Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w15 3/1 kur. 13-15
  • Zawadi Zilizofaa Mfalme

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zawadi Zilizofaa Mfalme
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUVUKA JANGWA LA ARABIA
  • “SIRI YA BIASHARA ILIYOTUNZWA KULIKO ZOTE”
  • Tamaa Ambazo Zilibadili Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Matumizi ya Vipodozi Katika Nyakati za Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Zeri ya Gileadi—Mafuta Yanayoponya
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
w15 3/1 kur. 13-15
Vikolezo mbalimbali vyenye harufu nzuri

Zawadi Zilizofaa Mfalme

“Wanajimu kutoka sehemu za Mashariki . . . wakafungua hazina zao na kumtolea zawadi—dhahabu na ubani na manemane.”—Mathayo 2:1, 11.

UNGEPENDA kumpa zawadi gani mtu aliye muhimu sana kwako? Katika nyakati za Biblia baadhi ya vikolezo vilikuwa na thamani kama dhahabu—thamani kubwa sana iliyomfaa mfalme.a Hii ndiyo sababu vikolezo vyenye harufu nzuri vilikuwa miongoni mwa zawadi ambazo wanajimu walileta kwa “mfalme wa wayahudi.”—Mathayo 2:1, 2, 11.

Mafuta ya zeri

Mafuta ya zeri

Biblia inasema hivi pia kuhusu malkia wa Sheba alipofunga safari kumtembelea Mfalme Sulemani: “Ndipo akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, na mafuta ya zeri kwa wingi sana, na mawe ya thamani; na kulikuwa hakujapata kuwa na mafuta ya zeri kama yale ambayo malkia wa Sheba alimpa Mfalme Sulemani.”b (2 Mambo ya Nyakati 9:9) Pia wafalme walimpelekea Sulemani mafuta ya zeri ili kumtakia mema.—2 Mambo ya Nyakati 9:23, 24.

Kwa nini vikolezo hivyo na vitu vilivyotengenezwa kwa vikolezo hivyo, vilikuwa vyenye thamani na gharama kubwa sana katika nyakati za Biblia? Kwa sababu vilitumiwa katika urembo, dini, na mazishi. (Tazama sanduku “Matumizi ya Vikolezo Vyenye Harufu Nzuri Katika Nyakati za Biblia.”) Mbali na kwamba vikolezo hivyo vilihitajiwa sana, viliuzwa bei ghali kwa sababu ya gharama za usafirishaji na upatikanaji.

KUVUKA JANGWA LA ARABIA

Kida

Kida

Katika nyakati za Biblia, baadhi ya mimea ya vikolezo ilisitawi kwenye Bonde la Yordani. Hata hivyo, vikolezo vingine vililetwa kutoka nchi nyingine. Biblia imetaja vikolezo vya aina mbalimbali. Vikolezo vinavyotajwa vinatia ndani waridi, udi, mafuta ya zeri, mdalasini, ubani, na manemane. Zaidi ya hayo, kulikuwa na vikolezo vingine vya chakula kama vile bizari, mnanaa, na dili.

Vikolezo hivyo vilitoka wapi? Udi, kida, na mdalasini vilipatikana katika nchi za leo za China, India, na Sri Lanka. Vikolezo kama vile ubani na manemane vilitokana na miti na mimea ambayo ilisitawi katika maeneo ya jangwa kuanzia Arabia kusini hadi Somalia iliyo Afrika. Nardo, kilikuwa kikolezo cha pekee kilichotoka India katika maeneo ya Himalaya.

Zafarani

Zafarani

Ili kufika Israeli, vikolezo vingi vilisafirishwa kupitia Arabia. Kwa sababu hiyo, katika milenia ya kwanza na ya pili K.W.K., Arabia ilikuja kuwa “msambazaji mkuu wa bidhaa hizo kati ya Mashariki na Magharibi,” kikasema kitabu The Book of Spices. Miji ya kale, ngome, na vituo vya safari vilivyo katika eneo la Negev kusini mwa Israel vinaonyesha njia walizotumia wafanyabiashara wa vikolezo hivyo. Shirika la World Heritage Centre la UNESCO liliripoti kwamba makazi hayo “yalichangia faida kubwa ya biashara hiyo  . . . kutoka Arabia kusini hadi Mediterania.”

“Kiwango kidogo kiliuzwa kwa bei ghali, na kwa kuwa watu wengi walivipenda sana, vikolezo vilitumiwa kufanya biashara.” —The Book of Spices

Kwa kawaida msafara uliobeba vikolezo hivyo vyenye harufu nzuri ulisafiri umbali wa kilometa 1,800 hivi ukipitia Arabia. (Ayubu 6:19) Biblia inataja msafara wa wafanyabiashara Waishmaeli waliokuwa wamebeba “ubani mweusi na zeri na gome lenye utomvu” kutoka Gileadi hadi Misri.” (Mwanzo 37:25) Wana wa Yakobo walimuuza ndugu yao Yosefu awe mtumwa kwa wafanyabiashara hao.

“SIRI YA BIASHARA ILIYOTUNZWA KULIKO ZOTE”

Dill

Dill

Wafanyabiashara wa Arabia ndio waliojulikana sana kwa kufanya biashara ya vikolezo kwa miaka mingi. Walikuwa wauzaji wakuu wa kida na mdalasini, vikolezo kutoka Asia. Ili kuzuia wafanyabiashara wa eneo la Mediterania wasianzishe uhusiano wa kibiashara na watu wa eneo la Mashariki, Waarabu walieneza hadithi za uwongo kuhusu hatari za kujihusisha na biashara hiyo. Kitabu The Book of Spices kinasema kwamba chanzo cha vikolezo hivyo “huenda ikawa ndiyo siri ya kibiashara iliyotunzwa kuliko zote.”

Bizari

Bizari

Waarabu walieneza hadithi gani? Herodoto mwanahistoria Mgiriki aliyeishi katika karne ya tano K.W.K., alieleza hadithi za ndege wanaotisha waliojenga viota kwenye gome la mdalasini juu ya jabali lisiloweza kufikika. Aliandika hivi: “Ili kupata vikolezo hivyo vyenye thamani, watu waliweka vipande vikubwa vya nyama chini ya jabali hilo. Kisha ndege wangebeba vipande hivyo vya nyama kwa pupa na kuvipeleka katika viota vyao ambavyo vililemewa na uzito na kuanguka chini. Kisha watu wangeyaokota haraka magome ya mdalasini na kuyauza kwa wafanyabiashara. Hadithi hizo zilienea kila mahali. Kitabu The Book of Spices kinasema hivi: “Madai ya hatari ya kupata kikolezo hicho yalifanya [mdalasini] kiuzwe kwa bei ghali.”

Mnanaa

Mnanaa

Mwishowe, siri ya Waarabu hao ilifichuliwa na wakapoteza umiliki wa biashara hiyo. Kufikia karne ya kwanza K.W.K., jiji la Aleksandria, Misri likawa bandari kubwa na kituo kikuu cha biashara ya vikolezo. Meli za Roma zilipitia bandari ya Misri kuelekea India kwa kuwa mabaharia walitumia pepo za msimu za Bahari ya Hindi. Matokeo ni kwamba vikolezo hivyo vyenye thamani vilianza kupatikana kwa wingi na kwa bei nafuu.

Leo, thamani ya vikolezo haiwezi kulingana na ile ya dhahabu. Wala hatuwezi kufikiri kwamba vikolezo ni zawadi inayomfaa mfalme. Hata hivyo, watu wengi ulimwenguni wanaendelea kutumia vikolezo ili kutengeneza manukato, dawa, na hata kuongeza ladha kwenye chakula. Kwa kweli, harufu yenye kuvutia imefanya vikolezo vipendwe sana leo kama tu ilivyokuwa maelfu ya miaka iliyopita.

Vijiti vya mdalasini vilivyofungwa pamoja

Mdalasini

a Katika Biblia, maneno “kikolezo” au “vikolezo” katika lugha ya awali yalirejelea hasa vitu vilivyotengenezwa kwa mimea yenye harufu nzuri wala si viungo vinavyowekwa katika chakula.

b “Mafuta ya zeri” yalirejelea mafuta yenye harufu nzuri au utomvu unaopatikana katika miti na mimea.

Matumizi ya Vikolezo Vyenye Harufu Nzuri Katika Nyakati za Biblia

Mafuta matakatifu na uvumba mtakatifu. Yehova alimpa Musa maagizo ya kutengeneza mafuta matakatifu, au marhamu, na uvumba mtakatifu. Matayarisho hayo yalihusisha vikolezo vya aina nne tofauti. (Kutoka 30:22-25, 34-38) Baadhi ya makuhani walitengeneza mafuta matakatifu na walisimamia ugawaji wa mafuta hayo—Hesabu 4:16; 1 Mambo ya Nyakati 9:30.

Manukato na marhamu. Watu waliokuwa na uwezo wa kununua manukato hayo waliyatumia katika nyumba zao, mavazi, vitanda, na kwenye miili yao. (Esta 2:12; Methali 7:17; Wimbo wa Sulemani 3:6, 7; 4:13, 14) Maria dada ya Lazaro alimimina juu ya kichwa cha Yesu na kupaka miguuni mwake “mafuta yenye marashi, nardo halisi” ya bei ghali. Chupa ndogo ya “nardo halisi” iligharimu mshahara wa mwaka mmoja.—Marko 14:3-5; Yohana 12:3-5.

Kutayarisha miili kwa ajili ya mazishi. Nikodemo alileta “msokoto wa manemane na udi” ili kutayarisha mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko. (Yohana 19:39, 40) Baadhi ya wanafunzi wa Yesu walitayarisha “manukato na mafuta yaliyotiwa marashi” na kuyapeleka kaburini.—Luka 23:56–24:1.

Kikolezo cha chakula. Inaelekea Waisraeli pia walitumia vikolezo ili kuboresha ladha ya samaki na nyama.Vikolezo vingine vilitumika kutengeneza divai.—Wimbo wa Sulemani 8:2.

Aina Mbili ya Vikolezo Alivyopewa Yesu

Ubani na manemane vilitokana na gundi ya utomvu ambayo hutengenezwa kwa utomvu wa gome la mti mdogo au mimea ya miiba.

Mti wa ubani ulisitawi katika maeneo ya pwani ya kusini ya Arabia, na manemane ilisitawi vizuri katika inchi zenye maeneo makavu ambazo leo ni Somalia na Yemen. Vikolezo hivyo vilikuwa na thamani kubwa sana kwa sababu ya harufu yake. Yehova aliagiza vikolezo hivyo vitumiwe katika ibada yake—manemane ilitumiwa kutengeneza mafuta matakatifu, na ubani ulitumiwa kutengeneza uvumba mtakatifu. (Kutoka 30:23-25, 34-37) Hata hivyo,vikolezo hivyo vilitumiwa kwa njia nyingine.

Kwa kawaida ubani uliotumiwa kama uvumba ulichomwa ili kutokeza harufu nzuri. Utomvu wa manemane ulitumiwa moja kwa moja. Manemane imetajwa mara tatu katika simulizi la Yesu: ikiwa zawadi aliyopewa alipokuwa mtoto (Mathayo 2: 11), alipokuwa katika mti wa mateso, alipewa divai iliyotiwa manemane ili apunguze maumivu (Marko 15:23), na ilikuwa mojawapo ya vikolezo vilivyotumiwa kuutayarisha mwili wake kwa ajili ya maziko (Yohana 19:39).

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki