Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w96 8/15 kur. 22-26
  • “Rundo la Mashahidi” Katika Bara la “Mlima wa Mungu”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Rundo la Mashahidi” Katika Bara la “Mlima wa Mungu”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Vichwa vidogo
  • Kusafiri Nchi Nzima kwa Mtumbwi, Teksi ya Mashambani, au Baiskeli?
  • Maeneo ya Ndani Kabisa ya Mashambani
  • Kaskazini Zaidi
  • Kutoa Ushahidi Katika Miji
  • Je, Wapanga Kuzuru?
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
w96 8/15 kur. 22-26

“Rundo la Mashahidi” Katika Bara la “Mlima wa Mungu”

KWENYE ramani ya kontinenti, ukifuata pwani ya Afrika Magharibi na kuelekea mashariki kupitia Ghuba la Guinea, mahali ambapo pwani hugeukia kusini, utaipata Kamerun. Ukiendelea kuelekea kusini kwenye pwani, utafika katika eneo pana la fuo zenye mchanga mweusi. Huo mchanga mweusi ni tokeo la utendaji wa kivolkeno wa Mlima Kamerun.

Kilele kilichochongoka cha mlima huu wa meta 4,070 ndicho kikubwa zaidi katika eneo hilo. Jua lishukalo liangazapo mitelemko ya Mlima Kamerun, hutoa wonyesho wenye kutazamisha wa rangi nyangavu—urujuani, rangi ya machungwa, rangi ya dhahabu, na nyekundu. Bahari na mabwawa ya karibu huonyesha rangi zote hizo kama kioo, kufanya karibu iwe vigumu kupambanua anga na dunia. Ni rahisi kuelewa kwa nini makabila ya eneo hili, yaabuduyo maumbile, yaliuita mlima huo Mongo Ma Loba, ambalo hutafsiriwa kuwa “Gari la miungu,” au kwa kawaida zaidi, “Mlima wa Mungu.”

Mbali zaidi kusini, kuna kilometa nyingi za fuo zenye mchanga mweupe, zenye safu ya minazi. Zaidi ya pwani yenye kupendeza sana, sehemu kubwa ya nchi imefunikwa kwa msitu mkubwa wa ikweta, ukienea kuelekea mpaka wa Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati na magharibi kuelekea kaskazini hadi Nigeria na Chad iliyo kusini ya Sahara. Sehemu ya magharibi ya nchi ni yenye milima-milima, ikimkumbusha msafiri sehemu za Ulaya. Hata hivyo, hali ya joto itaendelea kukukumbusha kwamba uko karibu sana na ikweta. Utofauti-tofauti wa maeneo ya mashambani hufanya viongozi wengi wa watalii kuifafanua Kamerun kuwa mfano halisi wa Afrika. Hali hiyo yenye kuvutia inatiwa nguvu na vikundi tofauti-tofauti vya kikabila na zaidi ya lugha na lahaja rasmi 220.

Ikiwa ungetembelea Kamerun, ungeweza kukaa katika moja ya hoteli kubwa za bandari ya Douala au katika jiji kuu, Yaoundé. Lakini ungekosa fursa murua sana ya kupata kujua mambo fulani juu ya maisha ya watu, hasa maisha ya Mashahidi wa Yehova zaidi ya 24,000 ambao wamekuwa na shughuli nyingi wakifanyiza “rundo la mashahidi” kotekote katika bara hili la “Mlima wa Mungu.”a Mbona usisafiri kuzunguka nchi nzima ili uwaone baadhi yao? Safari yako ya uvumbuzi katika bara hili la Afrika Magharibi bila shaka itathawabishwa sana.

Kusafiri Nchi Nzima kwa Mtumbwi, Teksi ya Mashambani, au Baiskeli?

Mahali ambapo Sanaga, mto mrefu kuliko yote katika Kamerun, huingia baharini hufanyiza delta kubwa. Ili kuwafikia wakaaji wote wa eneo hilo kubwa, Mashahidi wa Yehova mara nyingi hulazimika kusafiri ndani ya mitumbwi. Hilo ndilo wafanyalo wale wahubiri tisa wa Ufalme katika kikundi kidogo kilichoko Mbiako. Wawili kati yao huishi umbali wa kilometa 25, katika kijiji cha Yoyo. Ili wafike Mbiako, wao hulazimika kupiga makasia kwa juhudi sana, hata hivyo wao huhudhuria mikutano ya Kikristo sikuzote. Alipokuwa akitembelea kikundi hicho, Mwangalizi asafiriye alipendekeza kuonyesha vidio Jehovah’s Witnesses—The Organization Behind the Name. Lakini hilo ni rahisi kusema kuliko kutenda. Katika kijiji cha mbali hivyo mashambani, angepata wapi mashine ya vidio, televisheni na umeme ili kuonyesha vidio?

Juma la ziara, baadhi ya wahubiri walimtembelea pasta, wa kanisa la huko. Walishangaa pasta alipowakaribisha kwa uchangamfu, wakawa na mazungumzo mazuri ya Biblia. Walipojua kwamba pasta alikuwa na mashine ya vidio pamoja na jenereta ya umeme, ndugu waliweka kando hofu na wakajipa moyo mkuu kumuuliza ikiwa wangeweza kuazima chombo chake. Kwa kuwa alikuwa amefurahia mazungumzo ya Biblia ya mapema, pasta alikubali kusaidia. Jumamosi jioni watu 102 kutia ndani pasta na washiriki wengi wa kanisa lake walikuja kwenye wonyesho. Wale Mashahidi wawili kutoka Yoyo walileta wengi wenye kupendezwa kwa mitumbwi miwili. Hawakuona ugumu wowote kupiga makasia dhidi ya mkondo wa mawimbi ya maji yenye kuinuka. Baada ya kuona hiyo vidio, walivutwa na kutiwa moyo sana, na waliona fahari kuwa washiriki wa tengenezo hili kubwa ambalo kusudi lake ni kumheshimu Yehova.

Kwenda mahali ambako mtumbwi hauwezi kufika, mtu anaweza kutumia teksi ya mashambani. Mahali ambapo magari hayo hungoja abiria sikuzote kuna shughuli nyingi sana. Ukizungukwa na wauzaji wa maji-baridi, wauza-ndizi, na vijana wanaopakia mizigo kwenye gari, ni rahisi kuchanganyikiwa kabisa. Kazi ya vijana wanaopakia mizigo ni kuingiza abiria katika mateksi ya mashambani yanayongoja, ambayo kulingana nao, yote “yako tayari kwenda.” Hata hivyo, neno “tayari” halipaswi kueleweka kwa maana halisi ya neno hilo. Wasafiri wanalazimika kutumia muda wa saa kadhaa, au siku kadhaa wakingoja. Abiria wakiwa wamesongamanishwa ndani na dereva ameweka mizigo, mifuko yenye mazao, na nyakati nyingine kuku na mbuzi walio hai, juu ya sehemu ya kuwekea mizigo, teksi ya mashambani huondoka kuelekea vijia vilivyo na mashimo na mavumbi.

Mhudumu mmoja asafiriye, akiwa amekatishwa tamaa na aina hii ya usafiri, alichagua kujitegemea. Sasa anafunga safari zake zote kwa baiskeli. Yeye asema: “Tangu nilipoamua kutumia baiskeli kusafiri kutoka kutaniko moja hadi jingine, sikuzote mimi huwasili kwa wakati kwa ajili ya ziara. Ni kweli kwamba, safari yaweza kuchukua saa nyingi, lakini angalau silazimiki kutumia siku moja au mbili nikingojea teksi za mashambani. Wakati wa majira ya Mvua, barabara nyingine karibu hutoweka kabisa kwa sababu ya mafuriko. Lazima uvue viatu vyako ili kuvuka maeneo hayo ya matope na maji. Siku moja kiatu changu kimoja kilitumbukia katika kijito, na hakikupatikana hadi majuma kadhaa baadaye, wakati binti mmoja wa Shahidi fulani alipokipata bila kutazamia alipokuwa akivua samaki! Nina furaha kuvaa viatu hivyo tena baada ya kimojawapo kukaa kwa muda fulani pamoja na samaki. Mara nyingine mimi hupitia maeneo ambayo Mashahidi wa Yehova hawajahubiri kamwe. Sikuzote wana-vijiji huniuliza nimebeba nini. Hivyo mimi huweka magazeti na broshua karibu. Kila nisimamapo, mimi hutoa vichapo hivyo vya Biblia na kutoa ushahidi mfupi. Naamini Yehova atafanya mbegu hizo zikue.”

Maeneo ya Ndani Kabisa ya Mashambani

Mashahidi wa Yehova hujitahidi kushiriki habari njema ya Ufalme pamoja na wengine hata ndani kabisa katika Kamerun, katika vijiji vilivyofichwa ndani sana misituni. Hilo huhitaji jitihada kubwa sana, lakini matokeo huchangamsha moyo.

Marie, mhudumu wa wakati wote, alianzisha funzo la Biblia na msichana mchanga aitwaye Arlette. Mwishoni mwa funzo la kwanza, Marie alimuuliza Arlette kama angemsindikiza mlangoni kwani hiyo ndiyo desturi katika sehemu hii ya Afrika. Hata hivyo, msichana huyo mchanga alieleza kwamba aliweza kutembea kwa shida sana kwa sababu ya maumivu katika miguu yake. Miguu ya Arlette ilikuwa imeshambuliwa na aina ya funza ambao aina yao ya kike hujichimba katika mwili na kusababisha majipu. Kwa ujasiri, Marie aliondoa funza hao mmoja baada ya mwingine. Baadaye alijua kwamba msichana huyo mdogo alikuwa akiteswa na roho waovu usiku. Kwa subira, Marie alieleza jinsi mtu awezavyo kuweka tumaini katika Yehova, hasa kwa kuliita jina lake kwa sauti katika sala.—Mithali 18:10.

Arlette alifanya maendeleo ya haraka. Kwanza, familia haikuona ubaya wowote kuhusiana na funzo kwa sababu ya maendeleo makubwa ya kimwili na ya kiakili aliyokuwa akifanya. Lakini walipotambua kwamba alitaka kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, walimkataza asiendelee na funzo. Baada ya majuma matatu mama ya Arlette alipoona binti yake alivyo na huzuni, aliwasiliana na Marie na kumwomba waanzishe upya funzo.

Wakati wa kuhudhuria kusanyiko la mzunguko ulipofika, Marie alimlipa dereva wa teksi kumchukua Arlette siku zote mbili. Hata hivyo, dereva alikataa kwenda nyumbani kwa Arlette, baada ya kufikia mkataa wa kwamba kijia kitokacho nyumbani kwa Arlette kuelekea barabarani hakipitiki. Hivyo Marie alifanikiwa kumleta Arlette hadi barabarani ili aweze kupanda hiyo teksi. Kwa hakika, Yehova alibariki jitihada hizo. Leo Arlette huhudhuria mikutano yote ya kutaniko. Ili kumsaidia kufanya hivyo, bila kuchoka, Marie huja kumchukua. Pamoja hutembea safari moja ya dakika 75. Kwa vile mkutano wa Jumapili huanza saa 2:30 asubuhi, Marie hulazimika kuondoka nyumbani saa 12:30 asubuhi; na bado yeye hufanikiwa kufika kwa wakati. Karibuni Arlette anatumaini kufananisha wakfu wake kwa ubatizo. Marie aeleza: “Yeyote ambaye hakumwona alipoanza kujifunza hawezi kuwazia amebadilika kwa kadiri gani. Namshukuru sana Yehova kwa njia ambayo amembariki.” Bila shaka Marie ni mfano mzuri sana wa upendo wa kujidhabihu.

Kaskazini Zaidi

Kaskazini mwa Kamerun kuna unamna-namna na maajabu mengi. Nyakati za mvua, kunabadilika kuwa bustani kubwa, yenye majani mabichi na majimaji. Lakini jua kali linapoangaza, majani hunyauka. Mchana, jua linapokuwa utosini na kivuli hakipatikani kwa urahisi, kondoo hujisongamanisha pamoja karibu na kuta za nyumba zenye matope mekundu ili kupata kivuli. Miongoni mwa mchanga na nyasi kavu, masazo pekee ya rangi ya kijani kibichi ni majani ya mibuyu. Ingawa hiyo si mikubwa kama mingine ya jamii hiyo iliyo katika misitu ya ikweta, ina uwezo wa kuvumilia hali mbaya. Uwezo wao wa kuvumilia mazingira magumu huonyesha vizuri bidii na ujasiri wa Mashahidi wachache ambao wameenda kuishi katika eneo hili ili kuruhusu nuru ya kweli iangaze.

Baadhi ya makutaniko katika eneo hili yametenganishwa umbali wa kilometa 500 hadi 800, na hisia ya kutengwa inaonekana waziwazi. Lakini kuna kiasi kikubwa cha upendezi. Mashahidi kutoka sehemu nyingine huhamia huko ili kusaidia. Ili kufanya vizuri katika huduma, wao hulazimika kujifunza Foufouldé, lahaja ya huko.

Shahidi kutoka Garoua aliamua kutumia siku chache akihubiri katika kijiji cha kwao, umbali wa kilometa zipatazo 160. Alipata upendezi fulani, lakini gharama kubwa ya usafiri ilimzuia kurudi kwa ukawaida. Majuma machache baadaye, Shahidi huyo alipokea barua kutoka kwa mtu mmoja aliyependezwa ikimsihi aende kuwatembelea tena. Bado akiwa na upungufu wa fedha za nauli, hakuweza kwenda. Fikiria jinsi Shahidi huyo alivyoshangaa mtu yule wa kupendezwa alipomtembelea nyumbani kwake Garoua kumfahamisha kwamba watu kumi kule kijijini walikuwa wanangojea ziara yake!

Katika kijiji kingine, karibu na mpaka wa Chad, kikundi cha watu 50 waliopendezwa kimeunda funzo lacho chenyewe la Biblia. Kilipanga watatu miongoni mwacho wahudhurie mikutano katika kutaniko la karibu zaidi la Chad. Warudipo, hawa wangeongoza funzo la Biblia pamoja na kikundi chote. Kwelikweli maneno ya Yesu yanaweza kutumika vizuri hapa: “Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”—Mathayo 9:37, 38.

Kutoa Ushahidi Katika Miji

Baada ya miaka mingi ya upungufu wa vichapo karibu miaka miwili iliyopita, magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yalianza kupatikana kwa urahisi Kamerun. Kuna idili na upendezi mwingi kuelekea magazeti haya kwa kuwa watu wanayasoma kwa mara ya kwanza. Mapainia wa pekee vijana mume na mke katika moja ya majiji waliangusha magazeti 86 katika asubuhi ya kwanza ya kuhubiri katika eneo lao jipya. Baadhi ya wahubiri huangusha kufikia magazeti 250 katika mwezi mmoja! Siri ya mafanikio yao ni nini? Mtolee kila mtu magazeti.

Shahidi mmoja anayefanya kazi katika ofisi ya umma huacha magazeti yaonekane. Mwanamke mmoja aliyaangalia magazeti hayo lakini hakuchukua lolote. Shahidi huyo alitambua upendezi wake na akampa nakala moja, ambayo alikubali. Alishangaa kumwona tena siku iliyofuata. Hakutaka kuchangia tu yale magazeti aliyochukua bali pia alitaka mengine. Kwa nini? Kwa kuwa alikuwa amekuwa mhasiriwa wa kulalwa kinguvu, alikuwa amechagua magazeti yenye habari hiyo. Usiku kucha alikuwa amesoma tena na tena shauri lililotolewa. Akihisi amefarijiwa sana, alitaka kujua zaidi kuhusu Mashahidi wa Yehova.

Hata watoto wadogo wanaweza kushiriki katika kueneza ujumbe wa Biblia wenye tumaini. Msichana Shahidi wa miaka sita alipoambiwa na mwalimu wake aimbe wimbo wa kidini wa Kikatoliki, yeye alikataa, akitaarifu kwamba alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Kisha mwalimu huyo alimwomba aimbe wimbo mmoja wa dini yake mwenyewe ili aweze kumpima kutokana na uimbaji wake. Yeye alichagua wimbo wenye kichwa “Ahadi ya Mungu ya Paradiso” na akaimba kutoka moyoni. Mwalimu alimuuliza, akisema: “Ulitaja paradiso katika wimbo wako. Paradiso hiyo iko wapi?” Msichana akaeleza kusudi la Mungu la kuleta Paradiso duniani hivi karibuni. Kwa kushangazwa na jibu lake, aliwaomba wazazi wa yule msichana kitabu alichokuwa akijifunza. Alinuia kumpima kutokana na yale aliyojifunza kutokana na kitabu alichokuwa anajifunza badala ya yale aliyofunzwa wakati wa somo la dini. Wazazi walimpendekezea mwalimu kwamba ikiwa alikuwa anataka kumpima sawasawa, kwanza anapaswa ajifunze yeye mwenyewe. Funzo la Biblia likaanzishwa pamoja naye.

Je, Wapanga Kuzuru?

Leo katika sehemu nyingi za dunia, watu ni wenye ubaridi kuelekea habari njema za Ufalme. Hawapendezwi na Mungu wala Biblia. Wengine wanafadhaishwa na hofu na kukataa kumkubali mgeni yeyote mlangoni. Yote hayo ni mwito wa ushindani halisi kwa Mashahidi wa Yehova katika huduma yao. Lakini ni tofauti iliyoje huko Kamerun!

Kuhubiri mlango hadi mlango ni furaha huko. Badala ya kugonga mlango, ni desturi kuita “Kong, kong, kong.” Kisha kutoka ndani sauti hujibu, “Ni nani?” baada ya hapo sisi hujitambulisha wenyewe kuwa Mashahidi wa Yehova. Kwa kawaida wazazi huwaambia watoto wao wachukue benchi na kuziweka katika kivuli cha mti, labda mwembe. Wakati mzuri hutumiwa kueleza Ufalme wa Mungu ni nini na lile utakalofanya ili kuondoa hali ya huzuni ya wanadamu.

Kufuatia mazungumzo kama hayo, mwanamke mmoja alieleza hisia zake zote kwa uhuru, akisema: “Ninashuka moyo kuona kwamba kweli niliyokuwa nikiitafuta haipatikani katika dini niliyozaliwa ndani yayo na ambayo nimezeekea ndani yayo. Namshukuru Mungu kwamba amenionyesha kweli. Nilikuwa shemasi katika kanisa langu. Sanamu ya Bikira Mariamu hukaa juma moja katika kila nyumba ya shemasi ili kwamba kila mmoja aweze kumtolea maombi. Kwa upande wangu, wakati wote nilimwomba Mariamu anisaidie niijue kweli. Sasa Mungu amenionyesha kwamba Mariamu hana kweli. Namshukuru Yehova.”

Kwa hiyo ikiwa siku fulani wahisi uhitaji wa kujionea mwenyewe shangwe ya kweli ambayo yaweza kupatikana katika kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, mbona usitembelee sehemu hii ya Afrika Magharibi? Zaidi ya kuigundua “Afrika ndogo,” iwe ni kwa mtumbwi, teksi ya mashambani, au baiskeli, pia utachangia katika “rundo la Mashahidi” ambalo limekuwa likijengwa katika bara la “Mlima wa Mungu.”

[Maelezo ya Chini]

a “Rundo la Mashahidi” yaelekea ndiyo maana ya neno la Kiebrania linalotafsiriwa “Gileadi.” Tangu 1943 shule ya Biblia ya Gileadi imekuwa ikituma wamishonari ili kufungua kazi ya kuhubiri duniani pote, kutia ndani katika Kamerun.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Ramani: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki