Aroni
MWANA wa Amramu na Yokebedi wa kabila la Lawi, aliyezaliwa Misri mwaka wa 1597 K.W.K. Lawi alikuwa babaye babu ya Aroni. (Kutoka 6:13, 16-20) Miriamu alikuwa dadaye mkubwa, na Musa alikuwa nduguye mchanga kwa miaka mitatu. (Kutoka 2:1-4; 7:7) Aroni alimwoa Elisheba, binti Aminadabu, na alikuwa na wana wanne, Nadabu, Abihu, Eleazari, na Ithamari. (Kutoka 6:23) Alikufa mwaka wa 1474 K.W.K. alipokuwa na umri wa miaka 123.—Hesabu 33:39.
Kwa sababu ya kusitasita kwa Musa kwa kuwa aliona vigumu kusema kwa ufasaha, Yehova alimpa Aroni mgawo wa kutenda akiwa msemaji wa Musa mbele ya Farao, akisema hivi juu ya Aroni: “Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri.” Aroni alienda kumlaki Musa kwenye Mlima Sinai, akajulishwa matokeo makubwa ya ile programu iliyoonyeshwa kimungu ya hatua iliyohusisha Israeli na Misri, kisha hao ndugu wakasafiri kurudi Misri.—Kutoka 4:14-16, 27-30.
Sasa Aroni alianza kutumikia akiwa “kinywa” cha Musa, akisema kwa ajili yake kwa wanaume wazee wa Israeli na kufanya ishara za kimuujiza zikiwa uthibitisho wa asili ya kimungu ya ujumbe wao mbalimbali. Wakati ulipofika wa kuingia kwao katika ua wa Farao, Aroni mwenye umri wa miaka 83, akiwa msemaji wa Musa, alilazimika kumkabili mtawala yule mwenye kujigamba. Kama vile Yehova alivyomwambia Musa baadaye: “Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni [“Aroni,” NW] atakuwa nabii wako.” (Kutoka 7:1, 7) Aroni ndiye aliyefanya ile ishara ya kimuujiza ya kwanza mbele ya Farao na makuhani wake wafanya-mizungu; na baadaye, Aroni ndiye aliyenyoosha fimbo ya Musa, akaashiria mwanzo wa yale Mapigo Kumi, alipoagizwa na Musa. (Kutoka 7:9-12, 19, 20) Aliendelea kufanya kazi kwa ulinganifu wenye muungano pamoja na Musa kwa kumtii Mungu wakati wa mapigo yaliyofuata, hadi uhuru ulipopatikana hatimaye. Katika hayo alikuwa kielelezo chema kwa Wakristo wanaotumikia wakiwa “mabalozi walio badala ya Kristo, kama kwamba Mungu alikuwa akisihi sana kupitia sisi.”—Kutoka 7:6; 2 Wakorintho 5:20.
Utendaji wa Aroni akiwa msemaji wa Musa waonekana ulififia wakati wa ile miaka 40 ya kuzurura jangwani, kwa kuwa Musa aonekana kuwa alizidi kujisemea. (Kutoka 32:26-30; 34:31-34; 35:1, 4) Ile fimbo ilirudi pia mikononi mwa Musa baada ya pigo la tatu. Na Aroni, pamoja na Huri, walitegemeza tu mikono ya Musa kwenye pigano la Amaleki. (Kutoka 9:23; 17:9, 12) Hata hivyo, Yehova aliendelea kwa ujumla kushirikisha Aroni na Musa alipotoa maagizo, nao wanasemwa kuwa walitenda na kusema pamoja, hadi wakati wa kifo cha Aroni.—Hesabu 20:6-12.
Aroni, katika wadhifa wake wa chini, hakuandamana na Musa hadi kilele cha Mlima Sinai ili kupokea agano la Sheria, lakini, akiwa pamoja na wana wake wawili na 70 kati ya wanaume wazee wa hilo taifa, aliruhusiwa kuukaribia huo mlima na kuona ono tukufu la utukufu wa Mungu. (Kutoka 24:9-15) Aroni na nyumba yake walisifiwa katika agano la Sheria, na Mungu alimteua Aroni kwa ajili ya wadhifa wa kuhani wa cheo cha juu.—Kutoka 28:1-3.
Kwa Nini Aroni Hakuadhibiwa kwa Kosa la Kufanyiza Yule Ndama wa Dhahabu?
Ujapokuwa wadhifa wake wenye pendeleo, Aroni alikuwa na mapungukio. Musa alipokaa juu ya Mlima Sinai siku 40 kwa mara ya kwanza, “watu . . . wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.” (Kutoka 32:1) Aroni alikubali, akashirikiana na waasi hao katika kufanyiza sanamuumbo hiyo ya ndama wa dhahabu. (Kutoka 32:2-6) Alipokabiliwa na Musa baadaye, alitoa udhuru hafifu. (Kutoka 32:22-24) Hata hivyo, Yehova hakumwelekezea yeye kuwa mkosaji mkuu bali alimwambia Musa hivi: “Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize.” (Kutoka 32:10, italiki ni zetu.) Musa alifikisha jambo hilo kwenye mkatao kwa kupaaza kilio hivi: “Mtu awaye yote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu.” (Kutoka 32:26) Wana wote wa Lawi waliitikia, na hilo bila shaka lilitia ndani Aroni. Waabudu-sanamu elfu tatu, yaelekea wachocheaji wakuu wa huo uasi, wakauawa. (Kutoka 32:28) Hata hivyo, baadaye Musa aliwakumbusha watu waliobaki kwamba wao walikuwa na hatia pia. (Kutoka 32:30) Kwa hiyo, si Aroni tu aliyepokea rehema ya Mungu. Matendo yake ya baadaye yalionyesha kwamba hakuunga mkono kwa moyo ile harakati iliyohusisha ibada ya sanamu bali alishindwa tu na msongo wa wale waasi. (Kutoka 32:35) Yehova alionyesha kwamba Aroni alikuwa amepokea msamaha wake kwa kudumisha uhalali wa kuwekwa rasmi kwa Aroni kuwa kuhani wa cheo cha juu.—Kutoka 40:12, 13.
Baada ya kupata kumwunga mkono kwa uaminifu-mshikamanifu ndugu yake mchanga kupitia mambo magumu mengi yaliyoonwa na Musa akiwa mwakilishi wa Mungu, akisha kumtawaza majuzi tu kuwa kuhani wa cheo cha juu, Aroni alijishirikisha kwa upumbavu na dadaye Miriamu katika kumchambua Musa kwa sababu ya ndoa yake pamoja na mwanamke Mkushi na katika kupinga uhusiano na wadhifa wa kipekee wa Musa pamoja na Yehova Mungu, wakisema: “Je! ni kweli BWANA amenena na Musa tu? hakunena na sisi pia?” (Hesabu 12:1, 2) Yehova alichukua hatua upesi, aliwakusanya hao watatu mbele yake mbele ya hema la kukutania, akawakemea kwa nguvu Aroni na Miriamu kwa sababu ya kutostahi yule aliyewekwa rasmi na Mungu. Jambo la kwamba ni Miriamu tu aliyepigwa kwa ukoma huenda likamwonyesha kuwa mchocheaji wa hilo tendo na huenda likaonyesha kwamba Aroni alikuwa ameonyesha udhaifu tena kwa kuvutwa kujiunga naye. Hata hivyo, ikiwa Aroni angalikuwa amepigwa na ukoma jinsi hiyohiyo, hilo lingalibatilisha kuwekwa kwake rasmi kuwa kuhani wa cheo cha juu, kulingana na sheria ya Mungu. (Mambo ya Walawi 21:21-23) Mtazamo wake wa moyo ufaao ulijidhihirisha kwa kuungama kwake mara moja na kuomba radhi kwa upumbavu wa tendo lao na kwa ombi lake lenye maumivu makali la kutaka Musa atoe ombi kwa niaba ya Miriamu mwenye ukoma.—Hesabu 12:10-13.
Aroni alishiriki tena daraka la kukosea wakati yeye, pamoja na Musa, waliposhindwa kumtakasa na kumheshimu Mungu mbele ya kutaniko katika kile kisa kilichohusisha kuandaa maji huko Meriba katika Kadeshi. Kwa tendo hilo Mungu aliamuru kwamba hakuna yeyote kati yao ambaye angefurahia pendeleo la kuliingiza hilo taifa katika Bara la Ahadi.—Hesabu 20:9-13.
Siku ya kwanza ya mwezi wa Abi, katika mwaka wa 40 baada ya kule Kutoka, taifa la Israeli lilikuwa limepiga kambi mpakani pa Edomu mbele ya Mlima Hori. Katika miezi kadhaa wangekuwa wakiuvuka Yordani; lakini si Aroni mwenye umri wa miaka 123. Kwa agizo la Yehova, na kambi yote ikitazama, Aroni, mwanaye Eleazari, na Musa walipanda hadi kilele cha Mlima Hori. Huko Aroni alimruhusu nduguye amvue mavazi yake ya kikuhani na amvike mavazi hayo Eleazari, mwanaye na mwandamizi wake kwenye ukuhani wa cheo cha juu. Kisha Aroni akafa. Yaelekea alizikwa huko na nduguye na mwanaye, na Israeli likaomboleza kifo chake kwa siku 30.—Hesabu 20:24-29.
Yastahili kuonwa kwamba katika kila kimoja cha vile visa vitatu vya kukosea kwake, Aroni haonekani kuwa mchocheaji mkuu wa tendo baya, lakini badala ya hivyo, aonekana kuwa aliruhusu msongo wa hali au uvutano wa watu wengine umshawishi kutoka katika mwendo mnyoofu. Hasa katika kosa lake la kwanza, yeye angaliweza kutumia ile kanuni iliyo msingi wa sheria hii: “Usiandamane na mkutano kutenda uovu.” (Kutoka 23:2) Hata hivyo, baadaye jina lake linatumiwa katika Maandiko kwa njia ya kuheshimika, na Mwana wa Mungu, wakati wa maisha yake ya kidunia, alitambua uhalali wa ukuhani wa Kiaroni.—Zaburi 115:10, 12; 118:3; 133:1, 2; 135:19; Mathayo 5:17-19; 8:4.
Wazao wa Kikuhani wa Aroni
Usemi “Waaroni” umo katika King James Version na Moffatt kwenye 1 Mambo ya Nyakati 12:27; 27:17. (Maandishi ya Kimasora katika Kiebrania hutumia jina Aroni tu. LXX [chapa ya Lagardia, kwenye 1 Nya. 12:27] husema “wana wa Aroni.”) Ni wazi kwamba neno “Aroni” hutumiwa hapa kwa maana ya ujumla, sawa sana na jina Israeli, na huwakilisha nyumba ya Aroni au wazao wake wa kiume waliokuwa wa kabila la Lawi na waliokuwa wakitumikia wakiwa makuhani wakati wa Daudi. (1 Mambo ya Nyakati 6:48-53) Tafsiri ya New World Translation husomeka hivi: “Na Yehoiada alikuwa kiongozi [wa wana] wa Aroni, na pamoja naye walikuwa elfu tatu mia saba” (1 Mambo ya Nyakati 12:27), ikitia maneno “wa wana” katika mabano ili kuonyesha kwamba yametiwa ndani.