Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Kulingana na ripoti za habari, baada ya mtoto mchanga kuzaliwa, hospitali fulani-fulani huhifadhi kondo (plasenta) na kiungamwana (kitovu) ili kuzidua vitu kutoka katika damu yavyo. Je, hilo limhangaishe Mkristo?
Jambo hilo halitendeki katika sehemu nyingi, kwa hiyo Wakristo hawahitaji kuhangaika. Ikiwa kuna sababu za kutosha kuamini kwamba hilo hufanywa katika hospitali ambamo Mkristo atazaa mtoto, ingefaa kumwarifu tabibu tu kwamba kondo na kiungamwana vyapasa kutupiliwa mbali, visitumiwe kwa njia yoyote.
Mazao mbalimbali ya kitiba yamepatikana katika vyanzo vya kibiolojia, ama kutoka kwa wanyama ama kwa binadamu. Kwa kielelezo, homoni fulani zimeziduliwa kutoka katika mkojo wa farasi walio na mimba. Damu ya farasi ilikuwa chanzo cha damaji (umajimaji wenye kinga) ya ugonjwa wa pepo punda, na kwa muda mrefu globulini gama ya kupigana na maradhi imekuwa ikitolewa katika damu ya kondo za kibinadamu (kondo ya nyuma). Kondo zimehifadhiwa na kugandishwa na hospitali fulani-fulani na baadaye kuchukuliwa na maabara ya kutengenezea madawa ili damu iliyojaa fingo iweze kuchakatwa katika maabara ili kuzidua globulini gama.
Majuzi zaidi, watafiti wamedai kuwa na mafanikio katika kutumia damu ya kondo ya nyuma ili kutibu aina moja ya lukemia, na nadharia imetolewa kwamba damu hiyo huenda ikawa na mafaa katika miparaganyo fulani ya mfumo wa kinga au kutumiwa mahali pa miatiko ya mafuta ya mifupa. Kwa sababu hiyo, habari zimeenea kiasi fulani kuhusu wazazi wanaoagiza kwamba damu kutoka kondo ya nyuma iziduliwe, igandishwe, na kuhifadhiwa iwapo yaweza kuwa yenye mafaa katika matibabu ya mtoto wao katika miaka ijayo.
Kutumia damu ya kondo kwa njia hiyo ya kibiashara si jambo linalovutia Wakristo wa kweli, wanaoongoza kufikiri kwao kwa kutumia sheria kamilifu ya Mungu. Muumba wetu huiona damu kuwa takatifu, na yenye kuwakilisha uhai wenye kupewa na Mungu. Njia pekee ya kuitumia damu aliyoruhusu ilikuwa kwenye madhabahu, kuhusiana na dhabihu mbalimbali. (Mambo ya Walawi 17:10-12; linganisha Waroma 3:25; 5:8; Waefeso 1:7.) Kama sivyo, damu iliyotolewa katika kiumbe ilipasa kumwagwa ardhini, itupiliwe mbali.—Mambo ya Walawi 17:13; Kumbukumbu la Torati 12:15, 16.
Wakristo wawindapo mnyama au kuua kuku au nguruwe, wanaitoa damu na kuitupilia mbali. Hawahitaji kuimwaga ardhini kihalisi, kwa maana jambo kuu ni kwamba watupilie mbali damu badala ya kuitumia kwa njia yoyote ile.
Wakristo wanaolazwa hospitalini huelewa kwamba mazao ya kibiolojia yanayoondolewa mwilini mwao yanatupiliwa mbali, mazao hayo yawe ni takataka za mwili, tishu zenye maradhi, au damu. Ni kweli, huenda daktari akataka kwamba upimaji mbalimbali ufanywe kwanza, kama vile uchanganuzi wa mkojo, uchunguzi wa asili ya tishu zenye mtutuko, au upimaji mbalimbali wa damu. Lakini baada ya hapo, mazao hayo yanatupiliwa mbali kulingana na sheria ya mahali fulani. Kwa kawaida, mgonjwa aliyelazwa hospitalini hahitaji kutoa ombi la pekee kuhusu jambo hilo kwa sababu kuondolea mbali mazao hayo ya kibiolojia ni jambo linalofaa na lenye busara kitiba. Ikiwa mgonjwa angekuwa na sababu halali ya kushuku kwamba huenda zoea hilo la kawaida lisifuatwe, yeye angeweza kutaja jambo hilo kwa tabibu anayehusika, akisema kwamba kwa sababu za kidini yeye angetaka mazao yote hayo yatupiliwe mbali.
Hata hivyo, kama ilivyotajwa, mara nyingi hilo si hangaiko kwa mgonjwa wa kawaida kwa sababu katika hospitali nyingi kuhifadhi huko na kutumia tena kondo ya nyuma au mazao mengine ya kibiolojia hata hakufikiriwi, wala si zoea la kawaida.
Ile makala “Acheni Tukirihi Lililo Ovu,” iliyomo katika “Mnara wa Mlinzi” la Januari 1, 1997, ilionekana kukazia fikira upedofilia. Zoea hilo lapasa kufasiliwaje?
Kamusi ya Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary hufasili “upedofilia” kuwa “upotovu wa kingono ambao katika huo watoto ndio vyombo vya ngono vinavyopendwa zaidi.” Sehemu za zoea hilo zinashutumiwa kwenye Kumbukumbu la Torati 23:17, 18. Hapo Mungu alisema dhidi ya kuwa malaya wa hekaluni (“au, ‘shoga,’ mvulana awekwaye kwa sababu za upotovu wa kingono,” NW, kielezi-chini). Mistari hiyo ilikataza pia mtu yeyote asilete “katika nyumba ya BWANA” bei ya “mbwa” (“yamkini mtu azoeaye ngono ya mkunduni; hasa na mvulana,” NW, kielezi-chini). Marejezo hayo ya Kimaandiko na ya kilimwengu yathibitisha kwamba yale ambayo hilo Mnara wa Mlinzi lilizungumzia yalihusu kule kufanywa kwa mtoto kuwa chombo cha kutumiwa vibaya kingono, kutia ndani kufanyiwa mahaba, na mtu mzima.