Alifanya “Mizigo Mizito” Ikawa Myepesi
YESU alisema hivi kuhusu waandishi na Mafarisayo: “Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.” (Mathayo 23:4) Ukiwa ni ushuhuda wa jinsi hayo yalivyokuwa kweli, twasoma katika kitabu A Dictionary of the Bible, kilichohaririwa (kilichoandikwa) na James Hastings:
“Waandishi hawakuwa wanafalsafa; walikuwa wafasiri wa Sheria takatifu. . . . Kila sehemu ya maisha iliongozwa nayo. . . . Kila amri ya Biblia ilizungukwa na maagizo mengi madogo-madogo. Hakuna rekebisho lililoruhusiwa hata hali zikibadilika; utii kamili wa Sheria katika sehemu zayo zote ulitakiwa kabisa kwa kila Myahudi. Kwenye maagizo ya Sheria Iliyoandikwa kuliongezwa ‘Halakha’ au Sheria ya Kupokezwa, ambayo ilipokezanwa kama amana tukufu kutoka kizazi mpaka kizazi, na hatimaye ikaunganishwa katika Talmudi. . . . Kwa njia hiyo jaribio likafanywa kuingiza kila kisa kinachowazika ndani ya Sheria, na kuongoza mwenendo wote wa kibinadamu kwa kila jambo dogo kwa mawazo yasiyo na rehema. Mambo ya undani ya kisheria yalizidishwa mpaka dini ikawa biashara, na maisha yakawa mzigo usiovumilika. Watu wakawa wanatenda tu bila kufikiria. Sauti ya dhamiri ilinyamazishwa; uwezo wenye kutendesha wa neno la Kimungu ukazuiwa na ukafunikwa na amri nyingi zisizo na mwisho. Kwa sababu hiyo Bwana yetu aliwashtaki Mafarisayo, kwamba kwa mapokeo yao waliitangua Sheria.”
Lazima iwe kwamba watu wanyenyekevu na wanyofu walitiwa moyo kujua kwamba Mwana wa Mungu hakuiona ibada kwa njia hiyo! Lazima wawe walipendezwa na maneno yake: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”!—Mathayo 11:28-30.