Je, Wajua?
Katika karne ya kwanza, makuhani katika hekalu walifanya nini na damu ya wanyama waliotolewa dhabihu?
KILA mwaka, makuhani katika Israeli la kale walitoa maelfu ya wanyama wakiwa dhabihu katika madhabahu ya hekalu. Kulingana na mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Yosefo, katika siku ya Pasaka, zaidi ya wanakondoo 250,000 walitolewa dhabihu, jambo lililosababisha damu nyingi kumwagwa. (Law. 1:10, 11; Hes. 28:16, 19) Damu hiyo yote ilienda wapi?
Wachimbuaji wa vitu vya kale wamevumbua katika hekalu la Herode mfumo wa chini ya ardhi wa kuondoa maji machafu uliotumiwa kabla ya kuharibiwa kwa hekalu hilo mwaka wa 70 W.K. Inaonekana mfumo huo ulitumiwa kumwaga damu kutoka kwenye hekalu hilo.
Fikiria mambo mawili yaliyokuwa katika mfumo huo wa kuondoa maji machafu:
Mashimo yaliyokuwa chini ya madhabahu: Ufafanuzi kuhusu mfumo wa kuondoa maji machafu uliokuwa katika madhabahu unapatikana katika Mishna, mkusanyo wa sheria za mdomo za Kiyahudi zilizoandikwa kuelekea mwanzoni mwa karne ya tatu W.K. Kitabu hicho kinasema hivi: “Katika upande wa kusini-magharibi kulikuwa na mashimo mawili . . . ambamo damu iliyomwagwa upande wa magharibi na kusini, ilitiririka chini na kuchanganyika na mfumo wa maji machafu na kisha kutiririka kuelekea katika Bonde la Kidroni.”
Utamaduni huo wa kale wa kuwa na “mashimo” karibu na madhabahu, unapatana na uvumbuzi wa wachimbuaji wa siku zetu wa vitu vya kale. Kitabu The Cambridge History of Judaism kinathibitisha kupatikana kwa “mfumo mkubwa wa kuondoa maji machafu” karibu na hekalu. Kinasema hivi: “Huenda mfumo huo ulitumiwa kuondoa maji yaliyochanganyika na damu za wanyama waliotolewa dhabihu katika Eneo la Hekalu.”
Maji ya kutosha: Makuhani walihitaji maji ya kutosha ili wadumishe madhabahu na mfumo wa chini ya ardhi wa kuondoa maji machafu ukiwa safi. Ili kutimiza kazi hiyo muhimu, sikuzote makuhani walipata maji safi waliyohitaji kutoka katika jiji. Walipata maji hayo kupitia mifereji, matangi, na madimbwi. Mchimbuaji wa vitu vya kale, Joseph Patrich alisema hivi: “Mfumo huo mzuri wa kusambaza maji, kusafisha na kuondoa maji machafu hekaluni, ulikuwa wa kipekee wakati huo.”