Kukabiliana Na Uhalifu Katika Ulimwengu Wenye Machafuko
JE! WEWE huogopa kwenda nje usiku? Je! unahitaji makufuli mawili au matatu milangoni au madirishani mwako? Je! gari lako au baisikeli yako imepata kuibwa? Je! redio imepata kunyakuliwa kutoka kwenye gari lako? Je! unaona hofu katika maeneo fulani?
Ukijibu ndiyo kwa yoyote ya maswali haya, basi unajaribu kukabiliana na uhalifu katika ulimwengu wenye machafuko. Unaweza kufanya nini juu ya hilo? Je! Biblia yaweza kukusaidia ukabiliane?
Tabia ya Uhalifu na Haki
Katika ulimwengu wa uhalifu, kuna sehemu tatu za msingi: wahalifu, polisi, na wenye kudhulumiwa isivyo haki. Nini inahitajiwa ili wewe, ambaye huenda ukawa mdhulumiwa isivyo haki, uweze kukabiliana na uhalifu? Je, waweza kuathiri sehemu yoyote ya hizo sehemu tatu? Kwa mfano, je, waweza kuwabadilisha wahalifu?
Wahalifu wengi wamefanya uhalifu kuwa kazi-maisha yao. Wameichagua kuwa njia rahisi zaidi ya maisha. ‘Kwa nini ufanye kazi ikiwa waweza kupata riziki kutoka kwa yale yanayopatwa na wengine?’ hiyo yaonekana kuwa falsafa yao. Waviziaji hujua kwamba mwenye kudhulumiwa wa kawaida atakabidhi pesa zake bila kung’ang’ana. Na kwa sababu uwezekano wa kushikwa na kupelekwa gerezani si mkubwa sana, kwao uhalifu unalipa.
Tena, utaratibu wa baraza la hukumu ni wa kutatanika sana na wenye kutumia wakati mwingi. Katika nchi nyingi, kuna mabaraza ya hukumu, mahakimu, na magereza machache mno. Wingi wa kesi za uhalifu ni wa kupita kabisa mfumo huo. Mwenendo wa hukumu ni wa polepole sana hivi kwamba hali ni kama ile iliyoelezwa na Biblia miaka zaidi ya elfu tatu iliyopita: “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.” Kama vile kanuni hiyo ya Biblia inavyoonyesha, kuna tumaini dogo sana la kuwa na suluhisho kwa kupunguza idadi ya wahalifu au kwa kuwageuza kuwa wema.—Mhubiri 8:11.
Vipi juu ya ile sehemu ya pili, polisi? Je! kuna tumaini lolote kwamba polisi wataiweza hali? Wao wenyewe watajibu: Mara nyingi kukiwa na sheria ambazo huelekea kupendelea haki za mhalifu, na kukiwa na wanasheria wasio wanyofu ambao huvuta sheria kwa werevu ili mtu aliye na hatia aweze kwenda zake, kukiwa na jumuiya ambazo hazitaki kujitwika gharama kubwa ya kuongeza magereza mengine makubwa zaidi, na kukiwa na wafanya kazi wasiotosha katika jamii ya mapolisi, hawawezi kufanya maendeleo sana dhidi ya ongezeko la uhalifu.
Hiyo yaacha sehemu ya tatu, wale ambao huenda wakawa wadhulumiwa isivyo haki: sisi, raia. Je! kuna jambo lolote tunaweza kufanya kujisaidia kukabiliana vizuri zaidi katika hali hii ambayo karibu ni ya machafuko?
Hekima Yenya Kutumika na Akili ya Kikawaida
Kitabu cha Biblia cha Mithali kinataarifu hivi: “Yasiondoke haya machoni pako, shika hekima kamili na busara. Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, na neema shingoni mwako. Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautakwaa.” Shauri hilo laweza kutumika katika hali ambazo zingeelekea kumfanya mmoja awe mdhulumiwa katika uhalifu. Ni baadhi ya njia gani ambazo hekima yenye kutumika yaweza kutusaidia katika jambo hilo?—Mithali 3:21-23.
Wahalifu huelekea kuwa kama hayawani-mwitu wenye kuua na kula wengine. Wao hutafuta walio rahisi sana kutekwa. Hawataki kujihatirisha katika kung’ang’ana na huenda hata kukamatwa ikiwa wanaweza kupata mali ile ile kutoka kwa mwenye kudhulumiwa aliye rahisi. Kwa hiyo wao huendea walio wazee-wazee, walio wagonjwa, na wenye kuzubaa akili, na wale ambao huenda wasitambue sehemu yenye hatari. Wezi huchagua wakati na mahali panapowafaa zaidi kushambulia. Hapo ndipo wale ambao huenda wakawa wenye kudhulumiwa isivyo haki, waweza kutumia hekima yenye kutumika.
Kama vile Biblia huwaeleza, wapenda maovu mara nyingi hufanya kazi zao chini ya funiko la giza. (Warumi 13:12; Waefeso 5:11, 12) Ni kweli leo kwamba uhalifu mwingi dhidi ya watu na mali hufanywa usiku. (Linganisha Ayubu 24:14; 1 Wathesalonike 5:2.) Kwa hiyo, panapowezekana mtu wa hekima ataepuka kuwa nje katika maeneo yenye hatari wakati wa usiku. Katika mji wenye uhalifu mwingi wa New York, rekodi ya kila siku ya polisi huonyesha kwamba watu wengi huviziwa baada ya jua kushuka na hasa baada ya saa nne za usiku, mara nyingi wanaporudi kwenye nyumba zao. Wenye kuteka wako kwenye mabarabara yasiyo na watu, wakiwangojea watakaodhulumiwa. Hivyo, ikiwa unalo chaguo la kungojea basi au teksi au kutembea kupitia eneo lenye hatari, uwe na saburi na ungojee. Kama sivyo, unaweza kupata umizo.
Mkristo mmoja alipigwa vibaya sana na kuibiwa wakati alipotembea mwendo mfupi katika nusu-giza, badala ya kungojea basi saa nne hivi za usiku. Kulikuwako watu wengine barabarani, lakini wakora watatu walikuwa wameweka mtego kwa wasio na hadhari. Mmoja alionyesha wengine ishara wakati mtu huyo aliyeelekea kuwa mwenye kudhulumika alipokuwa akitembea njiani. Bila kusema neno, walimshambulia mdhulumiwa halafu wakamwibia. Ilikwisha haraka mno hivi kwamba hata jirani hakuwa na wakati wa kuingilia. Mwenye kudhulumiwa alikiri hivi baadaye: “Wakati ujao nitangojea basi.”
Yule Mlaghai Stadi, mwizi mchanga wa mifukoni katika kitabu cha Dickens Oliver Twist, alikuwa kwa kadiri chanzo kipole cha mkosaji wa barabarani wa ki-siku-hizi. Tofauti na huyo Mlaghai Stadi, wezi na waviziaji wa leo, bila kujali umri, wataelekea kubeba bunduki au kisu, na wataitumia. Watalii wenye kuzubaa akili, wageni, na wenye kutembea kilofa katika mji wenye shughuli nyingi ni shabaha rahisi kwa waovu hawa wabaya. Wataiba chochote kipatikanacho upesi kuliko unavyoweza kupepesa jicho! Ni nini huenda kikamsisimusha mwizi sana? Mkufu wa dhahabu au vito vingine vya bei ghali vinavyovaliwa kwa wazi. Au kamera inayoning’inia kwenye shingo la mtalii. Ni sawasawa na kuvaa ishara inayosema, “Njoo uninyakue!” Hivyo, busara inahitajiwa. Ficha vito vyovyote, na ubebe kamera kwa njia isiyo dhahiri sana, labda ikiwa imefichwa katika mfuko wa kuweka vitu vilivyonunuliwa. Hiyo ni hekima yenye kutumika.
Kuwa macho ni njia nyingine ya kukabiliana na uhalifu. Biblia inasema hivi: “Macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani.” (Mhubiri 2:14) Kutumia onyo hilo kwa tatizo la uhalifu kutamwongoza mtu kuwa mwangalifu kwa watu anaoshuku kuwa wanatanga-tanga bila kusudi dhahiri. Jihadhari na wezi ambao huenda wakaja nyuma yako na kunyakua mkoba wako unapotembea kwenye kijia kilicho upande wa barabara. Kwa kuwa wengine huendesha pikipiki na kunyang’anya mali ya watu wengine wanapowapita kwa mbio sana, usitembee kamwe kwenye ukingo kabisa kwenye upande wa barabara, hasa ikiwa unabeba aina yoyote ya sanduku dogo au mfuko wa mkono. Epuka magari yanayopita chini ya ardhi ambayo yako karibu tupu. Uko salama kukiwa na umati wa watu na katika mahali ambapo pana mwangaza mwingi. Wezi hawataki kuonwa na kutambuliwa.
Uvunjaji nyumba ni uhalifu mwingine wa kawaida ambao ungeweza kuepukwa ikiwa watu wangekuwa na utambuzi zaidi wa uhalifu. Biblia kwa kufaa ilitumia mlingano huu: “Huingia madirishani kama aingiavyo mwivi.” (Yoeli 2:9) Hekima yenye kutumika inataka kwamba usiache milango au madirisha bila kuyafunga. Sikuzote ni kweli kwamba kuzuia ni bora kuliko kuponya. Gharama ya ziada ili kulinda nyumba yako kwa kweli ni uhakikisho dhidi ya wizi na madhara ya kimwili.
Vipi Ikiwa Unaviziwa?
Ndiyo, vipi ikiwa, ijapokuwa umechukua hadhari zote, unasimamishwa na mviziaji? Jaribu kutobabaika au kufanya miendo yoyote ya harakaharaka. Kumbuka kwamba huenda mwivi akawa ana wasiwasi pia na huenda akaelewa vibaya vitendo vyako. Jaribu kuongea na kusababu pamoja na mtu huyo wa kiume au wa kike ikiwa aruhusu hilo. (Ndiyo, akushambuliaye huenda akawa hata mwanamke.) Nyakati nyingine waviziaji wametulizwa kwa kujua kwamba wanashambulia Mkristo aliye mnyofu na wa kweli. Bila kujali itikio-tendo, usijaribu kupinga ikiwa ni pesa au mali zako tu ambazo wanataka. Kabidhi chochote kinachoombwa kwa nguvu. Biblia hufundisha kwamba uhai wa mtu ni wa thamani kushinda kitu chochote ambacho huenda akamiliki.—Linganisha Marko 8:36.
Jaribu kuangalia alama za pekee ambazo huenda mviziaji akawa nazo, ama katika mavazi ama katika sura ya kimwili, bila kuifanya ionekane kama uchunguzi wa karibu. Mtamko wake wa maneno ni wa kilugha gani? Mambo hayo yote madogo madogo huenda yakatumika wakati unaporipoti uhalifu huo kwa polisi, kwa kuwa wahalifu walio wengi wana kawaida ya kila mmoja kwa namna yake katika modus operandi (namna yao ya kufanya) na kwa hivyo waweza kutambulishwa kwa urahisi zaidi.
Vipi kuhusu kubeba silaha kwa ajili ya kujilinda? Kwa uhakika halingekuwa jambo la hekima kwa Mkristo kubeba silaha. Ikiwa mkora anadhani kwamba unataka kutoa silaha, hatafikiri mara mbili juu ya kukuumiza au kukuua. Zaidi ya hayo, unawezaje kufuata kanuni ya Biblia ‘kukaa katika amani na watu wote’ ukiwa na silaha ili kujibu shambulio lenye jeuri?—Warumi 12:18.
Hata iwe umechukua hadhari zipi, hakuna uhakikisho kamili kwamba siku moja hutakuwa mdhulumiwa. Katika miji yenye uhalifu mwingi, unahitaji tu kuwa katika mahali pasipofaa wakati usiofaa. Si muda mrefu sana uliopita, mwanasheria mmoja katika New York, alitoka kwenye ofisi yake ili kununua kikombe cha kahawa. Alipokuwa akiingia dukani, vijana fulani waliendesha gari karibu na hapo wakaanza kupiga-piga bunduki mahali hapo. Mwanasheria huyo aliuawa na risasi ya bunduki kichwani. Kwa sababu ya “wakati na tukio lisilotazamiwa,” alipoteza uhai wake. Ni jambo la kuhuzunisha kama nini! Je! kuna tumaini lolote la utatuzi wa daima kwa uhalifu mwingi uliopo unaoenea ulimwenguni pote?—Mhubiri 9:11, NW.
Wakati Uhalifu Utakoma
Karibu miaka elfu mbili iliyopita, Yesu alitabiri kwamba kizazi kingekuja ambacho kingeona mambo yenye kuogopesha kuliko kizazi kinginecho kilichotangulia. Kukiwa na televisheni na uwasiliano wa mara moja tu, mamilioni, la, maelfu ya mamilioni, wanashuhudia katika stesheni za kupashia habari za kwao mambo ya ukatili yakiwa hasa yanatendwa. Ulimwengu umekuwa kijiji, na habari za ulimwengu huwa habari za mtaa mara ile ile. Tokeo ni kwamba, kila siku uhalisi wa mambo unaonekana, na kama vile Yesu alivyotoa unabii, watu wengi ‘wanavunjwa mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu.’—Luka 21:26.
Yesu aliona kimbele matukio ya tangu 1914, matukio ambayo yangekuwa mwanzo wa “umalizio wa mfumo wa mambo.” (Mathayo 24:3-14, NW) Lakini alisema pia: “Mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.” (Luka 21:31) Hiyo yamaanisha kwamba utawala wa Mungu wenye uadilifu karibuni utaathiri dunia kwa njia ya kutazamisha.—Mathayo 6:9, 10; Ufunuo 21:1-4.
Chini ya utawala huo, ni wapole, wenye amani, na wale ambao ni watiifu kwa Mungu tu ambao watashiriki hali za Paradiso ya dunia. Ni nini kitatokea kwa wahalifu na watenda mabaya? “Kama majani watakatika mara, kama miche mibichi watanyauka. Maana watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao BWANA [Yehova, NW] ndio watakaoirithi nchi [dunia, NW].” Chini ya hiyo serikali ya kimbingu yenye uadilifu, hakutakuwa ama uchafuko ama uhalifu.—Zaburi 37:2, 9.
Ikiwa ungependa kujua zaidi juu ya tumaini hilo lenye msingi wa Biblia la serikali ya ulimwengu yenye kudumu iliyo na amani, pashana habari na Mashahidi wa Yehova katika ujirani wako au huko kwenu kwenye Jumba la Ufalme lao. Wataterema kukusaidia kuelewa Biblia, bila malipo.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao BWANA [Yehova, NW] ndio watakaoirithi nchi [dunia, NW]”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mwizi wa mfukoni wa Charles Dickens, Mlaghai Stadi, alikuwa tu kama mwanafunzi wa uwizi akilinganishwa na waviziaji wa ki-siku-hizi
[Hisani]
Graphic Works of GEORGE CRUIKSHANK,
ya Richard A. Vogler, Dover Publications, Inc