Mnyanyaso Katika Burundiy—Ahadi Iliyovunjwa ya Uhuru wa Kidini!
Uhuru wa dini huchukuliwa kuwa jambo la kikawaida tu katika mabara mengi ya Magharibi. Hata hivyo, mnyanyaso wa kidini unaotukia katika bara la Kiafrika la Burundi ni kielezi cha jinsi uhuru huo uwezavyo kuwa wenye kuvunjikavunjika kwa urahisi. Kweli kweli, hakuna mtu yeyote aliye na usalama wa haki zake maadamu haki za kibinadamu zilizo za msingi za kikundi chochote cha watu zakanyagwa-kanyagwa. Kwa hiyo sisi twahimiza wasomaji wetu wachunguze yanayotukia katika Burundi.
FEBRUARI 16, 1989 iliona kivuli cha zile Enzi za Giza kikianguka juu ya bara la Kiafrika la Burundi. Tarehe hiyo rais wa Jamhuri ya Burundi, Pierre Buyoya, alifanya mkutano pamoja na magavana wa mikoa. Kufuata mkutano huo, mnyanyaso mkali sana wa kidini ulienea kwa mapana dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Muda si muda wanaume, wanawake, na hata watoto wakawa wakikamatwa, kupigwa, kuteswa-teswa, na kukoseshwa chakula kwa njia haramu.
Ni aibu kwamba matendo hayo ya kinyama yaweza kutukia leo hii na katika nyakati za kisasa. Hata hivyo, mnyanyaso wa Wakristo katika Burundi ni wa kuchukiza sana kwa sababu fulani hususa. Kwa nini? Kwa sababu huko ni kuvunja ahadi fulani ya uhuru wa kidini.
Serikali Yavunja Ahadi
Burundi ni taifa la sehemu ya ndani-ndani ya Afrika, chini kidogo tu kusini mwa ikweta, ingawa bara hili lenye milima-milima laona shangwe kuwa na tabia-nchi pole yenye kupendeza. (Ona ramani.) Ni watu wachache duniani waliokuwa na habari za kwamba kuna Burundi mpaka Agosti 1988, wakati ambapo ilivuma katika magazeti ya ulimwengu. Wakati huo magombano yenye umwagaji wa damu yalifoka kati ya makabila makubwa mawili ya bara hilo, Watutsi na Wahutu. Bila shaka jambo hili liliacha akili za watu wengi zikiwa na maoni mabaya juu ya Burundi.
Hata hivyo, kuna mema mengi ya kusemwa kuhusu bara hili lenye maendeleo. Watu walo hufanya kazi kwa kujikaza na ni wenye bidii. Makala moja katika The New York Times Magazine yaongezea maoni ya kwamba “ingawa Burundi ni maskini, hiyo hufanya kazi kwa njia mbali-mbali zenye kuonekana wazi na mtu anayeizuru. Maurice Gervais, mwakilishi-mkazi wa Benki ya Ulimwengu, aiita ‘nchi yenye kutenda kwa kiwango cha juu sana.’”
Hata hivyo, hali ya kidini katika Burundi yatisha kuharibu maoni haya ya mwelekeo mzuri. Karibu asilimia 80 ya watu wa huko hudai kuwa ni Wakristo, walio wengi wakiwa ni Wakatoliki wa Kiroma. Hata hivyo, tawala za kisiasa huko zimeweka kiolezo chenye kufadhaisha cha kukosa uvumilio wa kidini. Siku ya Oktoba 16, 1985, The Christian Century iliripoti hivi: “Katika muda wa mwaka mmoja uliopita serikali ya Burundi imezidisha mfululizo wa vitendo vyenye shabaha ya kudhoofisha kuwako kwa kanisa . . . Haki ya kuabudu na kusali peupe na faraghani imepunguzwa kwa kadiri kubwa. Makanisa yote ya madhehebu fulani-fulani . . . yamefungwa na kukatazwa yasifanye utendaji; . . . dazani kadhaa za Wakristo mmoja mmoja wametiwa gerezani, baadhi yao hata wakiteswa-teswa . . . na yote hayo kwa ajili ya kujizoeza haki yao ya kufanya zoea la kidini.”
Hivyo matumaini yaliinuka sana wakati, katika Septemba 1987, serikali mpya ikiwa chini ya uongozi wa Rais Pierre Buyoya ilipoingia mamlakani katika Burundi. Huyo rais mpya aliahidi taifa lake uhuru wa kidini, naye akachukua haraka hatua za kutimiza ahadi yake. Ripoti moja iliyotolewa na Idara ya Mambo ya Kiserikali United States yasema hivi: “Wakati wa mwaka wake wa kwanza kuwa ofisini, Rais Buyoya alifanya mabadiliko makubwa katika sera za Burundi kuelekea dini iliyopangwa kitengenezo, akibadili ukandamizi wa maoni ya kidini uliokuwapo chini ya utawala [uliotangulia]. Buyoya aliwafungua wafungwa-gereza wote wa kidini; akayafungua upya makanisa yaliyofungwa; akarudishia makanisa mali zote ambazo yalinyang’anywa.” Vitendo hivi vyenye kunururishwa vilifanya Rais Buyoya aheshimiwe sana na wapenzi wa uhuru ulimwenguni pote.
Basi, kwa nini Mashahidi wa Yehova peke yao wakachaguliwa hivi majuzi wawe lengo la uonevu wa kidini?
Mashahidi wa Yehova—Mng’ang’ano wa Kutambuliwa
Muda wa miongo ya miaka iliyopita, Kanisa Katoliki “liligeuka-geuka likawa muundo wenye nguvu nyingi kiuchumi na kisiasa,” laripoti The New York Times. Katika siku ambazo taifa hilo lilikuwa katika ukoloni, kanisa liliruhusiwa “kutawala nchi katika karibu mambo yote,” kwa kuwa hilo ndilo “lililoshiriki sehemu kubwa katika kuandaa utunzi wa kiafya na elimu.” Basi, si ajabu sana kwamba huenda ikawa serikali ilihisi ikitishwa na dini iliyopangwa kitengenezo.
Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova walipoanza kazi yao ya kueneza evanjeli peupe katika Burundi katika 1963, wao hawakufanya jaribio lolote la kuingilia-ingilia mambo ya Serikali. Bali, waliifanya kazi yao iwe ni kuhubiri tu “habari njema hizi za ufalme.” (Mathayo 24:14, NW) Kwa kuwa Biblia husema kwamba Wakristo wa kweli wapaswa wawe “si sehemu ya ulimwengu,” Mashahidi wa Yehova walibaki bila kuwamo katika siasa, huo ukiwa ni msimamo wenye kuchukuliwa na Mashahidi ulimwenguni pote.—Yohana 17:16, NW.
Mashahidi walijiepusha kidhamiri wasijiunge na vyama vya kisiasa na wasipaaze sauti kwa kutamka shime za chama cha kisiasa. Mara nyingi serikali zimeelewa vibaya kwamba msimamo huu wa kutokuwamo ni ukosefu wa uzalendo au hata unaonyesha kutaka mapinduzi. Lakini sivyo ilivyo. Mashahidi wa Yehova katika sehemu zote za ulimwengu wajulikana kuwa raia walio vielelezo kwa kufuata sana sheria. Wao huichukua kwa uzito amri ya Biblia ya ‘kutii’ serikali za kilimwengu. (Warumi 13:1) Ingawa wao hujiepusha kupiga saluti (salamu) au kuonyesha kicho kwa njia nyingineyo kuelekea ishara za kuwakilisha taifa kama vile bendera, hawakosi staha kwa vifananisho hivyo.—Kutoka 20:4, 5.
Katika 1975 Mashahidi wa Yehova walikuwa wameomba utambuzi wa kisheria kwa kazi yao. Lakini katika 1976 mapinduzi ya kijeshi yaliitupa nje serikali na kumtia mamlakani Rais Jean-Baptiste Bagaza. Yeye aliahidi uhuru wa ibada. Hata hivyo katika Machi 1977, Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku kirasmi! Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote walifanya jitihada kuelewesha mambo vizuri kwa washiriki wa serikali ya Bagaza, lakini barua zilizoandikwa, ziara zilizofanywa kwa ubalozi wa Burundi katika Ufaransa na Ubelgiji, na mikutano iliyofanywa pamoja na maofisa wa serikali katika Burundi, yote hayo hayakuzaa tunda. Katika 1987 Mashahidi kama 80 katika Burundi—wanaume na wanawake—walitupwa gerezani kwa miezi kadhaa. Shahidi mmoja alifia humo.
Halafu katika 1987 mapinduzi yakamleta Meja Pierre Buyoya mamlakani. Muda si muda Wakatoliki na Waprotestanti wakanufaika na uvumilio wake wa kidini—lakini si Mashahidi.
Kutokea kwa Mnyanyaso wa Kidini
Kufuata mkutano mmoja uliofanywa na Rais Buyoya pamoja na magavana wa mikoa siku ya Februari 16, 1989, ilitangazwa katika redio kwamba moja la matatizo makubwa ambayo Burundi ililazimika kuyakabili lilikuwa mtanuko wa Mashahidi wa Yehova. Kana kwamba wakitenda kwa kufuata ishara hiyo, magavana wa mikoa ya ndani-ndani wakaanzisha wimbi la mnyanyaso. Ingawa bado maelezo kamili hayapatikani kwa urefu, ripoti zinazofuata zatoa wazo fulani juu ya mambo yanayotukia huko:
Mkoa wa Gitega: Gavana Yves Minani aliagiza kwamba polisi na halaiki ya watu wajumuishwe pamoja kuwakamata Mashahidi wa Yehova wote. Jioni ya Machi 22, 1989, mawakili wa polisi wa usalama waliingia kinguvu ndani ya nyumba ya Ntibatamabi Edmond, mweneza-evanjeli aliye painia wa pekee, na wakamkamata. Akiwa kizuizini, alinyimwa chakula. Alizimia mara nyingi kwa kuwa na njaa. Pia aliteswa-teswa kwa jaribio la kumfanya ahakikishe ukweli wa uvumi fulani kwamba Mashahidi wa Yehova hula damu ya kibinadamu—uwongo wenye nia mbaya kama nini!
Baada ya Edmond kukamatwa, Ntikarahera Aaron na Ntimpirangeza Prime, wao pia wakiwa ni Mashahidi wa Yehova, walikamatwa wakawekwa gerezani katika Gitega. Vivyo hivyo wao wakatendwa kikatili.
Nijimbere Charlotte, mke wa mwangalizi wa mzunguko mmoja—mhudumu mwenye kusafiri anayezuru makundi kadhaa—alipata habari juu ya shida kubwa iliyowafikia ndugu zake Wakristo. Akajaribu kupeleka chakula gerezani lakini akakamatwa siku ya Machi 16, 1989 na kushikwa mateka humo, hilo likiwa ni jaribio la wenye mamlaka la kutaka kukamata mume wake.
Mkoa wa Muramuya: Gavana Antoine Baza aliwapelekea wito rasmi Mashahidi wote wajulikanao ili wakutane naye na kujibu maswali. Siku ya Machi 4 kikundi kimoja kilikubali kufuata ombi hilo. Ingawa walijibu maswali yake kwa staha, walikataa kupaaza sauti wakitamka shime za chama cha kisiasa.
Gavana huyo akajibu kwa kuchochea halaiki ya watu wa hapo wawashambulie Mashahidi wa Yehova. Siku ya Machi 16 polisi waliziingia nyumba za Mashahidi wajulikanao na kuanza kupiga wanaume na wanawake kwa kukataa kupaaza sauti wakitamka shime za chama. Duka la Shahidi mmoja lilinyakuliwa likafungwa—jambo hilo likinyima jamaa ile riziki yao.
Siku ya Machi 17 wanawake wanne walipigwa kwa sababu walikataa kukana imani yao. Walitiwa katika kijumba cha gereza kisicho na sehemu za kuingiza hewa, hata ingawa mmoja wao alikuwa mama mwenye kitoto cha siku 20 tu.
Siku ya Machi 20 wanaghasia wenye vijiti na tochi waliingia kinguvu ndani ya nyumba za wanawake fulani Mashahidi, wakawapiga na kuwafukuza kutoka nyumba zao. Miongoni mwa waliotendwa ubaya alikuwamo mwanamke wa miaka 75 aliyekuwa anajifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova na vijana kadhaa wa chini ya miaka 14!
Pierre Kibina-Kanwa, mkurugenzi wa shule ya msingi ya Nyabihanga, alijaribu kulazimisha wanashule Mashahidi waipigie saluti bendera ya taifa. Kwa kutoweza kufanya hivyo, yeye aliwafukuza. Mashahidi 22 kutoka mji huo walilazimishwa kukimbia, wakiacha nyuma mali zao zote. Miongoni mwa waliokamatwa walikuwamo Ndayisenga Leonidas, Kanyambo Leanard, Ntahorwamamiye Abednego, Bankangumurindi P., Kashi Gregoire, na Mbonihankuye Thadee.
Mkoa wa Bujumbura: Msimamizi wa mtaa wa Muhuta, Nahimana Macaire, alipeleka wito kwamba Kavunzo Vincent, Ndabazaniye Sylvestre, na Ndizwe-Nzaniye—wote wakiwa ni Mashahidi—waende kwenye mkutano. Huko aliwashtaki kuwa walihusika katika pambano fulani la kikabila lililotukia Agosti 1988. Baada ya hapo mapigo na visa vya kukamatwa vikafuata, ingawa ilikuwa wazi kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuhusika.
Mkoa wa Bubanza: Mashahidi wawili walikamatwa kwa sababu tu ya kuwa na fasihi za Biblia. Walipokataa kupiga ile saluti ya chama, Gavana Kimbusa Balthazar aliagiza wapelekwe kwenye kambi ya kijeshi. Huko wakateswa-teswa kwa kutwangwa-twangwa vidole.
Jambo Ambalo Wewe Waweza Kufanya
Yaliyo mengi ya matendo haya yasiyostahili yametukia katika sehemu za ndani-ndani, mbali na macho ya watu wa nchi za kigeni. Hata hivyo, nakala zaidi ya milioni 13 za makala hii zitagawanywa ulimwenguni katika lugha zaidi ya 105. Matendo ya unyama wa Burundi hayatakuwa siri tena. Watu walio wapenzi wa uhuru watagutuka sana kwamba haki za kibinadamu zinavunjwa kwa njia mbaya hivyo—haki ambazo maelfu ya Waafrika wamezifanyia jitihada kubwa.
Hivyo Burundi yajasiria kupata hasara ya mambo mengi kwa kutotimiza ahadi yayo ya uhuru wa kidini. Yajasiria kuharibu sifa ambayo imejithibitishia kwa bidii nyingi sana, ile ya kuwa taifa lenye maendeleo, la kufanya kazi kwa bidii. Je! Burundi yataka ipate jukumu la kuonwa kuwa taifa la wanyanyasi wa kidini walio washupavu? Sisi twafikiri haitaki hivyo. Jambo tu ambalo sisi twaweza kujichukulia ni kwamba Rais Buyoya amepashwa habari vibaya, akaongozwa vibaya na washauri wake.
Mashtaka yaliyofanywa dhidi ya Mashahidi wa Yehova ni mawongo ya kipuuzi yaliyokusudiwa kuchochea mwali wa harara zisizo za kiakili. Mashahidi wa Yehova si tisho kwa usalama wa serikali ya Burundi wala taifa jingine lolote. Wao ni wenye amani na wenye kufuata sana sheria, wakistahi vifananisho vya kitaifa. Tofauti na uvumi, wao hukataa kenyekenye kuingiza miilini mwao damu ya namna yoyote—hata maisha zao zikiwa hatarini.—Matendo 15:28, 29.
Kwa hiyo Wakristo wa kweli katika sehemu zote za ulimwengu watasali kwa umoja kwa ajili ya ndugu zao katika Burundi. (1 Timotheo 2:1, 2) Pia wasomaji wengi watasukumwa na moyo kumwandikia moja kwa moja Rais Pierre Buyoya, wakitoa ombi lenye staha kwamba mnyanyaso wa kidini ukomeshwe na kwamba Mashahidi wa Yehova wapokee utambuzi rasmi kuwa dini iliyothibitishwa imara. Ni lazima Burundi iitikie kusababu mambo kiakili ikiwa itajikomboa machoni pa ulimwengu.
His Excellency Major Pierre Buyoya
President of the Republic of Burundi
Bujumbura
REPUBLIC OF BURUNDI
[Ramani katika ukurasa wa 22]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
RWANDA
ZAIRE
BURUNDI
TANZANIA
ZIWA TANGANYIKA