Uamuzi Unaotegemeza Haki ya Mgonjwa ya Kuchagua Matibabu
HAKUNA yeyote isipokuwa Mwenye adhama zaidi ulimwenguni pote ategemezaye haki ya kuchagua baada ya kuarifiwa. Yeye ndiye Muumba wetu. Kwa kuwa ana ujuzi mwingi juu ya mahitaji ya mwanadamu, yeye hutoa kwa ukarimu maagizo, maonyo, na mwongozo juu ya mwendo wa hekima wa kufuata. Hata hivyo, hapuuzi hiari aliyowapa viumbe wake wenye akili. Nabii wake Musa alidhihirisha mtazamo wa Mungu aliposema hivi: “Nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.”—Kumbukumbu la Torati 30:19.
Kanuni hii yahusu matibabu. Ile dhana ya kuchagua matibabu baada ya kuarifiwa, au kutoa idhini baada ya kuarifiwa, yaendelea kupata kibali hatua kwa hatua katika Japani na nchi nyinginezo ambapo awali haikujulikana sana. Dakt. Michitaro Nakamura alitoa elezo hili juu ya idhini baada ya kuarifiwa: “Ni wazo la kwamba daktari amweleza mgonjwa kwa lugha inayoeleweka kwa urahisi juu ya ugonjwa wake, athari zake, na njia za matibabu, na uwezekano wa athari zozote, akistahi haki ya mgonjwa ya kujiamulia mwenyewe juu ya njia ya matibabu.”—Japan Medical Journal.
Kwa miaka mingi, madaktari katika Japani wametoa sababu mbalimbali za kupinga njia hii ya kutibu wagonjwa, na mahakama zimeonyesha mwelekeo wa kuiachia jukumu hilo desturi za kitiba. Hivyo, badiliko kubwa lilitokea Februari 9, 1998, Hakimu Mkuu Takeo Inaba wa Mahakama Kuu ya Tokyo alipotoa uamuzi juu ya uchaguzi wa baada ya kuarifiwa. Ni uamuzi gani uliotolewa, na ni suala gani lililofanya kesi hiyo ipelekwe mahakamani?
Nyuma huko mwezi wa Julai 1992, Misae Takeda mwenye umri wa miaka 63, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alienda kwenye Taasisi ya Hospitali ya Sayansi ya Kitiba ya Chuo Kikuu cha Tokyo. Uchunguzi ulionyesha alikuwa na uvimbe wenye kufisha kwenye ini naye alihitaji kufanyiwa upasuaji. Akitaka sana kutii amri ya Biblia inayokataza utumizi mbaya wa damu, aliwaelewesha matabibu wake waziwazi tamaa yake ya kupata matibabu yasiyohusisha damu. (Mwanzo 9:3, 4; Matendo 15:29) Madaktari walikubali fomu ya ondoleo la hatia, ambayo iliwaweka huru pamoja na hospitali kutokana na wajibu wowote unaotokezwa na uamuzi wake. Walimhakikishia kwamba wangeshikamana na ombi lake.
Hata hivyo, baada ya upasuaji, Misae akiathiriwa bado na madawa, alitiwa damu mishipani—kinyume kabisa na mapenzi yake yaliyoeleweshwa waziwazi. Jitihada za kuufanya utiaji-damu mishipani huo uwe siri zilifichuliwa, mfanyakazi wa hospitali alipomfunulia mwandishi wa habari siri hiyo. Kwa wazi, mwanamke huyo Mkristo mwenye moyo mweupe alivunjwa moyo sana alipojua kwamba alitiwa damu mishipani bila idhini yake. Aliwatumaini wafanyakazi wa kitiba, akiamini kwamba hawangevunja maagano na wangestahi masadikisho yake ya kidini. Kwa sababu ya maumivu makali ya kihisia-moyo aliyopata kutokana na mkiuko huo mbaya wa uhusiano kati ya daktari na mgonjwa na akinuia kuwaepusha wengine wasitendwe vibaya kitiba jinsi hiyo, alilipeleka jambo hilo mahakamani.
Utengamano wa Umma na Maadili
Mahakimu watatu wa Mahakama ya Wilaya ya Tokyo waliisikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi uliowapendelea matabibu na hivyo, uamuzi huo ulipinga haki ya mgonjwa kutoa idhini baada ya kuarifiwa. Katika uamuzi wao uliotolewa Machi 12, 1997, walitaarifu kwamba jitihada zozote za kufanya mkataba wa matibabu yasiyotumia damu haukuwa halali hata kidogo. Kusababu kwao kulikuwa kwamba ingekuwa mkiuko wa kojo ryozoku,a au viwango vya kijamii, kwa tabibu kufanya mapatano ya pekee ya kutotumia damu hata ikiwa hali ya dharura ingetokea. Maoni yao yalikuwa kwamba wajibu mkubwa wa tabibu ni kuokoa uhai katika njia bora zaidi awezayo, hivyo, mkataba huo haungekuwa halali kutoka mwanzoni, haidhuru masadikisho ya kidini ya mgonjwa. Waliamua kwamba, mwishowe maoni ya kitaaluma ya tabibu yapaswa kutangulizwa mbele ya maombi yoyote ya awali ambayo huenda mgonjwa akatoa.
Isitoshe, mahakimu walitaarifu kwamba kwa sababu izo hizo, huku wakitarajiwa waeleze utaratibu wa msingi, athari, na hatari za upasuaji uliopendekezwa, tabibu “angeweza kutosema iwapo anakusudia kutumia damu au la.” Waliamua hivi: “Haiwezi kuamuliwa kuwa kinyume cha sheria au kutofaa kwamba matabibu wakiwa Washtakiwa walielewa makusudio ya Mleta-Mashtaka ya kutokubali kutiwa damu mishipani chini ya hali zozote na walitenda kana kwamba wangestahi makusudio yake na hivyo hilo likamfanya akubali kufanyiwa upasuaji huo.” Walionelea kwamba iwapo matabibu wangelitenda vingine, mgonjwa angeliweza kukataa upasuaji na kuondoka hospitalini.
Uamuzi huo wa mahakama uliwashtua na kuwafadhaisha watetezi wa idhini ya baada ya kuarifiwa. Akizungumza juu ya uamuzi wa kesi hiyo ya Takeda na jinsi ingeathiri idhini ya baada ya kuarifiwa huko Japani, Profesa Takao Yamada, ajuaye sana sheria za madai, aliandika hivi: “Iwapo kusababu kwa uamuzi huo kwadumu kukiwa halali, kukataa kutiwa damu mishipani na ile kanuni ya kisheria ya kutoa idhini baada ya kuarifiwa itatokomea.” (Jarida la kisheria Hogaku Kyoshitsu) Alilaani kwa maneno makali kulazimisha utiaji-damu mishipani na kusema kulikuwa “ukiukaji mkubwa wa kutumainika, sawa na shambulizi la kunyemelea.” Profesa Yamada aliongeza kwamba matendo ya jinsi hiyo ya kuvunja kutumainika “hayapaswi kuruhusiwa kamwe.”
Hali ya upole ya Misae ilifanya iwe vigumu kwake kujulikana. Lakini kwa kuwa alitambua kwamba angeweza kutimiza fungu fulani katika kutetea jina la Yehova na viwango vya uadilifu kuhusiana na utakatifu wa damu, aliazimia kufanya sehemu yake. Aliandikia wakili wake hivi: “Mimi ni mavumbi tu, hata duni kuliko mavumbi. Sijui ni kwa nini mtu hafifu kama mimi natumiwa. Lakini nijitahidipo kufanya mambo ambayo Yehova—yeye awezaye kufanya mawe yapaaze kilio—husema, atanitia nguvu.” (Mathayo 10:18; Luka 19:40) Akiwa kizimbani wakati wa kesi, alifafanua kwa sauti yenye kutetema ile vurugu ya kihisia-moyo aliyopata kutokana na kusalitiwa. “Nilihisi kama mwanamke aliyebakwa.” Ushahidi wake ulifanya wengi waliokuwa mahakamani siku hiyo watoe machozi.
Kitia-Moyo Ambacho Hakikutarajiwa
Kwa sababu ya uamuzi wa Mahakama ya Wilaya, kesi hiyo ilikatiwa rufani kwenye Mahakama Kuu mara moja. Kesi kwenye mahakama ya kukata rufani ilianza kusikilizwa Julai 1997, na Misae aliyeonekana hafifu lakini mwenye kuazimia alikuwapo akiwa kwenye kiti chenye magurudumu. Kansa ilikuwa imejitokeza tena, naye alikuwa akidhoofika. Misae alichochewa sana hakimu mkuu alipoeleza hatua isiyo ya kawaida ambayo mahakama ilinuia kuchukua. Alielewesha wazi kwamba mahakama ya kukata rufani haikukubaliana na uamuzi wa mahakama ndogo—kwamba tabibu alikuwa na haki kupuuza mapenzi ya mgonjwa, kutenda kana kwamba angekubali lakini akiazimia kwa siri kufanya jambo jingine. Hakimu mkuu alisema kwamba mahakama haingeunga mkono yale maadili ya kutawala watu kama watoto ya “Shirashimu bekarazu, yorashimu besh,”b yaani, “Wafanyeni wajinga na wenye kutegemea” wataalamu wa kitiba. Misae alisema hivi baadaye: “Ninafurahi kusikia maelezo yasiyopendelea ya hakimu, yaliyo tofauti sana na uamuzi uliotolewa awali na Mahakama ya Wilaya.” Aliendelea kusema hivi: “Hili ndilo nimekuwa nikimwomba Yehova.”
Mwezi uliofuata Misae akafa, akiwa amezungukwa na familia yenye upendo na wafanyakazi wa hospitali nyingine, iliyoelewa na kustahi masadikisho yake. Ijapokuwa mwanaye Misami na washiriki wengine wa familia walihuzunishwa sana na kifo chake, waliazimia kuendelea na kesi hiyo hadi mwisho, kulingana na mapenzi ya Misae.
Uamuzi
Hatimaye, Februari 9, 1998, mahakimu watatu wa Mahakama Kuu walitoa uamuzi wao, wakibatilisha uamuzi wa mahakama ndogo. Chumba hicho kidogo cha hukumu kilijawa na waandishi wa habari, wanataaluma, na wengine waliofuatilia kesi hiyo kwa uaminifu. Magazeti ya habari na vituo vikubwa vya televisheni viliripoti uamuzi huo. Vichwa vikuu fulani vya magazeti vilisema hivi: “Mahakama: Wagonjwa Waweza Kukataa Matibabu”; “Mahakama Kuu: Utiaji-Damu Mishipani Ni Mkiuko wa Haki za Mtu”; “Daktari Aliyemtia Mgonjwa Damu Mishipani kwa Nguvu Ashindwa Mahakamani”; na “Shahidi wa Yehova Alipwa Ridhaa kwa Ajili ya Kutiwa Damu Mishipani.”
Ripoti juu ya uamuzi huo zilikuwa sahihi na zenye kufaa sana. Gazeti la habari The Daily Yomiuri liliripoti hivi: “Hakimu Takeo Inaba alisema haikufaa madaktari kufuata taratibu alizokataa mgonjwa.” Pia, lilitaarifu waziwazi hivi: “Madaktari waliotia [damu mishipani] walimnyima fursa ya kuchagua matibabu yake.”
Gazeti la habari la Asahi Shimbun lilitaja kwamba ijapokuwa kwenye kesi hii mahakama ilihisi hakukuwa na ushahidi wa kutosha kwamba kulikuwa na mapatano ambapo vikundi viwili vilivyohusika vilikubaliana kwamba damu isingetumiwa hata katika hali zenye kuhatarisha uhai, mahakimu hawakukubaliana na mahakama ndogo juu ya uhalali wa mkataba huo: “Iwapo kuna mapatano yaliyo wazi kati ya vikundi vinavyohusika kwamba damu isitiwe mishipani chini ya hali zozote, Mahakama hii hailioni hilo kuwa kinyume cha utengamano wa umma, na hivyo basi, kuwa usio halali.” Isitoshe, gazeti hilo la habari lilieleza maoni ya mahakimu hao kwamba “kila binadamu atakufa siku fulani, na hatua ielekeayo kwenye wakati huo wa kifo yaweza kuamuliwa na mtu mwenyewe.”
Kwa kweli, Mashahidi wa Yehova wamechunguza jambo hilo na wanasadiki kwamba wanachagua njia bora zaidi ya kuishi. Hilo hutia ndani kukataa hatari zijulikanazo za utiaji-damu mishipani na badala yake kukubali taratibu nyingine zisizotumia damu zitumiwazo sana katika nchi nyingi, na zinazopatana na viwango vya sheria ya Mungu. (Matendo 21:25) Profesa Mjapani wa sheria za kikatiba ajulikanaye sana alitaja hivi: “Kwa uhalisi, kukataa tiba inayozungumziwa [ya utiaji-damu mishipani] hakuhusu chaguo la ‘namna ya kufa,’ bali, la namna ya kuishi.”
Uamuzi wa Mahakama Kuu wapaswa kuwatahadharisha matabibu kwamba haki zao za kutumia utambuzi hazitumiki kwa kiwango kikubwa sawa na vile ambavyo wengine wamefikiri. Na huo wapaswa kuzifanya hospitali nyingi zianzishe kanuni za miongozo ya maadili. Ijapokuwa uamuzi wa mahakama hii umekubalika kijumla na kwamba huo wawatia moyo wagonjwa wasiokuwa na haki ya kujiamulia namna yao ya matibabu, si vikundi vyote vimeipokea kwa dhati. Hospitali ya taifa na wale matabibu watatu wamekata rufani katika Mahakama Kuu Zaidi. Hivyo lazima tusubiri tuone iwapo mahakama kuu zaidi ya Japani itategemeza haki za mgonjwa, sawa na afanyavyo Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu.
[Maelezo ya Chini]
a Dhana isiyofafanuliwa kisheria ambayo huachiwa hakimu kuifasiri na kuitumia.
b Hii ndiyo iliyokuwa kanuni ya mabwana wenye uhasama wa kudumu wa kipindi cha Tokugawa juu ya namna ya kuwatawala raia zao.