Kusaidia Familia Yetu ya Waamini Katika Bosnia
MASHAHIDI WA YEHOVA hawashiriki katika mizozo ya kisiasa. (Yohana 17:16) Lakini, kwa kufuata shauri la Paulo la kufanya mema “hasa kwa familia yetu ya waamini,” wao husaidia kwa utayari Wakristo wenzao walio katika maeneo ya vita. (Wagalatia 6:10, Beck) Kipupwe cha 1993-94 kilipokuwa kinakaribia, Mashahidi kutoka Austria na Kroatia walihatarisha uhai wao ili kusaidia familia yao ya waamini katika Bosnia. Ifautayo ni ripoti yao.
Kuanzia Machi hadi Oktoba 1993, hakukuwa na uwezekano wa kusafirisha msaada kwenda Bosnia. Lakini mwanzoni mwa Oktoba, wenye mamlaka walidokeza kuwa huenda ikawezekana kusafirisha bidhaa. Hilo lingekuwa mradi hatari, kwa kuwa vita ilikuwa imewaka katika mipaka yote ya Bosnia.
Hata hivyo, Jumanne, Oktoba 26, 1993, lori zetu zilitoka Vienna zikibeba tani 16 za chakula na kuni kwa Wakristo wenzetu katika Bosnia. Tulivaa kadi za shavu la koti za mkusanyiko wa wilaya kwa ajili ya kujitambulisha.
Tulipofika tu mpaka wa Kroatia na Bosnia, tulisindikizwa mpaka kituo cha kijeshi ambako lori zetu zilipekuliwa kabisa. Ombi letu la kusafiri kupitia eneo la Serbia lilikataliwa. Tungeruhusiwa kupitia Bosnia ya kati pekee—katikati kabisa ya vita!
Je, Zilikuwa Jitihada Ambazo Hazingefanikiwa?
Tulipokuwa tukisindikizwa na majeshi kutoka kituo kimoja hadi kingine cha ukaguzi barabarani, tulisikia milipuko mikubwa sana kutoka kwa vifaru na bunduki. Wakati wa usiku, tulisafiri katika msitu tukisindikizwa na vifaru viwili na gari aina ya jip. Lori zetu zilienda polepole kupitia mahali penyewe pa vita! Mambo yaliendelea vizuri hadi asubuhi ambapo risasi zilifyatuliwa juu ya vichwa vyetu ikitulazimu kujificha nyuma ya kilima kimoja. Baada ya muda ufyatuliaji ulikoma, nasi tukaendelea na safari.
Tulipofika katika kambi moja, kamanda msimamizi alituuliza sisi ni nani na tulitaka nini. “Mradi wenu hautafanikiwa,” yeye akasema tulipomweleza kusudi letu. “Hamwezi kuondoka katika kambi kwa usalama, hata kwenda hatua chache tu. Kuna njaa kali sana katika nchi hivi kwamba watu watawashambulia na kuiba bidhaa zenu.” Akatuhimiza turudi tulikotoka.
Je, jitihada zetu ‘hazingefanikiwa’? Je, ilikuwa kazi bure kutazamia kwamba tungesafiri kupitia maeneo ya vita na yenye njaa kali na bado tuhifadhi bidhaa zetu na uhai wetu? Ilibidi uamuzi mzito ufanywe. Tayari tulikuwa tumesikia milio ya bunduki na milipuko mikubwa na mabomu. Tulipokuwa na wanajeshi usiku, tungeweza kuona kwamba walikuwa wamejitayarishia magumu ya vita. Wao walivalia fulana za kukinga risasi nao walibeba silaha nyingi. Hata mpishi alikuwa na bunduki ya kumimina risasi mgongoni pake. Huku sisi tukiwa tumevalia shati, tai, na kadi za shavu la koti! Je, lilikuwa jambo la hekima kwetu kuendelea na safari?
Kufika Travnik
Ilionekana kama tumaini letu la pekee lilikuwa kushauriana na kikundi cha tatu kilichokuwa kikipigana katika vita hiyo. Asubuhi iliyofuata tuliuliza mwanamke mmoja mchanga ikiwa alijua mahali makao makuu ya kikundi hicho yalipokuwa. “Si mbali,” akasema. “Pitieni tu msitu huu, mtapata jengo lililokuwa hospitali zamani.” Tulikuwa na hamu ya kwenda. Wanajeshi walishangaa kwamba tulithubutu kutoka kambini bila kuwa na silaha.
Jengo hilo lililokuwa hospitali zamani lilikuwa magofu, lakini ofisa mmoja alikuwapo. Alikubali kusaidia, akitushauri tuseme na kamanda wake kwanza. Alitupeleka katika gari lake zee kwa mwendo wa kasi sana kandokando ya mahali penyewe pa vita. Tulisimama kwenye jengo moja ambako kamanda msimamizi alitupokea katika chumba chenye giza.
“Jana usiku tulitaka kuwafyatulia bunduki,” yeye akasema. “Mwataka nini?”
“Sisi ni Mashahidi wa Yehova, na twataka kupeleka bidhaa za msaada kwa ndugu zetu.”
Alishangaa sana—na kuvutiwa—kwa sababu kwa majuma kadhaa hakuna msafara wowote uliothubutu kuingia katika Bosnia. Baada ya kupekuliwa kabisa, tulipewa kibali kilichoandikwa. Usiku uliotangulia tulifikiri hatungeweza kuendelea na safari yetu, na sasa tungeendelea mbele bila ulinzi!
Tuliendesha kupitia msitu, tukipita kituo kimoja hadi kingine cha ukaguzi barabarani, na nyakati nyingine tuliendesha kandokando ya sehemu zenyewe za vita. Tulifika Travnik salama ijapokuwa hatari hiyo. Mwanajeshi aliyesikia juu ya kufika kwetu alikimbilia nyumba moja ambamo ndugu zetu walikusanyika. “Watu wenu wamefika hapa kwa lori!” akapaaza sauti. Waweza kuwazia shangwe yao. Tuliingiza chakula katika nyumba, tukasema maneno machache, lakini ilikuwa lazima tuendelee mbele. Giza lilikuwa linaingia, na tulikuwa na safari hatari ya kilometa 32 mbele yetu.
Kwenda Zenica
Gari la ulinzi lilituongoza kupitia msitu kwa mwendo wa kasi. Wengine walisema kwamba hatungefaulu kufika Zenica, lakini tulifika. Ilionekana kama huzuni ilikuwa imemeza mji huo. Hakukuwa na taa wala magari barabarani. Zenica ulikuwa umezingirwa kwa pande zote, jambo lililotokeza njaa kali na mtamauko.
Tulipokuwa tukipitia barabara ya mji, tuliona jambo la kushangaza sana—dada wawili Wakristo wakitoa ushahidi! Tuliambiwa kwamba siku iliyotangulia katika mkutano wao iliamuliwa kwamba ndugu wangeenda katika msitu kutafuta chakula, kwa kuwa ugavi ulikuwa umeisha. Tulifika kwa wakati barabara! Tulipakua mojapo lori hizo saa kumi ya usiku, wakati ambapo hakukuwa na mtu yeyote barabarani.
Siku iliyofuata tulimwona jenerali mmoja aliyeshangaa sana kwamba tulifaulu kufika Zenica. Sasa tuliuliza juu ya kusafiri kwenda mahali tulipotaka kwenda, Sarajevo.
“Hakuna mtu amepata kwenda huko kwa lori kwa muda wa miezi kadhaa,” jenerali huyo akasema. Hatimaye alitupa ruhusa ya kusafiri kwenye milima. “Lakini nawaambia ni vigumu,” yeye akaonya. “Sidhani kama lori zenu zina nguvu za kutosha kuwafikisha.”
Jenerali huyo hakuwa ametia chumvi. Tulipokuwa tumebakisha tu kilometa 40 kutoka Sarajevo, ilitubidi tuzunguke kwa kilometa 140 katika msitu! Hatuwezi kusahau kamwe safari hiyo iliyotoka Zenica kupitia Sarajevo hadi Jablanica iliyochukua siku tatu na usiku mbili, mara nyingi kwa mwendo wa kilometa tano kwa saa. “Barabara” hiyo ilikuwa kijia kilichotengenezwa na magari ya vita. Tuliendesha kupitia majabali na mashimo yenye kuogofya. Mara nyingi tulilazimika kwenda bila taa, na katika pindi mbili lori zetu karibu ziteleze chini kwenye milima hatari. Lori la kijeshi lililokuwa likifuata msafara wetu liliwasha taa kwa muda mfupi tu nalo lilifyatuliwa risasi. Nyakati nyingine tulilazimika kurekebisha madaraja na magurudumu yaliyoharibika.
Tulipofika viunga vya Sarajevo, tuliomba kuzungumza na jenerali msimamizi. Tukiwa tungali tunangoja, tuliona lori katika barabara ya mji ikiwa imebeba maiti kumi na gunia la vichwa; wanajeshi walikuwa wakijadiliana juu ya kujisalimisha kwa maiti—ono lisilopendeza hata kidogo, likitufanya tutamani siku ambayo vita itakoma.—Isaya 2:4.
Karibu saa 4:00 ya asubuhi, hatimaye mmoja wetu alipewa nafasi ya kuzungumza na jenerali huyo pamoja na maofisa wake wa ngazi za juu katika chumba chenye giza, kikiwashwa tu kwa mshumaa.
“Nyinyi ni nani?” jenerali huyo akauliza.
“Sisi ni Mashahidi wa Yehova. Tunataka kupeleka chakula kwa Mashahidi wenzetu walio Sarajevo.”
“Je, mwajua kwamba kuna wengi wa Mashahidi wa Yehova katika Sarajevo?”
“Ndiyo, hiyo ndiyo sababu tupo hapa.”
Kisha jenerali huyo akataja jina la Shahidi mmoja. “Je, mwamjua?”
“Ndiyo, yeye ni rafiki yetu.”
“Yeye ni rafiki yangu pia,” jenerali huyo akasema. “Tulisoma pamoja shuleni. Kwa kuwa amekuwa Shahidi, namthamini hata zaidi. Amewafanyia nyinyi watu mambo mengi sana. Tafadhali tuambieni zaidi juu ya Mashahidi wa Yehova.”
Mazungumzo ya muda wa saa moja yakafuata, na baada ya mazungumzo hayo magazeti na broshua zaidi ya 12 ziliangushwa. Baada ya mkutano wa pili, jenerali huyo alikubali kufanya mipango ya pekee ili bidhaa za msaada ziweze kupelekwa kwa ndugu wa Sarajevo.
Huo haukuwa mradi mdogo. Watu wapatao 30, kutia na wengine wasio Mashahidi, walikokota vifurushi vyenye uzito upatao kilo 27 kila kimoja. Walifanya kazi ngumu kuanzia saa 2:00 za usiku hadi saa 11:00 za alfajiri kwa usiku mbili tofauti-tofauti—jumla ya muda wa saa 18. Mzee mmoja alieleza kwamba majirani wake walishangaa sana na jitihada hizo za kuleta msaada hivi kwamba walipiga magoti pamoja na akina ndugu na kumshukuru Yehova! Bila shaka wao pia walipata chakula kiasi fulani.
Ebu wazia shangwe ya ndugu zetu walipopokea bidhaa za msaada za kilo zipatazo 11,000! Hali ilikuwa mbaya sana. Katika sehemu hiyo, kilo moja ya unga iligharimu kati ya DM450 na DM1,000 (dola 300 na 660, za Marekani). Gunia moja la kuni liligharimu karibu DM400 (dola 260, za Marekani), na lita moja ya mafuta ya dizeli ilikuwa DM30 (dola 20, za Marekani).
Ilikuwa kana kwamba kwa kila hatari tuliyokabili njiani, tulikuwa tukithawabishwa sasa. Tulifurahi sana kufikiria shangwe ya ndugu zetu walipopokea msaada huo uliopelekwa. Lilikuwa ni ono ambalo wao—na sisi—hatuwezi kusahau kamwe. Lakini sasa ilikuwa ni lazima tuanze kufikiria juu ya ugumu wa kurudi nyumbani.
Kurudi Nyumbani
“Tutarudi kwa njia gani?” tukamwuliza jenerali yule.
“Njia ileile mliyokuja nayo,” akajibu.
Tulikuwa tumechoka, hatukuwa na mafuta ya kutosha, na bila magurudumu ya akiba. Mvua ikaanza kunyesha, na hatungeweza kusafiri katika matope. Tukamwuliza jenerali huyo kama tungesafiri kuelekea kusini.
“Kuna vita kali huko,” yeye akasema. “Hata panya hawezi kupita.” Hata hivyo, baada ya muda akaifikiria tena. “Ijaribuni,” akasema. “Mlifaulu kufika hapa.”
Ilitubidi tuache lori moja na kugawa mafuta yayo kwa lori nyinginezo tatu. Tuliondoka katikati ya usiku na kuendesha katika msitu tena.
Safari yetu ya kurudi haikuwa bila matatizo. Tulikuta lori ya jeshi ikiwa imelalia upande wayo, ikizuia kidogo daraja tuliyopaswa kupita. Tuliona kwamba kama tungeondoa tu mojapo magurudumu yayo, kungekuwa na nafasi ya kupita.
Tukamsihi mwanajeshi mmoja mwenye silaha. “Je, tuondoe gurudumu na kulirudisha baada ya kuvuka daraja?”
“Ukigusa gurudumu hilo, bunduki yangu itakuwa na kazi ya kufanya,” mwanajeshi huyo akajibu, akilenga silaha yake.
Tulifikiri ingekuwa afadhali kutengeneza kahawa na kumpa mwanajeshi yule kikombe kimoja. Kwa muda wa saa kadhaa, tulimweleza juu ya mikusanyiko ya kimataifa ya 1991, kama ule uliokuwa katika Zagreb. Baada ya hapo, mtazamo wake ukawa mtulivu, naye akaturuhusu kutoa lile gurudumu.
Katika Jablanica, mmoja wetu akaongea na kamanda mmoja kuhusu njia tuliyotaka kuchukua. Hakuamini yale aliyokuwa akisikia. “Mwataka kupitia Bonde la Naretva?”
Kwa kueleweka alikuwa na wasiwasi. Kandokando ya vilima vya Bonde la Naretva zinashikiliwa na majeshi tofauti-tofauti. Sikuzote wao hufyatuliana risasi. Kwa karibu kilometa 16, barabara ni hatari. “Ndivyo ilivyo,” jenerali huyo akasema, “na bado mwataka kuipitia?”
Baada ya kufikiria jambo hilo kwa uzito, jenerali huyo akasema kwamba twaweza kwenda—lakini tukiandamana tu na maofisa. Lakini, maofisa hao hawakutaka kwenda na sisi! Hatimaye, tuliomba kwamba wawasiliane tu na upande mwingine na kutangaza kupita kwetu. Tungevuka bila ulinzi asubuhi iliyofuata.
Kwa herufi kubwa, tuliandika kwenye lori zetu kuwa zinabeba msaada wa kibinadamu. Baada ya kusali, tuliendesha kuingia katika bonde. Tulikubali kwamba iwapo risasi zitafyatuliwa, hatungeongeza mwendo wetu na kuzusha shaka.
Tulivuka daraja hadi upande mwingine wa mto na kuendelea hadi bonde jingine, tukipita mizoga ya wanyama pamoja na lori na vifaru vilivyoharibiwa. Kwa ghafula tukaona baruti za kutegwa ardhini zikiwa barabarani, zikifanya tusiweze kupita. Tukapiga honi ya lori mpaka wanajeshi wawili wakachungulia kutoka nyuma ya jabali. “Nyinyi ni nani? Mwataka nini?” wakataka kujua kwa lazima.
Baada ya kujitambulisha, tukauliza kama wangeondoa vitu hivyo barabarani, nao wakakubali. Hatimaye tulifika upande mwingine.
Wanajeshi waliokuwa huko walishangaa kutuona. Walitoka polepole kutoka maficho yao, wakikaribia lori bunduki zao zikiwa zimetulenga kabisa. Tuliwaonyesha hati zetu za kibali pamoja na leseni za gari ambazo tulikuwa tumeondoa kwa sababu ya usalama tulipokuwa tukiendesha kupitia eneo la vita.
“Hakuna mtu aliyewatarajia,” mwanajeshi mmoja akasema. “Mlipitaje?”
Tofauti na ombi letu, hakuna mtu katika vituo hivi vya mbali aliyejulishwa kwamba tulikuwa tukija! Ofisa huyo akaendelea kusema: “Bunduki zetu zilikuwa tayari, na tulikuwa karibu kuanza kufyatua risasi.”
Tukauliza kwa nini hawakufanya hivyo.
“Sijui,” mwanajeshi huyo akajibu. “Nafikiri ilikuwa bahati yenu. Lakini tulipowatazama kupitia darubini, tukaona maandishi ya ‘msaada wa kibinadamu,’ na hatukujua la kufanya nanyi. Kwa hiyo mkafika salama.” Baadaye tukamtolea Yehova sala za kutoka moyoni kwa ajili ya ulinzi wake.
Ingawa hali zao zilikuwa ngumu sana, roho ya ndugu na dada zetu Wabosnia inatia moyo sana. Wao hutumia pamoja vitu vyovyote vya kimwili walivyo navyo pamoja na maneno mengi ya imani na kitia moyo. Katika Zenica, kuna Mashahidi 40 walio watendaji, kutia na mapainia wa pekee 2, mapainia wasaidizi 11, na wapya 14 waliobatizwa. Mashahidi 65 pamoja na mapainia wasaidizi 4 ambao wangali wamebaki katika jiji la Sarajevo wanaongoza mafunzo ya Biblia 134. Mashahidi hao hutumia wastani wa muda wa saa 20 kila mwezi wakizungumza na wengine juu ya habari njema za Ufalme wa Mungu.
Kwa kweli Mashahidi wa Yehova ni familia ya waamini ulimwenguni pote. Wanajihatarisha kwa hiari ili kufanya mema kwa familia ya waaminio—hata wale ambao hawajapata kukutana nao kamwe. Kwa nini? Kwa sababu wanawapenda. Yesu Kristo alisema: “Hivyo wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:35) Hakika mambo yamekuwa hivyo kwa habari ya familia yetu ya waamini katika Bosnia.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Bahari ya Adriatiki
AUSTRIA
SLOVENIA
HUNGARIA
KROATIA
BOSNIA
Travnik
Zenica
Sarajevo
SERBIA
[Picha]
Kupeleka msaada Bosnia na Herzegovina
[Picha katika ukurasa wa 26]
Tukipita polepole lori iliyoanguka