aliyezaliwa na Mungu” anayekesha akiangalia wanafunzi wake, wafuasi wake. Kwa mfano, katika 1 Yohana 5:18 twasoma hivi: “Mwana mzaliwa wa Mungu humlinda, na Yule Mwovu hamgusi.” (The Jerusalem Bible) “Mwana wa Mungu ndiye humsalimisha, na yule mwovu hawezi kumgusa.” (The New English Bible) Kwa hiyo uhusiano wa Yesu na mama yake wa kidunia, Mariamu, ulibadilika. Tangu wakati huo alijitoa kwa mambo ya kiroho, hakujitoa awe seremala katika mji wa Mariamu wa Nazareti.
9. Kwa hiyo Yesu alitiwa mafuta kuwa Masihi wa namna gani, na atawale kutoka wapi?
9 Roho takatifu ya Mungu ilishuka juu ya Mwana wa Mungu wa kiroho, aliyekuwa ndiyo amezaliwa, na kumtia mafuta awe Masihi au Kristo. Alipaswa kuwa mkuu zaidi kuliko Masihi dhaifu wa kibinadamu mwenye nyama na damu. Alipaswa kuwa Masihi wa kiroho, ambaye mwishowe angetawala katika ufalme wa Mungu wa mbinguni. Wakati ambao Masihi huyu angepanda mbinguni “kiti cha enzi cha Daudi” kingetukuzwa kupelekwa mbinguni. Kwa hiyo lazima awe katika kiti cha enzi cha mbinguni ndipo ‘aimiliki nyumba ya Yakobo hata milele.’—Luka 1:32, 33.
10. Yesu akiwa Mtiwa Mafuta angeweza kuunganisha cheo gani na jina lake, na alitiwa mafuta kwa kitu gani?
10 Baada ya kutiwa mafuta kwa roho takatifu ya Mungu katika Mto Yordani, Yesu angeweza kuunganisha cheo Masihi au Kristo na jina lake, na kuitwa kwa kufaa Yesu Masihi au Yesu Kristo. Miezi mingi baadaye, wakati Yesu alipokuwa akielekea tena Galilaya, mwanamke Msamaria alimwambia: “Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.” Halafu Yesu alimwambia kwa upole hivi: “Mimi ninayesema nawe, ndiye.” (Yohana 4:25, 26) Kama Masihi au Kristo, Yesu alitiwa mafuta, si kwa mafuta rasmi ya halisi yaliyomiminwa juu ya kichwa chake, bali kwa kitu ambacho Mungu peke yake angeweza kumimina juu yake kama Mwana wa kiroho. Basi, ni kitu gani hicho? Mtume Petro ajibu: “Mungu alivyomtia mafuta kwa [roho takatifu] na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi.”—Matendo 10:38.
11. Kama katika habari ya Daudi, mara baada ya kutiwa mafuta Yesu alipatwa na matokeo gani, na kwa sababu gani hakupoteza roho takatifu?
11 Hapa twakumbuka kwamba, baada ya kivulana mchungaji Daudi kutiwa mafuta na nabii Samweli, nguvu ya utendaji ya Mungu ilitenda kazi juu yake afanye mambo makubwa. Vivyo hivyo ndivyo Yesu alivyofanya alipotiwa mafuta kutoka mbinguni, na Mungu. Luka 4:1, 2 yahakikisha hilo: “Na Yesu, hali amejaa [roho takatifu], alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na [roho] muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi.” Marko 1:12 yasema: “Mara [roho ikamtoa] aende nyikani.” Ni jambo lenye kufurahisha kwamba, kwa sababu Yesu aliendelea kuwa mwaminifu katika jangwa alipojaribiwa na Ibilisi, hakupoteza roho takatifu; hakuacha kuwa Masihi au Kristo. Akawa sawa na vile ubatizo wake majini ulivyoonyesha.
12. Baada ya Yohana kufungwa, Yesu alirudi Galilaya chini ya uwezo gani, naye alifanya jambo gani huko?
12 Mwaka wa 30 W.K. Yohana Mbatizaji, mtangulizi wa Yesu, alitiwa gerezani na Herode Antipa, gavana wa sehemu ya nne ya jimbo la Galilaya. Kwa hiyo Yesu aliondoka Uyahudi akapitia Samaria na kurudi Galilaya. Huko Yesu alitumia Maandiko ambayo yangeweza kumtambulisha kuwa Masihi au Kristo. (Mathayo 4:12-17) “Yesu akarudi kwa nguvu za [roho], akaenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.” (Luka 4:14, 15) Mafuta aliyotiwa na Mungu yalimsaidia alipokuwa akifundisha watu Maandiko Matakatifu.
13. Katika sinagogi la Nazarethi, Yesu alisoma kwa sauti unabii gani wa Isaya, na tangu wakati huo maelezo yake yalikuwa gani?
13 Katika sinagogi la mji wa kwao Nazareti, Yesu alikaza fikira za watu juu ya uhakika wa kwamba alikuwa ametiwa mafuta na Mungu kwa utimizo wa unabii wa Isaya 61:1-3 kwa habari ya kuwa Masihi. Juu ya hilo twasoma yafuatayo katika Luka 4:16-21:
“Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho [ya] Bwana [i] juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”
14. Zile “habari njema” alizoamriwa Yesu kuzitangaza zilikuwa juu ya kitu gani, naye alitumwa azitangaze kwa kadiri gani?
14 Lo! ni mwendo mzuri namna gani ambao unabii wa Isaya ulitabiri Mtiwa Mafuta wa Yehova angefuata! Lo! Jinsi nguvu ya utendaji wa Yehova aliyotiwa mafuta kwayo ilivyopaswa kutenda kazi kupitia kwake! Miaka yote mitatu iliyobaki ya utumishi wake wa Kimasihi duniani alitimiza agizo hilo la unabii kutoka kwa Mungu. “Habari Njema” alizotangazia maskini zilikuwa ujumbe wa ufalme wa Mungu wa Kimasihi. Aliambia kundi la watu wenye njaa ya kiroho waliotaka kumweka kizuizini hivi: “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa.”—Luka 4:43.
15. Ni nani walioandamana na Yesu alipokwenda kuhubiri kutoka sehemu moja mpaka nyingine?
15 Maandishi ya baadaye yatuambia hivi: “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale [mitume] Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”—Luka 8:1-3.
16. Yesu aliufanyaje utendaji wa Kiinjilisti kuwa mkubwa zaidi?
16 Si kwamba Yesu mwenyewe alizitangaza habari njema za ufalme wa Mungu tu, bali pia alituma wanafunzi wake wakazihubiri. Baada ya kuwazoeza zaidi ya mwaka, wanafunzi wake kumi na wawili walitumwa wakiwa peke yao wakautangaze ufalme. Luka 9:1, 2 atuambia: “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa.” Mwaka uliofuata Yesu aliongeza wengine 70 katika kundi la kueneza Injili: “Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, . . . Mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.”—Luka 10:1-9.
17. Ni kitu gani ambacho kingekuwa kikiwaongoza wainjilisti hao walipokuwa wakitoa ushuhuda mbele ya mamlaka zenye kutawala, na kwa hiyo kwa sababu gani katika nyakati zetu kutangaza ufalme kumekuwa kusikozuilika?
17 Nguvu ya utendaji ya Mungu ilikuwa ikimwongoza Yesu aliyetiwa mafuta alipokuwa akihubiri. Ingekuwa pia ikiongoza waenezaji hawa wa Injili waliotumwa na Yesu. Isingekosa kuwasaidia wakiitwa mbele ya watawala. Yesu alisema: “Msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni [roho ya] Baba yenu [isemayo] ndani yenu.” (Mathayo 10:18-20; Luka 12:11, 12) Ndivyo ingekuwa kwa wahubiri wa habari njema za ufalme wa Mungu hata wakati huu wa “mwisho wa taratibu ya mambo.” (Mathayo 24:3, 9-14, NW) Ni kwa sababu roho ya Mungu inaongoza kuhubiriwa kwa ufalme wa Kimasihi uliokwisha simamishwa mbinguni ukiwa mikononi mwa Masihi Yesu kwamba wanadamu wameshindwa kukomesha kazi hiyo.—Marko 13:10-13.
18. Ni kisa gani kinachoripotiwa katika Luka 5:17-26 kuonyesha kwamba uwezo wa Yesu haukudhoofishwa na upinzani wa kidini?
18 Kwa kuwa Yesu alitiwa mafuta na Baba yake wa mbinguni, si na wanadamu, “akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” (Matendo 10:38) Upinzani wenye chuki wa viongozi wa dini haukudhoofisha nguvu iliyokuwa ikifanya miujiza. Kwa habari ya kisa kimoja cha ajabu zaidi, imeandikwa hivi: “Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.” Ijapokuwa wanadini hao walikuwa na ukatili, Yesu aliponya mwenye kupooza aliyekuwa hoi, nao watu wenye kustajabu sana wakasema: “Leo tumeona mambo ya ajabu.”—Luka 5:17-26.
19. Yesu alimpa nani sifa kwa miujiza yake, naye aliwaonya washtaki wake wa uongo kuhusu dhambi gani?
19 Yesu alimpa sifa Yeye aliyemwezesha hasa kuponya kwa mwujiza. Kwa hiyo, Yesu aliwaambia wale waliomshtaki kuwa na ushirika mmoja na Shetani Ibilisi, waliyemwita “Beelzebuli mkuu wa pepo,” maneno yafuatayo: ‘Mimi natoa pepo kwa roho ya Mungu.’ Kwa hiyo, aliwaonya wapinzani kwamba ‘kwa kukufuru roho hawatasamehewa. Yeye atakayenena neno juu ya roho takatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.’ Wapinzani hao walitenda dhambi hiyo asiyoweza kusamehewa mtu kwa kuonyesha chuki wakisema Ibilisi ndiye aliyefanya mwujiza, na hali roho takatifu ya Mungu ndiyo iliyoufanya.—Mathayo 12:24-32. —Kutoka Holy Spirit—the Force Behind the Coming New Order, Sura ya 5.