Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 10/1 kur. 29-31
  • Singapore Yavunja Uhuru wa Ibada

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Singapore Yavunja Uhuru wa Ibada
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Wao Si Tisho kwa Taifa na Umoja
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 10/1 kur. 29-31

Singapore Yavunja Uhuru wa Ibada

JIONI ya Februari 24, 1995, nyumba nne katika jiji la Singapore zilivamiwa na polisi. Jumla ya watu 69 walishikwa.a Miongoni mwao mlikuwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 71 na wasichana wawili wenye umri wa miaka 15. Kwa nini? Je, ilikuwa ni kwa sababu ya tendo la uvunjaji wa sheria au tendo la kufitini serikali? La. Hakuna mmoja wao aliyekuwa akifanya lolote ambalo lingeweza kuonwa kwa vyovyote kuwa hatari, lisilo la adili, au lenye kudhuru jamii. Hawakuwa tisho kwa viwango vya maadili, usalama, na hali njema ya Wasingapore wenzao. Hata hivyo, baada ya kupekua nyumba hizo nne, polisi waliwapeleka hadi kituo cha polisi watu hao 69 waliokuwa wamekutana kujifunza Biblia na kufurahia ushirika. Huko walifungiwa usiku kucha, wakahojiwa, wakachukuliwa alama za vidole, na kupigwa picha—ndiyo, kutendewa kikatili kama wavunja-sheria wa kawaida! Wakati huo wote—wakiwa katika hali zilizo mbaya kabisa kwa muda wa saa 18—hawakuruhusiwa kutafuta msaada wa wakili na hata walikatazwa kupiga simu kuwaambia washiriki wa familia zao walikokuwa. Mtu anaweza tu kuwazia jinsi tendo hilo la kijuu-juu lilivyoathiri raia hawa wenye amani, wanaotii sheria!

Jambo hilo latukumbusha juu ya hali zilivyokuwa wakati wa siku za magumu za Ujerumani ya Nazi na enzi yenye ukatili ya Ukomunisti katika Muungano wa Sovieti na Ulaya Mashariki. Hiyo si hali ambayo mtembeleaji wa kawaida wa Singapore angetazamia kupata katika jiji hilo lenye kujitawala lililo safi na lenye ufanisi. Singapore imejipatia sifa kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii katika karne ya 20. Ni nchi iliyojitangaza kuwa ya kidemokrasi na yenye katiba inayohakikishia raia zayo haki za msingi za kibinadamu, kutia ndani uhuru wa kujieleza, dini, na kukutana.

Hata hivyo, wale walioshikwa katika Februari walionewa hasa kwa sababu walikuwa Mashahidi wa Yehova waliokutanika pamoja kujifunza Biblia na kushiriki katika ushirika wa Kikristo. Shtaka dhidi yao lilikuwa “kuhudhuria mkutano wa shirika lisilo halali.”

Kwa kweli, Mashahidi wa Yehova wamenyimwa utambulisho wa kisheria katika Singapore tangu 1972 wakati ambapo Kutaniko la Singapore liliondolewa kwenye orodha na fasihi kutia ndani Biblia, zilizotangazwa na Watch Tower Bible and Tract Society kupigwa marufuku. Hawakupewa fursa wajitetee kabla ya uamuzi huo kufanywa. Hivi majuzi, uhalali wa uonevu huo wa kiserikali ulibishaniwa katika mahakama ya Singapore kwenye kesi ya Mashahidi wanne waliokuwa wameshtakiwa katika Februari 1994 kwa kupatikana na fasihi za Biblia. Rufani waliyokata dhidi ya hukumu waliyopewa ilisikilizwa katika Agosti 1994 na kutupiliwa mbali. Hakimu Mkuu Yong Pung How wa Mahakama Kuu alieleza maoni yake mwezi uliofuata. Alionelea kwamba uhuru wa kidini haukuvunjwa na kwamba hukumu zilizotolewa zilikuwa za haki kwa msingi wa kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa hatari kwa usalama wa taifa kwa sababu wafuasi wa dini hiyo hawangeshiriki katika utumishi wa kijeshi. Katika Februari 17, 1995, wale Mashahidi wanne wakaomba ruhusa ya kukata rufani dhidi ya uamuzi huo mbaya kwa Mahakama ya Rufani ya Singapore. Wakanyimwa.

Uamuzi huo wa mwisho ulitangazwa sana na vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali ya Singapore. Bila shaka uamuzi huo na matangazo yaliyofuata katika vyombo vya habari yalitangulia kuonyesha matukio yaliyofuata. Kwa muda wa juma moja wale Mashahidi 69 wakashikwa. Mashtaka dhidi ya raia hawa wanne—wa Uingereza, Ufaransa, na Luxembourg—yakaondolewa. Hata hivyo, hata hao wanne walipata ono la kuogofya sana. Mwanamume mmoja pamoja na mkeye walikuwa wameishi na kufanya kazi Singapore kwa miaka mingi. Walipoteza kazi zao na nyumba waliyokuwa wamekodi nao wakalazimika kuwaaga marafiki wao wengi wa karibu.

Wale watu wazima 63 waliobaki walishtakiwa kwa kushirikiana na shirika lililopigwa marufuku, na wengine wao pia walishtakiwa kwa kupatikana na fasihi iliyopigwa marufuku. Wanakabili kifungo cha miaka mitatu gerezani au faini ya dola 3,000 za Singapore (dola 2,100 za Marekani) au yote mawili. Wasichana wale wawili wenye umri wa miaka 15 walishtakiwa kivyao katika mahakama ya watoto.

Wao Si Tisho kwa Taifa na Umoja

Mashahidi wa Yehova wanajulikana ulimwenguni pote kuwa watu wenye adabu, wafuatiaji haki, wenye kutii sheria katika nchi zaidi ya 200 wanamoishi. Wanajulikana kwa kukataa kwao katakata kushiriki katika tendo lolote la uhaini, lenye kupinga serikali—tendo lisilo la Kikristo liwezalo kutokeza kutengwa na ushirika, au kuondoshwa. Kwa kweli, serikali ya Singapore haina sababu ya kuwaogopa. Kwa vyovyote wao si tisho kwa usalama wa taifa au umoja. (Warumi 13:1-7) Jambo hilo lilielezwa waziwazi katika barua ya Machi 21, 1995, kutoka kwa Milton G. Henschel, msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, kwa Waziri Mkuu Goh Chok Tong wa Singapore. Barua hii imenakiliwa hapa kwa manufaa ya wasomaji.

Watu wenye kupenda uhuru katika biashara, serikali, na kampuni za binafsi watakuwa wakitazama kwa hamu kuona jinsi hali hii katika Singapore itakavyokuwa. Je, serikali ya Singapore itatenda kupatana na haki za msingi za kibinadamu na uhuru mbalimbali unaoendelezwa na katiba yayo yenyewe na jumuiya ya kimataifa? Kwa hakika, Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanajali sana hali ya waabudu wenzao katika Singapore. Wanawakumbuka katika sala zao na kukumbuka uhakikisho huu upatikanao katika Biblia: “BWANA hupenda haki, wala hawaachi watauwa wake.”—Zaburi 37:28.

[Maelezo ya Chini]

a Katika ile miezi tangu wale 69 kushikwa, Mashahidi wengine 11 wameshikwa na kushtakiwa kwa kupatikana na fasihi isiyo halali.

[Sanduku katika ukurasa wa 30]

Machi 21, 1995

Goh Chok Tong

Waziri Mkuu

Istana Annexe

Singapore 0923

Republic of Singapore

Lee Kuan Yew

Waziri Mkuu

Ofisi ya Waziri Mkuu

460 Alexandra Road

37-00 PSA Bldg

Singapore 0511

Republic of Singapore

Waheshimiwa Wapendwa:

Hivi karibuni habari ya shirika la habari la Reuters ya Februari 25, 1995, kutoka Singapore ilikuwa yenye kuvunja moyo sana. Iliripoti kwamba mikutano ya Mashahidi wa Yehova ya funzo la Biblia imekatishwa na polisi na watu wapatao 69 kushikwa. Ripoti hii imefanya ulimwengu ukazie fikira hali ya Mashahidi wa Yehova katika Singapore, ambapo utendaji wao na fasihi zao zimepigwa marufuku kwa zaidi ya miaka 20.

Ni vigumu kufahamu ni kwa nini shirika la kidini liendeshalo mambo yalo waziwazi na linaloungwa mkono kisheria katika nchi zaidi ya 200 lipigwe marufuku Singapore, nchi inayofuata kanuni za demokrasi. Inavunja moyo hata zaidi kufikiria kwamba katiba ya Singapore inahakikishia raia wayo uhuru wa ibada.

Mashahidi wa Yehova hawajawahi kamwe kuwa tisho kwa usalama wa taifa mahali popote. Kwa kweli, ulimwenguni pote wanajulikana kuwa wenye amani, wafanyakazi wenye bidii, wenye maadili safi, na wenye kutii sheria—sifa ambazo nina hakika zinapendekezwa katika nchi yako.

Ni kweli kwamba kwa sababu ya kushika kabisa viwango vya Biblia kwa Wakristo, wakati mwingine msimamo wa Mashahidi wa Yehova umeeleweka vibaya au kufikiriwa vibaya. Lakini, je, hilo halikuwa kweli kwa mwanzilishi wa Ukristo aliyefikiriwa vibaya kuwa dhidi ya “Kaisari,” serikali ya wakati wake? Mashahidi wa Yehova hufuata tu kielelezo cha Yesu na cha Wakristo wa mapema. Wanaheshimu serikali ya mahali wanapoishi, wanalipa kodi zao, na kupendekeza maadili safi. Wao ni wananchi waaminifu na wanyoofu. Mashahidi wa Yehova hawajawahi kamwe kushiriki katika vitendo vyovyote vya kuhaini serikali katika nchi yoyote nami naweza kukuhakikishia kwamba kuwapo kwao katika Singapore si tisho kwa masilahi ya nchi yako.

Hatua zenye ukandamizi zilizochukuliwa na serikali yako katika Singapore dhidi ya Mashahidi wa Yehova zinajulikana kila mahali sasa kutokana na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari. Ni jambo linalohangaisha hasa washiriki wenzao milioni 12 ulimwenguni pote. Nakuomba utumie cheo chako cha juu kurekebisha hali hiyo na kuwapa Mashahidi wa Yehova katika nchi yako uhuru wa ibada na wa dhamiri unaohakikishwa na Katiba.

Naamini kwamba mazungumzo manyoofu pamoja na wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova yatasaidia kuondoa kutoeleweka kokote kwa shirika letu na kwa utendaji wetu na kufanya hivyo kutakuhakikishia kwamba serikali ya Singapore haina sababu ya kuwaogopa Mashahidi wa Yehova. Ningefurahi kufanya mpango wa mkutano huo.

Natazamia jibu lenu.

Wako kwa staha,

Milton G. Henschel

Msimamizi

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

Nik Wheeler/H. Armstrong Roberts

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki