Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • km 6/95 kur. 3-6
  • Wahubiri wa Ufalme Wapendwa:

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wahubiri wa Ufalme Wapendwa:
  • Huduma Yetu ya Ufalme—1995
Huduma Yetu ya Ufalme—1995
km 6/95 kur. 3-6

Wahubiri wa Ufalme Wapendwa:

1 Tuna furaha sana kutia ndani pamoja na toleo hili la Huduma ya Ufalme Yetu picha yenye rangi ya kupendeza ya jengo letu jipya la tawi.

2 Pamoja na ramani iliyotolewa kwenye toleo la Oktoba 1994 la Huduma ya Ufalme Yetu mtaweza kutambua majengo saba makubwa ya ujenzi huu. Jengo la ghorofa nne lionekanalo upande wa mbali kulia litaandaa makazi kwa Wanabetheli 96. Jengo la chini la ghorofa moja lililo pekee kuelekea mbali kushoto litaandaa makazi kwa watu 36 zaidi kwa ajili ya shule mbalimbali za kihuduma zinazoendeshwa na Sosaiti. Kwa sasa, tuna karibu watu 60 katika familia ya Betheli. Kwa hiyo unaona tutakuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya upanuzi kadiri kazi ya Ufalme iongezekapo katika eneo letu. (Isa. 54:2) Na jambo jingine ni kwamba jengo hilo la ghorofa nne litakuwa na lifti mbili.

3 Majengo marefu ya ghorofa mbili upande wa kulia ni ofisi za usimamizi na huduma kwa familia ya Betheli, kama vile maktaba, jikoni, chumba cha kulia, mahali pa kusafishia nguo, na mahali pa kutunzia wagonjwa. Mwingilio mkuu kwa majengo haya na mahali pa mapokezi pako katikati ya majengo haya mawili.

4 Jengo refu la chini lililo juu katikati mahali unapoona kigari cha mizigo ni jengo letu la Bohari na Udumishaji. Uchukuzi wa fasihi na udumishaji wa majengo haya yote utafanyiwa hapa.

5 Mara tu baada ya jengo la Bohari kwenye upande wa kushoto ni Banda la Motokaa dogo, si la uegeshaji-magari wa ndani tu bali pia la kuandaa mahali pa kudumishia magari ya Sosaiti.

6 Jengo lililo chini, upande wa kushoto, lililozungukwa na miti na ua ni Jumba la Ufalme. Familia ya Betheli italitumia kwa funzo la Mnara wa Mlinzi lao la Jumatatu jioni, Shule ya Wanabetheli Wapya, na hotuba za Biblia nyinginezo zenye kujenga. Inatazamiwa kwamba angalau makutaniko mawili ya Nairobi yatatumia Jumba la Ufalme hilo kwa mikutano yao ya kutaniko.

7 Kuongezea majengo yaonekanayo katika picha, ni mipango ya kuweka tangi kubwa zaidi la hifadhi ya maji chini ya ardhi, si kwa kudumisha tu kuwepo kwa maji ya kutoshea ofisi ya tawi, bali pia kuandaa maji kwa makusudi ya kupambana na moto ikiwa jambo hilo litahitajika wakati wowote. Pia, majenereta makubwa yataandaa umeme wa dharura wakati wa kutoweka kwa nguvu za umeme. Twatumaini hili lawaandalia mwono mfupi wa jumla wa mradi wote.

8 Kwa sasa misingi ya Jumba la Ufalme, Banda la Motokaa, Bohari na Udumishaji, na jengo dogo la ghorofa moja la makazi, vimewekewa zege. Mwanzoni mwa Aprili shehena kubwa sana ya vifaa na zana ilifika katika vyombo vinane vikubwa. Zana hizi zenye kuhitajika kwelikweli zimewezesha kazi ya ujenzi iendelee kwa kiwango cha haraka sana. Inatazamiwa kwamba mradi wote utachukua muda wa karibu miaka miwili kukamilika.

9 Tayari makutaniko katika eneo la Nairobi yanaalikwa kushiriki kazi Jumamosi na Jumapili. Wakati wa uandikaji huu ndugu na dada wenyeji zaidi ya 50 wamealikwa kutumikia mahali pa ujenzi na wanafanya kazi pamoja na ndugu zao walio katika programu ya ujenzi wa kimataifa. Kwa hiyo kwenye mahali pa ujenzi tuna familia kubwa sana ya ujenzi. Kuongezea hiyo kazi yenye kutosheleza ndugu na dada hawa wanafurahia mipango ya kiroho kama vile ibada ya asubuhi, funzo la Mnara wa Mlinzi la familia, na kushirikiana na kujiunga katika huduma ya shambani pamoja na makutaniko kadhaa katika eneo la Nairobi.

10 Hata hivyo, kuna uhitaji mkubwa mno wa wajitoleaji zaidi. Kwa sababu ya nishati na nguvu za kimwili zinazotakwa kwa ajili ya kazi hii nyingi kuna uhitaji wa wanaume vijana waseja walio na afya. Ili kufanya ombi la utumishi wa ujenzi, mwanamume kijana apaswa kuwa aliyejiweka wakfu na kubatizwa kwa angalau mwaka mmoja na ni mkazi wa Kenya. Lazima awe mtu mwenye kujitoa, na wa kiroho. Pia, lazima awe tayari kufanya kazi ngumu. Katika ulimwengu leo, watu wengi huona kazi ngumu kuwa jambo la kuepukwa. Kwa hiyo mwanamume kijana anayetoa ombi la utumishi wa ujenzi ahitaji kuvaa utu mpya hivi kwamba atake kufanya kazi ngumu, akifanya kwa mikono yake kazi njema.—Linganisha Waefeso 4:28.

11 Je, wewe ni mwenye umri wa miaka 19 na si zaidi ya miaka 55? Wewe una afya nzuri, kimwili na kihisia-moyo? Je, wewe ni mtu wa kiroho anayependa Yehova na tengenezo lake kwa kina kirefu? Ukiitwa mahali pa ujenzi utafanya kazi yoyote utakayopewa? Ikiwa waweza kuyajibu ndiyo maswali haya twakutia moyo utoe ombi la pendeleo hili lisilo na kifani la utumishi wa ujenzi. Baraka ni tele.

12 Ikiwa mwangalizi-msimamizi katika kutaniko lako hana fomu za ombi basi tafadhali andikia ofisi ya tawi moja kwa moja. Tutafurahi zaidi kukupelekea ombi hilo.

13 Pia mtafurahi kujua kwamba makutaniko kadhaa na watu mmoja-mmoja tayari wameitikia mwaliko ulio katika Huduma ya Ufalme Yetu ya Oktoba 1994 wa kutoa michango ya mradi huu ulio mkubwa sana. Mnapopeleka michango yenu tafadhali hakikisheni mmeandika waziwazi hivi: “Mchango wa Ujenzi wa Betheli.”—Ona Kutoka 36:4-7.

14 Tutajaribu kuwajulisha maendeleo kazi izidipo kuendelea. Kwa wakati huu sisi sote twaweza kutia katika sala zetu kwamba mradi huu ufanikiwe kwa utukufu na heshima ya jina la Yehova. Twaitwaa fursa hii kuwatumieni kila mmoja wenu wonyesho wa upendo wetu mchangamfu wa Kikristo na salamu nyingi.

Ndugu zenu,

Ofisi ya Tawi ya Nairobi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki