Kayafa Alikuwa Mpinzani Mkali wa Ibada ya Kweli
“YAPASA midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake.” (Mal. 2:7) Maneno hayo yaliyoongozwa na Mungu yanaonyesha kwamba makuhani wa Israeli wangalipaswa kuitetea ibada ya kweli. Hasa ndivyo angalivyopaswa kufanya kuhani mkuu wa Israeli. Lakini Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu katika karne ya kwanza W.K., hakutimiza jambo hilo alilotazamiwa kufanya. Yeye alikuwa mmojawapo adui wakubwa zaidi wa kweli.
Valerius Gratus, aliyemtangulia Pontio Pilato Gavana wa Kirumi katika utawala, ndiye aliyemweka Kayafa katika cheo cha kuwa kuhani mkuu karibu na mwaka 18 W.K. (au, labda katika mwaka 26 W.K.). Kayafa alipinga vikali watumishi washikamanifu wa Yehova Mungu kwa sababu hasa hakutaka kuondoka katika cheo chake hata kidogo.
Watu wote walipojua kwamba Lazaro amefufuliwa, Kayafa alijaribu kumwua Yesu Kristo akiwa pamoja na wengi wa washiriki wale wengine wa baraza kuu ya hukumu ya Kiyahudi, yaani, Sanhedrin. (Yohana 11:43-53) Mwujiza huo uliiumiza sana madhehebu ya Masadukayo, waliokuwa ndio ukoo wa kikuhani, Kayafa akiwa mmoja wao. (Matendo 5:17) Waliumizwa na mwujiza huo kwa sababu wao hawakuwa wakikubaliana na fundisho la Maandiko kwamba kuna ufufuo.—Matendo 23:8.
Lakini, wakati habari za kufufuliwa kwa Lazaro zilipopelekwa katika Sanhedrin, maoni ya Masadukayo juu ya ufufuo hayakutajwa katika mazungumzo. Jambo waliloogopa hasa ni kupoteza cheo chao. Maandishi ya Biblia yanasema hivi: “Wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo. Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua.”—Yohana 11:47-53.
Kayafa alitaka kumwua Yesu Kristo kama wale washiriki wengi wa Sanhedrin. Hata hivyo, kwa sababu ya cheo chake kitakatifu, Kayafa alitumiwa na Yehova Mungu kutabiri habari za Yesu. Tendo hilo lilifanana kidogo na vile alivyomfanya mtabiri Balaamu awabariki Waisraeli na kutoa unabii mbalimbali wa kweli kuwahusu, ingawa alitaka kuwalaani ili apewe thawabu.—Hes. 23:1-24:24; 2 Pet. 2:15; Yuda 11.
Bila shaka Kayafa na Anasi baba-mkwewe ndio wakuu wa makuhani waliofanya mpango wa kumwua Lazaro baada ya hapo. Walitaka kuzuia watu hao wengi waliomwamini Yesu Kristo kwa sababu ya mwujiza wa kumfufua Lazaro waache kumwamini.—Yohana 12:10, 11.
KUPOTOA SHERIA YA MUNGU KWA MAKUSUDI
Baadaye, Kayafa na Anasi walijitahidi sana kumfisha Yesu Kristo. Muda mfupi kabla ya sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 33 W.K., Kayafa na washiriki wengine wa Sanhedrin ‘walifanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.’ (Mt. 26:3, 4) Walifaulu katika mpango wao kwa kusaidiwa na Yuda Iskariote baada ya kumhonga. (Luka 22:2-6, 47-53) Baada ya kundi la watu wenye silaha kumkamata Yesu wakati wa giza, ili wasionekane, walimpeleka kwanza nyumbani kwa Anasi. (Yohana 18:13) Ndipo Yesu alipopelekwa kwa Kayafa akiwa amefungwa, halafu mashahidi wa uongo wakatoa ushuhuda wenye kupingana. Mwishowe, Kayafa alimwapiza Yesu, akadai awaambie kama yeye alikuwa ndiye Kristo Mwana wa Mungu. Kayafa alipomsikia Yesu akikubali kwamba ndiye, alirarua mavazi yake na kuiagiza baraza imhukumu kuwa mkufuru Mungu. Baraza ilikubali, ikamhukumia Yesu kifo.—Mt. 26:59-66.
Baada ya kesi hiyo kufanywa kwa njia isiyo halali wakati wa usiku, Sanhedrin ilikutana mapema asubuhi iliyofuata ili kuhakikisha uamuzi wao. (Marko 15:1) Bila shaka Kayafa ni mmoja wa wale waliompeleka Yesu mbele ya Pilato baada ya hapo, wakamshtaki kwamba ‘aliwazuia watu wasilipe kodi na kusema yeye ni Kristo mfalme.’ (Luka 23:2) Tena, wakati Pilato alipotaka kumfungua Yesu, bila shaka Kayafa ni mmoja wa “wakuu wa makuhani” waliopaza sauti wakisema: “Msulibishe! Msulibishe!” (Yohana 19:6, 11) Inaonekana kwamba alitumia mamlaka yake kulisihi kundi hilo la watu liombe kwamba Baraba, aliyekuwa mwuaji, mfitini serikali na mnyang’anyi, afunguliwe badala ya Yesu. (Mt. 27:20, 21; Marko 15:11) Inaelekea kwamba Kayafa pia alipaza sauti akisema: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”—Yohana 19:15.
Walipokwisha timiza lengo lao la kufanya Yesu ahukumiwe kufa, wakuu wa makuhani hawakupendezwa bado na maneno yaliyokusudiwa kubandikwa juu ya mti wa kufishia. Walipinga, wakimwambia Pilato hivi: “Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.” Lakini Pilato hakuwasikiliza.—Yohana 19:21, 22.
Kweli Kayafa alishindwa kutimiza daraka lake la kuunga mkono Sheria (Torati) aliyopaswa kutii na kufundisha, maana alikuwa kuhani mkuu. Yeye alikubaliana na watu hao kuvunja sheria zilizokataza kutoa rushwa (hongo) (Kum. 16:19), kufanya mpango wa hila na kupotoa hukumu (Kut. 23:1, 6, 7), ushuhuda wa uongo (Kut. 20:16), kufungua mwuaji (Hes. 35:31-34), fujo za watu wenye ghasia (Kut. 23:2), kufuata sheria za mataifa mengine (Law. 18:3-5), kukubali mtu asiye wa taifa lao wenyewe awe mfalme (Kum. 17:14, 15) na uuaji.—Kut. 20:13.
KUPINGA IBADA YA KWELI BAADA YA UFUFUO
Baada ya Yesu kufufuliwa, Kayafa na makuhani wengine waliomba Pilato afanye mpango wa kulilinda kaburi. Lakini Pilato akawajibu: “Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.” (Mt. 27:62-65) Yesu alipofufuliwa kisha baadhi ya walinzi wakawapasha wakuu wa makuhani habari hizo, Kayafa wala wenzake hawakutubu. Bali, waliwahonga askari wakawapa agizo hili: “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi.”—Mt. 28:11-14.
Baada ya hapo Kayafa alijaribu sana kuikomesha kazi ya wanafunzi wa Yesu ya kuhubiri na kufundisha watu. Petro na Yohana walitiwa gerezani kwa sababu ya kuponya mtu aliyezaliwa kiwete, kisha kesho yake wakaburutwa na kupelekwa mbele ya Kayafa na mbele ya washiriki wale wengine wa Sanhedrin. Ndipo Sanhedrin ilipowaagiza waache kunena kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohana walikuwa wamekaza nia waendelee kuitangaza kweli, Kayafa atake asitake. (Matendo 4:1-20) Wakati mwingine Kayafa aliwahoji mitume wote na kuwaeleza agizo la Sanhedrin kwamba waache kuhubiri kwa jina la Yesu. Lakini mitume walitamka kwamba walikuwa wamekaza nia waendelee kumtii “Mungu kuliko wanadamu.”—Matendo 5:27-29.
Wakati fulani baadaye Kayafa ndiye aliyeshiriki kuagiza Stefano mtumishi mwaminifu wa Mungu apigwe kwa mawe. (Matendo 6:11—7:60) Alimpa Sauli (Paulo, ambaye baadaye akawa mtume mwaminifu wa Yesu Kristo) mamlaka ya kukamata wanafunzi wa Kristo katika Dameski na kuwaleta Yerusalemu wakiwa wamefungwa ili wahukumiwe.—Matendo 9:1, 2.
Walakini, baada ya muda mfupi kazi ya Kayafa ilikatizwa. Mwaka 36 au 37 W.K. Vitellius, aliyekuwa afisa wa Kirumi, alimwondoa katika cheo. Inasemekana kwamba Kayafa alijiua kwa sababu ya kushushwa hivyo, asiweze kumaliza aibu aliyoona.
Kwa kweli jitihada za Kayafa za kuipinga ibada ya kweli zilikuwa za bure tu. Alipoteza jambo lile lile alilolitaka sana, yaani, cheo, uwezo, mamlaka na fahari inayoletwa na cheo. Ingawa alikuwa kuhani mkuu ambaye angaliweza kutumia maongozi yake kwa njia yenye faida, alikufa akiwa mpinga Mungu.—Matendo 5:39.