Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • hb kur. 3-7
  • Damu—Ni Muhimu kwa Uhai

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Damu—Ni Muhimu kwa Uhai
  • Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • DAMU NA WAKRISTO WA KWELI
  • NAMNA GANI KUTUMIA DAMU KUWA DAWA?
  • Kuokoa Uhai kwa Damu—Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Heshima ya Kimungu kwa Uhai na Damu
    Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele
  • Azimio Letu Imara Juu ya Uhai na Damu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Thamini Ifaavyo Zawadi Yako ya Uhai
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
Pata Habari Zaidi
Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?
hb kur. 3-7

Damu—Ni Muhimu kwa Uhai

Damu inaweza kuokoaje uhai wako? Bila shaka hili lakupendeza wewe kwa sababu damu inafungamanishwa na uhai wako. Damu inapeleka oksijeni kotekote katika mwili wako, inaondoa kaboni dayoksaidi, inakusaidia ujipatanishe na mabadiliko ya hali-joto, na inakusaidia kupigana na magonjwa.

Ufungamanisho wa uhai kwa damu ulifanywa wakati mrefu kabla William Harvey hajachora ramani ya mfumo wa mzunguko wa damu katika 1628. Elimu ya maadili ya dini kubwa-kubwa huelekeza fikira juu ya Mpaji-Uhai, aliyejieleza mwenyewe juu ya uhai na juu ya damu. Mwanasheria Myahudi-Mkristo alisema kwa habari zake: “Ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu.”a

Watu wanaoamini Mpaji-Uhai huyo wanatumaini kwamba mielekezo yake ni kwa ajili ya mema yetu ya kudumu. Nabii Mwebrania alimweleza kuwa Yeye ‘atufundishaye ili tupate faida, atuongozaye kwa njia itupasayo kuifuata.’

Uhakikishio huo, kwenye Isaya 48:17, ni sehemu ya Biblia, kitabu ambacho kinapewa staha kwa ajili ya kanuni zacho za elimu ya maadili ambazo zaweza kutunufaisha sisi sote. Kinasema nini juu ya binadamu kutumia damu? Je! kinaonyesha jinsi uhai unavyoweza kuokolewa kwa damu? Kwa kweli Biblia inaonyesha waziwazi kwamba damu ni zaidi ya umajimaji tata wa kibayolojia. Kinataja damu mara zaidi ya 400, na baadhi ya mitajo hiyo inahusu kuokoa uhai.

Katika mtajo mmoja wa mapema, Muumba alijulisha wazi hivi: “Kila kitu kinachoishi na kujongea kitakuwa chakula kwako. . . . Lakini ni lazima usile nyama ambayo damu ya uhai wayo ingali ndani yayo.” Aliongeza: “Kwa maana damu ya uhai wenu nitadai itolewe hesabu,” ndipo aliposhutumu uuaji kimakusudi. (Mwanzo 9:3-6, New International Version) Alisema hayo kwa Noa, mzazi wa kale wa watu wote anayeheshimiwa sana na Wayahudi, Waislamu, na Wakristo. Hivyo binadamu wote walijulishwa kwamba kwa maoni ya Muumba, damu inasimamia uhai. Hiyo ilikuwa zaidi ya kirekebi cha ulaji. Kwa wazi kanuni ya kiadili ilihusika. Damu ya kibinadamu ina umaana mkubwa na haipasi kutumiwa vibaya. Baadaye Muumba aliongeza habari zaidi ambazo kwazo twaweza kuona kwa urahisi yale masuala ya kiadili ambayo alifungamanisha na damu ya uhai.

Alirejezea damu tena alipowapa Israeli wa kale lile fungu la sheria. Ingawa watu wengi hustahi hekima na elimu ya maadili iliyomo katika fungu hilo la sheria, ni wachache sana wanaojua sheria zalo nzito juu ya damu. Mathalani: “Ikiwa yeyote wa nyumba ya Israeli au wa wageni wanaokaa miongoni mwao anashiriki kula sehemu yoyote ya damu, nitaweka uso Wangu dhidi ya mtu huyo anayeshiriki kula sehemu ya damu, nami nitamkatilia mbali kutoka miongoni mwa ukoo wake. Kwa kuwa uhai wa mnofu umo katika damu.” (Walawi 17:10, 11, Tanakh) Ndipo Mungu akafafanua vile mwindaji alivyopaswa kufanya na mnyama aliyekufa: “Atamimina damu yake na kuifunika kwa ardhi. . . . Hamtashiriki kula sehemu ya damu ya mnofu wowote, kwa kuwa uhai wa mnofu wote ni damu yao. Yeyote anayeshiriki kula sehemu yayo atakatiliwa mbali.”—Walawi 17:13, 14, Ta.

Wanasayansi wanajua sasa kwamba fungu la Sheria la Kiyahudi liliendeleza afya njema. Kwa kielelezo, lilitaka kwamba kinyesi kiwekwe nje ya kambi na kifunikwe na kwamba watu wasile nyama iliyobeba hatari kubwa ya kuwa na magonjwa. (Walawi 11:4-8, 13; 17:15; Kumbukumbu 23:12, 13) Ingawa sheria juu ya damu ilikuwa na pande zinazohusu afya, mengi zaid yalihusika. Damu ilikuwa na maana yenye ufananisho. Ilisimamia uhai ulioandaliwa na Muumba. Kwa kuitendea kuwa kitu cha pekee, watu hao walionyesha utegemeo wao juu yake kwa ajili ya uhai. Ndiyo, sababu kuu ya kutokula damu, si kwamba haikuwa yenye afya, bali kwamba ilikuwa na maana ya pekee kwa Mungu.

Kwa kurudia-rudia Sheria ilitaarifu marufuku ya Muumba juu ya kula damu ili kuendeleza uhai. “Ni lazima msile damu; imimineni juu ya ardhi kama maji. Msiile, ili kwamba iwe vema kwenu na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya yaliyo sawa.”—Kumbukumbu 12:23-25, NIV; 15:23; Walawi 7:26, 27; Ezekieli 33:25.b

Tofauti na vile wengi hufikiri leo, sheria ya Mungu juu ya damu haingepuuzwa kwa sababu tu tukio la dharura limezuka. Pindi ya hatari ya wakati wa vita, baadhi ya askari Waisraeli waliua wanyama na ‘wakala pamoja na damu.’ Kwa sababu ya tukio la dharura, je! iliruhusika kwao kuendeleza uhai wao kwa kula damu? La. Amiri wao aliwaonyesha kwamba mwendo wao ulikuwa ungali kosa zito. (1 Samweli 14:31-35) Kwa sababu hiyo, ingawa uhai ni wenye thamani sana, Mpaji-Uhai wetu hakusema kamwe kwamba viwango vyake vingepuuzwa katika tukio la dharura.

DAMU NA WAKRISTO WA KWELI

Ukristo unasimama wapi kuhusu suala la kuokoa uhai wa kibinadamu kwa damu?

Yesu alikuwa mwanamume wa ukamilifu-mwaminifu, na ndiyo sababu anastahiwa sana. Yeye alijua Muumba alisema kwamba ni kosa kula damu na kwamba sheria hiyo ilikuwa ingali yatumika. Kwa sababu hiyo, kuna sababu nzuri ya kuamini kwamba Yesu angetegemeza sheria juu ya damu hata kama yeye angekuwa anasongwa afanye tofauti. Yesu “hakufanya kosa, [na] hakuna hila iliyopatikana juu ya midomo yake.” (1 Petro 2:22, Knox) Hivyo yeye aliwekea wafuasi wake kigezo, kutia ndani kigezo cha kustahi uhai na damu. (Tutazungumza baadaye jinsi damu ya Yesu mwenyewe ilivyohusika katika jambo hili muhimu linalohusu uhai wako.)

Angalia ilivyotukia wakati, miaka mingi baada ya kifo cha Yesu, swali lilipozuka juu ya kama mtu anayekuwa Mkristo angelazimika kushika sheria zote za Israeli. Jambo hilo lilizungumzwa kwenye mkutano wa baraza lenye kuongoza la Kikristo, ambalo lilitia ndani mitume. Yakobo ndugu-nusu wa Yesu alirejezea maandishi yaliyokuwa na amri juu ya damu ambazo alitaarifiwa Noa na taifa la Israeli. Je! amri hizo zingetumika kwa Wakristo?—Matendo 15:1-21.

Baraza hilo lilipelekea makundi yote uamuzi wao: Wakristo hawakuhitaji kushika fungu la sheria alilopewa Musa, lakini ilikuwa “lazima” kwao ‘wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa [nyama zisizoondolewa damu], na uasherati.’ (Matendo 15:22-29) Mitume hawakuwa wakitoa kawaida tu za kidini au amri ya ulaji. Amri hiyo iliweka kawaida za msingi za elimu ya maadili, ambazo Wakristo wa mapema walitii. Wapata mwongo mmoja baadaye walikiri kwamba wangali wapaswa ‘wajilinde nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati.’—Matendo 21:25.

Wewe unajua kwamba mamilioni ya watu huhudhuria makanisa. Pengine walio wengi wao wangekubali kwamba elimu ya maadili ya Kikristo inahusu kutoipa mifano ibada wala kushiriki katika ukosefu mbaya sana wa adili. Hata hivyo, tunastahili kuangalia kwamba mitume waliweka kujiepusha na damu katika kiwango kile kile cha kiadili kama vile kujiepusha na makosa hayo. Uamuzi wao ulimalizia hivi: “Ikiwa kwa uangalifu nyinyi mnajiepusha wenyewe na vitu hivyo, nyinyi mtafanikiwa. Afya njema kwenu nyinyi!”—Matendo 15:29, NW.

Uamuzi wa kimitume ulieleweka kwa muda mrefu kuwa ulikuwa ungali watumika. Eusebio asimulia juu ya mwanamke mmoja kijana karibu na mwisho wa karne ya pili, ambaye kabla ya kufa chini ya mateso, alikazia jambo la kwamba Wakristo “hawaruhusiwi kula damu hata ya wanyama wasiofikiri.” Yeye hakuwa akitumia haki yake ya kufa. Alitaka kuishi, lakini yeye hangeridhiana juu ya kanuni zake. Je! wewe hustahi wale ambao huweka kanuni juu ya pato la kibinafsi.

Mwanasayansi Joseph Priestley alifikia mkataa huu: “Katazo la kutokula damu, alilopewa Noa, laonekana kuwa lenye kutumika kwa uzao wake wote . . . Tukifasiri [lile] katazo la mitume kwa zoea la Wakristo wa kwanza, ambao hawawezi kudhaniwa ifaavyo hata kidogo kwamba hawakuelewa asili na kadiri yalo, hatuwezi kufanya lolote ila kukata kauli, kwamba lilikusudiwa liwe kamili na la muda wote; kwa kuwa damu haikuliwa na Wakristo wowote kwa karne nyingi.”

NAMNA GANI KUTUMIA DAMU KUWA DAWA?

Je! katazo la Biblia juu ya damu lingehusisha pia matumizi ya kitiba, kama vile kutiwa damu mishipani, ambayo bila shaka hayakujulikana katika siku za Noa, Musa, au mitume?

Ingawa utibabu wa ki-siku-hizi wenye kutumia damu haukuwapo huko nyuma, utumizi wa damu kuwa dawa si wa ki-siku-hizi. Kwa miaka 2,000 hivi, katika Misri na kwingineko, “damu [ya kibinadamu] ilionwa kuwa ndiyo ponyo kuu kupita yote kwa ukoma.” Tabibu alionyesha utibabu aliopewa mwana wa Mfalme Esar-hadoni wakati taifa la Ashuri lilipokuwa ndilo lenye kuongoza katika mambo ya tekinolojia: “[Mwana-mfalme] anapata nafuu zaidi; bwana wangu, mfalme, aweza kufurahi. Kuanzia siku ya 22 nampa (yeye) damu anywe, atainywa kwa siku 3. Kwa siku 3 zaidi nitampa damu kwa kuiingiza ndani.” Esar-hadoni alikuwa na shughuli pamoja na Waisraeli. Hata hivyo, kwa sababu Waisraeli walikuwa na Sheria ya Mungu, hawangekunywa kamwe damu kuwa dawa.

Je! damu ilitumiwa kuwa dawa katika nyakati za Kiroma? Mtaalamu wa wanyama na mimea Pliny (aliyeishi wakati mmoja na mitume) na tabibu wa karne ya pili Aretaeo huripoti kwamba damu ya kibinadamu ilikuwa utibabu kwa kifafa. Baadaye Tertuliano aliandika: “Fikiria wale ambao kwa kiu yenye pupa, kwenye wonyesho uwanjani, hutwaa damu inayotiririka kutoka kwa wahalifu waovu . . . na kwenda nayo wakaponye kifafa chao.” Aliwatofautisha na Wakristo, ambao ‘hawana hata damu ya wanyama kwenye milo yao. Kwenye majaribio ya Wakristo nyinyi mnawapa masoseji yaliyojazwa damu. Bila shaka, nyinyi mnasadiki sana kwamba kitu hicho si halali kwao.’ Hivyo, Wakristo wa mapema wangepatwa na hatari ya kifo badala ya kula damu.

“Damu katika namna yayo ya kila siku . . . haikuacha kutumiwa ikiwa sehemu ya dawa na uchawi,” charipoti kitabu Flesh and Blood. “Kwa kielelezo, katika 1483, Louis 11 wa Ufaransa alikuwa anakaribia kufa. ‘Kila siku alizidi kuwa mahututi, na dawa hazikumfaidi kitu, ingawa alikuwa jamaa wa ajabu; kwa kuwa yeye alitumainia sana kupona kwa damu ya kibinadamu ambayo alitwaa kutoka kwa watoto fulani na kuimeza.’”

Namna gani kutia damu mishipani? Majaribio ya jambo hilo yalianza karibu na mwanzo wa karne ya 16. Thomas Bartholin (1616-80), profesa wa anatomia (elimu ya mwili na viungo vyao) kwenye Chuo Kikuu cha Copenhagen, alipinga hivi: ‘Wale ambao hulazimisha matumizi ya damu ya kibinadamu kwa maponyo ya kindani ya magonjwa huonekana wakiitumia vibaya na hutenda dhambi nzito. Walaji wa nyama ya kibinadamu hulaaniwa. Kwa nini sisi hatukirihi wale ambao hutia koo zao madoa kwa damu ya kibinadamu? Hali inayofanana na hiyo ni ile ya kupokea damu ngeni kutoka kwa mshipa uliokatwa, ama kupitia mdomoni au kwa vyombo vya kutilia damu mishipani. Waanzishi wa utendaji huu wanatishwa na sheria ya kimungu, inayokataza ulaji wa damu.’

Kwa sababu hiyo, watu wenye kufikiri wa karne zilizopita waling’amua kwamba Sheria ya Biblia ilitumika kuhusu kuingiza damu katika mishipa sawa na kuila kwa kinywa. Bartholin alimalizia: “Yoyote ya namna hizo za kutwaa [damu] hupatana na kusudi lile lile moja, kwamba kwa damu hiyo mwili wenye ugonjwa unalishwa au kuponeshwa.”

Maoni hayo ya ujumla yaweza kukusaidia kuelewa ule msimamo wa kidini usiojadilika wanaochukua Mashahidi wa Yehova. Wao huthamini sana uhai, na wanatafuta utunzaji mzuri wa kitiba. Lakini wameazimia kutohalifu kiwango cha Mungu, ambacho kimekuwa bila ugeu-geu: Wale wanaostahi uhai kuwa zawadi kutoka kwa Muumba hawajaribu kuendeleza uhai kwa kuingiza damu mwilini.

Hata hivyo, kwa miaka mingi madai yamefanywa kwamba damu huokoa uhai. Madaktari wanaweza kusimulia visa ambamo mtu fulani alipoteza sana damu lakini akatiwa damu mishipani naye akafanya maendeleo kwa haraka. Hivyo huenda ukauliza, ‘Hilo ni la hekima au ni lisilo la hekima kitiba jinsi gani?’ Uthibitisho wa kitiba unatolewa kuunga mkono utibabu wa kutumia damu. Hivyo, una wajibu wa kujipatia mambo ya hakika ili ufanye uchaguzi baada ya kuarifiwa juu ya damu.

[Maelezo ya Chini]

a Paulo kwenye Matendo 17:25, 28, tafsiri ya Union Version.

b Makatazo kama hayo yaliandikwa baadaye katika Kurani.

[Sanduku katika ukurasa wa 4]

‘‘Mawazo yaliyoandikwa hapa kwa njia ya utaratibu na barabara [katika Matendo 15] yanastahilishwa kuwa ya lazima, yakitoa ithibati yenye nguvu zaidi kwamba katika akili za mitume huo haukuwa mpango wa kitambo, au hatua ya muda tu.” — Profesa Édouard Reuss, Chuo Kikuu cha Strasbourg.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

Martin Lutheri alielekeza kwenye vionyesho vya uamuzi wa kimitume: “Sasa ikiwa twataka kuwa na kanisa linalotii baraza hili, . . . lazima tufundishe na kusisitiza kwamba kuanzia sasa na kuendelea mwana-mfalme, bwana, mkaa-mjini au mkaa-mashambani yeyote asile bata, sungura, paa au nyama-nguruwe iliyopikwa ndani ya damu. . . . Na wakaa-mjini na wakaa-mashambani lazima washike mwiko hasa wa soseji nyekundu na soseji yenye damu.”

[Hisani]

Woodcut cha Lucas Cranach

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

‘‘Mungu na wanadamu huona mambo kwa njia tofauti kabisa. Linaloonekana kuwa la maana katika macho yetu mara nyingi sana halina maana kabisa likikadiriwa kwa hekima isiyo na mwisho; na lionekalo kuwa dogo kwetu mara nyingi ni lenye maana kubwa kwa Mungu. Ilikuwa hivyo tangu mwanzo.” — “An Enquiry Into the Lawfulness of Eating Blood,” Alexander Pirie, 1787.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Medicine and the Artist cha Carl Zigrosser/Dover Publications

[Picha katika ukurasa wa 4]

Kwenye mkutano wenye kufanyiza historia, lile baraza lenye kuongoza la Kikristo lilithibitisha kwamba sheria ya Mungu juu ya damu ilikuwa ingali yatumika

[Picha katika ukurasa wa 7]

Hata matokeo yawe nini, Wakristo wa mapema walikataa kuhalifu sheria ya Mungu juu ya damu

[Hisani]

Mchoro wa Gérôme, 1883, kwa hisani ya Walters Art Gallery, Baltimore

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki