Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 11/1 kur. 18-22
  • Sehemu ya Mamlaka za Juu Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sehemu ya Mamlaka za Juu Zaidi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wakristo wa Kweli
  • Kuitii Sheria
  • Kitu cha Hofu
  • “Ni Mhudumu wa Mungu”
  • Uhitaji wa Imani
  • Serikali Isiposaidia
  • Maoni ya Mkristo Kuhusu Mamlaka
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Maoni ya Mkristo Juu ya Mamlaka za Juu Zaidi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Ni Mamlaka ya Nani Unayopaswa Kutambua?
    Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele
  • Heshima kwa Mamlaka—Kwa Nini Ni Muhimu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 11/1 kur. 18-22

Sehemu ya Mamlaka za Juu Zaidi

“Ni mhudumu wa Mungu kwako wewe kwa ajili ya mema yako. Lakini ikiwa wewe unafanya lililo baya, uwe katika hofu.”—WARUMI 13:4, NW.

1, 2. Wengi katika Jumuiya ya Wakristo wamehusikaje katika utendaji wa kimapinduzi?

MIAKA miwili iliyopita, kusanyiko moja la maaskofu katika London lilifanya kutokee tahariri yenye ghadhabu katika New York Post. Kusanyiko hilo lilikuwa lile Kongamano la Lambeth, lililohudhuriwa na maaskofu zaidi ya 500 wa ushirika wa Kianglikana. Ghadhabu hiyo ilifyatushwa na azimio lililopitishwa na kongamano hilo juu ya kuwaelewa watu “ambao, baada ya kujaribu kabisa njia nyingine zote, wao huchagua kuifuata njia ya pambano la kutumia silaha kuwa ndiyo njia pekee ya kuleta haki.”

2 Gazeti Post lilisema kwamba hiyo ilikuwa sawa na kuunga mkono uvamizi-haramu. Hata hivyo, maaskofu hao walikuwa wakifuata tu elekeo fulani lenye kuongezeka. Mtazamo wao haukuwa tofauti na ule wa padri Mkatoliki katika Ghana aliyependekeza vita vya magaidi kuwa ndiyo njia iliyo ya haraka zaidi, ya uhakika zaidi, na ya usalama zaidi ya kukomboa Afrika; au wa askofu Mmethodisti Mwafrika aliyenadhiri kuisukuma “vita ya ukombozi hadi kwenye mwisho mchungu”; au wa wamisionari wengi wa Jumuiya ya Wakristo ambao wamepigana na waasi dhidi ya serikali zilizoimarika katika Esia na Amerika Kusini.

Wakristo wa Kweli

‘Hawapingi Mamlaka’

3, 4. (a) Ni kanuni gani zavunjwa na waitwao eti Wakristo ambao huunga mkono mapinduzi? (b) Mtu mmoja aligundua nini juu ya Mashahidi wa Yehova?

3 Katika karne ya kwanza, Yesu alisema juu ya wafuasi wake hivi: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi nisivyo sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:14, NW) Yeyote aitwaye eti Mkristo ambaye huunga mkono mapinduzi yuko sana sehemu ya ulimwengu. Yeye si mfuasi wa Yesu; wala ‘hatii mamlaka za juu zaidi.’ (Warumi 13:1, NW) Ingekuwa vema atii onyo la mtume Paulo kwamba “yeye ambaye hupinga mamlaka amechukua msimamo dhidi ya mpango wa Mungu; wale ambao wamechukua msimamo dhidi yayo watapokea hukumu kwao wenyewe.”—Warumi 13:2, NW.

4 Kwa utofautisho na wengi katika Jumuiya ya Wakristo, Mashahidi wa Yehova hawashughuliki na jeuri ya kutumia silaha. Mwanamume mmoja katika Ulaya aligundua hilo. Aandika hivi: “Kwa kuona matokeo ya dini na siasa, nilijitoa kuupindua utaratibu wa kijamii uliothibitika. Nilijiunga na kikundi cha wavamizi-haramu nikapokea mazoezi katika kushughulika na namna zote za silaha; nilishiriki katika visa vingi vya unyang’anyi wa kutumia silaha. Maisha yangu yalikuwa katika hatari daima. Kadiri wakati ulivyopita, ilionekana wazi kwamba tulikuwa tukipigana bure tu. Mimi nilikuwa mwanamume aliyevurugika fikira, aliye hoi kabisa kwa kukosa tumaini katika maisha. Ndipo Shahidi mmoja wa kike akabisha mlango wetu. Aliniambia juu ya Ufalme wa Mungu. Kwa kusisitiza kwamba kulikuwa ni kupoteza wakati wangu, nikadokeza kwamba mke wangu asikilize. Alifanya hivyo, na funzo la nyumbani la Biblia likaanzwa. Mwishowe, niliafiki kuhudhuria funzo hilo. Nashindwa kupata maneno ya kueleza kitulizo nilichohisi kwa kuielewa kani yenye kushurutisha ainabinadamu kuelekea uovu. Ahadi nzuri sana ya Ufalme imenipa tumaini lenye utegemezo na kusudi katika maisha.”

5. Kwa nini Wakristo hubaki wakizitii kiamani mamlaka za juu zaidi za kilimwengu, na itakuwa hivyo mpaka lini?

5 Wakristo ni mabalozi au wajumbe wa Mungu na wa Kristo. (Isaya 61:1, 2; 2 Wakorintho 5:20; Waefeso 6:19, 20) Wakiwa hivyo, wao hubaki kwa kutokuwamo katika mahitilafiano ya ulimwengu huu. Hata ingawa mifumo fulani ya kisiasa huonekana kuwa na mafanikio ya kiuchumi kuliko mingine, na baadhi yayo huruhusu uhuru mwingi kuliko mingine, Wakristo hawaungi mkono wala kutaja mfumo mmoja kuwa bora kuliko mwingine. Wao wajua kwamba mifumo yote si mikamilifu. Ni “mpango wa Mungu” kwamba iendelee kuwako mpaka Ufalme wake uipokonye mamlaka. (Danieli 2:44) Kwa sababu hiyo, Wakristo hubaki kwa amani wakitii mamlaka za juu zaidi huku wakisaidia kuleta hali njema ya milele ya wengine kwa kuhubiri habari njema za Ufalme.—Mathayo 24:14; 1 Petro 3:11, 12.

Kuitii Sheria

6. Kwa nini sheria nyingi za kibinadamu ni njema hata ingawa “ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu”?

6 Serikali za kitaifa huweka mifumo ya sheria, na zilizo nyingi za sheria hizi ni njema. Je! hilo litushangaze, kwa sababu ya uhakika wa kwamba “ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu”? (1 Yohana 5:19, HNWW) Sivyo. Yehova alimpa baba yetu wa awali, Adamu, dhamiri, na hisi hii ya kindani ya yafaayo na yenye makosa huonyeshwa kwa njia nyingi katika sheria za kibinadamu. (Warumi 2:13-16) Hammurabi, mpaji-sheria wa kale Mbabulonia, alitoa dibaji ya fungu la sheria zake kama ifuatavyo: “Wakati huo [wao wali-]nitaja mimi ili nisaidie kukuza hali njema ya watu, mimi, Hammurabi, yule mwana-mfalme mwenye ujitoaji, mwenye kuhofu mungu, ili kusababisha haki idumu katika bara, ili kuharibu waovu na uovu, kwamba walio imara wasiweze kuonea walio dhaifu.”

7. Mtu fulani akivunja sheria, nani ana haki ya kumwadhibu, na kwa nini?

7 Serikali zilizo nyingi zingesema kwamba kusudi la sheria zazo ni kama hilo: kusaidia kukuza hali njema ya raia na utaratibu mzuri katika jamii ya watu. Kwa sababu hiyo, hizo hutoa adhabu kwa vitendo vyenye kuharibu hali ya kijamii, kama vile uuaji na wizi, na huweka virekebi, kama mipaka ya kuendesha kasi na sheria za kuegesha magari. Wowote wavunjao sheria zao kimakusudi huchukua msimamo dhidi ya mamlaka nao “watapokea hukumu kwao wenyewe.” Hukumu kutoka kwa nani? Si lazima iwe kutoka kwa Mungu. Neno la Kigiriki lililotafsiriwa hukumu hapa laweza kurejezea taratibu za kiserikali kuliko hukumu zenye kufanywa na Yehova. (Linganisha 1 Wakorintho 6:7.) Ikiwa mtu yeyote atenda kwa njia isiyo ya kisheria, mamlaka ya juu zaidi ina haki ya kumwadhibu.

8. Kundi litaitikiaje mshiriki akitenda uhalifu mzito?

8 Mashahidi wa Yehova wana sifa njema kwa kutopinga mamlaka za kibinadamu. Ikitendeka kwamba mtu fulani mmoja katika kundi aivunja sheria, kundi halitamsaidia kuepuka adhabu ya kisheria. Mtu yeyote akiiba, kuua, kukashifu, kudanganya juu ya kodi zake, kunajisi, kupunja, kutumia dawa za kulevya zilizo haramu, au kwa njia nyingine yoyote kupinga mamlaka ya kisheria, atakabili nidhamu kali kutoka kwenye kundi—naye hapaswi kuhisi anyanyaswa wakati aadhibiwapo na mamlaka ya kilimwengu.—1 Wakorintho 5:12, 13; 1 Petro 2:13-17, 20.

Kitu cha Hofu

9. Wakristo wana mahali gani pa kutafuta msaada wakitishwa na visehemu visivyofuata sheria?

9 Paulo aendelea na mazungumzo yake juu ya mamlaka za juu zaidi, akisema: “Kwa maana wale wanaotawala ni kitu cha hofu, si kwa kitendo chema, bali kwa kibaya. Je! wewe, basi, wataka usiwe na hofu ya mamlaka? Endelea kufanya mema, na wewe utakuwa na sifa kutoka kwayo.” (Warumi 13:3, NW) Si Wakristo waaminifu-washikamanifu wapaswao kuhofu adhabu kutoka kwenye mamlaka bali ni watenda makosa, wale watendao ‘vitendo vibaya,’ vitendo vya uhalifu. Watishwapo na visehemu hivyo vyenye kuvunja sheria, kwa kufaa Mashahidi wa Yehova waweza kukubali ulinzi wa polisi au wa kijeshi kutoka kwenye mamlaka.—Matendo 23:12-22.

10. Ni jinsi gani Mashahidi wa Yehova ‘wamepokea sifa’ kutoka kwa mamlaka?

10 Kwa Mkristo ashikaye sheria ya mamlaka ya juu zaidi, Paulo asema hivi: “Utakuwa na sifa kutoka kwayo.” Kama kielelezo cha jambo hilo, fikiria barua fulani zilizopokewa na Mashahidi wa Yehova katika Brazili baada ya mikusanyiko ya wilaya yao. Kutoka kwa chansela wa idara ya michezo ya manispaa: “Sifa ya juu zaidi yastahiliwa kwa mwenendo wenu wenye amani. Inafariji katika ulimwengu wa leo wenye msukosuko kujua kwamba watu wengi sana bado huamini katika Mungu na ku-mwabudu.” Kutoka kwa mkurugenzi wa stediamu ya manispaa: “Kujapokuwa na hesabu kubwa sana ya wenye kuhudhuria, hakuna kituko kilichorekodiwa kuharibu sifa ya tukio hilo, asante kwa ule utengenezo usio na dosari.” Kutoka kwenye ofisi ya meya: “Twataka kuchukua fursa hii kuwapongeza nyinyi juu ya utaratibu wenu na nidhamu nzuri sana mwifuatayo kwa kujipendea wenyewe, nasi twawatakia kila fanikio katika matukio ya wakati ujao.”

11. Kwa nini kuhubiriwa kwa habari njema hakuwezi kwa njia yoyote kusemwa kuwa ni kitendo kibaya?

11 Mtajo huu “kitendo chema” warejezea vitendo vya kutii sheria za mamlaka za juu zaidi. Kwa kuongezea, kazi yetu ya kuhubiri, ambayo huamriwa na Mungu, si binadamu, si kitendo kibaya—jambo ambalo mamlaka za kisiasa zapaswa kutambua. Ni utumishi wa peupe ambao huinua uthabiti wa kiadili wa wale waitikiao. Kwa hiyo, ni tumaini letu kwamba mamlaka za juu zaidi zitalinda haki yetu kuhubiria wengine. Paulo aliomba rufani kwa wenye mamlaka ili athibitishe kisheria kuhubiriwa kwa habari njema. (Matendo 16:35-40; 25:8-12; Wafilipi 1:7) Hivi majuzi, Mashahidi wa Yehova pia wametafuta na kupata utambuzi wa kisheria wa kazi yao katika Ujeremani Mashariki, Hangari, Polandi, Romania, Benin, na Myanmar (Burma).

“Ni Mhudumu wa Mungu”

12-14. Mamlaka za juu zaidi zimetendaje zikiwa mhudumu wa Mungu (a) katika nyakati za Biblia? (b) katika nyakati za ki-siku-hizi?

12 Akiongea juu ya mamlaka ya kilimwengu, Paulo aendelea kusema hivi: “Hiyo ni mhudumu wa Mungu kwako wewe kwa ajili ya mema yako. Lakini ikiwa wewe unafanya lililo baya, uwe katika hofu: kwa maana si bila kusudi kwamba hiyo hubeba upanga; kwa maana yenyewe ni mhudumu wa Mungu, mlipiza kisasi ili kuonyesha hasira-jeuri juu ya mmoja ambaye anazoea lililo baya.”—Warumi 13:4, NW.

13 Nyakati fulani mamlaka za kitaifa zimetumikia zikiwa mhudumu wa Mungu kwa njia zilizo hususa. Sairasi alifanya hivyo alipowaagiza Wayahudi warudi kutoka Babuloni wajenge upya nyumba ya Mungu. (Ezra 1:1-4; Isaya 44:28) Artazakse alikuwa mhudumu wa Mungu alipotuma Ezra akiwa na mchango wa kuijenga upya nyumba hiyo na baadaye alipompa Nehemia utume wa kujenga upya kuta za Yerusalemu. (Ezra 7:11-26; 8:25-30; Nehemia 2:1-8) Mamlaka ya juu zaidi ya Kiroma ilitumikia hivyo ilipomkomboa Paulo kutoka kwenye umati wenye ghasia katika Yerusalemu, ilipomlinda wakati wa kuvunjikiwa meli, na ilipompangia kuwa na nyumba yake mwenyewe katika Roma.—Matendo 21:31, 32; 28:7-10, 30, 31.

14 Vivyo hivyo, mamlaka za kilimwengu zimetumikia zikiwa mhudumu wa Mungu nyakati za ki-siku-hizi. Kwa kielelezo, katika 1959 Mahakama Kuu ya Kanada ilikata kauli kwamba mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliyeshtakiwa katika Quebec juu ya kuchapisha kashifa za kufitini serikali na kuiharibia jina hakuwa na hatia—kwa njia hiyo ikazuia maoni ya ubaguzi ya waziri mkuu wa wakati huo wa Quebec, Maurice Duplessis.

15. Ni kwa njia gani ya ujumla wenye mamlaka hutenda kama mhudumu wa Mungu, na hiyo yawapa haki gani?

15 Zaidi ya hilo, kwa ujumla, serikali za kitaifa hutumikia kama mhudumu wa Mungu kwa kuhifadhi utaratibu wa umma mpaka Ufalme wa Mungu utakapopokonya daraka hilo. Kulingana na Paulo, ni kwa lengo hilo kwamba mamlaka “hubeba upanga,” ukifananisha haki yayo ya kutoa adhabu. Kwa kawaida, hiyo yahusisha kifungo gerezani au faini. Katika mabara fulani yaweza pia kuhusisha adhabu ya kifo.a Kwa upande mwingine, mataifa mengi yamechagua kutokuwa na adhabu ya kifo, na hiyo pia ni haki yao.

16. (a) Kwa kuwa mamlaka ni mhudumu wa Mungu, baadhi ya watumishi wa Mungu wamefikiria yafaa kufanya nini? (b) Ni kazi ya aina gani ambayo Mkristo hangekubali, na kwa nini asiikubali?

16 Uhakika wa kwamba mamlaka za juu zaidi ni mhudumu wa Mungu waeleza kwa nini Danieli, wale Waebrania watatu, Nehemia, na Mordekai waliweza kukubali vyeo vya madaraka katika serikali za Kibabuloni na Kiajemi. Hivyo wangeweza kusihi mamlaka ya Serikali kwa manufaa ya watu wa Mungu. (Nehemia 1:11; Esta 10:3; Danieli 2:48, 49; 6:1, 2) Leo Wakristo fulani hufanya kazi pia katika utumishi wa serikali. Lakini kwa kuwa wao wamejitenga na ulimwengu, hawajiungi na vyama vya kisiasa, hawatafuti cheo cha kisiasa, wala hawakubali vyeo vya kufanya sera za kufuatwa katika matengenezo ya kisiasa.

Uhitaji wa Imani

17. Ni hali gani huenda zikachochea watu fulani wasio Wakristo kukinza mamlaka?

17 Ingawa hivyo, namna gani ikiwa mamlaka huvumilia ufisadi au hata uonevu bila kuchukua hatua? Je! Wakristo wapaswa kujaribu kubadili mamlaka hiyo kwa moja ionekanayo kuwa bora? Hapo, ukosefu wa haki na ufisadi wa kiserikali si jambo jipya. Katika karne ya kwanza, Milki ya Kiroma ilikubalia mambo yasiyo haki kama vile utumwa. Pia ilivumilia maofisa wafisadi bila kuchukua hatua. Biblia husema juu ya watoza kodi waliofanya udanganyifu, hakimu asiye mwadilifu, na gavana wa mkoa aliyetafuta mahongo.—Luka 3:12, 13; 18:2-5; Matendo 24:26, 27.

18, 19. (a) Wakristo huitikiaje ikiwa kuna dhuluma au ufisadi kwa upande wa maofisa wa serikali? (b) Wakristo wameletaje maendeleo katika maisha za watu mmoja mmoja, kama ionyeshwavyo na mwanahistoria mmoja na sanduku lililo chini?

18 Wakristo wangaliweza kujaribu kukomesha dhuluma hizo wakati huo, lakini hawakufanya hivyo. Kwa kielelezo, Paulo hakuhubiri mwisho wa utumwa, na hakuambia Wakristo wenye watumwa waachilie watumwa wao. Bali, alishauri watumwa na wenye watumwa waonyeshe huruma ya Kikristo wanaposhughulikiana. (1 Wakorintho 7:20-24; Waefeso 6:1-9; Filemoni 10-16; ona pia 1 Petro 2:18.) Vivyo hivyo, Wakristo hawakuhusika katika utendaji wa kimapinduzi. Walikuwa wenye shughuli mno wakihubiri “habari njema ya amani.” (Matendo 10:36) Katika 66 W.K., jeshi la Kiroma lilizingira Yerusalemu halafu likaondoka. Badala ya kukaa pamoja na watetezi waasi wa jiji hilo, Waebrania Wakristo ‘walikimbilia milimani’ kwa kutii mwelekezo wa Yesu.—Luka 21:20, 21.

19 Wakristo wa mapema waliishi kwa kujiendesha kulingana na vile mambo yalivyokuwa na kujaribu kuleta nafuu katika maisha za watu mmoja mmoja kwa kuwasaidia wafuate kanuni za Biblia. Mwanahistoria John Lord, katika kitabu chake The Old Roman World, aliandika hivi: “Shangwe za mafanikio ya kweli ya Ukristo zilionekana katika kufanya wale waliodai kufuata mafundisho yao wawe watu wema, wala si katika kubadili mashirika yaliyoonekana kwa nje kuwa maarufu, wala serikali, wala sheria.” Je! Wakristo leo wapaswa kutenda tofauti na hivyo?

Serikali Isiposaidia

20, 21. (a) Mamlaka moja ya kilimwengu ilishindwaje kutenda kama mhudumu wa Mungu kwa ajili ya mema? (b) Mashahidi wa Yehova wapaswa kuitikiaje wanyanyaswapo kwa ukubalio wa Serikali?

20 Katika Septemba 1972, mnyanyaso mkali sana ulifoka dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika nchi moja ya Afrika ya kati. Maelfu walinyang’anywa mali zao zote na kutendwa mambo mengine ya ukatili, kutia na mapigo, kuteswateswa, na kuuawa. Je! mamlaka ya juu zaidi ilitimiza wajibu wayo wa kuwalinda Mashahidi? Sivyo! Bali, ilitia moyo jeuri, ikilazimisha Wakristo hawa wasio na madhara wakimbilie mabara jirani kwa ajili ya usalama.

21 Je! Mashahidi wa Yehova hawapaswi kuinuka kwa kasirani dhidi ya watesi kama hao? Sivyo. Wakristo wapaswa kuvumilia mitwezo hiyo, wakitenda kwa unyenyekevu kwa kumwiga Yesu: “Alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.” (1 Petro 2:23) Wao hukumbuka kwamba Yesu alipokamatwa katika bustani ya Gethsemane, alikemea mwanafunzi aliyekuja kumtetea kwa upanga, na baadaye akamwambia Pontio Pilato hivi: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.”—Yohana 18:36; Mathayo 26:52; Luka 22:50, 51.

22. Ni kielelezo gani kizuri ambacho Mashahidi fulani katika Afrika waliweka walipopata mnyanyaso mkali?

22 Kwa kufikiria kielelezo cha Yesu, Mashahidi hao Waafrika walikuwa na moyo mkuu wa kufuata shauri la Paulo: “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana [Yehova, NW].” (Warumi 12:17-19; linganisha Waebrania 10:32-34.) Ndugu zetu Waafrika ni kielelezo chenye kutuchochea kama nini sisi sote leo! Hata wakati mamlaka ikataapo kutenda kwa njia yenye kuheshimika, Wakristo wa kweli hawaachi kanuni za Biblia.

23. Ni maswali gani yabaki kuzungumzwa?

23 Ingawa hivyo, mamlaka za juu zaidi zaweza kutarajia nini kutoka kwa Wakristo? Na je! kuna mipaka yoyote kwa madai ambayo zaweza kufanya kihaki? Hili litazungumzwa katika makala inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

a Fungu la Sheria lililotolewa kwa njia ya kimungu katika Israeli ya kale lilihusisha adhabu ya kifo kwa vitendo vibaya sana vya uhalifu.—Kutoka 31:14; Walawi 18:29; 20:2-6; Hesabu 35:30.

Je! Wewe Waweza Kueleza?

◻ Ni nini baadhi ya njia ambazo mtu aweza ‘kuchukua msimamo dhidi ya’ mamlaka za juu zaidi?

◻ Ni nini “mpango wa Mungu” kwa habari ya mamlaka ya kiserikali?

◻ Ni kwa njia gani mamlaka ni “kitu cha hofu”?

◻ Serikali za kibinadamu hutumikiaje kama “mhudumu wa Mungu”?

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Barua Kutoka kwa Mkuu wa Polisi

BARUA yenye chapa ya “Utumishi wa Umma kwa Mkoa wa Minas Gerais” ilikuja kwenye ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Brazili. Ilitoka kwa mkuu wa polisi wa mji wa Conquista. Je! kulikuwa na kasoro fulani? Acha barua hiyo ieleze. Yataarifu hivi:

“Kwako Bwana:

“Ni furaha kujijulisha kwako kwa njia ya barua hii. Mimi nimekuwa mkuu wa polisi katika mji wa Conquista, Minas Gerais, kwa miaka yapata mitatu. Kazini, sikuzote mimi hujaribu kuwa na bidii ya kudhamiria mambo, lakini nilikuwa nikipata matatizo ya kuendeleza amani katika jela. Wafungwa humo, ingawa walipewa mazoezi ya kazi fulani-fulani, walikuwa wenye msukosuko.

“Miezi kadhaa iliyopita, Senhor [Bwana] O——alikuja kwenye mji wetu na kujijulisha kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alianza kuhubiri Biblia kwa baadhi ya wafungwa gereza, akiwafundisha kusoma na kuandika na kuwaonyesha mambo ya msingi ya kujali afya na stadi za kijamii na pia kuwaambia juu ya Biblia Takatifu. Jinsi mhubiri huyu alivyofanya kazi ilionyesha kujitoa, upendo, na kujidhabihu. Muda si muda mwenendo wa wafungwa humo ukabadilika kuwa bora kwa njia yenye kuonekana wazi, watazamaji wakashangaa na kuthamini sana.

“Kwa sababu ya lililotendeka katika jela yetu, mimi nataka kuiarifu rasmi Watch Tower Bible and Tract Society juu ya uthamini wetu kwa kazi nzuri iliyofanywa katika jumuiya yetu na mhubiri huyu mwenye ustahili.”

Kuhusu mamlaka ya kiserikali, mtume Paulo alisema: “Endelea kufanya mema, na wewe utakuwa na sifa kutoka kwayo.” (Warumi 13:3, NW) Hakika hilo lilikuwa kweli katika kisa kilicho juu. Huo ni ushuhuda ulioje wa nguvu za kubadili umbo za Neno la Mungu kuonyesha kwamba habari njema zilitimiza kwa muda wa miezi kadhaa tu jambo ambalo mfumo wa kutia adhabu haukuliweza kwa muda wa miaka!—Zaburi 19:7-9.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki