Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 8/15 kur. 25-28
  • Waguatemala Wazipokea Habari Njema kwa Furaha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Waguatemala Wazipokea Habari Njema kwa Furaha
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Mbiu ya Ufalme Yaanza Kupigwa
  • Kuhubiri Katika Nyanda za Juu
  • Twateremka kwa Kufuata Mabara ya Chini Pwani
  • Jeuri na Mnyanyaso Zatofautiana na Amani
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 8/15 kur. 25-28

Waguatemala Wazipokea Habari Njema kwa Furaha

MILIMA ya samawati na volkeno kubwa sana (milima milipusha-moto) zatokeza ghafula kule mbali wakati ndege ikaribiapo mji mkuu. Abiria katika upande mmoja watazama nje ya dirisha lao na kuona Mlima Pacaya ukilipuka, ukilipusha-lipusha moshi wenye kufanyiza safu yenye kuinuka na kuyeyuka angani. Abiria wa upande ule mwingine watazama chini na kuona mashua za kuendeshwa kwa matanga na mashua za kuendeshwa kwa makasia zikilivuka Ziwa Amatitlan kwa utulivu. Hii ni Guatemala, bara la mitofautiano mikubwa.

Ikiwa katika Amerika ya Kati, Guatemala yafunika eneo la karibu kilometa za mraba 109,000. Mandhari ya bara hilo yatofautiana kuanzia milima mirefu—kutia ndani volkeno 33, 4 kati yazo zikiwa zenye utendaji—hadi miitu ya nyanda za chini, misitu yenye mvua, na maziwa na miito yenye maji maangavu sana. Mwinuko wa ardhi watofautiana kuanzia kimo cha usawa wa bahari hadi meta 4,211. Katika mji mkuu, majira ya uchanuzi wa mimea ni ya daima, kukiwa na halijoto ya wastani wa digrii 24 Selsio mwaka mzima. Lakini juu zaidi milimani hali-joto yaweza kushuka na kuzizima kwa baridi inayozidi kiwango ambacho maji hugeuka yakawa barafu, huenda maeneo ya pwani yakawaka joto kali la digrii 38 Selsio. Hii ni nchi iwezayo kuufaa upendezi wa mtu yeyote, nayo ina fuo za bahari, miitu, milima, kanda kavu za ardhi, na mabonde yenye matunda. Na katika maeneo haya yote, habari njema za Ufalme zinahubiriwa.

Mbiu ya Ufalme Yaanza Kupigwa

Uhubiri wa Ufalme ulianza katika Guatemala karibu mwaka 1920. Baada ya muda vikundi vidogo vya watu wa kupendezwa na wapiga mbiu kuhusu Ufalme vilianza kufanyika katika sehemu mbalimbali za nchi. Wamisionari wa kwanza wawili walipowasili siku ya Mei 21, 1945, walipata upendezi mwingi. Mmoja asimulia hivi: “Mimi niliamua kufanya kazi ya magazeti barabarani katika Jumamosi ya pili baada ya kuwasili kwetu. Jioni hiyo nikaondoka nikiwa nimejaza fasihi katika mkoba wangu wa vitabu, na katika muda wa saa moja na nusu, ukabaki mtupu, nikiwa nimeangusha magazeti 32, vijitabu 34, vitabu 4, na Biblia moja.” Mwaka huo wa kwanza wao walianza kuongoza mafunzo 17 ya nyumbani ya Biblia! Dada misionari aliyekuwa wa kwanza kuwasili angali anahubiri habari njema za Ufalme kwa shauku miaka 44 baadaye.

Mitofautiano ni mingi sana katika eneo la kuhubiri. Mji mkuu, Jiji la Guatemala, lina ghorofa nyingi za ki-siku-hizi, na pia maeneo yenye makao tu, yakiwa na nyumba nzuri, ambako mayaya hujibu hodi za mlangoni kwa kutumia kikuza-sauti cha ndani ya nyumba. Lakini umbali wa kutupa jiwe kutoka hapo, kuna makao yenye kuta za matofali yasiyochomwa yakiwa na paa zilizoezekwa kwa majani, ambako huwa ni ndoto tu kuweza kutumia nguvu za umeme na maji ya mfereji. Kukiwa na eneo lenye unamna-namna wa jinsi hiyo, hakuna kitu kama siku ya kikawaida tu katika utumishi wa shambani.

Katika miaka ya majuzi milango mingi haifunguliwi kwa sababu mume na hata mke huwa wametoka wakafanye kazi. Kwa hiyo ili kuwapa ushahidi watu wa jinsi hiyo, mara nyingi Mashahidi hushiriki katika kazi ya barabarani. Baadhi yao huanza saa 11:30 asubuhi, wakitoa fasihi kwenye vituo vya basi vyenye pirika-pirika nyingi. Ni lazima Shahidi awe mwenye nguvu za kutosha kimwili ndipo awezane na mwendo wa watu wanaofanya kukuru-kakara ya kupanda basi yao. Asubuhi moja kikundi cha Mashahidi kiliamua kuwaendea madereva fulani wa taksi kwa sababu mabasi yalikuwa yamepunguza utendaji. Walishangaa kuona madereva kadhaa wa taksi wakiwatolea nakala zao za gazeti Mnara wa Mlinzi zikiwa tayari zimepigwa mistari. Mmoja au wawili alikuwa na maswali, nao akina ndugu wakafurahi kuyajibu kwa kutumia Biblia za hao madereva wenyewe wa taksi.

Kuhubiri Katika Nyanda za Juu

Panajachel ni kimoja cha vijiji vyenye kuzunguka Ziwa Atitlan, ziwa zuri la maji ya kijani-samawati yaliyozungukwa na milima yenye fahari na volkeno tatu. Vijiji fulani hupewa majina ya mitume. Karibu asilimia 95 ya watu hao ni wa ukoo wa Kimaya, huku Kikakchiquel na Kitzutuhil zikiwa ni mbili kati ya lugha zilizo kubwa. Ingawa wanaume hunena Kihispania pia, walio wengi kati ya wanawake hawafanyi hivyo, kwa maana wao hutumia sehemu kubwa ya wakati wao wakiwa nyumbani. Kila kijiji kina vazi lacho chenyewe la kimapokeo lililo la kupendeza, na kwa kawaida hilo hufumwa na wanawake kwa mikono.

Unapowasili katika Panajachel, utaona kwamba mji huo si kama miji mingine midogo katika Guatemala. Kando-kando ya nyumba za hali ya chini zilizojengwa kwa matofali yasiyochomwa au mawe, waona vijumba vya starehe vyenye kupendeza. Kwa kutofautiana hata zaidi na vijumba hivyo, zipo hoteli za ki-siku-hizi. Watu wa kutoka sehemu zote za ulimwengu huja Panajachel ili wavutiwe na uzuri wa Ziwa Atitlan.

Shahidi mmoja aeleza jinsi kazi ya kuhubiri inavyofanywa hapa: “Mashua hukodiwa mapema kwa utumizi wa siku moja, na ndugu zetu wa kutoka hapo karibu Solola, pamoja na wengine wanaozuru kutoka Jiji la Guatemala, hualikwa kusaidia kufanya kazi katika eneo kubwa hilo. Akina ndugu kutoka Solola ni msaada mkubwa kwa sababu walio wengi kati yao huishi juu katika mtambao wa milima-milima unaofanana na ule tutakaokuwa tukizuru. Pia wao hunena lugha ya kienyeji. Safari huanza mapema asubuhi. Huku mashua ikivuka ziwa hilo, watoto wavutiwa na yale maji maangavu sana ya samawati, na wazazi wajizoeza maneno kadhaa ya lugha hiyo.

“Wakati huu vijiji vitano vitafanyiwa ziara. Kwanza, mgawanyo wa vikundi vitatu wafanyizwa. Halafu vikundi hivyo vyatenganishwa —wale wenye kunena lugha ile wawe pamoja na wale wasioinena. Kuna gudi ndogo tatu tu ambapo sisi twaweza kushuka ufuoni ili tufikie vijiji hivi, kwa hiyo kikundi kimoja chashushwa kwenye kila gudi. Inachangamsha moyo kuwaona ndugu zetu wakiwa wamevaa vazi lao la kienyeji lenye kupendeza, huku wakifanya kazi kando-kando ya wale waliovaa vazi la mtindo wa kizungu. Huo wenyewe ni ushahidi mzuri kwa wanavijiji. Kwa kawaida watoto wadadisi watusalimu. Baada ya kujua kusudi la ziara yetu, wao wakimbia wakawajulishe wanavijiji wote.

“Tufikapo kwenye nyumba zile za hali ya chini, watu wengi wanakuwa wakingoja kwa hamu kuona broshua zetu zenye rangi za kupendeza au Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia ambacho watoto hao wamewaeleza. Kipande chochote cha fasihi iliyoachwa kwenye nyumba ya kwanza ndicho kitakachoombwa kwenye nyumba zinazofuata kwa sababu kila mtu ataka kupata kitu chenye uzuri ule ule ambacho jirani yake alipokea. Wengi hawawezi kusoma, kwa hiyo wao waona shangwe hasa kuhusu picha zilizomo kuhusu Paradiso inayokuja. Nyuso zao zang’aa huku wakisikiliza tumaini la wakati ujao ambalo Biblia yaahidi kwenye Ufunuo 21:3, 4. Sisi twasimama kwa ufupi tuone shangwe ya kula mlo wa mchana wenye kuandaliwa mtindo wa kipikniki halafu tuendelee kuongea na watu mpaka saa 9:00 alasiri. Halafu twarudi kwenye gudi tukangoje mashua ituchukue hapo. Kila mtu akiisha kuipanda, akina ndugu washirikiana kwa furaha mambo yao waliyoona.

“Dada mmoja akumbuka upendezo mwingi aliohisi wakati aliposikia mwanamke mmoja aliyekuwa juu yake akipaaza sauti hivi, ‘Dada, dada, mimi nipo hapa. Wewe umerudi kunifanyia mimi ziara. Asante, asante.’ Dada akatazama juu kwenye mtambao ule mwingine juu ya mlima na kumtambua mwanamke mwenye kumpungia-pungia mkono kwa msisimuko mwingi. Mara ya mwisho alipozuru kijiji hicho, mwanamke huyo alikuwa ameonyesha upendezi mwingi walipokuwa wakizungumza pamoja juu ya Biblia. Mwanamke huyo alikuwa amekuwa akilingojea rudio lililoahidiwa. Wao waliketi tena wafanye funzo jingine la Biblia lenye shangwe.

“Ingawa kila mmoja amechoka sana kwa kutembea miendo mirefu juu ya mtambao wenye miamba-miamba, wao wana hamu nyingi kujua safari ifuatayo itakuwa lini. Mashua ifikapo ufuoni, sisi twaagana kwa kuelezana kuhusu pindi yenye shangwe itakayofuata.

Twateremka kwa Kufuata Mabara ya Chini Pwani

Guatemala ina miambao miwili pia inayotofautiana: ile pwani ya Pasifiki yenye mchanga mweusi wa kutazamisha na ufuo wa Karibbea ulio na mchanga mweupe.

Mnamo mwendo wa dakika 45 kutoka mji mkuu kuelekea kwenye Pasifiki, badiliko la mazingira na tabia ya nchi ni kubwa. Hali ya joto na unyevunyevu hudumu pwani, ikiandamana na mzaano wa wadudu wengi. Mitende, minazi, na miseiba pamoja na wingi wa majani-majani hutoa ushuhuda wa kwamba wewe umo katika ukanda wa zile tropiki. Kuna makundi makubwa ya Mashahidi wa Yehova katika mingi ya miji ya jimbo hilo.

Hapa ile kawaida ya kumtumia farasi yabadilika kwa utumizi wa baiskeli, kwa hiyo si jambo lisilo la kawaida kuwaona ndugu zetu wakichochea baiskeli kasi sana kwa kupita katika mashamba ya miwa watoapo ushahidi kutoka kijumba hadi kijumba. Ndugu mmoja aliongoza funzo la Biblia pamoja na mwanamume aliyeishi kwenye umbali wa kilometa 35. Kila juma alikuwa akisafiri kwa baiskeli umbali ulio maradufu ya huo ili akamfundishe ukweli wa Biblia mtu huyu mwenye kupendezwa.

Ungeweza kuwazia umeingia nchi nyingine ukizuru zile bandari-pacha za Santo Tomas de Castilla na Puerto Barrios katika pwani ya Karibbea. Mtindo wa maisha huko ni tofauti na sehemu nyingine zote za Guatemala. Nyumba zina nyua za majani ambayo hukatwa vizuri na vichaka vya maua yenye kuonekana na watu wote; ni mara haba kuona nyumba ikiwa imezungukwa na ukuta wa matofali yasiyochomwa, ambao huwa alama moja ya kupambanua kwamba umo katika Meksiko na Amerika ya Kusini. Zaidi ya hilo, hapa hupati lile vazi la kikabila lenye kuvaliwa kikawaida sana katika sehemu nyingine zote za Guatemala.

Kwa sababu huu ni mji wenye bandari, mtu huwa na fursa ya kuwaeleza watu wa namna zote ujumbe wa Biblia,” akaeleza mhudumu mmoja wa wakati wote. “Mimi nilitembea nikipita katika milango yenye kufunguka-funguka ya nyumba moja ya pombe. ‘Memsabu’ yule alichukua toleo la kitabu kimoja na Biblia, naye akanialika nirudi kumfundisha jinsi ya kujifunza vitabu hivyo. Niliporudi juma lililofuata, yeye alikuwa akiningoja kwenye meza kubwa akiwa na Biblia ile na kitabu kile. Kwa kunipungia mkono wa kirafiki kwamba niketi, akasema ningoje kidogo huku akiwaita ‘wasichana’ wote. Alitaka wao pia wajifunze. Mimi kushtukia, nikaona meza nzima imezungukwa na ‘wasichana’ hao. Akinigeukia mimi, memsabu huyo akasema, ‘Sasa tuonyeshe jinsi ya kujifunza Biblia.’ Mimi niliwaza hivi: ‘Imekuwakuwaje hata nikajiingiza katika yote haya?’ Lakini niliendelea kwa utulivu, kana kwamba sikuzote nimekuwa nikijifunza Biblia katika nyumba ya pombe.” Memsabu huyo alifanya maendeleo ya haraka sana, akaacha biashara yake, akawa Shahidi aliyebatizwa. Leo yeye ni mtendaji katika kundi jingine, naye mwenyewe anaongoza mafunzo ya Biblia pamoja na watu wenye kupendezwa.

Mwendo wa saa moja kwa mtumbwi kwa kuivuka hori ndipo ulipo mji wa Livingston ulio na mandhari ya kuvutia, nayo ni jumuiya ya watu wenye urafiki ambao wameshawishwa sana na ushirikina na uchawi-vuduu wa Kiafrika. Si jambo lisilo la kawaida kusikia mvumo wa ngoma huko wakati wa usiku na kuona dansi ikichezwa mtindo wa Kiafrika nyakati za sherehe za sikukuu. Masikio yako yaweza pia kusikia kilugha fulani cha kigeni—Kikaribe, au Kigarifuna. Kikundi kidogo lakini chenye kuongezeka haraka cha wapiga mbiu ya Ufalme hutumikia masilahi ya watu huko.

Jeuri na Mnyanyaso Zatofautiana na Amani

Matatizo fulani yalitokea katika 1982 wakati rais mpya wa Guatemala alipokuwa akijaribu kukandamiza utendaji wa wapiganaji-haramu uliokuwa umeongezeka wakati wa utawala wa mtangulizi wake. Mbinu yake ilikuwa kufanyiza walinzi-raia wenye kutembea-tembea wakiwa na silaha kukagua sehemu za barabarani usiku, wakiilinda miji na kuwatia chonjo wanajeshi kuhusu utendaji wowote wenye kutiliwa shuku. Katika maeneo mengi harakati hii ya raia wenye kutembea wakikagua mambo ilithibitika kuwa mtihani wa kutokuwamo kwa ndugu zetu.

Katika mji mmoja kundi zima lilitiliwa mkazo ili livunje kutokuwamo kwao kwa Kikristo kwa kushiriki katika utendaji wa kutembea wakifanya ukaguzi huo. Kwa kutishwa na kifo, waliukimbilia mji mkuu, wakapokea makao huko kwenye Jumba la Ufalme mpaka walipoweza kupangiwa malazi katika nyumba za akina ndugu. Naam, ndugu wengi wamevumilia majaribu na mnyanyaso mkali wakati ambapo wanajeshi wamekuwa wakijaribu kuwalazimisha wafanye ukaguzi ule.

Ndugu mmoja asimulia hivi: “Mina nina miaka 20 nami naishi na ndugu yangu na mke wake. Magumu yangu yalianza wakati wapiganaji-haramu na harakati ya wanajeshi ilipofikia shamba nilikofanya kazi. Katika pindi moja, tulijionea kwa macho yetu wenyewe watu wanane wakichukuliwa kwa lazima kwa kuelekezewa bunduki. Wawili tu ndio waliorudi; wale wengine sita hawakuonekana tena.

“Katika Aprili 1984 majeshi yalikuja kwenye shamba hili kubwa la mifugo ili watafute waandikishwa wapya. Waliwaambia wafanya kazi wenzangu na mimi tujiunge nao. Baada ya mimi kukataa, hawakuacha kunipiga. Kuona hivyo, wafanya kazi wenzangu wakalia kama watoto, wakiniomba sana nichukue silaha nijiunge. Askari mmoja alinidukua shingo kwa vidole vyake na kuyapinda masikio yangu huku mwingine akinishikilia chini ili mwingine bado aweze kunipiga kofi na teke. Ofisa mmoja akapiga kelele kwa hasira, ‘Wewe una kasoro gani? Wewe ni mnyama, au wewe ni Mungu?’ Mwishowe ofisa mwingine akawasili na kusema, ‘Mwache tu kwa sababu hivyo ndivyo Mashahidi walivyo. Ni lazima kwanza uwaue kabla hawajakubaliana nawe.’ Ofisa yule wa kwanza akasema, ‘Mpige risasi!’ Lakini badala ya kufanya hivyo akanigonga tumbo kwa tako la bunduki yake. Waliposadiki kwamba singejiunga nao, wakaacha kunipiga. Baada ya siku tatu, waliniacha huru. Kwa msaada wa Yehova sikuvunja ukamilifu wangu. Ndiyo sababu mimi nawaambia vijana wengine wawe na uhakika mwingi sana katika Yehova, ambaye atatusaidia tuwe na uvumilivu wakati tuwapo tukiuhitaji.” Kwa furaha, hali ilibadilika sana baada ya rais mpya kukalia cheo katika Januari 1986.

Karibuni sana mitofautiano ya vita na amani, utajiri na umaskini, uhai na kifo, itatoweka milele. Katika Paradiso inayokuja ya tufe lote, mitofautiano ya kufurahisha ya usiku na mchana, milima na mabonde, bahari kuu zenye kunguruma na maziwa matulivu, itaonewa shangwe kama vile Yehova Mungu alivyokusudia. Waweza kuwapo pia ikiwa wewe, kama wale wapiga mbiu ya Ufalme walio zaidi ya elfu kumi katika Guatemala, utazipokea habari njema kwa moyo mzima.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki