Maisha na Huduma ya Yesu
“Imempasa Kuuawa”
YESU, akiwa amefungwa kama mhalifu wa kawaida, aongozwa kwenda kwa Anasi, ambaye hapo kwanza alikuwa kuhani wa juu aliye mashuhuri. Anasi alikuwa kuhani wa juu wakati Yesu akiwa kivulana wa miaka 12 aliwastaajabisha walimu wa kirabi hekaluni. Wana kadhaa wa Anasi walitumikia baadaye wakiwa kuhani wa juu, na wakati uliopo Kayafa mwana-mkwe wake ashikilia cheo hicho.
Labda kwanza Yesu aongozwa kwenda nyumba ya Anasi kwa sababu ya umashuhuri wa muda mrefu wa huyo aliye mkuu wa makuhani katika maisha ya kidini ya Wayahudi. Kituo hiki cha kumwona Anasi chamruhusu wakati Kayafa Kuhani wa Juu kuikusanya Sanhedrini, ile mahakama ya juu ya Wayahudi yenye washiriki 71, na pia kukusanya mashahidi bandia.
Sasa Anasi mkuu wa makuhani amwuliza Yesu maswali juu ya wanafunzi wake na juu ya fundisho lake. Hata hivyo, Yesu asema hivi kwa kujibu: “Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.”
Hapo, mmoja wa maofisa waliosimama karibu na Yesu ampiga kofi usoni, akisema: “Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?”
“Kama nimesema vibaya,” Yesu ajibu, “ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Baada ya mjibiano huu, Anasi apeleka Yesu kwa Kayafa akiwa amefungwa.
Kufikia sasa wakuu wote wa makuhani na wanaume wazee na waandishi, ndiyo, Sanhedrini yote, inaanza kukusanyika. Kwa wazi mahali pao pa mkutano ni kao la Kayafa. Hata hivyo, kufanya kesi kama hiyo katika usiku wa Kupitwa kwa wazi ni jambo lililo dhidi ya sheria ya Kiyahudi. Lakini hilo halizuii viongozi wa kidini kutofanya kusudi lao ovu.
Tayari, majuma kadhaa kabla ya wakati Yesu alipomfufua Lazaro, Sanhedrini ilikuwa imeamua miongoni mwao wenyewe kwamba ni lazima afe. Na siku mbili tu kabla ya hapo, siku ya Jumatano, wenye mamlaka wa kidini walifanya shauri pamoja kumkamata Yesu kwa mbinu ya ujanja ili wamwue. Wazia, yeye kwa kweli alikuwa amehukumiwa adhabu kabla ya kufanyiwa kesi!
Sasa jitihada zaendelea kutafuta mashahidi watakaotoa uthibitisho bandia ili kesi ikuzwe dhidi ya Yesu. Hata hivyo, hakuwezi kupatikana mashahidi wenye kuafikiana katika ushuhuda wao. Hatimaye, wawili waja mbele na kushikilia hivi: “Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.”
“Hujibu neno?” Kayafa auliza. “Hawa wanakushuhudia nini?” Lakini Yesu abaki kimya. Hata katika shtaka hili bandia, kwa aibu ya Sanhedrini, mashahidi hao hawawezi kufanya hadithi zao ziafikiane. Hivyo basi kuhani wa juu ajaribu mbinu tofauti.
Kayafa ajua jinsi Wayahudi walivyo wepesi kukasirikia mtu anayedai kuwa ndiye Mwana halisi wa Mungu. Katika pindi mbili mapema kidogo, wao walikuwa wamefanya haraka-haraka kumbandika Yesu jina la kuwa mkufuru astahiliye kifo, mara moja wakikosea kwa kuwazia kwamba alikuwa akikazania kwamba yuko sawa na Mungu. Sasa Kayafa adai kwa ujanja hivi: “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
Bila kujali ni nini Wayahudi wafikiri, kwa kweli Yesu ndiye Mwana wa Mungu. Na kubaki kimya kungeweza kutungiwa wazo la kukana kwake kuwa ndiye Kristo. Hivyo basi Yesu ajibu kwa moyo mkuu hivi: “Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”
Hapo, Kayafa, akijionyesha kwa njia ya kutazamisha, ararua mavazi yake na kupaaza mshangao: “Amekufuru; tuna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi?”
“Imempasa kuuawa,” Sanhedrini yapiga mbiu. Halafu waanza kumfanyia mzaha, nao wasema mambo mengine ya kufuru dhidi yake. Wampiga kofi katika uso wake na kuutemea mate. Wengine wafunika uso wake mzima na kumpiga kwa ngumi zao na kusema hivi kimadharau: “Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?” Mwenendo huu wa kutukana, usio wa kisheria watukia wakati wa ile kesi ya usiku. Mathayo 26:57-68; 26:3, 4; Marko 14:53-65; Luka 22:54, 63-65; Yohana 18:13-24; 11:45-53; 10:31-39; 5:16-18.
◆ Yesu aongozwa wapi kwanza, na nini latukia kwake huko?
◆ Yesu apelekwa wapi halafu, na kwa kusudi gani?
◆ Kayafa amewezaje kuifanya Sanhedrini ipige mbiu kwamba Yesu anastahili kifo?
◆ Ni mwenendo gani wa kutukana, usio wa kisheria watukia wakati wa ile kesi?