Hofu Imeshika Ulimwengu
MLIPUKO mkubwa wa bomu lililotegwa ndani ya gari ulitikisa jengo la World Trade Center lenye orofa 110 katika New York City mnamo Februari 26, 1993. Maelfu ya wafanyakazi walikwama ndani ya lifti zilizokwama au wakalazimika kutorokea ngazi zilizojaa mioshi. Wao walishikwa na hofu ambayo sasa imejaa katika ulimwengu huu wenye jeuri.
Watu katika nchi nyingi wametiwa hofu na mabomu, ambayo yamekuwa mengi katika nchi kama Ireland na Lebanoni. Kwani, mabomu 13 yalilipuka katika siku moja tu—Machi 12, 1993—katika Bombay, India, yakiua watu wapatao 200! Mchunguzi mmoja alisema hivi: “Kuna hofu kuu katika Bombay nzima.” Kulingana na gazeti Newsweek, “visa vingi vya milipuko [ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari] vyafanya yaogopeshe hata zaidi.”
Hofu za Nyukilia Zadumu
Kuna hofu kwamba mitambo ya nyukilia yaweza kulipuliwa na mabomu. Mashambulizi yenye mafanikio katika kituo cha nyukilia yaweza kusababisha hasara na mateseko makubwa sana. Jambo lililotokeza hofu hiyo lilikuwa jaribio la mtu mmoja kupitisha gari lake kwa nguvu katika lango la usalama la kituo cha nguvu ya nyukilia katika Three Mile Island nchini Marekani.
Wengi wanahofu kwamba magaidi na watawala wenye kutaka mamlaka watamiliki silaha za nyukilia. Wengine wahofu kwamba maelfu ya wanasayansi wa nyukilia katika Sovieti ambao wamekosa kazi watajaribu kuuza ustadi wao. Isitoshe, ingawa mapatano ya Kupunguzwa kwa Silaha Hatari Zilizolengwa (START) pamoja na mapatano mengine yataka silaha za nyukilia zilizolengwa zipunguzwe kabisa, kutimizwa kwa mapatano kama hayo hakutamalizika kwa miaka mingi. Na wakati uo huo, uwezekano wa kuinuka kwa kikundi fulani chenye ushupavu watisha kama wingu lenye dhoruba litishavyo wanadamu.
Jeuri Hutokeza Hofu
Ongezeko lenye kuenea la uhalifu wenye jeuri hufanya watu washikwe na hofu nyumbani mwao na barabarani. Waamerika wapatao 23,200 waliuawa kimakusudi katika 1990. Kwa kielelezo, katika jiji la Chicago, ongezeko la matumizi ya kokeini iitwayo kraki lilichangia karibu mauaji ya kimakusudi 700 kwa mwaka mmoja. Sehemu fulani za majiji zimekuwa viwanja vya vita ambapo wapita-njia, kutia na watoto, wameuawa katika vita vya vikundi vinavyopigana. Gazeti moja lilisema hivi: “Jeuri inaongezeka kwa kasi katika majiji yenye ukubwa wa kadiri. . . . Hakuna mtu aliye salama maadamu jumuiya za [Marekani] zimejaa dawa za kulevya na vijana wakora. Kila mwaka nyumba 1 kati ya 4 za Waamerika hupatwa na uhalifu wenye jeuri au kuibiwa kwa jeuri.”—U.S.News & World Report, Oktoba 7, 1991.
Hofu ya kunajisiwa hutia wanawake wasiwasi. Visa vya unajisi vilivyoripotiwa nchini Ufaransa vilipanda kwa asilimia 62 kutoka 1985 hadi 1990. Mashambulizi ya kingono yaliongezeka maradufu hadi 27,000 kwa muda wa miaka sita nchini Kanada. Ujerumani iliripoti kisa kimoja cha shambulio la kingono kwa mwanamke kwa kila dakika saba.
Watoto pia wahofia usalama wao. Newsweek laripoti kwamba kule Marekani, “watoto, hata walio katika darasa la nne na tano la shule ya msingi, wanajihami, na walimu na maofisa wa shule wanaogopa.” Hali imekuwa mbaya sana kiasi cha kwamba robo za halmashauri za wilaya za shule za miji mikubwa zinatumia vichunguza-chuma, lakini vijana wenye kuazimia hupata njia nyinginezo za kuepa vichunguza-chuma kwa kuwapa wengine bunduki kupitia madirisha.
Hofu ya UKIMWI
Idadi inayoongezeka ya watu wanahofu kushikwa na UKIMWI. Kumekuwa na visa zaidi ya 230,000 Marekani pekee. UKIMWI umekuwa namba sita katika kusababisha vifo miongoni mwa watu wenye umri wa miaka kati ya 15 na 24. “Wakati ujao una tazamio lenye kuogofya sana kwamba ugonjwa utaenea zaidi,” lasema Newsweek.
Vifo kutokana na UKIMWI vinatukia sanasana miongoni mwa watu katika nyanja za uchezaji-dansi, michezo ya kuigiza, sinema, muziki, mitindo, televisheni, sanaa, na kadhalika. Ripoti moja ilisema kwamba asilimia 60 ya vifo vya wanaume wenye umri wa miaka kati ya 25 na 44 waliohusika na uandishi wa habari, sanaa, na vitumbuizo jijini Paris vilitokana na UKIMWI. Shirika la WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) laripoti kwamba kati ya watu milioni 8 hadi milioni 15 ulimwenguni pote wameambukizwa virusi HIV. Dakt. Michael Merson, mkurugenzi wa WHO, asema hivi: “Ni wazi sasa kwamba idadi ya wenye kuambukizwa HIV yaendelea kuongezeka kwa haraka zaidi duniani pote, hasa katika nchi zinazoendelea.”
Bila shaka, kuna hofu juu ya mazingira na mambo mengineyo. Lakini, ripoti zilizotajwa hapa pekee zaonyesha wazi kwamba ulimwengu umeshikwa na hofu. Je! kuna umaana wowote katika jambo hilo? Je! twaweza kweli kutazamia kufurahia uhuru kutokana na hofu?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Cover photos: Left: Tom Haley/Sipa Press; Bottom: Malanca/Sipa Press
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Bob Strong/Sipa Press