Baa la Sasa la Ukosefu wa Usawa
“Sisi tunashikilia hizi kweli kuwa wazi, kwamba watu wote waumbwa wakiwa sawa, wapewa na Muumba wao Haki fulani zisizoweza kupingwa, kwamba miongoni mwazo ni Uhai, Uhuru na ufuatiaji wa Furaha.”—Azimio la Uhuru, lililokubaliwa rasmi na Marekani mwaka wa 1776.
“Wanadamu wote huzaliwa wakiwa huru na wakiwa na haki sawa.”—Azimio la Haki za Mwanadamu na za Raia, lililokubaliwa rasmi na Bunge la Kitaifa la Ufaransa mwaka wa 1789.
“Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika adhama na haki.”—Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote, lililokubaliwa rasmi na Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka wa 1948.
HAKUNA shaka kuhusu jambo hilo. Wanadamu wote wana tamaa ya kuwa sawa. Lakini kwa kusikitisha, uhakika wa kwamba imekuwa lazima kurudia mara nyingi wazo la usawa wa kibinadamu wathibitisha kwamba kufikia sasa, wanadamu wamekosa usawa.
Je, yeyote aweza hasa kubisha kwamba sasa kwenye umalizio wa karne hii ya 20 mambo yamekuwa bora? Je, raia wote wa Marekani na Ufaransa, au wale wa mataifa 185 yanachama ya Umoja wa Mataifa, yanafurahia haki sawa ambazo yadaiwa walizaliwa nazo?
Ingawa huenda wazo la wanadamu wote kuwa sawa likawa “wazi,” watu wote hawana kabisa haki sawa kuhusiana na “Uhai, Uhuru na ufuatiaji wa Furaha.” Kwa mfano, tunaweza kuzungumzia usawa gani kuhusu haki ya uhai wakati mtoto mmoja katika Afrika analazimika kutibiwa na daktari yuleyule anayetibu watu wengine 2,569, ilhali mtoto mmoja katika Ulaya hutibiwa na daktari anayetibu watu 289 tu? Au kuna usawa gani kuhusu haki za uhuru na kufuatia furaha wakati theluthi moja ya wavulana na theluthi mbili ya wasichana wa India watakua bila kujua kusoma na kuandika, ilhali katika nchi kama Japani, Ujerumani, na Uingereza, karibu kila mtoto ana uhakika wa kupata elimu?
Je, watu wa nchi za Amerika ya Kati, ambao kiwango chao cha mapato ni dola 1,380 za Marekani, hufurahia maishani “adhama na haki” zilezile ambazo Wafaransa, ambao kiwango chao cha mapato ni dola 24,990 za Marekani, hufurahia? Je, mtoto wa kike Mwafrika, anayetarajia kuishi miaka 56, anafurahia usawa gani kwa kulinganishwa na mtoto wa kike wa Amerika ya Kaskazini anayetarajia kuishi miaka 79?
Ukosefu wa usawa hudhihirika katika njia mbalimbali na zote huchukiza. Ukosefu wa usawa katika viwango vya maisha na katika fursa za kupata utunzaji wa kiafya na elimu ni baadhi tu ya njia hizo. Nyakati nyingine tofauti za kisiasa, za kijamii, au za kidini hutimiza fungu kubwa katika kuwanyima watu adhama na uhuru wao. Licha ya majadiliano yote kuhusu usawa, tunaishi katika ulimwengu usio na usawa. Kama baa—“kisababishi cha mateso makubwa au yenye kuenea,” kama vile neno hilo lifafanuliwavyo—ukosefu wa usawa uko katika kila tabaka la jamii ya kibinadamu. Mateso yasababishwayo na ukosefu wa usawa kwa njia ya umaskini, ugonjwa, kutokuwa na ujuzi, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, na ubaguzi huumiza sana.
“Watu wote waumbwa wakiwa sawa.” Ni wazo lenye kupendeza kama nini! Yahuzunisha kama nini kwa sababu mambo ya hakika ni kinyume kabisa!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
UN PHOTO 152113/SHELLEY ROTNER