Njia Iliyotatanika ya Kumfikia Mungu
“MIMI ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” akasema Yesu Kristo. Aliongezea hivi: “Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.”—Yohana 14:6; 16:23.
Hata hivyo, kwa karne kadhaa dini za Jumuiya ya Wakristo, hasa Kanisa Katoliki la Kiroma, likiwa na mafundisho yalo ya moto wa mateso, purgatori, na Utatu, zimetatanisha “njia.” Yesu alionyeshwa, si akiwa mwombezi kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi, bali akiwa mtoto mchanga mwenye kushikwa au akiwa hakimu mwenye kutia hofu, mwenye kujali zaidi kushutumu na kuadhibu watenda dhambi kuliko kuwaokoa. Basi, mtenda dhambi angewezaje kumfikia Mungu?
Kitabu The Glories of Mary (1750) chaeleza. Akimlinganisha Yesu na jua la haki lenye kuwaka sana, papa Innocent 3 alijulisha rasmi hivi: “Yeyote aliye katika usiku wa dhambi, acha atupe macho yake juu ya mwezi, acha amsihi sana Mariamu.” Katika Mariamu, mama ya Yesu, mwombezi mwingine alivumbuliwa. Labda kupitia ule usemwao eti ni uvutano wake wa kimama, pendeleo fulani lingeweza kupatikana kutoka kwa Yesu na kutoka kwa Mungu. Hivyo, kulingana na maneno ya Laurence Justinian, kasisi mmoja wa karne ya 15, Mariamu akawa “ngazi ya kwenda paradiso, lango la mbinguni, mpatanishi wa kike aliye wa kweli kupita wote kati ya Mungu na binadamu.”
Kwa kupewa sifa zote zile za kupita kiasi, baada ya muda hakuonwa tena kuwa “Bikira Mariamu” tu bali akawa “Malkia Mtakatifu, Mama wa Rehema,” mwenye kutajwa kuwa aliye safi kabisa na mwenye kukwezwa sana hivi kwamba pia alikuwa mtakatifu mno asiweze kufikiwa moja kwa moja. Je! mwombezi mwingine bado angeweza kupatikana? Namna gani juu ya mama yake?
Kwa kuwa Biblia haisemi lolote juu ya habari hiyo, jibu lilitafutwa mahali penginepo. Kitabu cha Kiapokrifa Protevanjelio ya Yakobo chasimulia hadithi ya Anne (au Anna), mke wa Yoakimu, aliyekuwa bila mtoto baada ya miaka mingi ya ndoa. Mwishowe, malaika mmoja akamtokea na kutangaza kwamba angezaa mtoto. Baada ya muda, akawa mama ya “Bikira Mariamu,” ikadaiwa.
Hivyo kukatokea kiibada cha “Mtakatifu” Anne. Visehemu vitakatifu na makanisa yalijengwa kwa kumheshimu. Heshima nyingi mno kwa “Mtakatifu” Anne ikaenea kote katika Ulaya katika karne ya 14.
“Dini ikawa imetatanika kama nini!” chasema kitabu The Story of the Reformation. “Watu walisali kwa Anna ambaye alimpelekea Mariamu maombezi naye akampelekea Mwana wake maombezi naye akampelekea Mungu maombezi kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi. Ilishangaza sana, lakini hiyo ndiyo aina ya imani ya kishirikina ambayo nafsi za wanadamu zilisitawishwa juu yazo.” Basi, hapa pana kisa kingine ambacho maneno ya Yesu yatumika kwa kufaa: “Mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu.”—Marko 7:13.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
The Metropolitan Museum of Art Bequest of Benjamni Altam, 1913. (14.40.633)