Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 2/15 kur. 30-31
  • Melkizedeki—Alikuwa Nani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Melkizedeki—Alikuwa Nani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Ukuhani wa Kristo Wafananishwa.
  • Kuwekwa Rasmi Moja kwa Moja.
  • Hakuwa na Watangulizi Wala Wafuataji.
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 2/15 kur. 30-31

Melkizedeki—Alikuwa Nani?

MELKIZEDEKI alikuwa mfalme wa Salemu ya kale na “kuhani wa Mungu Aliye juu sana,” Yehova. (Mwanzo 14:18, 22) Yeye ndiye kuhani wa kwanza anayetajwa katika Maandiko; alikuwa na cheo hicho muda fulani kabla ya mwaka wa 1933 K.W.K. Akiwa mfalme wa Salemu, jina limaanishalo “Amani,” Melkizedeki atambulishwa na mtume Paulo kuwa “Mfalme wa Amani” na, kwa msingi wa jina lake, anatajwa kuwa “Mfalme wa Uadilifu.” (Waebrania 7:1, 2) Salemu ya kale yaonwa kuwa ndiyo chanzo cha jiji lililotokea baadaye la Yerusalemu, na jina lake likaja kuwa sehemu ya jina la jiji hilo la Yerusalemu, ambalo mara nyingine huitwa “Salemu.”—Zaburi 76:2.

Baada ya Abramu (Abrahamu) kumshinda Kedorlaoma na wale wafalme walioshirikiana naye, mzee huyo Abrahamu akaja katika Bonde la Shawe au “Bonde la mfalme.” Hapo Melkizedeki “akaleta mkate na divai” akambariki Abrahamu, akisema: “Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako.” Ndipo Abrahamu akampa mfalme huyo aliyekuwa kuhani “fungu la kumi la vitu vyote,” yaani “nyara zilizo kuu” alizozitwaa katika ushindi wake kwenye vita dhidi ya wale wafalme walioungana.—Mwanzo 14:17-20; Waebrania 7:4.

Ukuhani wa Kristo Wafananishwa.

Katika unabii wenye kutokeza juu ya Mesiya, kiapo alichoapa Yehova kwa “Bwana” wa Daudi ni: “Ndiwe kuhani hata milele, kwa mfano wa Melkizedeki!” (Zaburi 110:1, 4) Zaburi hii iliyopuliziwa iliwafanya Waebrania wamwone huyo Mesiya aliyeahidiwa kuwa yule ambaye angekuwa mfalme na kuhani. Katika barua yake kwa Waebrania, mtume Paulo aliondoa shaka yoyote juu ya utambulisho wa yule aliyeahidiwa, akimtaja “Yesu, ambaye amekuwa kuhani wa cheo cha juu kulingana na namna ya Melkizedeki milele.”—Waebrania 6:20; 5:10.

Kuwekwa Rasmi Moja kwa Moja.

Inaonekana Yehova alimweka rasmi Melkizedeki kuwa kuhani. Paulo alipozungumzia cheo cha Yesu akiwa Kuhani wa Cheo cha Juu aliye mkuu, alionyesha kwamba mtu hachukui heshima hii “kwa hiari yake mwenyewe, ila tu aitwapo na Mungu, kama vile Aroni pia alivyoitwa.” Paulo aeleza pia kwamba “Kristo hakujitukuza mwenyewe kwa kuwa kuhani wa cheo cha juu, bali alitukuzwa na yeye aliyesema hivi kumhusu: ‘Wewe ni mwana wangu; mimi, leo, nimekuwa baba yako,’” kisha mtume Paulo ayatumia maneno ya kiunabii ya Zaburi 110:4 kumhusu Yesu Kristo.—Waebrania 5:1, 4-6.

Cheo cha kikuhani cha Melkizedeki hakikuhusiana na ukuhani wa Israeli, na kama vile Maandiko yanavyoonyesha, kilikuwa bora kuliko ukuhani wa Aroni. Jambo moja linaloonyesha hivyo ni jinsi ambavyo Abrahamu, yule baba wa zamani wa taifa lote la Israeli, na wa kabila la kikuhani la Lawi alivyomstahi Melkizedeki. Abrahamu, “rafiki ya Yehova,” aliyekuwa “baba ya wote wale walio na imani,” alimtolea huyo kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana “sehemu ya kumi.” (Yakobo 2:23; Waroma 4:11) Paulo aonyesha kwamba Walawi walikusanya sehemu ya kumi kutoka kwa ndugu zao, ambao pia walitoka katika viuno vya Abrahamu. Hata hivyo, Paulo aeleza kwamba Melkizedeki “ambaye hakufuatisha nasaba yake kutoka kwao alichukua sehemu za kumi kutoka kwa Abrahamu,” na “kupitia Abrahamu hata Lawi ambaye hupokea sehemu za kumi amelipa sehemu za kumi, kwa maana alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani wakati Melkizedeki alipokutana naye.” Hivyo basi, ingawa makuhani Walawi walipokea sehemu za kumi kutoka kwa Waisraeli, wao, kama wawakilishwavyo na mzazi wao wa kale Abrahamu, walimpa Melkizedeki sehemu za kumi. Zaidi ya hilo, ubora wa ukuhani wa Melkizedeki waonyeshwa na jambo la kwamba yeye alimbariki Abrahamu, Paulo akionyesha kwamba ‘mdogo hubarikiwa na mkubwa zaidi.’ Hizo ni baadhi ya zile sababu zinazomfanya Melkizedeki awe ufananisho unaofaa wa Kuhani wa Cheo cha Juu aliye mkuu Yesu Kristo.—Waebrania 7:4-10.

Hakuwa na Watangulizi Wala Wafuataji.

Paulo aonyesha waziwazi kwamba ukamilifu haungeweza kupatikana kupitia ukuhani wa Kilawi, hili likifanya iwe lazima kutokea kwa kuhani “kulingana na namna ya Melkizedeki.” Paulo aonyesha kwamba Kristo alitoka Yuda, kabila lisilo la kikuhani, lakini akitaja ufanani uliopo kati ya Yesu na Melkizedeki, aonyesha kwamba Yesu alikuwa kuhani, “si kulingana na sheria ya amri ikitegemea mwili, bali kulingana na nguvu ya uhai usioharibika.” Aroni na wanawe walikuwa makuhani bila kiapo, lakini ukuhani aliokabidhiwa Kristo umeagizwa rasmi kwa kiapo cha Yehova. Pia, kwa kuwa makuhani wa Kilawi walikuwa wakifa, walihitaji kuwa na wafuataji, Yesu Kristo aliyefufuliwa “kwa sababu ya kuendelea kuwa hai milele ana ukuhani wake bila kuwa na wafuataji wowote” na kwa sababu hiyo aweza “kuokoa kikamili wale wanaomkaribia Mungu kupitia yeye, kwa sababu yeye yuko hai sikuzote ili kuwaombea.”—Waebrania 7:11-25.

Paulo alitaja jambo lenye kutokeza kumhusu Melkizedeki aliposema hivi juu yake: “Katika kuwa asiye na baba, asiye na mama, bila nasaba, akiwa hana mwanzo wa siku wala mwisho wa uhai, bali akiisha kufanywa kama Mwana wa Mungu, yeye adumu kuwa kuhani daima dawamu.” (Waebrania 7:3) Kama wanadamu wengine, Melkizedeki alizaliwa kisha akafa. Hata hivyo, majina ya baba yake na mama yake hayatajwi, majina ya babu zake na ya vizazi vyake vya baadaye hayafunuliwi, Maandiko hayana habari zozote juu ya mwanzo wa maisha yake wala mwisho wake. Hivyo basi, Melkizedeki kwa kufaa aweza kufananisha kimbele Yesu Kristo, aliye na ukuhani usio na kikomo. Kama Melkizedeki ambaye hakutajwa kuwa na mtangulizi wala mfuataji katika ukuhani wake, ndivyo na Kristo asivyokuwa na kuhani aliyemtangulia aliyefanana naye, na Biblia huonyesha kuwa hakuna kuhani yeyote atakayemfuata. Zaidi ya hilo, ijapokuwa Yesu alizaliwa katika kabila la Yuda na katika nasaba ya kifalme ya Daudi, ukoo wake wa kimwili hauna uhusiano wowote na ukuhani wake, wala si kwa sababu ya ukoo wa kimwili kwamba alikuwa na cheo cha kuhani na cha mfalme. Mambo haya yalitokea kwa sababu ya kiapo cha Yehova mwenyewe alichomwapia.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki