Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Askari-jeshi wa Sauli walipokula nyama pamoja na damu, kwa nini wao hawakuuawa, kwa kuwa hiyo ilikuwa ndiyo adhabu iliyowekwa katika Sheria ya Mungu?
Kwa kweli wanaume hao waliikiuka sheria ya Mungu kuhusu damu, lakini huenda ikawa walionyeshwa rehema kwa sababu walikuwa wamestahi damu, hata ingawa wangalipaswa kuwa waangalifu zaidi kuhusu kuonyesha staha hiyo.
Ifikirie hali hiyo. Waisraeli chini ya Mfalme Sauli na mwanaye Yonathani walikuwa wakipiga vita dhidi ya Wafilisti. Hatua ilipofika ambayo ‘wanaume wa Israeli walikuwa wamekandamizwa sana’ vitani, Sauli aliapa harakaharaka kwamba watu wake hawakupaswa kula hadi adui aliposhindwa. (1 Samweli 14:24, NW) Upesi kiapo chake kikasababisha tatizo fulani.
Watu wake walikuwa wakishinda lile pigano walilokuwa wamepigana kwa juhudi, lakini jitihada hiyo nyingi ilikuwa ikiwaathiri vibaya. Waliumwa sana na njaa na kuchoka sana. Walifanya nini katika hali hiyo ya kupita kiasi? “Watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng’ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.”—1 Samweli 14:32.
Hilo lilikiuka sheria ya Mungu kuhusu damu, kama vile watu fulani wa Sauli walivyomwambia, wakisema: “Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu.” (1 Samweli 14:33) Ndiyo, Sheria ilikuwa imesema kwamba wanyama walipochinjwa, damu ilipasa iondolewe kabla ya nyama kuliwa. Mungu hakuamuru kwamba hatua za kupita kiasi zichukuliwe za kuondoa damu. Kwa kuchukua hatua zifaazo za kuiondoa, watumishi wake wangedhihirisha staha kwa ajili ya umaana wa damu. (Kumbukumbu la Torati 12:15, 16, 21-25) Damu ya wanyama ingeweza kutumiwa kwa njia ya kidhabihu madhabahuni, lakini haikupaswa kuliwa. Kukiuka kimakusudi kulikuwa na adhabu ya kifo, kwani watu wa Mungu waliambiwa hivi: “Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”—Mambo ya Walawi 17:10-14.
Je! askari-jeshi wa Mfalme Sauli walikuwa wakivunja Sheria hiyo kimakusudi? Je! walikuwa wakipuuza kabisa ile sheria ya kimungu kuhusu damu?—Linganisha Hesabu 15:30.
Hatuhitaji kukata kauli hivyo. Simulizi lasema kwamba ‘walikuwa wakichinja papo hapo juu ya nchi; na kula pamoja na damu.’ Kwa hiyo huenda ikawa walikuwa wakijaribu kwa kadiri fulani kuondoa damu. (Kumbukumbu la Torati 15:23) Hata hivyo, katika hali yao ya uchovu, na kuumwa na njaa, wao hawakuning’iniza wanyama hao waliochinjwa na kuruhusu wakati wa kutosha ili damu iondoke kwa njia ya kawaida. Waliwachinja kondoo na ng’ombe “juu ya nchi,” tendo ambalo lingeweza kuzuia ondoleo la damu. Na walikatakata nyama upesi kutoka kwa wanyama hao ambao huenda wakawa wamelalia damu. Kwa hiyo, hata ikiwa walitaka kutii sheria ya Mungu, wao hawakuifuata kwa njia zifaazo wala kwa kadiri ya kutosha.
Tokeo likawa kwamba “watu walikuwa wakiwala pamoja na damu,” tendo lililokuwa lenye dhambi. Sauli alitambua hilo akaamuru kwamba jiwe kubwa livingirishwe kwake. Akawaamuru askari-jeshi hao hivi: “Nileteeni hapa kila mtu ng’ombe wake, na kila mtu kondoo wake mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu.” (1 Samweli 14:33, 34) Askari-jeshi hao wenye hatia walitii, na “Sauli akamjengea BWANA, madhabahu.”—1 Samweli 14:35.
Kuwachinja wanyama kwenye jiwe labda kulisababisha ondoleo la damu la kutosha. Nyama kutoka kwa wanyama hao ingeweza kuliwa mbali na mahali pa kuchinjia. Huenda ikawa Sauli alitumia sehemu ya damu iliyoondolewa kwenye madhabahu akitafuta rehema ya Mungu kuelekea wale waliokuwa wametenda dhambi. Yaonekana Yehova alionyesha rehema kwa sababu alijua jinsi wale askari-jeshi walivyokuwa wamejaribu hata ingawa walikuwa wamechoka na wenye njaa sana. Huenda pia ikawa Mungu aliona kwamba kiapo cha Sauli cha harakaharaka kilikuwa kimewakandamiza watu wake kufikia hali hiyo ya kukatisha tamaa.
Simulizi hilo laonyesha kwamba hali ya dharura haitoi udhuru wa kupuuza sheria ya kimungu. Lapasa pia litusaidie tuone uhitaji wa kufikiria kwa uangalifu kabla ya kuapa, kwani kiapo cha harakaharaka chaweza kusababisha matatizo kwetu binafsi, na kwa wengine.—Mhubiri 5:4-6.