Mashahidi Hata Mwisho wa Nchi
ETAH
THULE
GODHAVN
GODTHÅB
JULIANEHÅB
ANGMAGSSALIK
THULE ni sehemu ya jina lililotumiwa tangu nyakati za kale ili kufafanua kifiko cha upeo, cha kijiografia au kinginecho. Leo Thule ndilo jina la kijiji kidogo katika kaskazini ya mbali ya Greenland, kisiwa cha ulimwengu kilicho kikubwa kupita vyote. Kijiji hicho kidogo kiliitwa hivyo katika 1910, wakati mvumbuaji Mdenmark Knud Rasmussen alipokitumia kuwa kituo cha muda kwa ajili ya safari za kikazi za kwenda nchani. Hata sasa, kwenda Thule ni kufanya safari ya kikazi kuliko kufanya safari ya raha.
Bado, kuna uhitaji wa hima wa kufanya safari za kikazi za kwenda Thule. Katika kuitikia amri ya Yesu: “Mtakuwa mashahidi wangu . . . hata mwisho wa nchi,” Mashahidi wa Yehova wana hamu ya kuleta habari njema ya Ufalme wa Mungu hadi mahali hapa, kimojapo vijiji vidogo vya kibinadamu vyenye kudumu vilivyo kaskazini zaidi duniani.—Matendo 1:8; Mathayo 24:14.
‘Twaweza Kwenda Thule Wakati Gani?’
Katika 1955 Mashahidi wawili wa Denmark waliotaka kushiriki katika kuhubiri “hata mwisho wa nchi” waliwasili Greenland. Wengine walikuja baadaye, na hatua kwa hatua kazi yao ya kuhubiri ilienea pwani ya kusini na ya magharibi hadi Ghuba ya Melville na kuelekea pwani ya mashariki. Lakini sehemu za mbali zaidi kama Thule zilifikiwa kwa barua au kwa simu pekee.
Siku moja katika 1991, Bo na mkeye, Helen, wahudumu wawili wa wakati wote, walikuwa wamesimama kwenye mwamba wenye kuelekea Ghuba ya Melville. Wakitazama kaskazini walijiuliza, ‘Tutaweza kwenda Thule wakati gani ili kuwapelekea watu huko habari njema ya Ufalme?’
Katika 1993, Werner, mhudumu mwingine wa wakati wote, alijasiria kuvuka Ghuba ya Melville katika mashua yake ya kwenda kasi yenye urefu wa meta 5.5 iliyoitwa Qaamaneq (Nuru). Alikuwa tayari amesafiri kilometa 1,200 kutoka Godthåb hadi eneo la Upernavik. Hata hivyo, kuvuka Ghuba ya Melville—kilometa 400 za maji ya Aktiki yaliyo wazi—si jambo lililo rahisi. Katika sehemu kubwa ya mwaka, ghuba hiyo inazuiwa na barafu. Werner alifaulu kuvuka ghuba hiyo, hata ingawa injini moja ya mashua yake iliharibika kwa sababu ya barafu. Naye akaweza kuhubiri kadiri fulani kabla ya kulazimika kurudi.
Kwenda Thule
Baada ya safari hiyo, Werner alianza kufanya mipango mipya. Aliongea na Arne na Karin kuhusu kusafiri pamoja kwenda Thule—wao pia walikuwa na mashua, yenye urefu wa meta saba iliyokuwa na vijumba vinne na, la maana zaidi, ilikuwa na vifaa vya kisasa vya kusafiri baharini. Mashua hizo zingeandaa makao, na kukiwa na mashua mbili zikisafiri pamoja, kuvuka Ghuba ya Melville kusingekuwa jambo la hatari sana. Ili kuhubiri katika mji mkuu wenye wakazi 600 na katika vile vijiji vidogo sita katika eneo hilo, walihitaji msaada zaidi. Kwa hiyo walialika Bo na Helen na Jørgen na Inge—wote wakiwa wahudumu wenye uzoefu waliofahamu usafiri katika nchi hiyo—waende pamoja nao. Watano katika kikundi hicho husema Kigreenland pia.
Walipeleka ugavi wa fasihi za Biblia kimbele. Mashua zilijazwa pia na fasihi, pamoja na maandalizi muhimu ya chakula na maji, fueli, injini ya ziada, na mashua ndogo ya mpira. Kisha, katika Agosti 5, 1994, baada ya miezi kadhaa ya matayarisho, kikundi hicho kilikusanyika na mashua zote mbili zilikuwa tayari na kupakiwa mizigo katika bandari ya Ilulissat. Safari ya kwenda kaskazini ikaanza. Werner, Bo, na Helen walisafiri katika mashua ndogo kati ya zile mbili. “Jambo pekee ambalo uliweza kufanya lilikuwa ni kuketi au kulala katika kijumba chako na kushikilia kitu fulani,” aandika Bo. Acheni tufuate rekodi ya safari hiyo kwa mashua.
“Kulikuwa na miendo mirefu baharini iliyokuwa yenye utulivu. Mandhari zenye kupendeza sana zilifunuka machoni petu—kumetameta kwa bahari, sehemu-sehemu zenye ukungu mzito, jua jangavu na anga la buluu, vilima vya barafu vyenye maumbo na rangi zenye kupendeza sana, kibokobarafu wa kikahawia akiota jua kwenye pande kubwa la barafu lenye kuelea baharini, pwani yenye pande za mlima zenye giza na nyanda ndogo-ndogo—kubadilika-badilika kwa mandhari kulikuwa bila mwisho.
“Bila shaka sehemu iliyokuwa yenye kupendeza zaidi, ni kuzuru vijiji vilivyokuwa njiani. Sikuzote kulikuwa na watu, kwa kawaida watoto, chini gatini ili kuona wageni walikuwa nani na kuwakaribisha. Tuligawanya fasihi za Biblia tukawaazima hao watu video kuhusu tengenezo letu. Wengi waliweza kuiona kabla ya sisi kulazimika kuondoka. Katika South Upernavik, watu kadhaa walisafiri kwa mashua hadi kwenye mashua zetu hata kabla ya sisi kuingia humo. Kwa hiyo kwa jioni nzima, tulikuwa na wageni katika mashua nasi tukajibu maswali mengi ya Biblia.”
Sasa, baada ya kilometa 700 za kwanza za hiyo safari, zile mashua mbili zilikuwa tayari kuvuka Ghuba ya Melville.
Jambo Gumu Lenye Hatari
“Hiyo ilionwa na wengi kuwa sehemu yenye hatari ya hiyo safari. Na ilikuwa lazima tuvuke moja kwa moja kwa sababu kijiji cha Savissivik (ambako eneo hilo laanza na ambako tungaliweza pia kupata makao) kilikuwa bado kimezuiwa na barafu.
“Kwa hiyo tukaanza kuvuka. Kwa kuwa kulikuwa na barafu nyingi, tulisafiri mbali zaidi katika bahari iliyo wazi. Kwa uzuri, maji yalikuwa matulivu. Saa kadhaa za kwanza hazikuwa na matukio—tukisafiri mwendo wa kilometa nyingi katika bahari-kuu. Kufikia jioni tuliona Cape York nasi tukageuka polepole kuelekea kaskazini, karibu zaidi na nchi. Sasa kulikuwa na barafu tena—nzee, nzito, na mapande makubwa ya barafu yenye kuelea yaliyokuwa yakivunjika-vunjika yaliyoweza kuonwa kufikia upeo wa macho. Tulifuata ukingo wa barafu kwa mwendo mrefu, nyakati nyingine tukijitahidi kupitia vijia vyembamba. Kisha kukawa na ukungu, umajimaji mzito wa kijivujivu, yenye kupendeza kwa njia ya ajabu katika nuru ya jua lililokuwa likishuka. Na yale mawimbi! Ukungu, mawimbi, na barafu vyote kwa wakati uo huo—kwa kawaida lolote moja la mambo hayo ni jambo gumu vya kutosha.”
Kukaribishwa Kwetu
“Tuliingia maji matulivu zaidi tulipokaribia Pituffik. Uumbaji ulitupa sisi ukaribishaji wenye kutokeza sana: Jua likiwa juu sana katika anga la buluu, tena buluu sana; mbele yetu, kile kilangobahari kipana chenye kumetameta, kilichokuwa na milima ya barafu yenye kuelea iliyotapakaa; na huko mbele zaidi kile kilichoonekana kama kivuli cheusi cha ule mwamba katika Dundas—mahali pa zamani pa Thule!” Karibu kilometa 100 kaskazini zaidi, hao wasafiri walifika kituo chao cha mwisho.
Sasa walikuwa na hamu ya kuanza kuhubiri nyumba hadi nyumba. Wawili wao walipokea itikio kali kwenye mlango wao wa kwanza. “Tulikataliwa kana kwamba tu tulikuwa Denmark,” wakasema. “Lakini walio wengi walitukaribisha kwa uchangamfu. Watu walikuwa wenye kufikiri na wenye kujua mambo. Watu fulani walitaja kwamba walikuwa wamesikia juu yetu na walifurahi kwamba tulikuwa tumekuja hatimaye. Tulikutana na watu wazuri ajabu, kama wawinda-sili waliokuwa wamefanya safari za kikazi hadi Ncha ya Kaskazini, na wenyeji, wenye kuridhika na wenye kiasi na walio na maoni ya kutilia shaka kwa kadiri fulani ustaarabu wa kisasa.”
Siku chache zilizofuata zililetea wote maono mazuri. Fasihi za Biblia zilipokewa kwa uthamini kila mahali. Katika nyumba kadhaa hao Mashahidi walianzisha mafunzo ya Biblia mara moja. Inge asimulia hivi kuhusu nyumba alimopata upendezi: “Ilikuwa nyumba safi na yenye ustarehe ya chumba kimoja. Kwa siku tatu mfululizo, tulimzuru yule mwanamume mpole aliyeishi humo nasi tukazidi kumpenda sana. Alikuwa mwinda-sili halisi, akiwa na kayak (mashua ya Waeskimo) yake nje ya nyumba yake. Alikuwa amewapiga risasi dububarafu, vibokobarafu, na, bila shaka, sili wengi. Katika ziara yetu ya mwisho, tulisali pamoja naye, na macho yake yakajaa machozi. Sasa ni lazima tuyaache mambo yote mikononi mwa Yehova na tutumainie wakati na fursa ya kurudi.”
Thule hupokea ziara nyingi kutoka kwa Waeskimo Wakanada. Inge aripoti hivi: “Helen nami tulikutana na Waeskimo kadhaa kutoka Kanada. Yapendeza kwamba wanaweza kuwasiliana na Wagreenland; watu wa eneo la Aktiki waonekana kusema lugha zinazofanana. Ingawa Waeskimo Wakanada wana lugha yao wenyewe ya kuandikwa, waliweza kusoma fasihi zetu katika Kigreenland. Huenda hilo likawafungulia fursa zenye kusisimua.”
Vile vijiji vidogo vilivyo umbali wa kilometa 50 hadi 60 kwa mashua vilitembelewa pia. “Tukiwa njiani kwenda kijiji kidogo cha Qeqertat, tulifuata pwani kwa ukaribu, tukitumaini kupata watu wakiwa nje wakiwinda nyangumi wenye pembe moja. Na kwa kweli, kwenye mwamba ulio sawa tulipata kambi yenye familia tatu au nne, zilizovalia manyoya ya wanyama, pamoja na mahema na kayak zao. Wakiwa na vyusa mkononi, wanaume waliketi mwambani kwa zamu ili kuona nyangumi hao wenye pembe moja wanaotamaniwa sana. Wakiwa tayari wamengojea siku kadhaa, hawakupendezwa sana kutuona kwa sababu huenda tukawafukuza nyangumi hao! Walionekana kuwa katika ulimwengu wao wenyewe kabisa. Wanawake walikubali fasihi kadhaa, lakini huo haukuwa wakati ufaao wa kuzungumza zaidi. Hatimaye tukafika Qeqertat saa tano za usiku tukamaliza ziara yetu ya mwisho katika kijiji kidogo hicho saa nane usiku!”
“Hatimaye tukafikia Siorapaluk, kijiji kidogo cha kaskazini zaidi katika Greenland. Kiko kwenye ufuo wenye mchanga chini ya miamba iliyofunikwa kwa nyasi za kijani-kibichi katika mazingira yaliyo jangwa hasa.” Angalau kuelekea kaskazini, wale Mashahidi wamefika kihalisi hata mwisho wa nchi, kwa kazi yao ya kuhubiri.
Safari Yakamilika
Wale Mashahidi wamekamilisha kazi yao. Wamehubiri nyumba hadi nyumba na hema hadi hema, wametoa fasihi, wamepata maandikisho, wameonyesha video, wameongea na Wagreenland wengi, na kuongoza mafunzo ya Biblia. Sasa ni wakati wa kwenda nyumbani. “Tulipoingia mashua yetu ya mpira jioni hiyo kupiga makasia kutoka kijiji kidogo cha Moriusaq, watu kadhaa walikuwa chini ufuoni ili kutuaga, wakipunga vitabu au broshua walizokuwa wamechukua.”
Baadaye, katika sehemu ya pwani iliyo ukiwa, hao Mashahidi walishangaa kumwona mtu akipunga mkono kutoka mwamba—huku kuliko mbali sana! “Bila shaka, tulienda ufuoni ili kukutana naye. Kumbe alikuwa kijana kutoka Berlin, Ujerumani, aliyekuwa akisafiri kando ya hiyo pwani katika kayak yake naye alikuwa amesafiri kwa mwezi mmoja. Katika Ujerumani alitembelewa na Mashahidi wa Yehova kwa ukawaida naye alikuwa na vitabu vyao kadhaa. Tulitumia muda wa saa mbili naye, na kwa kweli alivutiwa kukutana na Mashahidi mahali kama hapo.”
Katika safari ya kurudi, wahudumu hao wenye kusafiri walipokea ukaribishaji wenye kutokeza katika kijiji kidogo cha Savissivik, ambacho hakikuwa kimetembelewa. Watu fulani huko walikuwa wamepokea na kusoma fasihi mwaka uliotangulia, na walikuwa na njaa ya kupata chakula cha kiroho zaidi.
Kuvuka Ghuba ya Melville wakati wa kurudi kulichukua muda wa saa 14. “Tulijionea mshuko wa jua, ambao katika sehemu hiyo ya juu ni ono la muda wa saa nyingi, kukiwa na mabadiliko ya daima ya rangi zenye kuvutia sana. Macheo ya jua, yanayofuata mara hiyo, yalichukua muda mrefu pia. Huku mawingu mekundu-mekundu ya mshuko wa jua yakiwa bado yamefunika anga la kaskazini-mashariki, jua lilipanda kuelekea upande wa kusini kidogo tu. Ni mandhari isiyoweza kufafanuliwa—au hata kupigwa picha—ifaavyo.” Mabaharia hao walikaa macho usiku kucha.
“Tulipofika Kullorsuaq, tulikuwa tumechoka sana. Lakini tulikuwa wenye furaha na wenye kuridhika. Tulikuwa tumekamilisha hiyo safari kwa mafanikio! Katika sehemu ya safari iliyobaki, tulipata kupendezwa kwingi katika miji na vijiji vidogo vya kando ya pwani. Swali hili lilirudiwa mara nyingi, ‘Kwa nini baadhi yenu msikae pamoja nasi? Tunahuzunika kuwaona mkiondoka upesi sana!’”
Katika Qaarsut familia yenye urafiki ilialika watano wa hao wageni kula mlo nayo. “Hiyo familia ilitaka tukae usiku kucha. Lakini kwa kuwa kulikuwa na mahali pazuri zaidi pa kutia nanga umbali wa kilometa 40 kutoka hapo, tulikataa kukaa, tukaendelea na safari ya mashua. Baadaye tulisikia kwamba kilima kikubwa cha barafu kilikuwa kimevunjika mapema asubuhi iliyofuata, na wimbi likapindua juu chini mashua ndogo-ndogo 14 mahali tulipokuwa tumetoka!”
Hatimaye, hicho kikundi kilikuwa kimerudi Ilulissat, kikiwa kimekamilisha safari yacho ya kikazi ya kwenda Thule. Karibu na wakati uo huo, watangazaji wengine wawili walikuwa wamesafiri kwenda sehemu za mbali kwenye pwani ya mashariki mwa Greenland. Katika safari hizo mbili, hao watangazaji waligawanya jumla ya vitabu 1,200, broshua 2,199, na magazeti 4,224, na walikuwa wamepata maandikisho 152. Kuwasiliana na wale wengi waliopendezwa karibuni kunadumishwa sasa kwa simu na barua.
Zijapokuwa wakati, nishati, na gharama zinazohusika, Mashahidi wa Yehova hupata shangwe kubwa katika kutimiza agizo la Bwana-Mkubwa wao la ‘kuwa mashahidi wake . . . hata mwisho wa nchi.’—Matendo 1:8.
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
Kwenye Pwani ya Mashariki mwa Greenland
KARIBU wakati uleule ambapo kikundi cha watangazaji kilipofika Thule, mume na mke Mashahidi, Viggo na Sonja, walisafiri kwenda eneo jingine lisilohubiriwa—Ittoqqortoormiit (Scoresbysund) kwenye pwani ya mashariki mwa Greenland. Ili kufika huko walilazimika kusafiri kwenda Iceland, wachukue ndege kurudi Constable Point kwenye pwani ya Greenland, kisha waende kwa helikopta.
“Huo ulikuwa wakati wa kwanza ambapo Mashahidi wa Yehova walikuwa wamekuja hapa,” wasimulia mapainia wawili hao, ambao lugha yao ni Kigreenland. “Ijapokuwa wanaishi mbali, watu hawa ni wenye kujua mambo kwa njia ya kushangaza. Lakini, walifurahi pia kujifunza mambo mapya. Wakiwa wenye kipawa cha kusimulia hadithi, walituambia kwa hamu kuhusu vipindi vyao vya kuwinda sili na maono mengine katika maumbile.” Waliitikiaje kazi ya kuhubiri?
“Tukihubiri nyumba hadi nyumba, tulikutana na J——, ambaye ni katekista. ‘Asanteni kwa kunitia ndani katika ziara zenu,’ akasema. Tulimwonyesha fasihi zetu na jinsi ya kuzitumia. Siku iliyofuata alitujia, akataka kujifunza kuhusu jina la Yehova. Tulimwonyesha elezo katika kielezi-chini katika Biblia yake mwenyewe ya Kigreenland. Tulipoondoka, alipigia simu marafiki wetu katika Nuuk ili kuwatolea shukrani zake kwa ziara yetu. Ni lazima tujaribu kuendelea kumsaidia mtu huyu.
“Tulikutana pia na O——, mwalimu anayejua kuhusu Mashahidi wa Yehova. Alitupa sisi muda wa saa mbili ili kusema na darasa lake la wanafunzi wenye umri wa miaka 14 hadi 16. Kwa hiyo tuliwaonyesha video yetu na kujibu maswali yao. Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazia na vitabu vingine vilikubaliwa kwa hamu sana. Tulikutana na wasichana watatu baadaye. Walikuwa na maswali mengi, mmoja wao akiwa mwenye kupendezwa sana. Aliuliza, ‘Mtu anakuwaje Shahidi? Kwa hakika ni lazima iridhishe kuwa kama nyinyi. Babangu huwaunga mkono pia.’ Tuliahidi kumwandikia.
“Katika mojawapo vijiji vidogo hivyo, tulikutana na katekista mwingine, M——, nasi tukawa na mazungumzo yenye kupendeza. Alijitolea kuhakikisha kwamba wanaume waliokuwa nje wakiwinda watapokea fasihi zetu mara warudipo. Kwa hiyo sasa yeye ndiye ‘mtangazaji’ wetu katika mahali hapo pa mbali.”
Ingawa safari hiyo ilikuwa ya kuzungukazunguka na ya kujitahidi, wale mapainia wawili walihisi kwamba jitihada zao zilithawabishwa sana.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.