Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 10/15 kur. 24-28
  • Maamuzi ya Moyo Mkuu Yatokeza Mibaraka Katika Suriname

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maamuzi ya Moyo Mkuu Yatokeza Mibaraka Katika Suriname
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Uamuzi Uliookoa Maisha Yake
  • Upendo Ulimsukuma Aponyoshe Ndugu Zake
  • Yeye Hakuridhiana Msimamo Wake
  • Kafunga Ndoa Jumatano, Kabatizwa Jumamosi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 10/15 kur. 24-28

Maamuzi ya Moyo Mkuu Yatokeza Mibaraka Katika Suriname

WAKATI mmoja, Suriname ilikuwa “moja ya nchi zilizo tajiri zaidi za Karibea,” ndivyo likaarifu South gazeti la habari za kimataifa. Mapato yenye kutokana na madini ya bokzaiti, uduvi, mchele, ndizi, na mbao za plai, kuongezea na msaada waliopewa ili kufanya maendeleo, yaliwaandalia wakaaji 400,000 wa hili lililokuwa koloni la Kiholanzi ufanisi mwingi kuliko walio wengi wa jirani zao.

Hata hivyo, katika miaka ya 1980 uchumi ulishuka ghafula sana. Wingi ukageuka kuwa upungufu, na ikawa kawaida kuona watu wamepanga mistari mirefu wapate chakula. Katika 1986 kutokea ghafula kwa vita ya maharamia kulilazimisha wakaaji kama kumi elfu wakimbie kutoka mashariki mwa Suriname kwenda French Guiana iliyo karibu, wakaanze upya maisha huko katika kambi za wakimbizi. Kwa sasa, sehemu kubwa za pori hilo—likiwa ni makao ya watu karibu 50,000 walio Wanigro wa Vichakani na Wahindi-Waamerika—zilikuja chini ya udhibiti wa maharamia, hiyo ikifanya iwe hatari kusafiri kuingia sehemu za ndani-ndani. Mabadiliko haya, likaeleza gazeti South, liliiacha nchi ikiwa imelemaa.

Je! hali hizo zililemaza pia utendaji mbali-mbali wa Mashahidi wa Yehova? Kinyume cha hivyo, zimeharakisha mwendo wa kazi yao. Mathalani, hesabu ya Mashahidi imeinuka kutoka 920 katika 1980 ikawa zaidi ya 1,400 leo. Katika Aprili 1989 walikuwako mapainia wasaidizi 338—karibu asilimia 25 ya Mashahidi waliokuwako wakati huo. Hata hivyo, mibaraka hiyo ilikuja kutokana tu na moyo mkuu, uaminifu wa kimaadili, na upendo ambao Mashahidi walionyesha wakiwa chini ya jaribu. Hivi hapa ni vielelezo vya hivi majuzi kuhusu jinsi maamuzi ya moyo mkuu yalileta mibaraka mingi katika Suriname.

Uamuzi Uliookoa Maisha Yake

Lumey Hoever, ofisa wa polisi mwenye maungo mapana aliye katika miaka yake ya mwisho-mwisho ya 30 na ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, aliamua kwamba angeacha kazi yake ijapokuwa hali ya uchumi ilikuwa mbaya. Kwa nini? Lumey aeleza hivi:

“Tangu niliposoma makala ya Mnara wa Mlinzi ikituweka chonjo kuhusu hatari za kutembea ukiwa na silaha za kufyatua, nilijua ingekuwa lazima kuiacha kazi hii.a Ingawa hivyo, nilisita-sita kwa sababu nina mke na watoto wa kutunza. Hata hivyo, kadiri nilivyozidi kuahirisha uamuzi wangu ndivyo dhamiri yangu ilivyozidi kunisumbua. ‘Ikiwa tengenezo la Yehova lanihimiza kufikiria kwa uzito kufaa kwa kazi ya namna hii, lazima kuwe kuna sababu nzuri,’ nikajikumbusha hivyo. Kwa hiyo katika Januari 1986, nilifanya uamuzi wangu.”

Lakini chifu wa polisi hakutaka kumwacha aende zake, hata akaahidi kumpa mgawo kwenda Tamanredjo, kituo cha karibu na mji mkuu ambako wengi walitaka sana kupelekwa. Lakini Lumey aliazimia kabisa. Aliandikia waziri wa polisi, akaeleza imani zake za kidini, na kuomba afutwe kazi. Katika Aprili 1986 jibu hili lilikuja: ‘Kapewa ombi lako!’

Muda si muda Lumey alipata kazi kwenye Idara ya Misitu. Malipo hayakuwa mazuri kama yale ya kwanza, lakini alikuwa na wakati mwingi zaidi wa kuandamana na jamaa yake mikutanoni kwenye Jumba la Ufalme. Miezi kumi ilipita. Siku moja, baada ya kufanya kazi mchana kutwa katika shamba la jamaa, Lumey na ndugu yake walikuwa njiani kwenda nyumbani. Yeye asimulia hivi:

“Nilipokuwa ninakaribia nyumba ya humo shambani, niliona wanaume wawili waliovaa mavazi ovyoovyo, wakiwa wamezungusha skafu vichwani pao. ‘Kon dja (Njoo hapa),’ wakaita katika Kisuriname. Nilipokuwa nikitembea kuwaendea, mwanamume wa tatu mwenye bunduki fupi yenye kuning’inia kwenye kamba ya begani alitokea. Hapo tu ndipo nilipozinduka nikajua ilivyokuwa: kumbe ni maharamia haramu!

“Walinitazama juu chini. Halafu mmoja wao mwenye skafu akapaaza sauti hivi: ‘Mimi namjua jamaa huyu. Yeye ni polisi!’ Hapo nyuso zao zikakazika. Kwa sekunde chache, tulikodoleana macho. Mimi nikafunga pumzi. Halafu nikasikia kikelele kidogo. Kikili, kangala—kumbe mwanamume yule wa tatu katayarisha kidude cha kufyatua bunduki. Polepo-o-le, yeye kanilenga shabaha kifuani, tayari kuniua. ‘Usifyatue! Unakosea. Mimi si polisi tena,’ maneno yakaniboboka.

“Ndipo nikaona maharamia kumi na wawili wengine nyuma ya nyumba ile. Mmoja wao—mwanamume mwenye misuli aliyevaa shuka ya kiunoni, akiwa amepitanisha mishipi mwili ya risasi kwenye kifua chake kilicho uchi, na kushika silaha ya ufyatuzi wa moja kwa moja mkononi—alipiga hatua akaja mbele. ‘Wewe wasema hu polisi tena. Kwa nini?’ akadai kinguvu. Nilijitambulisha upesi kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. ‘Mashahidi wa Yehova hawatembei wakiwa na silaha,’ nikaeleza, ‘kwa hiyo niliacha kazi yangu ya kuwa polisi na sasa nafanya kazi kwenye Idara ya Misitu. Sisi huwa hatumo katika siasa zote,’ nikaongezea.

“Aliposikia nilikuwa Shahidi, hali ya uso wake ilipungukiwa kidogo na mkazo. ‘Je! ataniamini?’ nikajiuliza kwa mshangao. Ndipo ndugu yangu mchanga akawasili. Mwanamume yule aliyekuwa amevaa shuka ya kiunoni, ambaye ilionekana wazi kuwa ndiye amiri, akaanza kumuuliza maswali. Baada ya ndugu yangu kuthibitisha taarifa yangu, amiri yule alionekana kuwa ameridhika. ‘Saka yu gon! (Shusha bunduki yako)’ akamwagiza haramia yule mwingine. Nikahisi kitulizo. ‘Asante, Yehova, kwa kunilinda!’ nikasali.”

Siku chache baadaye, Lumey alipata mshtuko mwingine. Wafyatua bunduki wasiojulikana walikuwa wameua maofisa watatu wa polisi kwenye kituo cha polisi cha Tamanredjo, kituo kile kile ambapo chifu alikuwa amejitolea kumgawia! “Kama mimi ningalikuwa nimepuuza ushauri ule kutoka makala ile ya Mnara wa Mlinzi, ningalikuwa mwanamume mfu sasa,” akasema Lumey. Halafu aongezea hivi kwa shukrani: “Kwa kweli Yehova hulinda watumishi wake.”

Upendo Ulimsukuma Aponyoshe Ndugu Zake

Pigano lilipotokea ghafula kati ya vikosi vya serikali na maharamia katika ule mji wa Moengo wenye uchimbaji madini ya bokzaiti katika Oktoba 1986, Frans Salaoema, Mnigro wa Vichakani aliye katika miaka yake ya 40, alilazimika kuamua la kufanya. Mwishowe, yeye, mke wake mjamzito, na wanaye saba, pamoja na wengine kutoka mji huo, walikimbia kwa kufuata vijia-vijia vya porini wakavuka Mto Maroni ulio mpana ili wapate usalama katika French Guiana.

Na bado, Frans alikuwa na wasiwasi. Hakupata Shahidi yeyote wa kundi lake miongoni mwa wakimbizi wale. ‘Wako wapi? Je! nitaenda nikawatafute?’ akajiuliza kwa mshangao Lakini ingekuwa hatari kufanya hivyo. Maharamia walikuwa Wanigro wa Vichakani sana-sana. ‘Askari za serikali wakitupa jicho wanione nikinyemelea kupita porini, mimi kwisha ‘ yeye akawaza. Hata hivyo, aliamua kurudi akatafute ndugu zake Wakristo. Akawaambia hivi Mashahidi kadhaa katika French Guiana: “Juma lijalo, vukeni mto huu ili mje kunichukua.”

Juma moja baadaye walivuka, lakini Frans hakuwapo. Walingoja mpaka kesho yake. Bado Frans hakuonekana. “Acheni tukae usiku mmoja zaidi,” wakaamua hivyo. Ndipo Frans na kikundi cha Mashahidi wakatokea. Ilikuwa imekuwaje?

“Baada ya kuwapata akina ndugu,” Frans akasimulia, “sisi tulipita ndani ya eneo lenye pigano kali kweli kweli, tukapita polepole kuingia porini, na kusonga mbele kuelekea mpakani.” Lakini kwa nini kukawa na ukawivu huo? Frans alielekeza kidole kwenye kartoni tatu alizokuwa ameleta. Alikuwa ameenda kwenye mji mkuu akakusanye vifaa vya fasihi za Biblia kwa ajili ya Mashahidi hao wakimbizi. Ndugu hao wenye kungojea walifurahi sana. Siku iyo hiyo, Frans, wale Mashahidi walioponyolewa, na zile kartoni tatu waliuvuka mpaka wakiwa salama.

Baadaye Frans alifunga safari nyingine akasaidie Mashahidi zaidi. Hatimaye, Mashahidi 37 waliuvuka mpaka na kulowea katika kambi za wakimbizi. Frans aliwekwa katika sehemu moja iliyokuwa koloni la wakoma katika French Guiana, ambako wakimbizi hawapaswi kufanya lolote ila kujibembeza-bembeza wakiwa wamelalia vitanda vya kuangikwa kwenye miti na kupunga-punga mbu ili wawaondokee.

Hata hivyo, Frans na jamaa yake hawakujikalia kitako tu. Muda mfupi baada ya kuwasili katika kambi hiyo, Frans (ambaye sasa alikuwa pia ni baba ya binti mmoja) alijishughulisha kuzihubiri habari njema za Ufalme kwa wakaaji wa hapo wasiofanikiwa kuwa na hali bora. Kwa sababu ya uvutano wake mwema, hata alipewa ruhusa ya kusafiri kwa pikipiki akahubiri katika kambi zile nyingine. Tokeo likawa nini? Leo yeye huongoza mafunzo 14 ya Biblia pamoja na wakimbizi wenzake. Watatu kati yao wamebatizwa tayari!

Yeye Hakuridhiana Msimamo Wake

“Nitarudi katika muda wa majuma mawili nikiwa na vifaa vipya,” ndivyo Victor Wens alivyojulisha wazi, huyo akiwa ni painia wa pekee mwenye umri wa miaka 58. Alikuwa akimwacha mke wake na wanafunzi fulani wa Biblia katika kijiji cha porini katika Suriname ya kati. Hiyo ilikuwa katika Juni 1987, alipokuwa akisonga kwenda kwenye mji mkuu.

Mke wa Victor na wengine walipokuwa wakipunga mikono kusema aende salama, mifuko yao ya mchele ilikuwa karibu kuwa mitupu. Vita ya maharamia ilikuwa imekatiza upokeaji wa vifaa. Muda si muda kungekuwa na njaa. Ingawa hivyo, wao waling’amua kwamba safari ya Victor ya kutumia mtumbwi ilikuwa hatari. Yeye angeweza kujikuta katikati ya mtupiano wa risasi au adhaniwe kimakosa kuwa ni haramia. ‘Je! atarudi akiwa salama?’ wakajiuliza kwa mshangao huku mvumo wa injini ya mtumbwi ukififilia mbali.

Majuma mawili baadaye, mke wa Victor alitazama kila mahali mtoni—lakini haikuwapo ishara ya Victor. Majuma zaidi yakapita. Chakula kikaisha, na mke huyu akawa mgonjwa. “Tafadhali, Yehova, linda mume wangu,” yeye akasali. “Na iwe kwamba atarudi huku!” Miezi mitatu ikapita. Bado Victor hakuonekana. Ilikuwa imetokea kasoro gani?

“Baada ya kufika mji mkuu,” Victor akasimulia baadaye, “nilipata ruhusa ninunue chakula na petroli ya utumizi wa miezi sita. Halafu nikaomba hati ya kuniruhusu nije nyumbani. Ofisa mwenye kusimamia akasema: ‘Waweza kwenda, lakini katafute uone ni wapi ambapo maharamia wanajificha, halafu rudi utupashe habari.’ Moyo wangu ukalegea. ‘Siwezi kufanya hivyo,’ mimi nikasema, ‘Yehova hataki sisi tujiunge na upande wowote katika siasa. Sisi Mashahidi huwa wenye kutokuwamo.’ Yeye akajibu: ‘Ikiwa ndivyo, hutaenda nyumbani.’

“Kila juma nilirudi kuomba ruhusa, lakini jibu likawa lile lile. Kwa sasa, nilisikia kwamba mke wangu alikuwa mgonjwa. Nilitaka kwenda nyumbani nikamtunze. Hata hivyo, mimi sikutaka kuridhiana msimamo wangu. Nikahisi nikiwa hoi.

“Niliporudi mara nyingine tena, nilishangaa waliposema ningeweza kwenda. Wakaeleza kwamba walikuwa wamewapa ruhusa mapasta fulani Wapentekoste wa kutoka eneo langu wasafiri kurudi nyumbani, na kwamba ningeweza kwenda pamoja nao. Kwa kufurahi sana, nikaanza kufanya matayarisho mpaka nilipopata habari kutoka kwa rafiki mmoja kwamba makasisi hawa walikuwa wamekubali kuwa wapelelezi. Kwa kuwa sikutaka kutoa wazo la kwamba Mashahidi wa Yehova wamo katika mpango huo kama pete na chanda, nikapangua safari hiyo. Hapo tena nikakwama.”

Mwishowe maofisa wale walizinduka wakaona kwamba Victor hakutaka kuacha masadikisho yake. Mara ile nyingine alipowaendea, walimpa ruhusa.

Hatimaye, katika Oktoba 1987, kile kikundi kidogo cha Mashahidi kilisikia kelele ya ile injini ya nje na kuuona mtumbwi uliopakiwa vitu vizito ukitokea. “Mimi nilihisi huzuni nilipoona mke wangu,” Victor asimulia. “Alionekana amekonda sana. Hata hivyo, yeye pia alifurahi kwamba sikuridhiana msimamo wangu.”

“Uamuzi wa moyo mkuu wa Victor umekuwa baraka kwetu,” aeleza mhudumu mwenye kusafiri anayefanya kazi sehemu za ndani-ndani. “Maofisa na maharamia wamejifunza kwamba Mashahidi wa Yehova ni wasiokuwamo. Sasa wao hustahi maoni yetu, na kazi yetu inasitawi.”

Kafunga Ndoa Jumatano, Kabatizwa Jumamosi

“Msiwe wapumbavu,” wakabanwa na watu wa ukoo. “Msifunge ndoa!” Wale wanaume sita wa kabila la Wanigro Waukaneri wa Vichakani, katika pembe ya kusini-mashariki mwa nchi hiyo, walielewa hisia za watu wa ukoo wao. Ingawaje, desturi ya kikabila yaamuru kwamba mwanamume asifunge ndoa, hivyo aweza kumwacha mwanamke wakati wowote atakapo. Hata hivyo, baada ya kujifunza katika funzo lao la Biblia maoni ya Yehova kuhusu uasherati, wanaume hawa walikuwa wamerekebisha kufikiri kwao, wakavumilia mbano wa jumuiya yao, na kuamua kwa moyo mkuu wafunge ndoa ifaavyo.

Na bado, kulikuwako vipingamizi. Hali za vita zilikuwa zimefanya Ofisi ya Usajili ifungwe katika sehemu hizo za ndani-ndani, na ilikuwa ni kama haiwezekani kabisa kusafiri kwenda kwenye mji mkuu. Wanawake wale sita pia ambao wangekuwa mabibi-arusi wakati ujao walitamani pia kuvaa gauni halisi za ubibi-arusi katika siku ya arusi yao. Hiyo ilionyesha upendezi wa eneo lao katika mavazi hayo, hata ingawa hakuna uhitaji wa lazima kwamba Wakristo wavae mavazi hayo.b ‘Tutapata wapi gauni za arusi katika msitu wenye mvua?’ wale wanaume wakajiuliza kwa mshangao. Hata hivyo, maamuzi ya moyo mkuu yaliyofanywa kwa kupatana na kanuni za Biblia yalileta mibaraka. Siku ya Jumatano, Septemba 16, 1987, mabibi-arusi sita waliovaa gauni za kupendeza sana na mabwana-arusi sita waliovaa suti nadhifu walifunga ndoa. Hiyo iliwezekanaje?

“Katika Septemba, tulipanga mkusanyiko wa wilaya katika St. Laurent, French Guiana, tukawaomba Mashahidi wanaoishi sehemu za ndani-ndani wahudhurie,” aeleza Daniel van Marl, mmoja wa wahudumu wanaosafiri aliyeungisha arusi zile. “Mkusanyiko huo ulianda fursa ya kufunga ndoa.”

Cecyl Pinas, mshirika wa Halmashauri ya Tawi mwenye kutunza kazi katika sehemu za ndani-ndani aeleza hivi: “Mimi nilizuru jamaa ya Betheli katika Uholanzi mapema kidogo mwaka huo nikataja arusi hizo zenye kuja. Baada ya kutaja kwamba sisi hutumia gauni moja tena na tena, sikuzote tukiirekebisha ilingane na bibi-arusi atakayefuata, dada wanne wa Betheli walijitolea kuchanga mavazi yao ya arusi kuwa zawadi kwa ‘dada’ zao katika Suriname. Niliguswa moyo sana. Baadaye, kwenye kusanyiko moja katika Uholanzi, gauni zaidi zilichangwa.”

Asubuhi ya siku ya arusi, ilikuwa lazima bado mavazi hayo yafanyiwe marekebisho fulani. “Tulifanya haraka kupanua kiuno cha mavazi fulani na tukarekebisha urefu wa mengine, lakini tulimaliza kwa wakati ufaao,” asema Margreet van de Reep.

Ndoa hizo zilipofanywa, watano wa hao waliofunga arusi karibuni walikuwa tayari kwa ajili ya hatua nyingine. Jumamosi juma hilo hilo, walibatizwa katika Mto Maroni. Walikuwa na hamu nyingi ya kurudi kwenye vijiji vyao porini wakiwa wenzi waliofunga ndoa ili wakashiriki kazi ya kuhubiri. Je! Yehova alibariki uamuzi wao?

“Wenzi hao walionyesha jumuiya yao kwamba sisi huzoea yale ambayo twahubiri,” asema Nel Pinas mshirika wa Halmashauri ya Tawi, ambaye alianzisha kazi ya kuhubiri katika eneo ilo hilo katika 1967. “Uamuzi wao kufunga ndoa ili wawe Wakristo wa kweli umeamsha kupendezwa katika vijiji vya mbali. Sasa Mashahidi wa huko wanaendesha mitumbwi yao kuingia katika mito ambamo sisi hatukuhubiri kamwe, wakitafuta watu wengi zaidi walio na nia ya kujifunza kuhusu Yehova.

Kweli kweli, maamuzi ya moyo mkuu yaliyofanywa na Lumey, Frans, Victor, na wengine wengi yamewaletea wao na Wakristo wenzao katika Suriname na kwingineko mibaraka mingi. Maono kama haya yathibitisha tena na tena ukweli wa mithali ya Biblia: “Mtumaini Bwana [Yehova, NW] kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako.”—Mithali 3:5, 6.

[Maelezo ya Chini]

a Ona makala ‘Tafuteni Amani, Mwifuate Sana’ katika Mnara wa Mlinzi wa Desemba 15, 1983, kurasa 14-20.

b Ona “Arusi za Kikristo Ambazo Zinaleta Furaha,” katika Mnara wa Mlinzi wa Septemba 15, 1984, kurasa 8, 9.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ATLANTIC OCEAN

GUYANA

SURINAME

PARAMARIBO

Tamanredjo

Moengo

St. Laurent

Maroni River

FRENCH GUIANA

BRAZIL

300 km

200 mi

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mandhari mbili za Jumba la Ufalme zuri lililo katika sehemu ya kandokando nchini

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mashua halisi iliyotumbuliwa kutokana na gogo la mti katika Suriname

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki