Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w13 2/15 kur. 13-16
  • Walinzi wa Mfalme Wahubiriwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Walinzi wa Mfalme Wahubiriwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MTUME AHUBIRI “BILA KIZUIZI”
  • PAULO ATOA USHAHIDI KWA WADOGO NA WAKUBWA
  • ‘SEMA NENO LA MUNGU BILA WOGA’
  • “Kutoa Ushahidi Kamili”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Ile Serikali Kubwa ya Sita ya Ulimwengu Roma!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Kutetea Habari Njema Mbele ya Maofisa Wakuu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2016
  • Piga Mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa Ujasiri!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
w13 2/15 kur. 13-16

Walinzi wa Mfalme Wahubiriwa

[Picha katika ukurasa wa 13]

Ni mwaka 59 W.K. Wafungwa kadhaa walio chini ya ulinzi wa askari-jeshi waliochoka kwa sababu ya safari, wanaingia Roma kupitia lango la Porta Capena. Juu ya Kilima cha Palatine kuna jumba la Maliki Nero, linalolindwa na Walinzi wa Mfalme walio na panga zilizofichwa ndani ya mavazi yao rasmi ya kiraia.a Yulio, ofisa Mroma wa kijeshi anawapitisha wafungwa mbele ya Baraza Kuu la Roma kuelekea juu ya Kilima cha Viminal. Wanapita bustani iliyo na madhabahu nyingi za miungu ya Kiroma na pia katika uwanja wa mazoezi ya kijeshi.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mchongo wa Walinzi wa Mfalme. Inadhaniwa kwamba ulikuwa katika Tao la Klaudio, lililojengwa mwaka wa 51 W.K.

Mtume Paulo ni miongoni mwa wafungwa hao. Miezi kadhaa mapema alipokuwa katika meli iliyokuwa ikisukwa-sukwa na dhoruba, malaika wa Mungu alimwambia Paulo hivi: “Utasimama mbele ya Kaisari.” (Mdo. 27:24) Je, Paulo atafanya hivyo? Anapogeuka ili kuuangalia mji mkuu wa Milki ya Roma, bila shaka Paulo anakumbuka maneno ambayo Bwana Yesu alimwambia alipokuwa kwenye Mnara wa Antonia huko Yerusalemu. Yesu alisema hivi: “Jipe moyo! Kwa maana kama vile ambavyo umekuwa ukitoa ushahidi kamili katika Yerusalemu juu ya mambo yanayonihusu, vivyo hivyo utatoa ushahidi katika Roma pia.”—Mdo. 23:10, 11.

Huenda Paulo anasimama na kuiangalia ngome kubwa ya Castra Praetoria yenye kuta ndefu zilizojengwa kwa matofali mekundu, zenye buruji na minara. Walinzi wa Mfalme wanaotumika wakiwa walinzi wa maliki na pia polisi wa mji wanaishi katika ngome hizo. Vikosi 12b vya Walinzi wa Mfalme pamoja na vikosi kadhaa vinavyolinda jiji viliishi ndani ya ngome hiyo ambayo ingeweza kutoshea maelfu ya askari-jeshi, kutia ndani askari wapanda-farasi. Ngome ya Castra Praetoria ni kikumbusho cha chanzo cha mamlaka ya mfalme. Kwa kuwa kikosi cha Walinzi wa Mfalme kina jukumu la kuwalinda wafungwa katika majimbo, Yulio analiongoza kundi hilo la wafungwa kupitia moja kati ya malango manne makuu. Baada ya safari hatari iliyowachukua miezi kadhaa, hatimaye Yulio amewafikisha wafungwa mwisho wa safari yao.—Mdo. 27:1-3, 43, 44.

MTUME AHUBIRI “BILA KIZUIZI”

Katika safari hiyo, Mungu alimwambia Paulo kupitia maono kwamba watu wote melini wangeokoka baada ya kuvunjikiwa na meli. Paulo hakupata madhara baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu. Aliwaponya wagonjwa waliokuwa katika kisiwa cha Malta, kisha wenyeji wakaanza kusema kwamba Paulo ni mungu. Huenda habari hizo zilienea miongoni mwa Walinzi wa Mfalme walioamini ushirikina.

Tayari Paulo ameonana na ndugu kutoka Roma waliokuja ‘kukutana naye katika Soko la Apio na Mikahawa Mitatu.’ (Mdo. 28:15) Hata hivyo, akiwa mfungwa, Paulo atatimizaje hamu yake ya kutangaza habari njema jijini Roma? (Rom. 1:14, 15) Wengine wanafikiri kwamba wafungwa walipelekwa kwa kapteni wa walinzi. Ikiwa ndivyo ilivyokuwa, inaelekea Paulo alipelekwa kwa Liwali wa Walinzi wa Mfalme aliyeitwa Afranius Burrus, ambaye huenda alikuwa wa pili katika mamlaka baada ya maliki.c Kwa vyovyote vile, badala ya kulindwa na maofisa wa kijeshi, Paulo analindwa na askari-jeshi mmoja mwenye cheo cha kawaida katika kikosi cha Walinzi wa Mfalme. Paulo anaruhusiwa kujitafutia mahali pa kuishi na pia anaruhusiwa kutembelewa na wageni na kuwahubiria “bila kizuizi.”—Mdo. 28:16, 30, 31.

Walinzi wa Mfalme Katika Siku za Nero

[Picha katika ukurasa wa 14]

Sarafu hii iliyotolewa katika karne ya kwanza inaonyesha kambi ya Walinzi wa Mfalme

Walinzi wa Mfalme walikuwa chini ya kiapo cha kumlinda maliki na familia yake. Walipokuwa vitani, walibeba bendera zao zenye sanamu za maliki pamoja na ngao, ambazo mara nyingi zilichorwa nge, iliyokuwa alama ya nyota ya Kaisari Tiberio. Chini ya amri ya baraza na maofisa wa kijeshi, walidumisha usalama katika michezo na ndani ya majumba ya michezo, nao waliwasaidia wazima-moto. Walinzi hao walitumikia kwa miaka 16, badala ya miaka 25 ambayo wangetumikia katika vikosi vya kijeshi, na mshahara wao ulikuwa mara tatu ya mshahara wa askari wa kawaida, walilipwa pia marupurupu na pesa nyingi walipostaafu. Pia, Walinzi wa Mfalme walitumiwa kuwatesa na kuwaua wafungwa. Alipofungwa gerezani kwa mara ya pili, huenda Paulo aliuawa na askari-jeshi hao aliojitahidi sana kuwaokoa.—2 Tim. 4:16, 17.

Courtesy Classical Numismatic Group, Inc./cngcoins.com

PAULO ATOA USHAHIDI KWA WADOGO NA WAKUBWA

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kuta za Castra Praetoria zinavyoonekana leo

Alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kihukumu, huenda Burrus alimhoji mtume Paulo, labda katika jumba la kifalme au katika kambi ya Walinzi wa Mfalme, kabla ya kuwasilisha kesi hiyo mbele ya Nero. Paulo hakosi kuitumia nafasi hiyo ya pekee ya “kutoa ushahidi kwa wadogo na wakubwa pia.” (Mdo. 26:19-23) Hata iwe Burrus alifikia mkataa gani, Paulo hakufungwa gerezani alipokuwa katika kambi ya Walinzi wa Mfalme.d

Nyumba aliyokodi Paulo ina nafasi ya kutosha kupokea “wakuu wa Wayahudi” na kuwatolea ushahidi pamoja na ‘hesabu kubwa zaidi ya wengine waliokuja katika makao yake.’ Walinzi wa Mfalme wanaweza kumsikia ‘akitoa ushahidi kamili’ kwa Wayahudi kuhusu Ufalme na Yesu, “tangu asubuhi mpaka jioni.”—Mdo. 28:17, 23.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Paulo alipokuwa kifungoni, askari-jeshi walimsikia akisema maneno yaliyoandikwa katika barua zake

Kikosi cha Walinzi wa Mfalme katika jumba la mfalme kinabadilishwa kila siku katika saa ya nane. Mlinzi wa Paulo alibadilishwa pia kwa ukawaida. Kwa miaka miwili ambayo mtume Paulo amefungwa, askari-jeshi wanaomlinda wanamsikia akisema maneno yanayoandikwa katika barua kwa Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, na Wakristo Waebrania na kumwona akiandika mwenyewe barua kwa Mkristo anayeitwa Filemoni. Akiwa kifungoni, Paulo anapendezwa kibinafsi na mtumwa aliyetoroka, Onesimo, ‘aliyemzaa alipokuwa katika vifungo vyake vya gereza,’ naye anamrudisha kwa bwana mkubwa wake. (Flm. 10) Bila shaka, Paulo anapendezwa pia kibinafsi na walinzi wake. (1 Kor. 9:22) Tunaweza kuwazia akimuuliza mlinzi kuhusu kusudi la kila sehemu ya mavazi na silaha za kivita na kisha anatumia habari hiyo katika mfano unaofaa.—Efe. 6:13-17.

‘SEMA NENO LA MUNGU BILA WOGA’

Kifungo cha Paulo kinasaidia “kuendeleza mbele habari njema” miongoni mwa Walinzi wote wa Mfalme na wengine. (Flp. 1:12, 13) Wakazi wa ngome ya Castra Praetoria wana uhusiano na watu wengi katika Milki ya Roma, kutia ndani maliki na wale walio katika nyumba yake kubwa. Watu wa nyumba hiyo wanatia ndani washiriki wa familia yake, watumishi, na watumwa, baadhi yao wanakuwa Wakristo. (Flp. 4:22) Kwa sababu Paulo anatoa ushahidi kwa ujasiri, ndugu katika Roma wanakuwa na uhodari wa “kulisema neno la Mungu bila woga.”—Flp. 1:14.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Hata tuwe katika hali gani, tunaweza kuwahubiria wale wanaokuja kututembelea au kutuhudumia

Mfano wa Paulo wa kutoa ushahidi huko Roma unatutia moyo ‘tunapolihubiri neno katika majira yanayofaa na majira yenye taabu.’ (2 Tim. 4:2) Baadhi yetu hatuwezi kutoka nyumbani kwetu, tunaishi katika makao ya kuwatunzia wazee au hospitalini, au huenda tumefungwa gerezani kwa sababu ya imani yetu. Hata tuwe katika hali gani, tunaweza kuwahubiria wale wanaokuja kututembelea au kutuhudumia. Tunapotumia kila fursa tunayopata kuhubiri kwa ujasiri, tunajionea kwamba ‘neno la Mungu haliwezi kufungwa.’—2 Tim. 2:8, 9.

Sextus Afranius Burrus

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mchongo wenye maandishi yenye jina la Sextus Afranius Burrus

Huenda Burrus alizaliwa huko Vaison-la-Romaine, iliyo sasa kusini mwa Ufaransa, ambako maandishi yanayotaja jina lake yalipatikana mwaka wa 1884 W.K. Agripina Mchanga, mke na mpwa wa kike wa Kaisari Klaudio alimpandisha cheo Burrus kuwa Liwali pekee wa Walinzi wa Mfalme mwaka wa 51 W.K. Agripina alitumia walimu wawili kumtayarisha mwana wake mdogo, Nero, ili awe maliki. Mmoja wa walimu hao alikuwa Burrus, askari-jeshi mashuhuri aliyetoa mafunzo ya kijeshi. Mwingine alikuwa mwanafalsafa Seneca, aliyemfundisha Nero kufanya maamuzi. Alipopata fursa inayofaa, Agripina alimuua mume wake kwa sumu. Kabla ya habari za kifo cha Klaudio kujulikana, Burrus alimsindikiza Nero mpaka Castra Praetoria na kuhakikisha ametangazwa na Walinzi wa Mfalme kuwa maliki, na hivyo Baraza Kuu halingeweza kupinga uamuzi huo. Nero alipomuua mama yake mwaka wa 59 W.K., Burrus alificha jambo hilo. Wanahistoria Waroma, Suetonius na Cassius Dio wanadai kwamba Nero alimuua Burrus kwa sumu mwaka wa 62 W.K.

Musée Calvet Avignon

a Tazama sanduku lenye kichwa “Walinzi wa Mfalme Katika Siku za Nero.”

b Kikosi kimoja cha jeshi la Roma kilikuwa na askari-jeshi wapatao 1,000.

c Tazama sanduku lenye kichwa “Sextus Afranius Burrus.”

d Herode Agripa alifungwa kambini humo na Kaisari Tiberio mwaka wa 36 au 37 W.K. kwa sababu ya kusema kwamba huenda Kaligula angekuwa maliki. Kaligula alipowekwa kuwa maliki, alimpa Herode zawadi kwa kumchagua awe mfalme.—Mdo. 12:1.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki