Nchi ya Wavenda Yenye Kuzaa Sana
KWA miaka kumi iliyopita, mke wangu nami tumekuwa waeneza-evanjeli wa wakati wote miongoni mwa Wavenda. Wavenda hukaa kusini mwa Mto Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini, nalo taifa lao ni la makabila yaliyovuka Limpopo karne zilizopita. Wavenda fulani hudai kwamba babu zao walianza kuishi hapa zaidi ya miaka 1,000 iliyopita.
Kwa kweli, wakati mmoja eneo hili lilikuwa sehemu ya ustaarabu wa kale ulioitwa Ufalme wa Mapungubwe. Ulikuwa mji mkubwa wa kwanza wa Afrika Kusini, nao ulimiliki lile bonde kubwa la Mto Limpopo, tokea Botswana upande wa magharibi hadi Msumbiji upande wa mashariki. Tangu wapata mwaka wa 900 W.K. hadi mwaka wa 1100 W.K., wafanya-biashara Waarabu walipata pembe za tembo, pembe za kifaru, ngozi za wanyama, shaba, na hata dhahabu kutoka Mapungubwe. Vyombo vilivyonakshiwa kwa ustadi na kufunikizwa kwa dhahabu vimefukuliwa kwenye kilima kiitwacho Mapungubwe walikozikwa wafalme. Ensaiklopedia moja yadokeza kwamba hizo ni baadhi ya “ithibati za mapema zaidi za uchimbaji-migodi huko kusini mwa Afrika.”
Dhahabu haichimbwi huko tena kamwe. Leo, nchi ya Wavenda yajulikana sana kwa sababu ya kuzaa matunda. Kusini mwa Milima ya Soutpansberg mna bonde lenye rutuba, ambapo matunda kama vile maparachichi, ndizi, maembe, na mapera hukua sana. Mbali na kokwa kama vile pekani na makadamia, pia kuna mboga chungu nzima. Hizo zatia ndani magugu yaitwayo muroho, yenye ladha kama ya mchicha nayo hupendwa sana na wenyeji.
Taifa la Wavenda ni lenye amani na lenye ukarimu. Si ajabu kichwa cha familia kuagiza kwamba mgeni ambaye hakutarajiwa apikiwe kuku. Kuku huyo huliwa kwa vhuswa, chakula kikuu, kinachopikwa kwa mahindi. Baada ya ziara hiyo, kichwa cha familia hiyo atamsindikiza mgeni wake hatua chache. Hiyo ndiyo njia ya kitamaduni ya kumstahi mgeni. Watoto hufundishwa kuwasalimu wageni vizuri kwa kuwainamia na kuukingamanisha mkono mmoja juu ya mwingine. Kwenye ukurasa huu wawaona wanawake wawili Wavenda wakisalimiana katika njia hiyo ya kidesturi.
Lugha Ngumu
Si rahisi kwa watu kutoka Ulaya kuongea Kivenda kwa ufasaha. Tatizo moja ni kwamba maneno mengi huendelezwa kwa tahajia zilezile lakini hutamkwa tofauti. Siku moja nilipokuwa nikitoa hotuba ya Biblia kwenye kutaniko la Mashahidi wa Yehova la Kivenda, nilikuwa nikijaribu kuwatia moyo wasikilizaji wanene na kila mtu. Msikilizaji mmoja aliangua kicheko kwa kuwa nilisema “kidole kwa kidole” badala ya kusema “mtu kwa mtu.”
Nilipojaribu kuongea Kivenda mara ya kwanza katika mahubiri ya hadharani, mwanamke Mvenda alijibu hivi: “Sielewi Kiingereza.” Nilidhani nilikuwa nimeongea Kivenda kwa ufasaha, lakini alifikiri kilikuwa Kiingereza! Nilipoenda kwenye nyumba fulani pindi nyingine, nilimwomba kijana mmoja amwite kichwa cha familia. Kichwa cha familia katika Kivenda ni thoʹho. Kimakosa, nilikuwa nimesema thohoʹ, nikiomba kuongea na tumbili wa nyumba hiyo! Makosa kama hayo yalinivunja moyo, lakini kwa kuvumilia, mke wangu nami sasa twaweza kuwasiliana vya kutosha katika Kivenda.
Mazao ya Kiroho
Nchi ya Wavenda inazaa sana kiroho. Miaka ya 1950, kutaniko la Mashahidi wa Yehova lilifanyizwa miongoni mwa watu waliokuwa wamehamia huko kutoka nchi jirani ili kufanya kazi kwenye mgodi wa shaba katika mji wa Messina. Utendaji wao wenye bidii uliwajulisha Wavenda wengi kweli za Biblia. Miaka kumi baadaye kikundi cha Mashahidi Wavenda kilikuwa kikifanya mikutano katika nyumba ya kibinafsi katika mji wa Sibasa.
Ili kuharakisha ongezeko, ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ya Afrika Kusini ilituma waeneza-evanjeli wa wakati wote kwenye eneo hilo lenye kuzaa sana. Punde si punde kile kikundi cha Sibasa kilikuwa kimekua, kikawa kutaniko kubwa. Mikutano ya Kikristo ilikuwa ikifanyiwa katika darasa wakati huo. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova katika eneo la Pietersburg lililo kilometa 160 hivi upande wa kusini, walisaidia kujenga Jumba la Ufalme huko Thohoyandou, mji jirani.
Wakazi waongeao Kivenda kaskazini mwa Afrika Kusini hujumlika kuwa zaidi ya 500,000. Kazi ya kuhubiri Ufalme ilipoanza hapa katika miaka ya 1950, hakukuwa Mashahidi wowote Wavenda. Sasa wako zaidi ya 150. Lakini bado kuna maeneo mengi ambayo hayajahubiriwa na kuna kazi nyingi ya kufanywa. Mwaka wa 1989 tulianza kutembelea kijiji cha Wavenda kiitwacho Hamutsha. Ni Shahidi mmoja tu, aliyekuwa akiishi huko wakati huo. Sasa wapiga-mbiu wa Ufalme zaidi ya 40 wanaishi katika kijiji hicho. Tuna shughuli ya kumalizia ujenzi wa Jumba letu la Ufalme, jambo ambalo tena limewezekana kwa sababu ya msaada wa Mashahidi wa makutaniko ya Pietersburg na michango ya kifedha ya ndugu katika nchi zenye utajiri zaidi.
Twaishi kwenye gari linalotumiwa kama nyumba (trela ndogo) katika shamba fulani. Kwa kudumisha maisha yetu yakiwa sahili, tunapata wakati mwingi zaidi wa kuwahubiria wenyeji habari njema. (Marko 13:10) Kwa sababu hiyo, tumebarikiwa sana kuwa na pendeleo la kuwasaidia wengi waweke maisha zao wakfu kwa Yehova Mungu. Kielelezo kimoja ni mwanamume aitwaye Michael, ambaye aliona kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani nyumbani kwa rafiki yake.a Alianza kukisoma na mara moja akatambua kweli. Kwa hiyo akaandikia Watch Tower Society ili apate vichapo zaidi vya Biblia. Katika barua yake Michael alieleza kwamba majuzi tu alikuwa amebatizwa akiwa mshiriki wa kanisa la Kimitume. “Nimegundua,” akaendelea kusema, “kwamba siko katika njia inayoelekea kwa Ufalme wa Mungu. Nimeamua kuwa mmoja wa washiriki wenu, lakini sijui jinsi ya kufanya hivyo.” Akatoa anwani yake na kuomba atumiwe mmoja wa Mashahidi wa Yehova amsaidie. Nilimpata Michael na kuanza kujifunza naye Biblia nyumbani. Leo, ni Shahidi aliyebatizwa na anamtumikia Yehova kwa uaminifu-mshikamanifu.
Mwezi wa Desemba 1997, tulihudhuria Mkusanyiko wa Wilaya wa Mashahidi wa Yehova wa “Imani Katika Neno la Mungu” uliofanywa kwenye uwanja wa michezo, Thohoyandou. Watu 634 walihudhuria, na wapya 12 wakabatizwa. Nilikuwa na pendeleo la kutoa hotuba mbili katika Kivenda. Hiyo ilikuwa hatua kubwa kwelikweli kwa muda wa miaka kumi ambayo tumeishi katika nchi hii yenye kuzaa sana!—Imechangwa.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.