Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w81 2/15 kur. 22-24
  • Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova—Lebanoni na Syria (Shamu)

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova—Lebanoni na Syria (Shamu)
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Vichwa vidogo
  • BARAKA YAKIWAPO MATESO
  • KUENDELEA WAKATI WA VITA VYA WENYEWE KWA WENYEWE
  • WENYE AMANI NA WOTE
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
w81 2/15 kur. 22-24

Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova—Lebanoni na Syria (Shamu)

SiKU moja Dada Lagakos alibisha hodi mlangoni mwa Bi. Kafina Nicolaidou, ambaye alikuwa mwenye kujibidiisha sana kwa ajili ya mapokeo ya Kanisa la Orthodoksi. Kwa kweli, mara tu alipoingia nyumba hiyo, Dada Lagakos aliona ukuta wote ukiwa umefunikwa kwa sanamu na picha za watakatifu wa kidini, kukiwa na taa ndogo yenye kutumia mafuta imewaka mbele yazo. Lilikuwa zoea la mwanamke huyo kupiga magoti na kusali mbele ya vitu hivyo kila siku.

Muda si muda, kwa msaada wa wenzi wawili wa ndoa, Lagakos na mkewe, Bi. Nicolaidou alifanya maendeleo ya kupata maarifa ya Maandiko. Karibuni ukafika wakati wa kuamua la kufanya na picha na sanamu zake zote za kidini. “Pengine naweza kuzipeleka kanisani,” akasema.

“Hasha,” ndilo jibu alilotoa Ndugu Lagakos.

“Basi, nina rafiki wengi wa kidini; nitawapa tu rafiki zangu,” akajibu.

Walakini Ndugu Lagakos akasema hilo vilevile si ndilo jambo la kufanya.”

“Basi,” akauliza, “nizifanyeje?”

“Ala, zapaswa kutendewa kama ambavyo neno la Mungu linavyoagiza,” akaelezwa. “Zapaswa kuvunjwa-vunjwa na kuharibiwa kabisa.”

Huo ulikuwa uamuzi mkubwa kwa mwanamke huyo kufanya baada ya kusali mbele ya vitu hivyo “vitakatifu” kwa miaka mingi sana. Walakini alifanya uamuzi huo, nazo picha na sanamu hizo zilivunjwa-vunjwa zipate kutumiwa kama kuni za kuchemsha maji ya kuogea ya jamaa hiyo.​—2 Fal. 18:1-5.

Wakati Bi. Nicolaidou alipofanya badiliko hilo kubwa maishani naye akawa Shahidi, ujamii wa Kigiriki uliazimia kuharibu biashara yake ya kushona. Wote waliazimia kwamba wasingeshonewa tena naye, na ndivyo walivyofanya. Lakini pasipo hofu, dada huyo mpya baada ya muda mfupi akaona kwamba alikuwa na wanunuzi wengi zaidi kuliko wakati wo wote uliotangulia. Naye vilevile alikuwa na uhusiano wenye thamani pamoja na Yehova Mungu! Zaidi ya hayo, yeye na mumewe walilea watoto wao katika kweli.

BARAKA YAKIWAPO MATESO

Muda mfupi baada ya kurudi Lebanoni kutoka Damasko, wamisionari wawili, wenzi wawili wa ndoa, walipewa mgawo huko Zahle, mji fulani katika Bonde Kubwa kama maili 32 (kilometres 51) kaskazini mwa Mlima Hermoni unaotajwa katika historia. Ulikuwa mji wa Kikatoliki kwa sehemu kubwa, ukiwa na ujamii mkubwa kiasi wa Orthodoksi ya Ugiriki na Waislamu wengi. Sehemu kubwa ya Zahle ilipata ushuhuda kwa muda wa miezi sita hivi. Mara nyingi walitupiwa mawe, baadhi yake yakawapiga. Iwapo wamisionari hao walikuwa wanatembea kupitia shule fulani wakati wa kupumzika, walitupiwa chungu nzima ya mawe yenye kufuatana yaliyotoka upande wa uwanja wa kuchezea.

Wamisionari hao walipokuwa wakitembea kupitia barabara za Zahle, jina ambalo watu walipenda kuwaita lilikuwa Shuhoud Yahwah (“Mashahidi wa Yehova”). Hata hivyo, wakaaji wa hapo walikuwa wamejifunza Yehova ni nani nao walitambua alikuwa na mashahidi katika kijiji hicho.

Ikatokea kwamba miaka mingi baadaye, katika kusanyiko la Kikristo huko Beirut, wamisionari ambao walikuwa wametumikia katika Zahle walifikiwa na mwanamume mmoja kijana. Alijijulisha na kusema hivi: ‘Inawezekana kwamba hamnikumbuki, walakini mimi nawakumbuka. Nilikuwa kati ya watoto wale waliokuwa wakiwatupia mawe mlipokuwa katika Zahle.’ Huyo ambaye hapo kwanza alikuwa Mwislamu alikuwa amekuwa ndugu yao Mkristo, akiwa ameweka wakf maisha yake kwa Yehova Mungu.

KUENDELEA WAKATI WA VITA VYA WENYEWE KWA WENYEWE

Katika Aprili 1975, vita vya silaha vilianza katika viunga vya mji wa Beirut. Viliendelea kuongezeka hatua kwa hatua mpaka nchi yote ikaingizwa ndani ya vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. Vita hivyo viliendelea kwa miaka miwili hivi, mwishowe hesabu ya waliokufa ikazidi makumi ya maelfu. Nyumba, biashara na mali nyinginezo za akina ndugu ziliharibiwa, Mashahidi watatu waliuawa na hesabu isiyojulikana walijeruhiwa.

Shahidi mmoja aliuawa na risasi alipokuwa akianika nguo zake. Na mwingine aliyepuza maonyo ya kutotoka nyumbani ambapo Mashahidi walikuwa wamekusanyika, alipigwa risasi akafa aliporudi nyumbani. Mashahidi wengine walijeruhiwa na risasi, naye mmoja akajeruhiwa na upanga wa bunduki. Walakini ni jambo la shukrani kwamba visa kama hivyo vilikuwa vichache sana.

Sehemu ya kidini ya vita hivyo imekuwa na matokeo makubwa kweli kweli, na pengine ndiyo yenye kuleta woga mwingi zaidi katika vita vyote hivyo. Katika maeneo ambayo Waislamu walikuwa wengi, Wakristo wa jina walitwaliwa kutoka nyumbani mwao usiku wa manane na wengi wao hawakuonekana tena. Waislamu walitendewa vivyo hivyo na Wakristo wa jina. Walakini inajulikana kwamba Mashahidi wa Yehova ni tofauti.

WENYE AMANI NA WOTE

Sikuzote Mashahidi wa Yehova wamejaribu kutendea watu wote sawasawa, wawe ni Wakristo wa jina au Waislamu, wakitumia kanuni hii ya Biblia: “Kadiri inavyowezekana, kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.” (Rum. 12:18, HNWW) Pindi moja washiriki wa Katoliki wa Ushirika wa Maronite walimtembelea Shahidi mmoja wakitaka kumshawishi yeye na watoto wake wajiunge na wenye kulinda na watoe mchango wa pauni 300 za Kilebanoni za kununua risasi.

Shahidi huyo akawaambia hivi: “Siwezi kushiriki katika jambo lo lote linalohusiana na vita. Ingawaje vita yenu si ya Mungu. Kwa kweli, karibuni Mungu atakomesha watu wote pamoja na bunduki zao na kuleta taratibu yenye amani chini ya utawala wa Kristo.” Baadaye, hali katika eneo hilo zilipopata nafuu, Shahidi huyo aliona kwamba msimamo wake thabiti na wa kutokuwamo ulimletea heshima kutoka kwa jirani zake.

Mara nyingi msimamo huo wa kutokuwamo umeletea Mashahidi wa Yehova faida. Mara nyingi kuweza kuthibitisha kwamba mtu ni Shahidi kuliokoa maisha. Ndugu mmoja alitoa kadi aliyokuwa akibeba sikuzote ya kukataa kutiwa damu mishipani, nayo maisha yake yakaponyoka. Vivyo hivyo, ndugu mwingine aliokoka kuuawa kwa kurudia hotuba ya wanafunzi ambayo alikuwa ameitoa mapema kidogo katika Shule ya Kitheokrasi apate kuthibitishia kikundi cha waliotaka kumwua kwamba yeye alikuwa Shahidi. Kulikuwako visa vingi ambapo mwenendo wa Kikristo wa Mashahidi wa Yehova uliokoa maisha zao.

Mfano mwingine, jioni moja Shahidi mmoja alimpeleka nyumbani kwake mfanya kazi mwenzake Mwislamu kwa gari lake. Walisimamishwa na wanaume wenye silaha ambao walitaka kumwua Shahidi huyo kwa sababu alikuwa Mkristo. Walakini mwenzi wake Mwislamu akatetea maisha yake, akaeleza hivi: Mwanamume huyu ni tofauti na wengine wanaojiita Wakristo. Yeye hayumo. Hajiingizi katika siasa.”

Wanaume hao wenye bunduki walipokataa kusikiliza, mwanamume huyo Mwislamu alisema hivi: ‘‘Msipotuacha, mtalazimika kutuua sote wawili.” Kwa sababu ya kusihi kwake kwa unyofu, wote wawili waliachiliwa.

Shahidi mwingine anasimulia kwamba hakuwa na chakula nyumbani kwake, na kwa sababu ya wanaume wenye silaha kila mahali haikuwa salama kukanyaga nje. Lakini ndipo mvulana mchanga Mwislamu kutoka kijiji cha karibu alipokuja nyumbani kwake “Wazazi wangu,” akasema, “wamekutumia mkate huu. Na cho chote kinginecho unachohitaji, tafadhali utuambie. Tuko tayari kukupa.”

(Itaendelezwa baadaye)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki