Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 11/15 uku. 26
  • Wakati wa Mavuno Katika Bara la Barafu na Theluji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wakati wa Mavuno Katika Bara la Barafu na Theluji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Kufanya Mwanzo
  • Watu wa Kuongezea Nguvu Wawasili
  • Mavuno Hatimaye!
  • Kuzuru Shamba la Greenland
  • Mavuno Yaendelea
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 11/15 uku. 26

Wakati wa Mavuno Katika Bara la Barafu na Theluji

GREENLAND, kisiwa kilicho kikubwa zaidi ulimwenguni, kwa kweli ni bara la barafu na theluji. Sehemu kubwa ya kisiwa hiki chenye urefu wa karibu kilometa 2,720 kiko kaskazini ya Duara ya Aktiki na kiko chini ya kileleta cha barafu ya daima yenye unene wa kilometa moja hivi. Sehemu ile nyingine yote ya Greenland hufunikwa na theluji kuanzia miezi mitano hadi minane au zaidi mwakani. Yasemwa kwamba Maharamia wa mapema wenye kupeleleza bahari walikiita Greenland ili kuvutia walowezi. Hata hivyo, wakati wa kile kiangazi kifupi maeneo fulani ya pwani huwa na hali zenye kulingana na jina hilo.

Katika masika, ile bahari yenye kugandamana barafu kando ya kaskazini-mashariki mwa Greenland huvunjika-vunjika, na barafu iliyoshikamana sana hutokea. Barafu hii hupita ikiteremka pwani ya mashariki, kuzunguka Cape Farewell, na nusu fulani hupanda juu kwenye pwani ya magharibi, hiyo ikifanya usafiri wa baharini uwe mgumu mno muda wa miezi mingi. Wakati wa kipupwe, bahari yenye kuzunguka sehemu kubwa ya kisiwa hugandamana, ikitenganisha sehemu zile zenye kukaliwa. Kwa uhalisi, barafu hutawala bara, bahari, na njia ya maisha ya watu. Ni vigumu kuwazia ni nini kingeweza kuvunjwa katika nchi hii.

Kufanya Mwanzo

Waeskimo wa tamaduni za Kiinuit wameishi wakiwa wawindaji katika Greenland kwa karne kadhaa. Katika 1721 mhudumu Mlutheri Hans Egede alikuja Greenland akiwa misionari. Baadaye, Misheni ya Moravia iliendesha utendaji wayo katika maeneo mbalimbali ya ulowezi. Baadhi ya wamisionari wao walitafsiri vitabu fulani vya Biblia katika lugha ya Greenland, wakihifadhi jina la kibinafsi la Mungu, Yehova, katika tafsiri yao. Lakini tangu 1900, ni Kanisa Lutheri la Kidenmark tu ambalo limeendesha shughuli katika Greenland.

Katika 1953, Greenland ilipokuwa ingali koloni la Denmark, badiliko la matukio ya maana lilitukia. Kulingana na Katiba mpya ya Kidenmark iliyoanza kutumika mwaka huo, vikundi vingine vya kidini vilivyo tofauti na Kanisa Lutheri viliruhusiwa tena kuwa katika Greenland. Hivyo, katika Januari 1955, wawili wa Mashahidi wa Yehova kutoka Denmark waliwasili wakiwa wamisionari. Mgawo wao ulikuwa eneo kubwa la kilometa 1,920 kandokando ya pwani ya kusini-magharibi, ambapo karibu Wagreenland wote waliishi —idadi ya watu 27,000, ambayo sana-sana ilikuwa ya wawindaji na wavuvi.

Kristen Lauritsen, mmoja wa wale Mashahidi wawili, akumbuka hivi: “Maarifa yetu juu ya lugha ya Greenland yalikuwa haba mno, lakini tulikuwa na tamaa kubwa sana ya kuwafundisha Wagreenland ukweli wa Neno la Mungu. Tulikuwa na trakti chache katika lugha ya Greenland, na kijitabu ‘Habari Njema Hizi za Ufalme’ kiliwasili baadaye mwaka huo wa kwanza.” Wao walifanya-fanyaje kazi yao ya kuhubiri?

“Mwanzoni tulitumia kadi zilizopigwa chapa ili kueleza kusudi la ziara yetu. Lakini baadaye tukajifunza kukariri sentensi fulani kwa moyo. Sikuzote usafiri kati ya mji na mji ulifanywa kwa mashua na ulikuwa usiotegemeka sana, kwa kuwa jedwali za kufuata wakati zilikuwa ni kama hazitumiki kabisa. Lilikuwa jambo la kawaida mtu kupatwa na kuhisi vibaya kwa kupatwa na kichefuchefu cha kusafiri baharini. Pia tulikuwa na matatizo ya kupata mahali pa kukaa. Mara nyingi, tulilazimika kutosheka na hema tulilolichukua siku-zote pamoja na mizigo yetu.”

Lakini zilikuwako hali nyingine za kusawazisha magumu hayo. Wagreenland ni jamii ya watu wenye urafiki na ukaribishaji-wageni. Ni asili yao kuamini katika Mungu na kustahi Biblia. Karibu kila kao lina Biblia kamili katika lugha ya kienyeji. Kristen akumbuka kwamba wakati mmoja msichana mdogo aliwajia akiwa na barua ndogo iliyosema kwamba: “Ikiwa nyinyi bado hamjapata mahali pa kukaa, mwaweza kuja mkae nasi.” Jamaa hii iliwasaidia pia wapate mahali ambapo walipanga kuonyeshea moja ya filamu za Sosaiti.

Watu wa Kuongezea Nguvu Wawasili

Kufikia 1961 jamaa za kutoka Denmark zilianza kuhamia Greenland ili kutumikia mahali ambako uhitaji wa Mashahidi ulikuwa mkubwa zaidi. Walijitahidi ajabu kujifunza ile lugha ngumu mno ya Greenland na kuvumilia kuwa mbali na waamini wenzao. Walifanya mikutano kwa ukawaida na wakabaki wakiwa imara katika imani yao na utendaji wa Kikristo. Hakika kazi zao za jasho hazikuwa za bure. Mwaka huo makundi mawili ya kwanza yalianzishwa katika Greenland, moja likiwa katika mji mkuu Nuk (Godthab) na lile jingine likiwa katika Qaqortoq (Julianehab), upande wa kusini. Mashahidi hao walipata shangwe kubwa wakati Wagreenland fulani waliokuwa wamehamia Skandinavia walipobatizwa.

Katika miaka ya 1970 vijana kadhaa waliofunga ndoa waliwasili wakiwa mapainia wa pekee wenye bidii, wakiwa kwenye usukani wa kazi ya kutoa ushahidi. Kufikia 1973 Mnara wa Mlinzi na kitabu Kweli Iongozayo kwenye Uzima wa Milele vilipatikana katika lugha ya Greenland. Wakiwa wameandaliwa hivyo, mapainia walijishughulisha sana pwani, wakizuru miji na vijiji, wakipanda kwa wingi mbegu ya ukweli. Kwa mara ya kwanza, kazi ya kuhubiri ikawa imefikia pwani ya mashariki iliyojitenga karibu-karibu na Ammassalik (Angmagssalik). Hatimaye ikawa shangwe iliyoje wakati Mgreenland alipoukubali ukweli kwa moyo katika Greenland mwaka huo!

Mavuno Hatimaye!

Misaada mingine ya kujifunzia Biblia ilipotangazwa kwa chapa katika lugha ya kienyeji, fasihi nyingi ziliangushwa. Kwa kielelezo, halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa wenzi Mashahidi waliofunga ndoa kuangusha kuanzia vitabu 300 hadi 400, na vijitabu vya kadiri iyo hiyo, na magazeti 1,000, na pia kupata maandikisho 60 au 70, wakati wa kufanya kazi katika eneo asilogawiwa mtu.

Kutokana na upandaji wote na utiliaji maji uliofanywa, ‘Mungu amekuza vitu’ miongoni mwa Wagreenland wenyeji na pia Wadenmark wanaoishi katika Greenland. (1 Wakorintho 3:5-7) Leo, wapiga mbiu wa Ufalme 117 hutumikia katika makundi saba na kikundi kimoja kilicho peke yacho, wakiwa wametapakaa sehemu zote za bara hili la barafu na theluji. Acheni tukutane na baadhi ya wafanya kazi hawa wenye bidii.

Kuzuru Shamba la Greenland

Mahali pazuri pa kuanzia ni kundi la kusini kabisa, katika Qaqortoq (Julianehab). Jamaa tano zimepanda juu kutoka Denmark zikaja kutumikia hapa. Baadhi yao wametia bidii kujifunza lugha ya Greenland ili waweze kuwatolea ushahidi Wagreenland wasioelewa Kidenmark. Flemming, ambaye ni mwanamume wa jamaa na ni painia (mpiga mbiu wa wakati wote wa Ufalme) katika kundi hili, asema hivi: “Eneo letu ni kubwa. Latia ndani vijiji vingi vya uvuvi na vituo vya ukulima vilivyobanwa kati ya mtataniko wa vijito vingi vyenye kupita magengeni ili vikaingie katika pwani ya kusini.” Kwa kutumia mashua-mota zao wenyewe, Mashahidi hufunga safari ndefu hata kufikia kilometa 640 ili watembelee watu wanaoishi katika sehemu hizi za kando sana.

Baada ya kusafiri muda wa saa tatu kwa mashua kupitia vile vijito vyenye kupita katika magenge ya kuvutia sana, twaja kwenye kundi lifuatalo, kule Narsaq. Hapa inaishi jamaa ya peke yake yenye wahubiri wanne wa Ufalme. Ingawa wako mbali na wengine, wao huweza kutiana moyo na kujengana kiroho kupitia tabia zenye afya za kujifunza na kwa kushiriki kwa ukawaida katika mikutano na huduma ya shambani.

Sasa twapanda meli ya pwani ya abiria ambayo huja hapa kila juma katika miezi ya kiangazi. Safari hii ya saa 24 yatufikisha Paamiut (Frederikshab), ambako kuna Mashahidi kumi. Lakini tukiwa nusu ya mwendo huo, twapita kijiji kimoja ambako kuna wahubiri wawili walio peke yao. Mmoja wao, Ane Marie, ana mwana katika Nuk ambaye alijifunza ukweli miaka michache iliyopita na akaanza kumtolea yeye ushahidi kwa simu na barua. Yeye alithamini aliyoambiwa na mwanaye. Kwa kusoma kila kitu kipatikanacho katika lugha ya Greenland na kusikiliza kanda za Mashahidi Wagreenland wakisimulia maono yao, Ane Marie amechukua msimamo wake upande wa ukweli. Akiwa na miaka zaidi ya 60 na bila msaada wa kundi la kienyeji, yeye alifaulu kuvunja tabia yake ya uvutaji sigareti wa miaka 50, akaacha kuadhimisha Krismasi na siku za kuzaliwa, na kuanza kutolea kijiji chote ushahidi. Kutokana na jitihada yake yenye saburi na kielelezo chema, karibu watu kumi wenye kupendezwa hukusanyika kwa ukawaida kujifunza Biblia na kusikiliza mikutano ya kunasa sauti katika ukanda.

Tuondokapo Paamiut, twasafiri mwendo wa saa 14 kwa mashua katika bahari wazi iliyochafuka na kufika Nuk. Katika mji mkuu huu wenye watu 13,000, mna wahubiri 43 katika kundi, na zaidi ya theluthi moja ni Wagreenland. Mikutano ya kila juma ni mchanganyiko wa lugha ya Denmark na ya Greenland, kwa uhakika hilo likiwa ni takwa la jitihada kubwa kwa vikundi vya lugha zote mbili.

Turudipo tena kwenye ile meli ya pwani ya abiria, safari ya saa nane yatufikisha Maniitsoq (Sukkertoppen). Hapa, jamaa nne kutoka Denmark zafanya kazi pamoja na wahubiri wachache wa Ufalme walio wa uenyeji huo. Wamelimaliza kikamili sana eneo la mjini na wameangusha fasihi nyingi sana za Biblia hivi kwamba kila nyumba ya pili ina nakala ya Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia katika lugha ya Greenland. Kwa kutumia mashua-mota zao, wao hupanga pia safari za ukawaida za kuvitolea ushahidi vijiji vya kandokando.

Tukiendelea mbele upande wa kaskazini, kituo chetu kifuatacho kiko mwendo wa saa kumi, kule Sisimiut (Holsteinsborg). Jamaa tano za Kidenmark na wahubiri wachache wa kienyeji ndio hufanyiza kundi la huko. Mume na mke walio mapainia wa pekee hutoka hapa kwenda kufanya ziara za pindi kwa pindi kwenye pwani ya mashariki. Hii yahusisha safari ya mwendo wa nusu-saa kwa helikopta kwenda kwenye uwanja wa ndege, safari ya mwendo wa saa mbili kwa ndege kuvuka kile kileleta cha kati chenye barafu, na mruko mwingine mfupi wa helikopta ili kuvuka ghuba iliyopo ndiyo ufike Ammassalik katika pwani ya mashariki. Mandhari ya huko huvutia kweli kweli—milima yenye kujipinda-pinda iliyoinuka juu sana na mimomonyoko ya barafu yenye kujaza mashimo yaliyo chini. Watu hupokea sana ujumbe wa Ufalme, lakini ni wachache tu ambao mpaka sasa wamechukua msimamo wao upande wa ukweli.

Baada ya kuruka kurudi ng’ambo nyingine kwa kuvuka kile kileleta cha barafu, twafanya kituo chetu cha mwisho katika Ilulissat (Jakobshavn), kundi lililo mbali zaidi kaskazini. Ilulissat ni neno la Kigreenland la kusema “vilima-barafu,” na jina hilo lafaa. Hapo karibu pana momonyoko lililo na barafu nyingi zaidi katika Kizio cha Kaskazini, na vilima-barafu huelea katika sehemu zote za ghuba ile na vijito vya magengeni, vikifanya mandhari ile ipendeze ajabu. Jamaa sita kutoka Denmark na Wagreenland kadhaa ndio hufanyiza kundi hili lenye utendaji sana. Kuongezea mji wa Ilulissat na eneo zima la Ghuba ya Disko, labda wao ndio wenye eneo la kutolea ushahidi lililo mbali zaidi upande wa kaskazini wa ulimwengu, likifikia kule juu kabisa kwenye kijiji cha Kullorsuaq (Kidole-Gumba cha Ibilisi) karibu na digrii 75 za latitudo ya kaskazini.

Mapainia wa pekee katika Ilulissat huzuru eneo hili la mbali kwa ukawaida, wakitolea watu ushahidi katika Upernavik na Uummannaq. Bo na Helen waripoti hivi: “Maeneo haya ya kaskazini yaliyo na uwazi mpana yangali ni paradiso ya Aktiki ambayo haijaguswa bado. Eneo hili lina wakaaji wachache waliotawanyika, na watu huishi kwa kutegemea uindaji kuliko uvuvi. Maisha yao ni sahili, nao hawafanyi wasiwasi mno kuhusu wakati ujao. Wengi wao hupendezwa na mambo ya kiroho. Wao husikiliza kwa nia ujumbe ambao twawaletea.” Baada ya muda kupita ndipo tu itakapojulikana kama watu hao walio kama kondoo watakusanywa waingie katika lile “kundi” moja la kweli chini ya yule “mchungaji mmoja,” Yesu Kristo.—Yohana 10:16.

Mapainia Wadenmark tu ndio wamepata kufanya kazi katika eneo hili, lakini karibu Wagreenland wanane katika Nuk walinasa katika ukanda wa vidio ushahidi wa ujumla kuhusu imani zetu na njia yetu ya maisha. Mapainia walipotumia ukanda huu katika huduma yao ya nyumba kwa nyumba, ulifanya watu waongee sana na kuuliza maswali mengi, hasa kuhusu kutoadhimisha kwetu Krismasi na kutobatiza vitoto. Ingeweza kuongezewa kwamba karibu vitabu 200 viliangushwa wakati wa safari nzima ya majuma manne ambayo imesimuliwa sasa hivi.

Mavuno Yaendelea

Kujapokuwako na zile hali baridi za kiasili na kile kizuizi cha lugha, mavuno ya Ufalme yaendelea. Wagreenland wengi wamejifunza lugha ya Denmark ili wanufaike kutokana na mikutano ya kundi. Hata hivyo, hesabu ya mikutano yenye kufanywa katika lugha ya Greenland inaongezeka, hiyo ikifanya iwezekane wengi zaidi kushiriki katika ulishaji wa kiroho.

Kwa kielelezo, ingawa programu ya “Haki ya Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya wa 1988 ilifanywa katika Kidenmark kule Nuk, hotuba za karibu theluthi moja zilitafsiriwa katika lugha ya Greenland. Jumla ya watu 163 walihudhuria. Wajumbe kutoka kundi lile la mbali zaidi kaskazini kule Ilulissat na kundi lile la mbali zaidi kusini kule Qaqortoq yalilazimika kusafiri sana hata kufikia muda wa siku mbili kwa kila safari moja ya kuja au kurudi. Wanne walibatizwa kwenye mkusanyiko.

Ni matazamio gani yaliyopo kuhusu mavuno ya wakati ujao? Ni mazuri kweli kweli! Katika 1989 ilikuwa shangwe kuona watu 205 wakihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo. Kwa sasa, mafunzo ya nyumbani ya Biblia zaidi ya mia moja yanaongozwa. Ndiyo, Yehova anabariki sana kazi ya bidii ya watumishi wake katika bara hili la barafu na theluji.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki