Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w86 4/15 kur. 22-25
  • Upeo Unaofurahisha wa Miaka 80 ya Mkusanyo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Upeo Unaofurahisha wa Miaka 80 ya Mkusanyo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Vichwa vidogo
  • Nuru ya Ukweli Inakuja India
  • Matunda Vijapokuwapo Vipingamizi
  • Vitabu katika Lugha Nyingi
  • Matunda ya Miaka 80
  • Miaka Sita ya Kazi
  • Matokeo ya Mwisho
  • Tukio la Pekee
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
w86 4/15 kur. 22-25

Upeo Unaofurahisha wa Miaka 80 ya Mkusanyo

INDIA! Nchi yenye hali nyingi zinazotofautiana—katika utamaduni, dini, desturi na hali ya hewa. Ni nchi inayotofautiana na nchi nyingi, tena inakuwa fumbo kwa hizo nyingine. Hata hivyo inamvutia sana kila mtu anayetembelea pwani zake zenye kusisimua.

Katika sehemu zote za nusu-bara hilo, linalomiminika watu milioni 775, watu wanaopenda Yehova Mungu walikuwa wakifikiria tukio fulani la pekee katika mji mdogo wa Lonavla, juu katika Msafa wa Milima ya Magharibi ya Mkoa wa Maharashtra. Ilikuwa siku ya Jumapili, Januari 20, 1985.

Kwa sababu gani siku hiyo watu wengi walikaza mawazo yao juu ya kituo hicho cha kupendeza kilimani kilometa 110 kutoka kwenye mji uliosongamana watu wa Bombay? Jibu linahusiana na miaka 80 ya mkusanyo wa vitu vyenye thamani vya Yehova—watu wake—katika India. Hiyo ni sababu ya kuwafurahisha, si Mashahidi wa Yehova zaidi ya 7,000 tu walio hapa bali pia ushirika mzima wa watu wa Mungu ulimwenguni pote.’

Lakini ili kufahamu vizuri zaidi umaana wa tukio hilo la pekee, acheni tupeleleze kifupi jinsi misingi ya ukweli ilivyosimamishwa katika miongo zaidi ya minane iliyopita.

Nuru ya Ukweli Inakuja India

Mwaka 1905, Mwanafunzi wa sayansi kutoka India, S. P. Davey, alitembelea United States ya Amerika. Alipokuwa huko, alihudhuria hotuba ya Biblia iliyotolewa na C. T. Russell, aliyekuwa wakati huo msimamizi wa Sosaiti yetu. Davey akapendezwa sana na ukweli, akarudi Madras ambao ni mji wa kwao kwenye pwani ya mashariki ya India, na mwishowe akaanzisha vikundi 40 vya kujifunza Biblia.

Karibu na wakati uo huo, mwanamume kijana Mhindi alikuwa akitafuta majibu kwa maulizo juu ya fundisho la Utatu na ubatizo wa vitoto vichanga. A. J. Joseph alikuwa wakati huo ni mshiriki wa Kanisa la Uingereza, lakini alipokea kwa njia ya posta nakala ya kitabu cha Russell kinachoitwa At-One-Ment Between God and Men. Kichapo hicho kiliwezesha Joseph kuona ukweli juu ya ukubwa wa Yehova unaopita wa watu wote. Joseph, baba yake, na binamu yake wakaanza baada ya muda mfupi kueneza ukweli wa Biblia katika vijiji vile vyenye kukuza mpunga na minazi ambavyo sasa ni sehemu ya ule unaoitwa mkoa wa Kerala. Baada ya ziara ya mwaka 1912 ya Ndugu Russell, Joseph akawa mtangazaji wa Ufalme wa wakati wote. Mwaka 1924 yeye akiwa peke yake alifunga ziara ya kilometa 5,800 ya kuhutubu katika India, ikawezesha watu wengi wausikie ukweli. Ndugu Joseph alikuwa mfanya kazi mwenye bidii mpaka kifo chake mwaka 1964.

Mwaka 1926, msimamizi wa pili wa Sosaiti yetu, J. F. Rutherford, alitembelea Uingereza. Alipokuwa huko, alimwomba Edwin Skinner, kolopota (mhubiri wa wakati wote) hivi: “Ungependa kwenda India? ” Bila kusita-sita, Ndugu Skinner akaitikia hivi: “Unataka niende lini?” Katika muda wa majuma matatu yeye na mwenzake wakaelekea India!

Katika muda wa miaka 50 iliyofuata, Edwin Skinner alitumikia akiwa mtumishi wa tawi hapo kwanza akisimamia India, Ceylon, Uajemi, Afghanistan, na Burma. Alisafiri katika sehemu nyingi za India kwa reli, akawa akibadilishana-badilishana madaraka ya afisini na kazi ya kusafiri na kuhubiri pamoja na mwenzake. Baadaye wakajipatia “gari-nyumba” na kupanua ushuhuda wao kwenye maeneo yasiyoweza kufikiwa na gari-moshi. Akiwa na umri wa miaka 91, Ndugu Skinner angali ni mfanya kazi mwenye shauku katika afisi ya tawi ya India na ni mtangazaji wa kutokeza wa habari njema

Wahitimu wa Shule ya Sosaiti ya Gileadi walianza kufika mwaka 1947. Richard Cotterill aliye mzaliwa wa Uingereza alikuwa mmoja wa wale wa kwanza, na angali mtendaji baada ya miaka 38. Kwa muda fulani sasa, mwongozo wa kiserikali umekataza wamisionari wapya wa nchi za kigeni kuingia India. Lakini ndugu na dada 17, wenye wastani ya miaka 30 kila mmoja wakiwa wamisionari, wanatumikia kwa uaminifu katika nchi hii.

Ndugu wa India wenyewe wamefanya maendeleo makubwa ya kiroho, na wengi sasa wanastahili kuwa mapainia wa pekee na waangalizi wanaosafiri. Mwaka 1983, madarasa mawili ya majuma kumi ya Shule ya Sosaiti ya Gileadi yalifanywa kwenye afisi ya tawi. Mapainia wa pekee 46 waliojiandikisha walitiwa moyo na kutayarishwa vizuri zaidi wakatimize madai makubwa ya kazi ya mkusanyo katika India. Wao wamekuwa vyombo vya kuipeleka kazi kwenye maeneo mapya.

Matunda Vijapokuwapo Vipingamizi

Ijapokuwa kumekuwa na matatizo mbali-mbali kutokana na eneo la India lenye kutapakaa—miji mikubwa iliyosongamana, mitaa mizima-mizima ya watu wanaojikaza sana ili waendelee kuishi, mapokeo ya kidini yaliyokolea sana utendaji wa kila siku wa maisha ya watu, tangu kuzaliwa mpaka kufa—mkusanyo unaendelea. Kati ya mamilioni ya India wenye kumiminika, wengine wanatafuta utatuzi kwa matatizo ya wanadamu na kutamani ufahamu mwingi zaidi juu ya Mungu.

Mtu mmoja wa namna hiyo ni Dadu. Kijana huyo wa kiume, Dadu, alikuwa ameshangazwa na jambo la kwamba watu wasiohesabika wana abudu miungu mingi sana. Akaanza kusoma Biblia, lakini hakuelewa sehemu kubwa yake. Ndipo akaenda kwenye mahekalu ya Kihindu na kuanza kusoma vitabu vya dini hiyo.

“Niliambiwa kwamba Mheshimiwa Krishna ndiye aliyekuwa mwongozi wa dini zote na kwamba kila dini inawakilishwa katika kila punje ya mkufu aliovaa shingoni,” Dadu anakumbuka. “Nikawaza kwamba kama ndivyo ilivyo, basi mbona kuna chuki kati ya dini mbalimbali, na mara nyingi ikitokeza umwagaji wa damu?” Alipochunguza dini ya Waislamu baadaye, Dadu aliamini kwamba aliweza kupashana habari na wengi wa babu zake waliokufa. Lakini kwa kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, Dadu na mkeye walijifunza chanzo cha dini nyingi zilizopo ulimwenguni na kwamba wale wanaoitwa roho wema waliokuwa wamepashana nao habari walikuwa wadanganyifu, mashetani. “Tunamshukuru Yehova Mungu kwa maarifa yaliyotufungua na uvutano wao,” anasema Dadu. Sasa yeye na mkeye ni wahudumu wa wakati wote.

Miaka saba iliyopita, mama mmoja alipata Biblia na vitabu vya Kibiblia kutoka kwa Mashahidi wa Yehova. Ingawa yeye na jamaa yake walihamia maeneo ambako hakukuwa na Mashahidi, aliendelea kujifunza yeye peke yake. Alipofikiwa na Mashahidi tena hivi majuzi, alisimulia hivi: “Wakati wa miaka hiyo iliyopita, singeweza kuzisahau kweli nilizokuwa nimejifunza kutokana na Biblia. Haikuwezekana nizirudie njia zangu za zamani za kuabudu.”

Vitabu katika Lugha Nyingi

Lugha kumi na tano kubwa-kubwa zinasemwa katika sehemu zote za India, na namna tisa mbalimbali za kuandika herufi kwa maumbo ya picha zinatumiwa. Kuandaa chakula cha kiroho katika lugha zote hizi kumekuwa tatizo. Hata kule mwanzo mwaka 1912, Ndugu Russell alipanga vijitabu vya Kibiblia vitafsiriwe katika Hindustani, Gujarati, Malayalam, Marathi, Telugu, na Tamil. Lugha nyingine za kienyeji zilitiwa ndani baadaye, na sehemu kubwa ya vitabu hivyo vilichapwa ng’ambo na kusafirishwa nchini. Halafu mwanzoni-mwanzoni mwa miaka ya 1960 amri ya kiserikali ikakataza kuingizwa nchini kwa vichapo vya lugha yo yote ya India.

Kwa kuwa pesa hazikuwapo za kuwezesha tawi lijifanyie uchapaji, Sosaiti ilifanya mkataba na wachapaji wa kibiashara. Mapainia fulani walichaguliwa wakafundishwa kuelekeza uchapaji katika sehemu zao. Kwa sasa kuna sehemu 11 mbalimbali za uchapaji, zinazochapisha vitabu vya Kibiblia katika lugha 16, kutia na chapa tisa za gazeti Mnara wa Mlinzi. Karibuni, kompyuta ya MEPS ya Sosaiti (mfumo wenye lugha nyingi wa kupanga maandishi kwa upigaji picha kielektroni) ikiisha kusimamishwa, upangaji wa maandishi na kurasa za vichapo utafanywa kwenye afisi ya tawi, na hiyo itawaweka huru mapainia wengi watumie wakati mwingi zaidi katika kazi ya kukusanya.

Matunda ya Miaka 80

India ikiwa ndilo taifa la pili duniani kwa wingi wa watu, kazi kubwa sana inabaki kufanywa humo. Ni asilimia 6.6 tu ya idadi ya watu wa huko ambao mpaka sasa wamekwisha kufikishiwa habari njema. Kwa kulinganishwa na nchi zilizo nyingi, ukuzi wa watu wa Yehova katika India umekuwa wa pole. Ilichukua miaka 53 kufikia kiwango cha wahubiri 1,000 tu. Lakini wamisionari na ndugu wa hapa wameendelea kujikaza na kusubiri katika kufanya mapenzi ya Baba yao. (Isaya 60:22) Sasa tunafurahi kuona ongezeko la asilimia 10 juu ya mwaka uliopita, na kilele kipya cha wahubiri 7,410 katika makundi na vikundi vilivyo peke yavyo 340 katika nchi hii.

Ukuzi huo wa utaratibu ulionyesha dalili ya kuhitaji makao makubwa zaidi ya tawi. Lakini haikuwezekana kulipanua tawi la India katika Bombay. Na ardhi katika mji huo ilikuwa haba na yenye gharama kubwa. Pia hewa ya Bombay ilisemwa kuwa inapunguza urefu wa maisha ya mtu kwa miaka kumi. Hivyo, mwaka 1978 uwanja ulipatikana katika eneo la Lonavla lenye vilima, hapo pakiwa ndipo mahali pa kwanza kusini mwa mji wa Bombay ambapo barabara na reli zinakutana. Mji huo uko kwenye mwinuko wa meta 610, na hewa ya hapo haijachafuliwa sana.

Miaka Sita ya Kazi

Kazi ya utangulizi ilihitaji kuta zijengwe, na mahali fulani-fulani urefu wazo ulifikia meta 4.6, ili kuilinda ardhi na pia kudumisha udongo wa nyanja jirani katika vilima-vilima vya karibu. Vibonde vyenye kina kirefu vilihitaji kujazwa kisha vifyekwe vichaka vilivyosongamana sana vyenye kujawa na nyoka wenye sumu, kama fira na wengineo. Nyumba moja moja na majengo mengine yaliyokuwapo yalihitaji kazi nyingi ya kuyatengeneza upya ili yawe makao na pia sehemu nyingine ziwe afisi kwa muda.

Mafundi wa mikataba walikodiwa, lakini ndugu wenye kustahili wakasimamia kila hatua ya ujenzi, na wengine wengi wakatoa usaidizi wakati wo wote walipoweza. Fundi mmoja wa mikataba, aliyeajiriwa kutengeneza barabara ndani ya uwanja, aliamua kwamba kazi ikawizwe muda wa miezi sita, kwa maana uso wa barabara ulikuwa mbaya-mbaya na mipango ya kuumwagia maji uwe mwororo haukuweza kufanywa. Makubwa yalionekana yakifanyika wakati jamaa nzima ya tawi ilipokuwa ikimwaga maji kwenye barabara hiyo jioni baada ya jioni ili kazi iweze kufanywa kulingana na ratiba.

Hakukuwa kamwe na mlio wa tingatinga, kwa maana sehemu kubwa ya kazi katika India hufanywa kwa mikono. Hivyo kazi iliendelea bila kizuizi mpaka ghorofa ya kwanza ya lile jengo kuu ikamalizika. Wakati uo huo kukawa na upungufu mkubwa wa saruji. Lakini jambo la kufurahisha ni kwamba tawi la Korea la Sosaiti yetu lilipanga kusafirishiwe mifuko 10,000, ikawezesha ujenzi wote ulimalizike kama ulivyopangwa. Kwa hiyo, mwaka 1984, tawi jipya la kupendeza sana lilisimama pale likiwa limemalizika—kwa sifa ya Yehova.

Matokeo ya Mwisho

Sasa nyumba nane zipo ndani ya uwanja wa Sosaiti wenye ekari 4.6, nao umepambwa kwa kupandwa migomba, miembe, mitini, na mipapai, pamoja na mimea na vichaka vingi ambavyo huchanua maua.

Jengo kuu la tawi lina ghorofa mbili na chumba cha chini ya sakafu, ambapo ndipo penye nafasi za kutengenezea magari na kufulia nguo. Nafasi ya kiwanda katika ghorofa ya chini ina sehemu ya mashine tatu ndogo za uchapaji, na pia sehemu ya mashine ya kukatia karatasi, ya kuzikunja, na kufunganisha kurasa kwa kuzichoma pini. Kwenye ghorofa hiyo pia kuna vile vyumba vya kompyuta ya MEPS na eneo la kusafirishia vitabu, na kutoka hapo vitabu vinavyochapishwa katika nchi yetu vinapelekwa kwenye nchi nyingine 56. Afisi, maktaba, na vyumba vya kulala vinajaza ghorofa ya pili.

Jumba la Ufalme jipya liko kwenye ukingo wa mbele wa uwanja. Jukwaa lililojengwa kwa konakona, lenye kupambwa upande wa nyumba kwa mbao ngumu za kuvutia zilizochongwa kwa mkono liko mbele ya jumba kuu lenye nafasi ya watu 250. Karibu nalo, kuna majengo ya zamani yaliyotengenezwa upya yaliyo na makao, sehemu ya jikoni, na chumba cha kulia jamaa ya tawi yenye watu 31. Pia pana ardhi isiyo na kitu ikiwa mpanuko zaidi utahitajiwa.

Tukio la Pekee

Kwa hiyo, baada ya miaka 80 ya kuvikusanya vitu vya Yehova vyenye thamani kubwa, fikira zilikazwa siku hiyo nzuri sana ya mwezi Januari juu ya kuweka wakfu jengo jipya la tawi la India.

Wakati wa programu ya wakfu, maelezo yalitolewa juu ya matukio ya miaka hiyo 80 ya kuhubiri. Mambo makuu ya kazi ya ujenzi yalitolewa. Mwangalizi wa eneo la dunia Gunter Kunz, kutoka tawi la Ujeremani, alisema katika hotuba yake ya wakfu kwamba kumekuwa na ongezeko la asilimia 30 la watu wa Yehova ulimwenguni pote katika miaka mitano iliyopita. Lakini alifurahia kuripoti kwamba India imeizidi hesabu hiyo kwa kuwa na ongezeko la asilimia 34, naye akawakumbusha wasikilizaji kwamba India ingeendelea kusonga mbele ikiwa kazi ya bidii nyingi ingefanywa.

Wote waliokuwapo waliusisimukia ushuhuda huo wa kuonyesha baraka ya Yehova. Akina ndugu katika India wamepiga moyo konde wafanye kazi kwa bidii ili watu wengi zaidi waweze kusaidiwa waziitikie habari njema za Ufalme.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Edwin Skinner (wa pili kutoka kulia) akiwa na “gari-nyumba”

[Picture katika ukurasa wa 24]

Makao makuu mapya ya tawi kusini mwa Bombay

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki