Batiza! Batiza! Batiza!—Lakini kwa Nini?
“KATIKA muda wa miezi michache nimebatiza wanaume, wanawake, na watoto zaidi ya elfu kumi.” Ndivyo alivyoandika mishonari mmoja Myeswiti Francis Xavier kuhusu kazi yake katika ufalme wa Travancore, India. “Mimi nilienda kijiji kwa kijiji nikawafanya wawe Wakristo. Na kila mahali nilipokwenda niliacha nakala ya sala na amri zetu katika lugha ya kienyeji.”
Akivutiwa sana na barua za Francis Xavier, Mfalme John wa Ureno aliamuru kwamba zisomwe kwa sauti kutoka kwenye kila mimbara kotekote katika ufalme wake. Barua ya Januari 1545 ambayo imetoka tu kunukuliwa hata ilikubaliwa kuchapishwa. Tokeo likawa nini? “Punde si punde wanafunzi wengi katika Ulaya, ‘wakipiga magoti na kulia machozi kwa msisimuko,’ walikuwa wakisisitiza sana kwenda India na kuwafanya wapagani kuwa waongofu,” aandika Manfred Barthel katika kitabu chake The Jesuits—History & Legend of the Society of Jesus. Aliongeza hivi: “Yaonekana kwamba wengi wakati huo hawakuwa wamefahamu kwamba huenda ikahitaji zaidi ya watu wachache tu wenye kunyunyiza maji matakatifu na mikoba iliyojaa trakti ili kufanya watu wote katika ufalme mmoja wawe waongofu.”
Ni nini hasa lililotimizwa na maongofu hayo ya matungamano ya watu? Yeswiti Nicolas Lancilloto aliripotia Roma mambo haya halisi: “Wengi wa wale wanaobatizwa wana kusudi la kisiri. Watumwa wa Waarabu na Wahindu hutumaini kupata uhuru wao [kwa ubatizo] au kupata himaya kutokana na bwana mkubwa mwonevu au kupata tu joho au kilemba kipya. Wengi hufanya hivyo ili kuponyoka adhabu fulani. . . . Wowote wanaosukumwa na usadikisho wao wenyewe wa kutafuta wokovu katika mafundisho yetu huonwa kuwa watu wenye kichaa. Wengi huasi imani na kurudia mazoea yao ya kipagani ya zamani, muda mfupi tu baada ya kubatizwa.”
Tamaa ya kufanya wapagani kuwa waongofu na kuwabatiza ilishirikiwa pia na wavumbuzi wa Ulaya wa enzi hiyo. Yasemwa kwamba Christopher Columbus aliwabatiza “Wahindi” wa kwanza aliokutana nao katika Karibea. “Sera rasmi ya Serikali ya Hispania ilitanguliza kabisa kuwafanya wenyeji wa mahali waongofu,” chasema The Oxford Illustrated History of Christianity. “Kufikia mwisho wa karne ya kumi na sita, wale wahindi 7,000,000 wa milki ya Hispania, walikuwa hatimaye Wakristo, kwa jina. Mahali ambapo tuna takwimu ya maongofu (Pedro de Gante, mtu wa ukoo wa Maliki Charles wa 5, aliyekuwa amejiunga na wamishonari, alisema juu ya kuwabatiza watu 14,000 kwa msaada wa mwandamani mmoja katika siku moja), ni wazi kwamba hakuna mafunzo yoyote ya kwanza yenye uzito yaliyowezekana.” Maongofu hayo ya kijuujuu mara nyingi yaliandamana na kuwatenda wenyeji kwa ukali, kwa ukatili, na kwa uonevu.
Umaana uliowekwa juu ya ubatizo uliwachochea wavumbuzi na wamishonari hao waendelee kwa bidii. Katika 1439, Papa Eugenio wa 4 alitoa amri kwenye Baraza la Florence iliyosema hivi: “Ubatizo mtakatifu una mahali pa kwanza miongoni mwa sakramenti, kwa sababu huo ndio mlango wa uhai wa kiroho; kwani kwao twafanywa washiriki wa Kristo na twaungamanishwa na Kanisa. Na kwa kuwa kupitia mtu wa kwanza kifo kiliwaingia wote, tusipozaliwa mara ya pili kwa maji na Mzuka Mtakatifu, hatuwezi kuingia katika ufalme wa Mbinguni.”
Lakini ugomvi ulitokea, kuhusu ni ubatizo wa nani hasa uliokuwa halali. “Kwa sababu [ubatizo] ulikuwa pia ndiyo desturi ya msingi ya kuingia jumuiya ya kanisa, ubatizo ulidaiwa kuwa jambo la lazima na makanisa kadhaa ya upinzani, ambayo kila moja yayo lilijiita lenyewe kuwa lenye imani halisi na liliyashtaki yale mengine juu ya uzushi na kufarakana. Kubadilisha-badilisha desturi za ubatizo kwa madhehebu mbalimbali kukawa jambo lisiloweza kuepukika,” yasema The Encyclopedia of Religion.
Hata hivyo, zoea la ubatizo, latangulia kwa tarehe imani ya Kikristo. Ubatizo ulitumiwa katika Babulonia na katika Misri ya kale, ambako maji baridi ya Naili yalifikiriwa kuongeza nguvu na kutoa hali ya kutokufa. Wagiriki waliamini pia kwamba ubatizo ungeweza kuleta kuzaliwa upya au ungeweza kumpatia mwenye kubatizwa hali ya kutokufa. Dhehebu la Kiyahudi katika Qumran lilizoea ubatizo ili kuwaingiza wapya katika jumuiya yao. Wasio Wayahudi waliokuwa waongofu wa Dini ya Kiyahudi walihitaji kutahiriwa na baada ya siku saba kubatizwa kwa kuzamishwa mbele ya watazamaji.
Kwa wazi, umaana mwingi umewekwa juu ya ubatizo muda wote wa enzi ambazo zimepita. Lakini namna gani leo? Je! hilo ni jambo la lazima katika nyakati za ki-siku-hizi? Ikiwa ndivyo, kwa nini? Je!, kwa kweli, wewe wapaswa ubatizwe?