Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w87 3/1 kur. 21-24
  • Sifa Iwe kwa Mungu, Yule Chanzo cha Uzima na Ukuzi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sifa Iwe kwa Mungu, Yule Chanzo cha Uzima na Ukuzi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mtiifu kwa Chanzo cha Uzima
  • Kumsifu Yeye Hata Chini ya Shida
  • Wenye Shukrani kwa Wema wa Yehova
  • Mungu Atoa Uzima na Ukuzi
  • Pigo Lenye Kuvunja Moyo
  • Ahadi Ambayo Nimeazimia Kutimiza
    Amkeni!—1998
  • Kwa Msaada wa Yehova, Tuliokoka Serikali za Kimabavu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Nilimtumikia Mungu Licha ya Magumu
    Amkeni!—2005
  • Nililindwa na Imani Katika Mungu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
w87 3/1 kur. 21-24

Sifa Iwe kwa Mungu, Yule Chanzo cha Uzima na Ukuzi

Kama ilivyosimuliwa na Eduard Warter

MACHO yanafurahia kuona vigongo-vigongo vya milima yenye fahari iliyochangamana-changamana na vibonde vyembamba vyenye kina kirefu, na mabonde mapana. Mabubujiko ya maji yanapita haraka katika mitaro —yakitia unyevu katika bustani, mashamba ya mizabibu, na makonde yaliyo katika nyika zenye mazao. Lakini je! mtazamaji anamfikiria yule Chanzo cha uzima, ambaye anafanya ukuzi huo uwezekane, mwenye kustahili sifa?—Zaburi 36:9, NW.

Mandari hiyo yenye milima-milima yenye kuangazwa na jua imo katika Jamhuri ya Kirghiz—jamhuri ya Kisovieti yenye wingi wa watu katika Esia ya Kati. Makumi ya maelfu ya raia Wasovieti wenye asili ya Ujeremani wanaishi kule. Jamaa yetu, pia, iliishi katika mahali hapo penye mazao kwa muda fulani, nasi tulimstaajabia Mungu anayetokeza ukuzi huo mzuri ajabu. Ndiyo, tulimsifu na kueleza wengine peupe juu ya matendo yake makuu.

Mtiifu kwa Chanzo cha Uzima

Wakati mimi nilipozaliwa katika 1901, wazazi wangu walikuwa wakiishi katika Memelland (ambayo sasa ni Klaipeda), iliyokuwa wakati huo sehemu ya Prussia Mashariki, katika pwani ya Baltiki, karibu kilometa kumi kutoka mpaka wa Urusi. Nilipokuwa bado nikienda shuleni, vita ya ulimwengu wa kwanza ilifyatuka, nasi tukawa mashahidi wenye kujionea kwa macho maogofyo ya mauaji ya kuangamiza halaiki ya watu. Sisi wakaaji wa mpaka wa Ujeremani tulikuwa tumekuwa na masikilizano pamoja na jirani zetu Warusi na tukajiuliza hivi: ‘Lilikuwa kosa la nani? Mungu alikuwa upande wa nani?’ Ijapokuwa hivyo, misemo kama “Kwa Ajili ya Mungu, Mfalme, na Nchi” ilichochea hisia za uzalendo shuleni.

Muda fulani ulipopita, baada ya vita, mimi nikaja kushindwa na uvutano wa mambo hayo, nikajitolea utumishi katika ulinzi wa mpakani na baadaye katika Jeshi la Ujeremani katika Konigsberg, ambayo sasa ni Kaliningrad. Nikiwa hapo nikakata shauri kwamba kwa maoni yangu askari wa kawaida alikuwa kibaraka tu, mwenye kusukumwa-sukumwa huku na huku kulingana na mapendezi ya wengine. Muda mfupi baada ya Memelland kutwaliwa na Lithuania katika Januari 1923, mama yangu aliniandikia hivi: “Hupaswi kamwe kwenda vitani, kwa kuwa amri ya tano inasema, ‘Usiue.’ Wala Wanafunzi wa Biblia [Mashahidi wa Yehova] hawaendi vitani.” Mimi nilishangaa sana. Wanafunzi wa Biblia hao walikuwa akina nani? Nilipokuwa nyumbani katika likizo, nilijifunza juu ya kweli zao za msingi za Biblia. Kufanya hivyo kukawa na matokeo makubwa juu yangu —matazamio yangu yote ya kidini na kisiasa juu ya maisha yakapata badiliko kubwa.

Sasa akili zangu zikashika jambo la kwamba mwisho wa mfumo mbovu wa mambo ya sasa ulikuwa karibu, uondokee Ufalme wa Mungu. Mbona basi nitumie wakati zaidi nikijaribu kusaidia Ujeremani isimame tena? Bila kukawia nilifanya mipango ya kuacha utumishi wa kijeshi, nami nikarudia mji wa kwetu nyumbani nikajifunze mengi zaidi juu ya kweli hizo. Ubatizo ukafuata 1924, nami nikafahamu jambo moja waziwazi: Hatua hiyo ilimaanisha kutumikia Mungu si mpaka tarehe fulani tu bali milele na katika kila hali. Moyo wangu ulijaa furaha. Pendeleo lililo la juu zaidi linalowezekana kwa sisi wanadamu dhaifu sana—kutumikia Aliye Juu Zaidi na kupelekea wengine ujumbe wake —ndilo nililokuwa nimepewa.

Nilipiga moyo konde nijithibitishe kuwa nastahili. Tulikuwa na eneo kubwa la mashambani lenye vijiji vingi vya walowezi vilivyotawanyika na nyumba za mashamba makubwa ambako ningeweza kupeleka ujumbe. Basi siku za Jumapili halikuwa jambo lisilo la kawaida kwetu kutembea muda wa saa 10 mpaka 12 tukitembelea watu tukiwa na ujumbe. Waamini wenzetu wenye makao yenye nafasi kubwa walitutolea tuyatumie kwa ajili ya mikutano yetu ya Kikristo. Hakukuwa na safari yo yote tuliyoiona kuwa mbali mno, wala hali ya hewa tuliyoiona kuwa yenye mvua mno hata ituzuie kuhudhuria vikusanyiko hivyo vyenye thamani kubwa. Vilitutia nguvu kwa ajili ya nyakati zenye majaribu zilizokuwa mbele.

Kumsifu Yeye Hata Chini ya Shida

Kazi ya Ufalme ilianza kukua katika nchi za Baltiki, na sasa ikawa chini ya usimamizi wa Afisi ya Kaskazini ya Ulaya ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi katika Denmark. Katika 1928, mimi nilioa, na mke wangu Ruth nami tukashirikiana na Kundi la Hydekrug. Wakati ndugu zetu katika Ujeremani ya Nazi walipokuwa wakipatwa na mateso ya ukatili, sisi hatukupatwa nayo —mpaka 1939. Mapema ya asubuhi ya Machi 22 habari zilikuja kwa ghafula: “Memelland imekombolewa! Fũhrer [Kiongozi] anakuja!”

Mngurumo wenye kuogofya wa ndege nyingi zilizopita angani ulijaa masikioni mwetu asubuhi yote. Kukaliwa kwa nchi na Hitler kulikuwa kumeanza. Siku ile iliyofuata nyumba za Mashahidi wa Yehova wote zilipekuliwa-pekuliwa, na wengine wao wakakamatwa. Tulinyang’anywa vitabu vyetu, hata Biblia, vikateketezwa peupe sokoni. Mara tu baada ya utendaji wetu kupigwa marufuku tulianza kufanya kazi chini-chini, tukizungusha vitabu kila mahali na kutembelea wenye kupendezwa kwa siri.

Ilipofyatuka Vita ya Ulimwengu ya Pili, mimi niliitwa nikaingie utumishi wa kijeshi. Niliendelea kukataa bila ugeugeu, na Mahakama ya Kijeshi ya Serikali katika Berlin ikafikiliza hukumu ya kifo juu yangu siku ya Aprili 10, 1940. Mke wangu alienda kuletwa kutoka nyumbani anibembeleze nijiunge na jeshi. Yeye, pia, alibaki akiwa asiyeondoleka, akaheshimiwa na afisa mmoja mzee-mzee, aliyesema hivi: “Mimi nalazimika kukubali kwamba mwelekeo wenu ni sawa kabisa. Vita haina huruma ya kibinadamu.” Mke wangu aliachwa bila mtafuta-riziki wa kumtunza yeye, watoto wetu wanne, na mama yake mwenye kuendelea kuzeeka. Je! Ruth alilalamika wakati wo wote? Katika barua chache alizoruhusiwa kuandika, yeye alinitia moyo nibaki nikiwa mshikamanifu wala nisidhoofike kwa sababu ya wapendwa niliokuwa nikiacha nyuma.

Katika Oktoba 1940 hukumu yangu ilifutwa. Ijapokuwa hivyo, bado niliendelea kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya uzuizi, na mwishowe nikajikuta katika kambi ya mateso kule Stutthof, karibu na Danzig (ambayo leo ni Gdansk). Mashahidi washikamanifu waliokuwa kambini tayari, kama vile Joseph Scharner, Wilhelm Scheider, Herman Raböse, na Hermine Schmidt, wangekuja kuwa masahibu wangu wa karibu, nao waliitia nguvu imani yangu.a Tukiwa huko, katikati ya wafungwa 30,000 kila mmoja wao akiwa na matazamio ya kufa tu bila tumaini lo lote, sisi tulipata pendeleo la kuwaeleza taraja la Ufalme wa Yehova.

Wenye Shukrani kwa Wema wa Yehova

Katika Januari 1945, wakati vita katika ukingo wa mashariki ilipokaribia zaidi na zaidi, watu walianza kuondolewa kambini. Katika bandari ya Danzig, meli inayoitwa Wilhelm Gustloff ilikuwa ikingojea kutuchukua tupelekwe upande wa magharibi. Kwa kuwa sisi tulifika tukiwa tumechelewa mno—meli za kivita zilizopasa kuambatana nasi ili kutulinda safarini zilikuwa zimekwisha kuangushiwa makombora na ndege—hivyo sisi tukaikosa safari ya baharini iliyokuwa ya msiba, kwa kuwa ni watu wachache waliookoka kuzamishwa kwa meli hiyo.b Ndipo tulipowekwa kwa muda katika ghala ya mawe iliyozungushiwa ua wenye wafungwa wengine karibu 200. Chini ya hali zisizo za usafi, mimi nikapatwa na homa ya matumboni. Ndipo agizo lilipokuja: “Rudini kwenye kambi ya Stutthof!” Joto la mwili wangu likiwa limepanda, niliweza kutembea kwa shida, nami nikafanikiwa kuumaliza mwendo ule mrefu wa kurudi kwa msaada tu wa ndugu mmoja, Hans Deike. Ilichukua siku kumi homa ile ipungue nikiwa katika nyumba ya wagonjwa kambini.

Aprili 25, 1945, ilifika sisi tukiwa safarini kurudi pwani. Nilikuwa ningali mgonjwa sana, na akina dada walitatizwa sana kuendelea kunisimamisha. Hata hivyo, wengine wao walikuwa wakiimba nyimbo zetu. Sisi tulipakiwa katika mashua kubwa isiyo na vifaa vingi ili tuanze safari yetu hatari. Watu zaidi ya 400 wakiwa humo ndani, chombo kile kilikuwa kikiyumba-yumba vibaya sana. Ili mashua hiyo isafiri kwa ulaini, wafungwa walipigwa na kulazimishwa waingie katika sehemu ya chini ya kuwekea shehena. Humo, watu walilaliana kweli kweli. Waliokufa walitupwa nje baharini. Ilikuwa baraka kwamba kikundi chetu kidogo cha Mashahidi 12 kiliruhusiwa kibaki katika sitaha ya mashua ile, nasi tukampigia Mungu asante kwa ajili ya hilo.

Tukiwa tumekauka mwili kwa kugandishwa na baridi tulifika asubuhi iliyofuata kwenye Sassnitz kisiwa cha Rügen. Wenyeji wa kisiwa hicho hawakutaka kutupokea, wakatupa kiasi fulani tu cha maji ya kuburudisha. Katika usiku wa Aprili 29/30, mashua yetu ilitua chini ya mmoja wa miamba ya majini karibu na kisiwa cha Eulenbruch. Ile meli ya kuvuta mashua zilizokwama ilikuwa imeziondoa kamba zilizokuwa zikivuta chombo chetu katika eneo lililotegwa baruti nayo ikatupotelea. Je! hiyo ilikuwa njia ya kutuangamiza sisi sote? Kwa kusikia miamba iliyo chini ya maji ikikwaruza-kwaruza mwili wa mashua yetu, sisi tukamtumaini Mungu asituache peke yetu.

Walinzi wa pwani walituleta kwenye nchi kavu tukiwa katika mashua ya mpira kwa matumizi ya kuokoa uhai. Wenye kuendesha mashua yetu walilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kusonga mbele na safari wakiwa katika chombo kingine. Vibandari vyote vya Kijeremani vilikaliwa na askari wa Muungano, kwa hiyo sisi tukawapita na mwishowe tukaegesha mashua katika nchi kavu katika kisiwa cha Denmark cha Møn. Tukiwa huru hatimaye, tukawauliza watazamaji kama Mashahidi wa Yehova wo wote walikuwa katika kisiwa kile. Katika muda wa saa mbili tangu hapo tukawa tunakumbatiwa kwa uchangamfu na dada wawili. Wenye kusimama karibu nasi walistaajabu sana. Afisi ya tawi ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ilipopata habari juu ya kufika kwetu, Filip Hoffmann alitumwa akapange ili sisi tupate utunzaji na uangalifu wenye upendo. Tulimshukuru Yehova kama nini!

Mungu Atoa Uzima na Ukuzi

Tulipona haraka tukio hilo la kuogofya nasi tukafurahi sana kuhudhuria katika Septemba kusanyiko la Mashahidi wa Yehova katika Copenhagen. Wanawake wawili vijana, mmoja wa asili ya Lett na mwingine wa Ukrainia, waliokuwa wamejifunza ukweli katika ile kambi ya Stutthof walibatizwa. Wote wawili walirudi Urusi wakiwa dada zetu wa kiroho. Na bado Mungu angetupa sisi ukuzi zaidi!

Sasa Memelland ilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Lithuania ya Ujamaa ya Kisovieti. Tofauti na mahimizo niliyopewa na wakimbizi Warusi, mimi nilielekea upande wa mashariki katika Juni 1946, nikajiunge tena na jamaa yangu. Nilienda nikiwa na furushi zito la vitabu vya Kibiblia. Nilipovuka mipaka, askari wenye kulinda eneo hilo walipuuza furushi langu, wakaelekeza fikira zaidi kwenye wingi wa vitunguu-saumu nilivyokuwa navyo. Ndugu wa kule walifurahi kama nini kupokea chakula cha kiroho hicho chenye thamani kubwa.

Mimi nilijawa na shukrani kwa Yehova kwa kuhifadhi jamaa yangu vizuri ajabu ikapita kipindi kile cha vita na nyakati za magumu zilizofuata hata tukaweza kuendelea na kazi yetu. Sisi hatujakoma kamwe kumsifu Mungu!

Pigo Lenye Kuvunja Moyo

Ijapokuwa hivyo, katika Septemba 1950 Mashahidi wote katika eneo letu walikamatwa na kusafirishwa mahali kwingineko. Hesabu fulani kati yetu tulihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 10 na 25 katika kambi ya kazi ya jasho. Washiriki wote wa jamaa yetu waliharimishwa na kupelekwa Siberia maisha yao yote.c

Hilo lilikuwa pigo lenye kutuvunja sana moyo, lakini upesi tukaja kutambua kwamba ujumbe wa Ufalme ulipasa kuenezwa katika nchi hii kubwa sana pia. Lilikuwa pendeleo langu, pamoja na Mashahidi wengine karibu 30, kuwahubiri wale wafungwa 3,000 wa kambi ya Vorkuta kaskazini mwa Urusi ya Ulaya. Wengi waliukubali ukweli, wakabatizwa, na kuendeleza kazi katika maeneo bikira baada ya kufunguliwa kwao.

Baada ya karibu miaka mitano, katika masika ya 1957, mimi nilipewa ruhusa nihamie eneo la Tomsk, na kufanya hivyo kuliunganisha tena jamaa yetu. Ndugu zetu katika Siberia walilazimika kufanya kazi tangu asubuhi mpaka jioni, bila siku ya mapumziko ya kazi. Mwishowe, karibu wote wale waliofukuziwa mbali wakae pekee yao walifunguliwa, na mhamo mkubwa wa kuelekea kusini wa wanataifa Wajeremani ukafuata. Kama ilivyotajwa mwanzoni, sisi tulifanya makao katika Jamhuri ya Kirghiz ya Esia ya Kati katika 1960. Hapo, katika mji wa Kant karibu na Frunze, tulikuta jamaa kadha za Mashahidi wa Yehova waliokuwa wamefika kabla yetu.

Miaka michache ya kwanza ilipita kwa amani ya kutosha. Wakati maji ya ukweli yalipokolea vizuri, paradiso ya kiroho ilianza kukua hapa na katika sehemu nyingine za nchi. Ijapokuwa hivyo, usifaji wetu wa bidii kwa Yehova haukuendelea bila kuonwa. Magazeti yalichapisha makala za uchochezi juu yetu. Viongozi wa dini zilizoandikishwa rasmi walitukataza tusitembelee “kondoo” zao, wakitisha kuchukua hatua dhidi yetu. Katika 1963, ndugu watano walinyakuliwa kwa ghafula kutoka katikati yetu na kuhukumiwa kifungo cha kati ya miaka saba na kumi katika kambi za kazi ya jasho. Msimamo usio wa woga na wa kutokubaliana na wapinzani wa ndugu zetu katika mahakama ulistaajabisha watu. Wao waliona kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wamepiga moyo konde ‘kutii Mungu kuliko wanadamu.’—Matendo 5:29.

Nilipofikia umri wa kustaafu, tuliambiwa kwamba tungeruhusiwa tuhamie Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani. Kabla ya kuondoka kwetu, akina ndugu na dada katika Kirghiz na Kazakhstan Kusini walitukazia kwamba inatupasa tuwapitishie Mashahidi wa Yehova wote katika mapana ya ulimwengu upendo na salamu zao, wakitumia vifungu vya Ayubu 32:19-22 na Yeremia 20:9, 10. Ruth na mimi sasa tumeishi katika Bremerhaven tangu 1969. Ijapokuwa umri wetu unaozidi kusonga mbele, sisi tunaendelea kumsifu Yehova, yule Chanzo cha uzima na ukuzi, kwa ajili ya wema wake. Tunatazamia kwa uhakika siku ile ambapo dunia nzima itakuwa paradiso halisi, na kila kitu kinachopumua kitakapomsifu Yeye!—Zaburi 150:6.

[Maelezo ya Chini]

a Ona gazeti Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), la Machi 15, 1968, kurasa 187-90.

b Ona gazeti Amkeni! (Kiingereza), la Mei 22, 1978, kurasa 16-20.

c Ona gazeti Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), la Aprili 15, 1956, kurasa 233-6.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Eduard na Ruth Warterleo

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kikundi cha Mashahidi kutoka Kambi ya Mateso ya Stutthof baada ya kufika Denmark katika 1945, pamoja na Eduard Warter aliye mwisho kabisa upande wa kushoto

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki