Mnara wa Mlinzi—Msaada wa Kuzuia Uhalifu
NAOMI, msichana wa miaka saba anayeishi katika Manchester, Uingereza, aliandikia afisi ya Sosaiti yetu ya London kwa msisimuko akisema hivi: “Nilipoingia Afisi ya Posta yetu, niliona kibandiko kikubwa ukutani cha moja la magazeti yetu, lile linaloonyesha bibi mmoja akiibiwa kibeti chake na mwanamume mwenye kisu. Polisi wa mjini Greater Manchester wamelinakili ili waonye watu wajihadhari wasishambuliwe na wakora wa kuotea! ” Mambo ya karatasi hiyo iliyobandikwa ukutani yalianzaje?
Alipokuwa akitoa ushuhuda katika barabara moja ya Manchester, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alimwachia mwanamume mmoja nakala ya toleo la Novemba 1, 1984 la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) lenye kichwa “Nyakati Zetu za Hatari—Sababu Gani Zina Jeuri Nyingi? ” Bwana huyo aliweka gazeti mfukoni, lakini akashambuliwa na mkora wa kuotea alipokuwa akienda nyumbani. Alipokuwa ameketi ili moyo utulie baada ya tukio hilo, alikumbuka gazeti lile na kuanza kulisoma. Alipotembelewa na afisa wa Idara ya Polisi ya Kuzuia Uhalifu, alimwonyesha gazeti hilo, akamwambia hakufikiri kwamba yeye mwenyewe angeshambuliwa kwa kuotewa.
Afisa huyo wa polisi alivutwa sana na picha hiyo ya jalada, akasema ilikazia vizuri sana jambo lililohitajiwa ili kuonya watu wote wajihadhari wasishambuliwe kwa kuotewa. Ruhusa ya kuinakili picha hiyo ili ibandikwe-bandikwe ilitolewa kwa hiari, kisha nakala 3,000 zikabandikwa katika eneo la Greater Manchester.