Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Biblia huonyesha nini kuhusiana na adhabu ya kifo, kwa wahalifu?
Kwa kueleweka, kila mmoja wetu huenda akawa na hisia zake mwenyewe za kibinafsi juu ya hilo kwa kutegemea mambo aliyoona au hali yake maishani. Hata hivyo, tukiwa Mashahidi wa Yehova twapaswa kujaribu kujipatanisha na mawazo ya Mungu juu ya adhabu ya kifo, huku tukibaki katika hali ya kutokuwamo kwa habari ya misimamo ya kisiasa ambayo wengi huchukua katika suala hili.
Kwa kueleza kihususa, katika Neno lake lililoandikwa, Mungu haonyeshi kwamba adhabu ya kifo ni kosa.
Mapema katika historia ya kibinadamu, Yehova alishiriki mawazo yake juu ya jambo hilo, kama tusomavyo katika Mwanzo sura ya 9. Hilo lilihusisha Noa na familia yake, waliokuwa wazazi wa kale wa familia nzima ya kibinadamu. Baada ya kutoka katika safina, Mungu alisema kwamba wangeweza kula wanyama—yaani, wanyama wangeweza kuuawa, damu yao yote itolewe, na waliwe. Kisha kwenye Mwanzo 9:5, 6, Mungu akasema: “Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.” Kwa hiyo Yehova aliidhinisha adhabu ya kifo kwa habari ya wauaji-kimakusudi.
Mungu aliposhughulika na Israeli wakiwa watu wake, makosa kadhaa mazito dhidi ya sheria ya kimungu yalistahili adhabu ya kifo. Kwenye Hesabu 15:30, twasoma taarifa hii ya kijumla: “Lakini mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo amtukana BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.”
Lakini namna gani baada ya kutaniko la Kikristo kuanzishwa? Twajua kwamba Yehova aliidhinisha serikali za kibinadamu ziweko, naye aliziita mamlaka zilizo kubwa. Kwa kweli, baada ya kuhimiza Wakristo wawe watiifu kwa mamlaka hizo za kiserikali, Biblia husema kwamba hizo hutumika zikiwa “mhudumu wa Mungu kwako kwa faida yako. Lakini ikiwa unafanya lililo baya, uwe katika hofu: kwa maana haichukui upanga bila kusudi; kwa maana hiyo ni mhudumu wa Mungu, mlipiza-kisasi ili kuonyesha hasira ya kisasi juu ya yeye anayezoea kufanya lililo baya.”—Waroma 13:1-4.
Je, hilo lamaanisha kwamba serikali zimeidhinishwa kuua watu wanaofanya makosa mazito? Kutokana na maneno ya 1 Petro 4:15, twalazimika kufikia mkataa wa kwamba, ndivyo ilivyo. Katika fungu hilo la maneno, huyo mtume aliwahimiza sana ndugu zake: “Acheni mmoja wenu asiteseke akiwa muuaji-kimakusudi au mwizi au mtenda-maovu au akiwa mjishughulishaji katika mambo ya watu wengine.” Je, uliona, “acheni mmoja wenu asiteseke akiwa muuaji-kimakusudi”? Petro hakudokeza kwamba serikali hazikuwa na haki ya kumtesa muuaji-kimakusudi kwa sababu ya uhalifu wake. Kinyume cha hilo, alionyesha kwamba muuaji-kimakusudi huenda akapokea kwa kufaa adhabu astahiliyo. Je, hiyo ingetia ndani kuadhibiwa kwa kifo?
Yawezekana. Hilo ni wazi kutokana na maneno ya Paulo yapatikanayo katika Matendo sura ya 25. Wayahudi walikuwa wamemshtaki Paulo kwa makosa dhidi ya Sheria yao. Kwa kumpeleka mfungwa wake, Paulo, kwa gavana Mroma, kamanda wa kijeshi aliripoti, kama ionyeshwavyo kwenye Matendo 23:29: “Nilikuta ameshtakiwa juu ya maswali ya Sheria yao, lakini hajashtakiwa hata jambo moja la kustahili kifo au vifungo.” Baada ya miaka miwili Paulo alijikuta mbele ya Gavana Festo. Twasoma kwenye Matendo 25:8: “Paulo akasema katika kujitetea: ‘Wala dhidi ya Sheria ya Wayahudi wala dhidi ya hekalu wala dhidi ya Kaisari sijafanya dhambi yoyote.’” Lakini sasa kazia fikira kwenye maelezo yake kuhusu adhabu, hata adhabu ya kifo. Twasoma hivi kwenye Matendo 25:10, 11:
“Paulo akasema: ‘Mimi nimesimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ambako napaswa kuhukumiwa. Sijawatendea Wayahudi kosa, kama vile wewe pia unavyogundua vema kabisa. Ikiwa, kwa upande mmoja, mimi ni mkosaji kwa kweli na nimefanya jambo lolote linalostahili kifo, sitoi udhuru nisife; ikiwa, kwa upande mwingine, hakuna hata moja la mambo hayo lililoko ambalo watu hawa wanishtakia, hakuna mtu awezaye kunikabidhi kwao ili kujipendekeza. Mimi nakata rufani kwa Kaisari!’”
Paulo, akisimama mbele ya mamlaka iliyowekwa rasmi, alikiri kwamba Kaisari alikuwa na haki ya kutia adhabu wakosaji, hata kuwaua. Hakupinga adhabu katika kisa chake ikiwa alikuwa na hatia. Zaidi ya hayo, hakusema kwamba Kaisari angeweza kutumia adhabu ya kifo kwa wauaji-kimakusudi pekee.
Ni kweli, mfumo wa kihukumu wa Roma haukuwa mkamilifu; wala mifumo ya mahakama ya kibinadamu leo. Watu fulani wasio na hatia wakati huo na leo wametiwa hatiani na kuadhibiwa. Hata Pilato alisema hivi juu ya Yesu: “Mimi sikupata jambo lolote linalostahili kifo katika yeye; kwa hiyo hakika mimi nitamwadhibu na kumfungua.” Ndiyo, hata ingawa wenye mamlaka ya kiserikali walikubali kwamba Yesu hakuwa na hatia, mtu huyo asiye na hatia aliuawa.—Luka 23:22-25.
Lakini ukosefu huo wa haki haukumsukuma Paulo au Petro kubisha kwamba adhabu ya kifo kwa msingi si ya kiadili. Badala ya hivyo, mawazo ya Mungu juu ya hilo jambo ni kwamba maadamu mamlaka zilizo kubwa za Kaisari ziko, hizo ‘zauchukua upanga ili kuonyesha hasira ya kisasi juu ya hao wanaozoea kufanya lililo baya.’ Hilo latia ndani kutumia upanga katika maana ya kutumia adhabu ya kifo. Lakini inapohusu swali lenye kuzusha ubishi la kama serikali yoyote ya ulimwengu huu yapaswa kuzoea haki yayo ya kuua wauaji-kimakusudi, Wakristo wa kweli hubaki kwa uangalifu katika hali ya kutokuwamo. Tofauti na makasisi wa Jumuiya ya Wakristo, wao hujiondosha katika mjadala wowote unaohusu habari hii.